Na Stephano Mango, Songea
WAKULIMA wa zao la tumbaku wa wilaya za Songea na Namtumbo mkoani Ruvuma wameulalamika uongozi wa chama kilele (APEX ) ya tumbaku na Chama Kikuu cha Ushirika cha Songea na Namtumbo ( SONAMCU) kwakuwaletea mbolea ambayo iko chini ya kiwango na kuwasababishia hasara kubwa wakulima wa zao hilo.
Wakizunguza na wandishi wa habari mjini Songea wakulima zaidi ya 20 ambao waliongozwa na Salum Brashi ambaye ni Mkulima toka Chama cha Ushirika cha Msingi cha Mnazini kilichapo Wilayani Namtumbo walisema kuwa katika kipindi cha mwaka 2009/2010 na 2010/2011 wakulima wa zao hilo walipata hasara kubwa baada ya kutumia mbolea hiyo na kusabisha kuzalisha tumbaku isiyo kuwa na ubora.
Wakulima hao walieleza zaidi kuwa hali hiyo ya kutumia mbolea ambayo ipo chini ya kiwango jambo ambalo wamekuwa wakitumia nguvu kubwa isiyo kuwa na tija katika uzalisha wa zao hilo na kuwafanya hali zao kuwa duni kimaisha na kuendelea kuwadhofisha kiuchumi .
Walifafanua kuwa mfano kwa kawaida mbolea aina ya NPK 20.10.10 ambayo ndio inayofaa kwa zao la tumbaku wao badala yake walileta mbolea aina ya NPK 1.2.10.10 na msimu wa 2010/2011 ililetwa mbolea aina 6.10.10 badala ya mbolea iliyozoeleka ya NPK 20.10.10.
Walisema kwakuwa mbolea hiyo iliyoletwa haikuwa na nitrogen 20 ndio maana tumbaku hiyo ilikosa nikotin (sumu) hivyo wameiomba Serikali kuchua hatua za haraka za kuwasiliana na Uongozi wa chama kilele (APEX) ya tumbaku na Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya ya Songea na Namtumbo (SONAMCU) kuhakisha kuwa wanaleta mbolea inayofaa kwa zao hilo.
Aidha wakulima hao wameiomba Serikali ione umuhimu wa kuzuia mbolea ambayo kwa hivi sasa imeifadhiwa kwenye maghala ikisubili kusambazwa kwa wakulima wa zao la tumbaku wakihofia kuwa mbolea hiyo haina sifa kama iliyo letwa kwa misimu miwili ya kilimo iliyopita na badala yake ichukuliwe sampuli kwenda kupima kwenye maabara ya mkemia mkuu ,TBS na maabara nyingine zilipo hapa nchini ambazo zitaweza kubaini ukweli huo.
Kwa upande wake Meneja shughuli wa Chama Kilele (APEX) ya tumbaku yenye makao makuu mkoani Morogoro Samuel Jokeya akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Songea alisema kuwa wakulima wa tumbaku wa Wilaya ya Songea na Namtumbo wamekuwa na malalamiko kuwa Vyama APEX na SONAMCU vimekuwa wakileta mbolea kwa wakulima ambayo iko chini ya kiwango jambo hilo ambalo alidai siyo la kweli.
Jokeya alisema kuwa malalamiko ya wakulima wa zao la tumbaku kuwa haifai kwa matumizi ni gumu na halina udhibitisho kwani wakulima inawezekana hawazingatii kanuni bora za wataalum wa zao hilo na matumizi ya za duni za kilimo.na kwamba utatuzi wa jambo hili unafanyika huku akiwa ameshauri maabara zilizopo kupima vipimo vyote wanavyo pelekewa badala ya vichache nakuomba kupewa cheti kinachothibitisha ubora wa mbolea inayoletwa.
Alifafanua kuwa chama chake kinaleta mbolea kutokana na mahitaji yanayotolewa na Vyama vya Ushirika vya msingi na amedai kwamba endapo wanaona mbolea inayoletwa haiwafai SONAMCU inalo jukumu la kusitisha mahitaji ya wakulima na wakaagiza mbolea ambayo wanaona inawafaa kwa ajili ya zao hilo.
Alisema mpaka sasa tayari mbolea kwa ajili ya tumbaku ya mvuke (VFC ) imeletwa mifuko 7735, mbolea aina ya CAN imeletwa mifuko 1878 , UREA mifuko 16394 na mbolea ya moshi mifuko 2323 .
Naye mbunge wa Jimbo la Namtumbo Vita Kawawa alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusiana na malalamiko alikili kupokea kero hiyo kutoka kwa wapiga kura wake na ameeleza kuwa kila Chama cha Ushirika cha msingi kina wajibu wa kutafuta pembejeo na siyo kutegemea toka kwenye Vyama vikuu ambayo vimeoneka kuwa vinaleta mbolea ambayo haifai kwa matumizi ya kilimo cha tumbaku.
Kawawa ambaye pia ni Mwenekiti wa Bodi ya tumbaku nchini alieleza kuwa kama malalamiko yanaendelea kuwepo zaidi ya mbolea hiyo ni vyema Chama Kilele APEX ya tumbaku na SONAMCU wakatafuta njia mbadala ya kumaliza utata uliopo kati yao na wakulima wa zao hilo.
Hata hivyo jitihada za kuwapata Maafisa Kilimo wa Wilaya ya Namtumbo na Songea kutolea ufafanuzi juu ya tatizo hilo ziligonga mwamba baada ya kutopatikana kwenye simu zao za mikononi.
Mwisho.