About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Sunday, July 8, 2012

MAHOJIANO YA GAZETI LA JAMHURI NA ACP MSANGI KUHUSU DKT ULIMBOKA

 

Askari anayetuhumiwa kumteka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, Kamishna wa Polisi Msaidizi (ACP), Ahmed Msangi, amehojiwa na kuzungumzia kilichotokea kuhusiana na tuhuma kwamba aliambiwa arejeshe simu ya mkononi na pochi ya Dk. Ulimboka. Akizungumza, ACP Msangi alikiri kwenda katika wodi ya wagonjwa mahututi katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa nia ya kumhoji Dk. Ulimboka, ila akaeleza mshangao wake kutokana na habari zilizochapishwa mwishoni mwa wiki, kuwa aliambiwa arejeshe pochi na simu ya Dk Ulimboka kwa maana kuwa alivipora walipomteka.
Vyombo vya habari mwishoni mwa wiki vilichapisha taarifa bila kutaja jina la askari anayetuhumiwa, lakini pia ukawa unasambazwa ujumbe mfupi kupitia simu za mkononi ambao ulisema hivi:


“Kamanda Msangi aliyemkamata na kumtesa Dr. Ulimboka, yuko katika jopo la kuchunguza nini kilimtokea Dk. Ulimboka. Alipofika kumhoji Dk. Ulimboka alimwambia ‘Nirudishie simu na wallet yangu’. Kamanda Msangi taratibu akaondoka wodini kichwa chini. Kama wewe ni mpenda haki na unapinga ujinga na dhuluma, watumie ujumbe huu watu wengi kadri uwezavyo ili wamjue dhalimu aliyeongoza unyama huu,” ulisema ujumbe huo unaosambazwa kupitia simu za mkononi.


Tume ya Jeshi la Polisi iliyoundwa kuchunguza tukio la Dk. Ulimboka kutekwa nyara, kwa mujibu wa Kamanda Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, inaongozwa na Kamanda Msangi.


Kamanda Msangi azungumza

Jamhuri: Afande umetangazwa kuongoza hii Tume ya Polisi kuchunguza suala la Dk. Ulimboka, lakini taarifa zilisosambaa zinaonyesha Ulimboka alikwambia umerejeshee simu na wallet yake. Unalizungumziaje hili?


Kamanda Msangi: Hata mimi nimesikia hizi taarifa, na zimenisikitisha mno. Naamini taarifa hizi zina malengo ya ziada. Si kweli kwamba nilishiriki kumteka Dk. Ulimboka na wala sijawahi kuwa na wazo hilo.



Jamhuri: Ikiwa hukushiriki kumteka iweje wodini akwambie nirudishie simu yangu?


Msangi: Kwanza ifahamike mimi huyu Dk. Ulimboka na mwenzake Dk. Deo nimewafahamu siku nyingi sana. Kwa maana hiyo ni mtu anayenifahamu vizuri tu. Kuna upotoshaji wa makusudi umefanywa ambao mimi nadhani una msukumo wa kisiasa.


Alichosema Dk. Ulimboka nilipozungumza naye, ni kwamba simu moja ilidondoka, nyingine wale watu waliomteka wameichukua pamoja na wallet yake. Hivyo alikuwa ananitajia vitu vilivyopotea. Nilipomuuliza iwapo anakumbuka namba ya simu, aliniambia nikamuulize Dk. Deo. Sasa nashangaa mtu aliyepenyeza uongo huu kwamba alisema mimi ndiye niliyempora hivyo vitu… sielewi ni nani na ana malengo gani.


Jamhuri: Haya unayasema wewe, hivi unadhani jamii itakuamini kwa kauli hizi, haitaonekana unajitetea tu?


Msangi: Wakati anazungumza maneno haya, alikuwapo Profesa Museru ambaye ni Mkurugenzi wa MOI. Sina cha kuficha kamuulize tu, atakwambia alichosema Dk. Ulimboka. Yupo pia Dk. Deo, huyu ananifahamu na Dk. Ulimboka anasema walikuwa wote wakati anatekwa. Dk. Deo ananifahamu, akaulizwe iwapo mimi ndiye niliyemteka Dk. Ulimboka.


Jamhuri: Tuhuma hizi zilianza kusambaa mapema tu Ijumaa. Je, wewe hukuwa na hofu kwenda pale MOI kumhoji Dk. Ulimboka?


Msangi: Ndugu yangu, nchi hii ina askari wengi mno. Hivi mimi kwa akili ya kawaida naweza kushiriki kumteka Dk. Ulimboka kisha nikaenda wodini kumhoji? Hata katika akili ya kawaida ya binadamu hilo haliwezekani.


Jamhuri:
Hizi tuhuma zilizoelekezwa kwako ni nzito. Wewe ndiye uliyeteuliwa kuongoza Tume ya Uchunguzi wa tatizo hili. Je, unadhani uchunguzi utakaofanya utaaminiwa na wananchi ukitoa ripoti?


Msangi: Mimi ninachokuhakikishia sikushiriki kumteka na si kweli kwa kila hali. Mambo kama haya yanakatisha tamaa. Kama tunaanza kuzushiana uongo kwa kiwango hiki, nchi hii sijui inaelekea wapi! Kimsingi imenikatisha tamaa mno. Wapo wanaosema nijiuzulu katika Tume hii lakini mimi nasema wakubwa wangu wamenipa kazi hii na watakaloamua nitalipokea.


Hivi wewe gazeti lako likituhumiwa unaacha kuendelea kutafuta habari? Nitaendelea kufanya kazi hii kama nilivyoapa siku nilipohitimu mafunzo kwamba nitalitumikia taifa kwa uadilifu na uaminifu wa hali ya juu katika kiapo changu cha utii. Na hilo ndilo nitakaloendelea kufanya. Watu wanapenda kuharibiana maisha tu.
Profesa Museru asema alichokisikia


Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru, akizungumza na JAMHURI kuhusiana na sakata kwamba Dk. Ulimboka, alimweleza Kamanda Msangi arejeshe simu na wallet yake.


Jamhuri: Profesa nimezungumza na Kamanda Msangi juu ya tuhuma zinazomkabili kuwa aliambiwa na Dk. Ulimboka amrejeshee simu na wallet yake, na akakutaja wewe kuwa ulikuwapo wakati wa mazungumzo hayo. Wewe nini ulichokisikia kuhusiana na tuhuma hizi.


Profesa Museru:
Mimi ndiye niliyempeleka pale wodini. Ni bwana mzuri tu. Nilimu-introduce (nilimtambulisha), akaanza mahojiano. Mimi hilo sikulisikia kwamba ameambiwa arejeshe simu na wallet, hilo sikulisikia.


Jamhuri: Kuna habari kuwa Kamanda Msangi baada ya kuambiwa kauli hiyo alitoweka wodini bila kuaga akikwepa kipigo kama ilivyomtokea askari mwenzake siku mbili kabla. Je, unalizungumziaje hilo profesa?


Profesa Museru: Nini? Kwamba alikimbia? Jamani nchi hii inakwenda pabaya. Mimi nilimsindikiza hadi nje ya wodi akapanda gari lake na kurejea ofisini kwake, sasa hilo la kukimbia limetokea wapi? Jamani ehee, mimi niseme katika hali kama hii sintofahamu zipo nyingi. Ni vyema kuchuja taarifa tunazozipata.