About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Wednesday, July 16, 2014

TIDO ATIMKA MWANANCHI

 
 Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando akizungumza na wafanyakazi wa MCL jijini Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory
CHANZO: MWANANCHI
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando amewaaga wafanyakazi wa kampuni hiyo baada ya kumaliza mkataba wake wa miaka miwili na nusu.
Mkataba wa Tido katika kampuni ya Mwananchi utafika kikomo mwishoni mwa mwezi huu.
Taarifa ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Nation Media Group (NMG), Linus Gitahi kwa wafanyakazi wote wa Afrika Mashariki ambako kampuni hiyo inamiliki vyombo vya habari, inasema Mhando anaondoka MCL huku akiacha mafanikio makubwa katika nyanja zote na kwamba atakumbukwa kwa mchango wake.
MCL ni kampuni tanzu ya NMG inayochapicha magazeti ya Mwananchi, Mwananchi Jumamosi, Mwananchi Jumapili, The Citizen, The Citizen on Saturday, Sunday Citizen na Mwanaspoti.
Kabla ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MCL mwaka 2012, Mhando alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kati ya mwaka 2006 na 2010. Awali alikuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la BBC (1999-2006).
Mhando aliiwezesha MCL kukua kwa kasi kubwa katika mapato na katika mpango wa uchapishaji wa magazeti ya MCL Kanda ya Ziwa ambako wakazi wa mikoa hiyo sasa wamekuwa wakisoma magazeti asubuhi tofauti na zamani.
Wafanyakazi wa MCL walimpongeza kwa kuboresha masilahi yao kwa kipindi cha uongozi wake na kuandaa misingi bora ya uongozi, ikiwamo kumwandaa mrithi wake.
Akiwaaga wafanyakazi jana asubuhi, Mhando aliwashukuru kwa ushirikiano wao pia alisema amejifunza mambo mengi mapya, ikizingatiwa kuwa kwa miaka mingi alikuwa kwenye sekta ya habari ya utangazaji tofauti na uchapishaji. “Safari hii ilinipa uzoefu mpya na wenye changamoto nyingi lakini kupitia ushirikiano wenu wa dhati tulifanikiwa kuiweka kampuni katika hali nzuri,” alisema Mhando.
Gitahi alisema nafasi ya Mhando itachukuliwa na aliyekuwa Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa MCL (COO), Francis Nanai.
Nanai alijiunga MCL , Agosti mwaka jana akitokea Kampuni ya Saruji ya Mbeya Cement (Lafarge Tanzania) ya mkoani Mbeya akiwa Mkurugenzi wa Biashara.

Thursday, June 5, 2014

MATUKIO MUHIMU YA KUMBUKUMBU YA KUZALIWA SANGA ONE

Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma Golden Sanga  akipokea maelezo kutoka kwa Viongozi wa Ligi ya SANGA ONE CUP kabla hajakagua timu ya TMK na Timu ya Manispaa katika mchezo wao muhimu ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu yake ya kuzaliwa, ingawa pia ni kawaida yake kila mwaka kuanzisha Ligi katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea
SANGA ONE akipokea salamu za kuzaliwa kwake kupitia simu kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki kabla hajala nao chakula cha jioni katika ukumbi wa Hotel ya Top one inn

SANGA ONE ATIMIZA MIAKA 50 YA KUZALIWA KWAKE

Mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Ruvuma Golden Sanga (Sanga One) leo Juni 5, 2014 anatimiza miaka 50 ya kuzaliwa kwake 
HONGERA KWA KUTIIMIZA MIAKA HIYO SANGA NA MUNGU AKUJALIE AFYA TELE

Monday, March 3, 2014

MWANJA ; MAFANIKIO YA MBIO ZA BENDERA YAMELETA HAMASA MPYA CCM



Ni miaka minne sasa toka nilipoandika makala haya, leo kutokana na umuhimu wake naomba ndugu wasomaji wa Blog hii muweze kujikumbusha nilichokiandika na kama itawapendeza niko tayari kufanya uchambuzi mpya na wa kina kuhusu makala haya, endelea kutafakari kupitia maandisha haya 

picha nitaziweka hivi punde

MWANJA ; MAFANIKIO YA MBIO ZA BENDERA YAMELETA HAMASA MPYA CCM

Na: Stephano Mango, Songea
MIONGONI mwa kazi za chama cha siasa kilichopo Madarakani ni kuwa daraja la kuwaunganisha watu na serikali waliyoichagua katika kufanikisha ahadi zilizo ahidiwa wakati wa kampeni.

Mbali na jukumu  hilo, wajibu wa chama ni kusaidia watu kuielewa serikali yao inafanya nini kwa wakati gani na kwa lengo lipi.

Ni wajibu wa chama kutumia mbinu mbalimbali za kidemokrasia kuwahamasisha watu ili washirikiane na serikali yao ili kuwaondolea matatizo sugu ya umaskini, maradhi na ujinga ambao umewaelemea.

Chama pia kina wajibu wa kuhakikisha kuwa serikali inaendelea kuyajua maoni, shida na matakwa ya watu katika kufanikisha vita dhidi ya maadui ujinga, umaskini na maradhi.
Hata hivyo, chama kinawajibu wa kuwakemea wanachama wanaokwenda kinyume na matakwa ya kanuni na taratibu za chama.

Ingawa pia kina wajibu wa kuwaelimisha watu na wanachama wote kwa ujumla ili waweze kuona shughuli zinazofanywa na serikali yao katika kuwaletea maendeleo kusudiwa.

Hivyo basi, chama cha mapinduzi (CCM) kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka huu, na mwaka 2010 katika uchaguzi wa Madiwani, Wabunge na Rais

Kimejiandaa kushinda kwa kishindo katika chaguzi hizo kwa sababu katika uwanja mpana wa siasa mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa uchaguzi mwingine

Na lengo kubwa la Chama chochote cha siasa katika Nchi yoyote duniani ni kushinda katika uchaguzi Mkuu na kuunda Serikali yaani kukamata dola

Kwa mantiki hiyo, Uongozi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Ruvuma iliamua kupeleka ujumbe kwa Wanachama na Wananchi kwa kutumia mbio za Bendera ya Chama Cha Mapinduzi

Mbio hizo za Bendera zilizinduwa rasmi Mei 28 mwaka huu wa 2009 Wilayani Tunduru katika Kijiji cha Matemanga Mkoani Ruvuma na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa  Ruvuma  Coleneus Msuha.

Akizungumzia malengo ya mbio hizo za Bendera Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Bw. Emmanuel Mteming’ombe anasema kuwa mbio za Bendera ni ngeni na kwa mara ya kwanza zimekimbizwa Mkoa wa Ruvuma na kuleta mafanikio.

Anasema malengo ya mbio hizo za Bendera ni kukifanya Chama kionekane kwa watu na kwa Wanachama, kisha kisikike na watu waonyeshe dalili ya kusikia uwepo wa Chama hicho.

Ni lazima Chama kitumie mbinu mpya katika kujipenyeza kwa Wananchi katika Siasa za ushindani ili kuweza kuwahamasisha waingie Chamani anasema Kiongozi wa Mbio za Bendera Nestory Mwanja

Mwanja anaendelea kufafanua kuwa tumeamua kukimbiza Bendera ili kuwahamasisha Wanachama wawe hai kwa kulipia ada zao za Uanachama na kuhudhuria vikao vya Chama kuanzia ngazi ya mashina, matawi, Wilaya na Mkoa. 

Mbio hizo za Bendera zimefanya kazi kubwa ya kuwaeleza Wanachama wote ujumbe kutoka Halmashauri Kuu ya CCM Taifa NEC kuhusu mabadiliko ya upigaji kura za maoni kuhusu kumpigia kura Diwani, Mbunge na Rais anasema Kiongozi huyo.

Anasema pia mbio hizo zimetumika kupeleka ujumbe kwa Wananchi kuhusu umuhimu wa kujiandikisha katika daftari la wapiga kura katika 

Misingi ya Demokrasia.Kueleza Sera imara za CCM kwa Wananchi ili waweza kuzitafakari na kushawishika kuingia Chamani
Kwani kila Chama kinapaswa kujipambanua kwa Wananchi ili waweze kuchukua maamuzi sahihi ya Chama gani Wajiunge nacho anasema Kiongozi huyo wa CCM  Mwanja

Kinachoonekana sasa, baadhi ya Watu wanakimbilia kujiunga katika Chama chochote cha Siasa, wanakimbilia katika hivyo sio kwa sababu ya kuvutiwa na itikadi zake zinazo ambatana na imani, bali wanakwenda kwa sababu wamevutiwa na sera papo kwa papo ambazo huwa zinamwagwa jukwaani bila kuwepo kwa mikakati stahiki ya kuzitekeleza sera hizo anasema Mwanja

Mbio za Bendera zimetumika pia kuwahamasisha Wanachama kuanzisha miradi mipya na kuiendeleza miradi ya zamani ya Chama ili kijikwamue Kiuchumi. Kwa sababu Siasa ni Uchumi bila Uchumi imara hatuwezi kufanya Siasa katika Chama hivyo Chama imara ni chenye Uchumi imara anasema Mwanja

Anaendelea kufafanua kuwa, mbio hizo za Bendera zimetumika kuelezea bayana mafanikio ambayo Serikali ya CCM imeyapata kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita. 

Kwani kuyaanika hadharani mafanikio hayo kutawafanya Wananchi waelewe jinsi ilani ya Chama Cha Mapinduzi ilivyotekelezwa chini ya Mwenyekiti wa Chama hicho Taifa ambaye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete.

Kwani tunatambua kufanya hivyo kutaziba mianya kwa Viongozi wa vyama vya upinzani ambao kila kukicha wanajifanya vipofu na viziwi kwa kudai eti hakuna jambo lolote la maendeleo ya Watanzania linalofanywa na Serikali ya CCM huku wakijua wanayoyasema sio ya kweli anasema Mwanja

 Anaendlea kufafanua kuwa, CCM bado ni Chama makini kilicho na malengo makubwa ya kuwainua Wananchi wake hivyo wanapaswa kuwa na subira na kuridhika kwa yale mazuri yanayofanywa na Serikali pamoja na Chama tawala.

Kwani mambo mengi tumetekeleza kama ilani inavyoelekeza na katika maeneo mengine hasa katika Nyanja za miundo mbinu ya barabara, maji, afya na elimu, kuna mipango mbalimbali ya utekelezaji inaendelea  anasema kiongozi huyo.

Mwanja anasema kuwa mbio hizo zimetumika pia kumpongeza Rais Kikwete kwa kazi nzuri alayoifanya ya kutekeleza vyema ilani ya Chama Cha Mapinduzi. Kwani ni dhahiri juhudi zake za kuanzisha saccos na kutoa mitaji kwa wajasiriamali, kukuza Demokrasia katika misingi ya amani.utulivu na mshikamano.

Hata kuendeleza miradi ya Afya, barabara, maji, elimu na maboresho mbalimbali ya mishahara katika Sekta za Umma na mengineyo ni miongoni mwa utekelezaji mzuri wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi anasema Mwanja

Anaendelea kufafanua  Mwanja , mbio hizo za Bendera zimepita kwenye mashina na Matawi yote ya Chama Cha Mapinduzi Mkoani Ruvuma na kufanikiwa kuingiza jumla ya wanachama wapya 3951.

Na imezindua jumla ya miradi 35 ya Chama kwa Mkoa mzima, yaani imeweka mawe ya Msingi katika Ofisi za Matawi na pia zimefanikiwa kufungua Ofisi tano za Matawi.

Miradi hiyo imeghalimu jumla ya shilingi Milioni 380 ikiwa ni jitihada za Wanachama kutoka kwenye mashina na Matawi kwa ushirikiano Mkubwa na Uongozi wa CCM Mkoa.

Hata hivyo anasema mbio hizo zimepita kuangalia pia miradi ya Maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya nne.
Pia zimepita kuangalia miradi ya Wananchi na Wanachama wa CCM ya ufugaji wa Kuku, mbuzi,ng’ombe pamoja na ujenzi wa nyumba bora za watu binafsi ambapo miradi hiyo yote inagharimu Milioni  750.

 Katibu wa CCM Mkoa Ruvuma Emmanuel Mteming’ombe, amewashukuru wakimbiza Bendera kutoka katika Jumuiya ya umoja wa Vijana wa CCM Mkoa UVCCM.   

Ambao amewataja majina ya Mwanahamisi Ngaje kutoka Wilaya ya Namtumbo, Doris Ngareka kutoka Mbinga, Hamis Nkali kutoka Tunduru, Mkandu Ngonji kutoka Songea Vijijni, Nestory Mwanja ambaye ndio Kiongozi Mkuu, Hilda Mgao na Mwajuma Rashid kutoka Songea Mjini,   

Mteming’ombe anamalizia kwa kusema mbio hizo zenye mafanikio makubwa zilifikia kilele chake Juni  19 katika Kata ya Mletele iliyopo Manispaa ya Songea ambapo mgeni Rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa Coleneus Msuha.

Hata hivyo, Nestory Mwanja ambaye ndiye kiongozi wa mbio hizo za bendera amewataka Vijana wajiunge katika Chama kwani mhimili wa Taifa lolote ni Vijana.

Mwandishi wa Makala hii
Anaptikana kwa simu no.   0755 335051
Barua pepe:  Stephano12mango@yahoo.com



Sunday, March 2, 2014

FUIME ATANGAZA NIA YA UBUNGE 2015 JIMBO LA SONGEA MJINI KUPITIA CHADEMA


MWENYEKITI WA CHADEMA RUVUMA AMTIMULIA VUMBI DKT NCHIMBI



 MTANGAZA NIA YA UBUNGE JIMBO LA SONGEA MJINI JOSEPH FUIME AKIHUTUBIA MOJA YA MIKUTANO YAKE
MAMIA YA WAKAZI WAKIMSIKILIZA MTANGA NIA YA KUGOMBEA UBUNGE KATIKA KATA YA LIZABONI

Na Stephano Mango, Songea


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoa wa Ruvuma Joseph  Lusius Fuime ametangaza nia ya  kugombea Ubunge kwa tiketi ya Chama hicho katika Jimbo la uchaguzi la Songea mjini ifikapo mwaka 2015 katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu

Fuime  ambaye Diwani wa Kata ya Mjini katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea akitangaza nia hiyo  jana ya kutaka kugombea jimbo ambalo kwa sasalinaongozwa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt Emmanuel Nchimbi  kwenye mkutano wa hazara uliofanyika kwenye viwanja vya Soko kuu la Songea Mjini alisema kuwa ametafakari kwa muda mrefu pia ameombwa na makundi mbalimbali ya jamii ya Songea kuchukua fomu ya kugombea kiti hicho


Alisema kuwa baada ya kutafakari ameamua kwa dhati kusikiliza kilio cha makundi hayo na kugombea ubunge kwa tiketi ya CHADEMA  ili kwa pamoja kuweza kuondoa kero mbalimbali ambazo zinawasumbua wakazi hao


“Naomba niwaondoe hofu wanachama wenzangu ndani ya Chadema kuwa kutangaza kwangu nia  ya kutaka kugombea Ubunge hakuna maana kuwa wanachama wengine wanaotaka kugombea washindwe kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo”


Alisema kuwa wanachama ndio wenyewe  mamlaka ya kumchagua mgombea mwenye kujua matatizo ya wakazi wa Manispaa ya Songea na mbinu ya kushirikiana na wananchi hao kuweza kuyatatua kwa maslahi mapana ya ustawi wa jamii hiyo, pia atakayeweza kupambana na mgombea wa Ubunge kwa tiketi ya ccm.


Alieleza zaidi kuwa baada ya kufikia uamuzi huo kabla ya kutangaza nia aliamua kukaa na wazee wote wa Songea Mjini ambao wote kwa pamoja wameonyesha ushirikiano mkubwa na wamemwakikishia kuwa mwaka 2015 wakati wa uchaguzi watamuunga mkono kama walivyomuomba


Fuime ambaye pia ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ccm katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea alijigamba na kuwaeleza wakazi wa Songea kuwa yeye ndiye anayefaa kupambana na Mbunge wa Songea Mjini kwa tiketi ya Ccm  Dkt Emmanuel Nchimbi.


Alifafanua zaidi kuwa Chadema imejipanga kwa dhati kutotoa nafasi tena ya uongozi kwenye Jimbo la uchaguzi la Songea Mjini kuchukuliwa na Ccm ambalo lina kata 21 na kati ya hizo 8 zinaongozwa na Madiwani wa Chama cha Chadema na kwamba mwaka 2015 kata zilizobaki zitanyang’anywa na Chadema.


Aliongeza kusema kuwa dawa ya kupambana na manyang’au waliomo ndani ya Ccm ni kujipanga na kuwabana kwa kutowapa nafasi ya aina yeyote kuanzia sasa na mpaka ifikapo 2015 kwani hivi sasa miradi mbalimbali katika Halmashauri ya Manispa ya Songea imekuwa ikijengwa chini ya viwango ambapo alitoa mfano kuwa miundombinu ya barabara, ujenzi wa vyumba vya madarasa na ofisi zimekuwa zikijengwa chini ya viwango huku manyang’au wa Ccm wakineemeka.


Alisema kuwa Wananchi wa Songea ambao wamekuwa wakikabiliwa na shida mbalimbali kutokana na ombwe la uongozi unaotokana na mfumo mbovu wa Ccm wana kila sababu ya kuunga mkono wazo lake la kuwania kiti cha Ubunge ili kuweza kufanikisha ustawi bora wa maisha ya wakazi wote kwa ushirikiano


Awali katika vipindi viwili vya uchaguzi mkuu vilivyopita Chama cha Demokrasia na Maendeleo kilikuwa kinamnadi Wakiri wa kujitegemea Edson Osward Mbogoro kugombea nafasi hiyo ambapo alikuwa akibwagwa na Mgombea wa Ccm  Dkt Emmanuel Nchimbi  ambaye ndiye Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini hadi sasa.


MWISHO

Monday, February 10, 2014

WAFANYABIASHARA SONGEA WAIGOMEA SERIKALI MASHINE ZA TRA

Na Stephano Mango, Songea.
 
WAFANYABIASHARA   wa maduka mbalimbali katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wamegomea kufungua maduka  yao  kwa kile kinachodaiwa  kuwa    serikali imeshindwa kuwasikiliza kilio chao cha mashine za kielektroniki   (EFD) ambazo zinatakiwa kwa muda mrefu waliomba zishushwe bei .

Uchunguzi uliofanywa na waandishi wa habari  wa mjini Songea  umebaini kuwa  katika mitaa yote  ya Manispaa ya Songea  maduka yote yamefungwa  na kwamba katika eneo la soko kuu  kwenye vibanda  vinavyolizunguka soko hilo  navyo vimefungwa isipokuwa  wafanya biashara ndogondogo wanaouza mchele, unga , nyanya na mbogamboga ndio wanaoendelea kufanya biashara .

Badhi ya wafanya biashara  waliohojiwa  kuhusiana na mgomo huo walisema kuwa  kwa muda mrefu     waliiomba mamlaka ya mapato Tanzania (TRA)  Mkoa wa Ruvuma  iangalie uwezekano  wa kushusha   bei ya mashine  za kielektroniki  amabazo zimekuwa zikiuzwa kati ya shilling laki sita  na laki nane  jambo ambalo walidai kuwa bei hiyo wafanyabiashara wengi wanashindwa kuimudu .

Walisema kuwa hivi karibuni alifika mijini Songea Naibu Waziri  wa fedha Mwigulu Nchemba na kufanya mkutano mkubwa kati yake na  wafanya biashara  lakini alishindwa kutoa maelezo yakinifu kuhusiana na bei   ambayo imeonekana kuawa ni kandamizi kwa wafanyabiashara hao.

Walifafanua kuwa wafanyabiashara hawagomei kuzinunua mashine hizo isipokuwa wamedai kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakivutana kwa kuitaka serikali iangalie namna ya kuzishusha bei ambayo wafanyabiashara wanaweza kuimudu tofauti na hivi sasa.

 Wameelezakuwa  mawakala wa kuuza mashine hizo mkoani Ruvuma wameteuliwa wachache na kuonekana kuwa kuna viwingu namna ya upatikanaji wa mashine hizo hivyo wameiomba serikali itumie mfumo wa soko huria.

 Kwa upande wake meneja wa mamlaka ya mapato [TRA] mkoani Ruvuma Apili Mbaruku alithibitisha kuwa maduka katika manispaa ya Songea kuwa yamefungwa lakini alieleza kuwa ofisi yake inafanya utaratibu wa kuangalia tatizo jinsi lilivyo.

 Naye katibu mtendaji wa chama cha wafanyabiashara [TCCIA]mkoani Ruvuma ,Moyo akiongea kwa njia ya simu alisema kuwa kuanjia majira ya saa za asubuhi wafanyabiashara kwa pamoja waliamua kufunga maduka yao wakidai kuwa bei za mashine za kielektroniki ni kubwa tofauti na biashara wanazo zifanya lakini kufuatia tukio hilo la mgomo tayari mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu ameitisha kikao kwa mazungumzo zaidi.
 
Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Ruvuma Mwambungu akiongea kwa njia ya simu alithibitisha kuwepo kwa mgomo huo na kwamba anatarajia kukutana na wafanyabiashara pamoja na maafisa kutoka mamlaka ya mapato ili kuangalia tatizo hilo.
    MWISHO.
 

Wednesday, January 29, 2014

LOWASSA HATARINI KWA TAMKO LA VIJANA



 Paul Christian Makonda,Katibu wa Hamasa na Chipukizi.
“..Chama Cha Siasa chochote duniani hubomoka kutokana na migongano iliyokithiri ya muda mrefu. Uzoefu wa vyama vikubwa vilivyoporomoka umeonyesha hivyo! Chama lazima kidhibiti uchu wa madaraka wa baadhi ya viongozi wake na ndani ya serikali yake...” – Dr Eginald P. Mihanjo
“..Chama cha siasa ni itikadi. Chama cha siasa ni siasa kwa maana halisi ya neno lenyewe siasa –“siasa”. Ni mahali ambapo watu wenye madhumuni mamoja yaliyoainishwa waziwazi hukutana na kuwa kitu kimoja. Chama cha siasa sio mkusanyiko wa “majini dume yenye tamaa”, - majini ambayo yametanguliza mbele tamaa kufa na kupona-tamaa ya kutengeneza pesa au kupata vyeo kwa gharama yoyote! – Dr Bashir Ally

UTANGULIZI:
Hili ni tamko la vijana makini wa jumuiya ya umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kuunga mkono juhudi na utendaji wa sekretarieti ya halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi ikiongozwa na Katibu Mkuu Komredi Abdulrahaman Kinana.

Maneno ya utangulizi yamebeba dhima ya tamko hili, kufuatia taarifa zilizoripotiwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari vikiwanukuu baadhi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi, wakiwatuhumu Viongozi wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM, Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahaman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndugu Nape Moses Nnauye.

Sisi Vijana tunatambua kuwa tuhuma hizo na maneno hayo ya hovyo yametolewa kwa nia ovu yenye kulenga kuwakatisha tamaa Viongozi hao wa Chama. Tunafahamu kuwa upo mkakati wa kiuhaini ulioandaliwa na kuratibiwa na “mtandao” ndani ya Chama ambao umejipanga kuendesha uhaini huo.

Sisi vijana wa UVCCM tunatambua na kuthamini juhudi za Katibu Mkuu na Sekretarieti yake katika kukijenga na kukiimarisha Chama kwa kuisimamia barabara misingi na shabaha ya kuundwa kwake, katika umri wetu hatukuwahi kuona Chama kikiwa karibu na wananchi kwa kufuatilia, kusikiliza na kushiriki katika utatuzi wa kero, shida na changamoto zao kama ilivyo katika kipindi hiki chini ya Comrade Kinana na timu yake. Juhudi hizi ni za kuungwa mkono na kamwe si za kubezwa na mwanaCCM muadilifu, muaminifu na mwenye mapenzi ya kweli kwa Chama.

Juhudi za kukiimarisha Chama kutoka ngazi za chini, kwa mabalozi ni mkakati bora kuwahi kutekelezwa na Chama, kukirudisha Chama kwa wanachama ni kutimiza lengo la kuundwa kwa Chama hiki, Chama hiki ni cha wanyonge, masikini wa Taifa hili, HAIWEZEKANI matajiri watake kukihodhi na waratibu mikakati ya kukihujumu kwa pesa zao hali sisi vijana tukitazama, tunasema tutakilinda Chama chetu na tutawalinda viongozi wetu waadilifu.

Ni hawa ambao wanabezwa leo ndio wameweza kurudisha Imani ya wananchi kwa Chama, Imani na matumaini ambayo tayari yalishaanza kupotea na Chama kuonekana si tena cha wanyonge, wakulima na wafanyakazi wan chi hii.

Ni Comrade Kinana na timu yake ndio waliozunguka kwenda kukutana na wakulima wa Pamba kule mikoa ya Kanda ya ziwa na kumpeleka balozi wa China na kumshawishi kujenga viwanda ili kuboresha manufaa kwa wakulima.

Ni Comrade Kinana na timu yake ndio waliokwenda Kusini kukutana na wakulima wa Korosho na kushirikiana nao pamoja na bodi kutatua tatizo la Korosho.

Ni Comrade Kinana na timu yake ndio walioibua hoja na kero za wafugaji, walimu na wananchi kwa ujumla, na kuwataka viongozi wa Serikali kuhakikisha wanawajibika kwa wananchi walipa kodi wa Taifa hili.

Kupinga mafanikio ya Ziara hizo ni kupinga utetezi wa wanyonge.

Mtu anayebeza ziara hizo na kuwaita Viongozi waliozifanya waropokaji na wahuni wahuni ni mtu mjinga, mtu wa hovyo,hana maadili, asiyekipenda Chama, mhaini na mzandiki anayepaswa kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu ili iwe fundisho kwa wengine.

TAMKO hili limezingatia wosia wa Baba wa Taifa, muasisi wa Chama Cha Mapinduzi Mwl Julius Kambarage Nyerere katika kitabu Chake TUJISAHIHISHE.

“Inapofikia wasimamizi wa Kanuni za Chama wanapigwa vita ya wazi kwa uamuzi wao wa kukisimamia Chama, tafsir yake ni moja tu watu wanaowapiga vita hawakitakii mema chama chetu.”

Imetolewa na Paul Christian Makonda.

Katibu wa Hamasa na Chipukizi.

Monday, January 27, 2014

WAFANYABIASHARA MANZESE WAUCHARUKIA UONGOZI WAO



Na, Stephano Mango, Songea
WAFANYABIASHARA  wa Soko la Manzese B lililopo katika halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wameutaka Uongozi wao ujiudhuru mara moja kutokana na utawala mbovu wanaoufanya na kuendeleza vitendo vya hujuma katika soko hilo

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa Habari jana katika viwanja vya soko hilo walisema viongozi hao wamekuwa wakishirikiana na Viongozi wa Halmashauri ya Manispaa kukiuka maadili ya uongozi na kusababisha migogoro ya mara kwa mara inayopelekea uvunjifu wa amani

Walisema kuwa toka kuwepo kwa mpango wa ujenzi wa vibanda 68 vya Soko hilo, viongozi wamekuwa wakifanya vikao vya siri vya kuwahujumu wafanyabiashara waliopo sokoni hapo kwa kupanga mipango ya kuwanyang’anya ili vibanda hivyo wapewe wafanyabiashara  vigogo ambao hawafanyi biashara katika soko hilo

Walisema kuwa mipango hiyo ya siri imezua malalamiko makubwa sana miongoni mwa wafanyabiashara kwani makubaliano ya awali yalikuwa ni lazima wafanyabiashara waliopo wapewe kipaumbele katika ujazaji wa mikataba katika ujenzi huo

“ Tunashangaa kuona viongozi wa Soko na Viongozi wa Halmashauri wanatoa mikataba kwa siri kwa wafanyabiashara vigogo kutoka maeneo mengine kinyume na utaratibu kitendo ambacho kimetusikitisha sana kwani hakijawa na uhalali wa kidemokrasia zaidi ya ubabe”

Walisema hali hiyo inaonyesha wazi kabisa kuwa kuna vitendo vya rushwa, ukiukwaji wa haki za binadamu kwani mara kwa mara wafanyabiasha wakihoji uhal wa mambo ambayo yanafanywa na viongozi hao wanatishiwa kwa maneno ya kuudhi

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mwenyekiti wa Soko hilo Omary Masai alisema kuwa yeye sio msemaji wa jambo hilo kwani linafanywa Mstahiki Meya wa Halmashauri Charles Mhagama hivyo kwa maelezo zaidi atafutwe yeye

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Misufini ambako soko hilo lipo Salumu Mfamaji alisema kuwa ujenzi huo unafanywa kihuni kwani kuanzia viongozi wa Serikali ya Mtaa na Serikali ya Kata haijashirikishwa na kuwa jambo hilo linaonekana limegubikwa na rushwa

Mfamaji alisema kuwa amewasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria na wataalamu wake kusitisha mara moja ujenzi huo mpaka pale mkutano wa wafanyabiashara utakapoitishwa ili waweze kutendewa haki ikiwemo ya kuonyeshwa ramani ya Soko hilo na mikataba

Naye Meya wa Manispaa hiyo Charles Mhagama alipohojiwa kuhusiana na malalamiko ya Wafanyabiashara alisema kuwa tatizo hilo lipo lakini alidai kuwa msababishaji mkubwa ni Diwani wa kata hiyo na ndio maana Halmashauri imeamua kusimamia yenyewe ujenzi huo

Hata hivyo juhudi za kumtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri kupitia simu yake ya kiganzani Nachoa Zakaria ziligonga mwamba kwani simu yake ilikuwa inaita tu bila kupokelewa

MWISHO