Na Gideon Mwakanosya, Songea
POLISI mkoani Ruvuma imewatia mbaroni wakazi kumi na tatu wa Songea mjini kwa tuhuma za kukutwa wakivuta bangi na pia wakiwa na misokoto kumi na tisa na glamu 250 ya bangi ndani ya uwanja wa michezo wa majimaji wakati wa mashindano ya mpira wa miguu ligi ya daraja la kwanza ngazi ya taifa kati ya timu ya Majimaji na JKT Mlale.
Habari zilizopatikana jana mjini hapa ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda zimesema kuwa tukio hilo lilitokea February 4 mwaka huu majira saa kumi na moja na nusu jioni ndani ya uwanja wa Majimaji ambapo watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na kiongozi wao Ally Hassani (20) mkazi wa majengo Songea.
Kamhanda alisema kuwa wakati timu za Majimaji na JKT Mlale zikiendelea kucheza kwenye mpambano wa ligi ngazi ya kwanza ya Taifa watuhumiwa hao wanadaiwa kuwa waliendelea kuvuta bangi na Ally Hassani ndiye anadaiwa kuwa alikuwa akipita kuiuza.
Alifafanua kuwa watuhumiwa wote kumi na tatu ambao wengine hakuwataja majina, watafikishwa Mahakamani mara tu upelelezi wa tukio hilo utakapo kamilika na kwamba kwa hivi sasa polisi inaendelea kuwasaka wengine ambao wanadaiwa kuwa walikimbia pindi walipoona wenzao wanakamatwa na polisi.
Katika pambano hilo ambalo lilihudhuliwa na wapenzi wa Club za majimaji na JKT Mlale katika pambano hilo pamoja na kuwepo purukushani zilizo sababishwa na watuhumiwa hao mpira uliendea kuchezwa hadi dakika ya mwisho ambapo majimaji na JKT Mlale zilitoka bila bila.
Mwisho.