About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Sunday, January 22, 2012

WATAKIWA KUWAPIMA WABUNGE WAO KWA USHIRIKISHAJI WA WANANCHI


                                  Afisa Kazi Ruvuma Oddo Hekela

Na Stephano Mango,Songea

WANANCHI wametakiwa kuwapima Wabunge na Madiwani wao ili kuweza kubaini ubora wao katika ushirikishaji wa wananchi katika eneo lake la uongozi katika kuleta maendeleo ya nchi kwa kutumia dhana shirikishi
Wito huo umetolewa jana na Afisa Kazi Ruvuma Oddo Hekela kwenye mdahalo  wa wazi wenye lengo la kupata taswira ya uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi wao ulioitishwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Songea(Sonngo)kwa ufadhiri wa Shirika la The Foundation For Civil Society
Hekela alisema kuwa Mbunge na Diwani wote ni wawakilishi katika eneo lao la kazi ambao wamebeba jukumu la kuhamasisha wananchi katika kutekeleza majukumu ya maendeleo hivyo ushirikishwaji bora ndio maendeleo bora
Alisema kuwa ili kupima ubora wa Mbunge na Diwani lazima upime uwezo wa ushirikishwaji wa wananchi katika eneo lake ili kuweza kuleta maendeleo ya nchi kwani wote ni wawakilishi wa wananchi katika Serikali ya watu hivyo wajibu wao unafanana
Alieleza kuwa miongoni mwa majukumu ya Mbunge akiwa jimboni ni kukaa ofisini na kuhudumia wananchi kwa kusikiliza hoja zao ili aweze kuzitatua au kuzipeleka sehemu husika kwa hatua zaidi,kufanya ziara kwa wananchi ili kuweza kujua mikakati ya maendeleo,kufuatilia utekelezaji wa miradi ya kitaifa jimboni kwake inayotekelezwa na Serikali kuu kusikiliza maoni ya wananchi kuhusiana na utekelezaji wa miradi hiyo
Alieleza zaidi kuwa majukumu yake mingine akiwa jimboni ni pamoja na kusimamia utekelezaji wa sera mbalimbali kwa kutoa tafsiri ya sera zenyewe ili wananchi wazielewe,kutoa elimu na kuwahamasisha wananchi ushiriki wao katika miradi ya maendeleo
Kwa upande wake Katibu wa Mtandao wa Sonngo Mathew Ngarimanayo alisema kuwa Viongozi wanapaswa kutimiza wajibu wao kikamilifu katika kuhakikisha Sera mbalimbali zinawanufaisha wananchi ili kuweza kupunguza umaskini wa kipato unaowakabili na kuweza kuchangia pato la Taifa
Ngarimanayo alieleza kuwa ni jambo la aibu kuona Mbunge anazunguka mjini huku wapiga kura wake wanahangaika kutokana na sera mbalimbali kutokuwa wazi na wakati mwingine kushindwa kumnufaisha mwananchi kutokana na kuwa katika mazingira magumu ya upatikanaji wake na zimewekwa katika lugha ambayo mwananchi mnyonge hawawezi kuielewa
MWISHO

WAZIRI MAGHEMBE ATAKIWA KUTEMBELEA MIKOA INAYOZALISHA MAZAO YA CHAKULA

Ukiwaona kwa mara ya kwanza unaweza kusema ni vijana wa familia moja(Baba mmoja) lakini hawa sio ndugu ila ni Wanaharakati wakubwa wa Haki za Binadamu katika Mkoa wa Ruvuma

Picha hii walipiga nje ya ukumbi wa mdahalo uliofanyika katika Wilaya ya Songea,Jimbo la Peramiho,Kata ya Mtyangimbole mara baada ya kumalizika kwa mdahalo huo ikiwa ni furaha ya kumalizika kwa mdahalo huo kwa upendo na amani

Hawa vijana wana vyeo vingi sana katika jamii,lakini kwa eneo hili na madhumuni ya picha hii kila mmoja atakuwa na cheo kimoja kilichowakutanisha hapo

Kutoka kushoto ni Katibu wa Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Songea (Sonngo) Mathew Ngarimanayo,wa kwanza kulia na Afisa Habari wa Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Songea(Sonngo) Andrew Chatwanga


Mmiliki wa Mtandao huu,Stephano Mango akiendelea kuhabarisha umma katika mdahalo huo,wa pili toka kulia ni  Mwanafunzi wa Chuo cha Ustawi na maendeleo ya Jamii Rungemba Mariana Nyoni,wa tatu ni Msaidizi wa Ofisi ya Sonngo Sophia Limbuya

Na Stephano Mango,Songea
WANANCHI wa kata ya Mtyangimbole wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wamemtaka Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika Profesa Jumanne Maghembe kuona umuhimu wa kutembelea mikoa inayozalisha mazao ya chakula ili kuweza kutatua changamoto zinazowakabili katika msimu huu wa kilimo ili kuweza kupunguza uhaba wa chakula nchini
Wito huo umetolewa jana na Diwani wa Kata ya Mtyangimbole Meckezedeck Mwella  kwenye mdahalo  wa wazi wenye lengo la kupata taswira ya uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi wao ulioitishwa na Mtandao wa Asasi za Kiraia Wilaya ya Songea(SONNGO kwa ufadhiri wa Shirika la The Foundation For Civil Society
Mwella alisema kuwa Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kama mahindi,mihogo lakini wananchi wake wamekuwa wakiendelea kukwamisha na mipango mbalimbali ya Serikali yenye malengo ya kuinua kilimo
Alisema kuwa wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia mfumo mbovu wa ugawaji wa pembejeo za ruzuku zinazotolewa na Serikali kwa lengo la kuwainua wakulima kutokana na urasimu mkubwa unaojitokeza kuanzia ngazi ya mtaa hadi Wilaya na kusababisha kero kubwa kwa wakulima hao
Alieleza kuwa siku zote mkulima hana likizo kwani kwa kipindi chote cha mwaka yeye anahangaika na shughuli za kilimo lakini amekuwa ni maskini wa kutupwa kutokana na uzembe toka kwa viongozi wa Serikali ambao wamekosa huruma dhidi ya wakulima kwa kuwanyonya haki zao mbalimbali
Alieleza zaidi kuwa kitendo cha Serikali kushindwa kununua mahindi toka kwa mkulima msimu wa 2011/2012 na kusababisha mahindi hayo kuanza kuota yakiwa kwenye magunia maeneo mbalimbali ya maghala ni cha uonevu mkubwa kwani wakulima wengi wamekata tamaa kutokana na madeni mbalimbali yanayowakabili kutokana na uzalishaji walioufanya katika msimu uliopita
“Wakulima walitegemea kuwa msimu wa uuzaji wa mahindi wangeweza kupata fedha kwa ajili ya kuandaa msimu mwingine wa kilimo,kulipia karo za watoto,kupata mahitaji muhimu ya kibinadamu,na kulipia huduma mbalimbali za kijamii lakini imeshindikana kutokana na mipango mibovu ya Serikali kuhusu kumkomboa mkulima kwenye upatikanaji wa masoko ya uhakika wa mazao hayo”alisema Mwella
Akizungumza kwenye Mdahalo huo Katibu wa Sonngo Mathew Ngarimanayo alisema kuwa Viongozi wanapaswa kutimiza wajibu wao kikamilifu katika kuhakikisha Sera za kilimo,ushirika na masoko zinawanufaisha wakulima ili kuweza kupunguza umaskini wa kipato unaowakabili na kuweza kuchangia pato la Taifa
Ngarimanayo alisema kuwa katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo Waziri wa Kilimo,Chakula na Ushirika, maafisa kilimo wa ngazi zote wanapaswa wawatembelea wakulima kwenye maeneo yao ili kuweza kubaini vikwazo mbalimbali wanavyokutana navyo wakulima  katika msimu wa kilimo badala ya kukaa ofisini wakisubiri taarifa potofu toka kwa wasaidizi wao
Alieleza kuwa ni jambo la aibu kuona Mbunge anazunguka mjini huku wapiga kura wake wanahangaika na kilimo kwa kutumia dhana duni zisizokidhi viwango vya uzalishaji wa mazao kwa wengi  bila kusaidiwa na wataalamu wa kilimo na kusababisha uzalishaji kupungua kutokana na kutumia pembejeo duni
Awali Mwenyekiti wa mtandao wa Asasi zisizokuwa za Kiserikali Wilaya ya Songea (Sonngo)Siwajibu Gama akifungua mdahalo huo alisema kuwa lengo la mdahalo huo ni kuwawezesha wananchi kutambua wajibu wao na kuelewa wajibu wa viongozi wao ili waweze kukaa pamoja,kupanga na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa pamoja
MWISHO

MDAHALO WA WAZI KUHUSU KUIMARISHA MAHUSIANO KATI YA WABUNGE NA WANANCHI WAO WAMALIZIKA

 Viongozi wa Asasi ya Sonngo na Viongozi wa Serikali wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea wakiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa mdahalo huo mara baada ya kumalizika