Na Stephano Mango,Songea
MTUHUMIWA wa kesi ya mauaji ya Thomas Jibaba (22)mkazi wa Mwanza amehukumiwa kwenda kutmikia kifungo jela miezi 12 kwa kosa la kukimbia mahakamani akiwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi alikokuwa amepelekwa kwa ajili ya kutajwa kesi zake mbili za awali zinazomkabili ikiwemo ya mauaji
Akisoma hukumu hiyo Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Songea Sara Mbise alisema kuwa Mahakama imeridhika na maelezo yaliyotolewa na upande wa mashtaka ambayo yamebainishwa Mahakamani hapo kuwa Jibaba alitenda kosa hilo kwa kudhamiria
Mbise alisema kuwa vilevile Mahakama hiyo imekubariana na ushahidi uliotolewa Mahakamani hapo kuwa kosa alilolifanya Jibaba ni la pili kutokea ambapo inadaiwa kuwa novemba mwaka jana napo alitenda kosa la kuwakimbia Askari wakati wanampeleka Hospital kwenda kutibiwa na alikamatwa baada ya kushindwa kuruka uzio wa Hospital ya Mkoa ya Songea
Alisema kuwa kutokana na hivyo Mahakama imemtia hatiani na imemuhukumu kwenda kutumikia kifungo cha miezi 12 jela na adhabu hiyo itakuwa ni fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia mbaya kama hiyo
Kwa upande wake Mwendesha mashtaka Koplo Samwel alidai Mahakamani hapo kuwa mnamo Januari 6 mwaka huu majira ya saa za asubuhi alipangiwa kazi na viongozi wake ya kwenda kuwachukua mahabusu wawili kwenye Gereza la Mahabusu la Songea na kuwapeleka Mahakamani ambako kesi zao zilipangwa kutajwa
Koplo Samwel akiwa na Askari wenzake walifika Gerezani na kuwachukua Mahabusu hao na baadaye waliwapeleka Mahakamani ambako Jibaba alikuwa ni mmoja kati ya Mahabusu hao ambaye anakabiliwa na kesi ya wizi na mauaji
Alifafanua kuwa kesi yake ya mauaji Jibaba ilitajwa kwa mara ya pili na ilihahirishwa hadi Januari 17 mwaka huu na kesi nyingine ya wizi wa vifaa vya studio zikiwemo kamera na Kompyuta ilitajwa na kuhahirishwa hadi Januari 19 mwaka huu mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa
Alieleza zaidi kuwa baada ya kesi hizo kuhahirishwa Jibaba aliamuriwa kuondoka Mahakamani hapo kwenda mahali walipohifadhiwa Mahabusu wengine ghafla majira ya saa 4:30 asubuhi alianza kukimbia na kuwaacha Askari wakati wanajiandaa kumfunga pingu ndipo Askari wengine waliokuwa nje na Siraha walianza kumkimbiza huku wakipiga risasi hewani na baadaye ilipopigwa risasi ya tatu hewani bado mtuhumiwa aliendelea kukimbia ghafla walijitokeza Askari wengine mbele yake ndipo walipofanikiwa kumkamata nje kidogo ya Mahakama hiyo na kumrudisha mahakamani ambako alifunguliwa shtaka la kukimbia akiwa chini ya ulinzi mkali wa Polisi
MWISHO