About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Tuesday, October 4, 2011

TAKUKURU WAMNASA AFISA MTENDAJI WA KATA WA HALMASHAURI YA MANISPAA YA SONGEA KWA RUSHWA KIDUCHU

Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Shule ya Tanga Expedito Luambano(aliyesimama)
Na Mwandishi Wetu ,Songea
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoani Ruvuma inamshikilia Kaimu Afisa Mtendaji wa Kata ya Shule ya Tanga iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 20,000 kutoka kwa mwananchi ambaye jina lake limehifadhiwa wa Kata hiyo ambaye alikwenda Ofisini kwake kuomba asaidiwe kulipwa deni toka kwa Mfanyabiashara mmoja ambaye naye jina lake limehifadhiwa.
Akizungumza na mtandao huu wa www.stephanomango.com Ofisini kwake Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoani Ruvuma Daudi Masiko amesema tukio hilo limetokea Octoba 2 mwaka huu majira ya saa za mchana huko kwenye eneo la nane nane Msamala Songea Mjini.
Masiko amemtaja anayeshikiliwa na Takukuru kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya shilingi elfu 20,000 Expedito Luambano (36) ambaye ni Kaimu Afisa Mtendaji wa Shule ya Tanga ambapo amebainisha zaidi kuwa siku chache zilizopita Luambano akiwa Ofisini kwake alifikiwa na mwananchi mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa ambaye alikuwa anataka asaidiwe na Ofisi hiyo ili Mfanyabiashara anayemdai aweze kumlipa deni ambalo ni la muda mrefu.
Amefafanua zaidi kuwa mwananchi huyo akiwa kwenye Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata hiyo alishawishiwa na Luambano kuwa atafute shilingi elfu 20,000 ili aweze kumsaidia kumsaka Mfanyabiashara huyo anayemdai aweze kulipwa deni .
Ameeleza kuwa mwananchi huyo alikubaliana na maelezo aliyopewa na Luambano kisha alitoka kwenye Ofisi hiyo kwa makubaliano kuwa wangekutana kwenye eneo la nane nane lililopo Msamala kwenye bar iliyopo kwenye eneo hilo.
Amesema kuwa mwananchi huyo baadae alishtuka na kupata wazo kwenda kwenye Ofisi za Takukuru ambako alitoa taarifa na kuwaeleza kwa kina juu ya maelezo aliyopewa na Afisa Mtendaji Luambano ambapo baadae Maafisa wa Takukuru waliweka mtego kisha walimtaka mwananchi huyo awasiliane na Afisa Mtendaji mahali watakapokutana kupeana fedha hizo.
Mkuu wa Takukuru Mkoani Ruvuma Masiko amesema kuwa baada ya mwananchi huyo kufanya mawasiliano na Afisa Mtendaji  Luambano Takukuru ilimpatia fedha shilingi elfu 20,000 na kumtaka ande mahali walipokubaliana kupeana fedha hizo huku maafisa wa Takukuru wakiwa wanamfuatilia kwa karibu na walipofika kwenye eneo la tukio alimkuta Luambano akiwa anamsubiri kwenye bar ambako alimkabidhi fedha hiyo na baada ya muda mfupi maafisa wa Takukuru waliizingira bar hiyo na kumkuta Luambano akiwa na fedha shilingi elfu 20,000 aliyopewa na mwananchi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa.
Amefafanua zaidi kuwa Luambano ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Serikali wa Mtaa wa Tanga anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kwa tuhuma za  kuomba na kupokea rushwa ya shilingi elfu 20,000 ambayo ni kosa chini ya kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007
MWISHO

MAJAMBAZI WAPORA,WAJERUHI ABIRIA NA KUSABABISHA KIFO CHA MTOTO

Na Mwandishi Wetu,Songea.
JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linawasaka majambazi wawili ambao walivamia gari lililokuwa limebeba abiria 14 kutoka Mbamba bay kwenda Mbinga na kufyatua  risasi tano ambazo ziliwajeruhi watu wawili akiwemo mtoto wa umri wa mwaka mmoja na nusu  ambaye alikuwa amepigwa risasi kwenye mguu wa kushoto akiwa amebebwa na mama yake mzazi kisha majambazi hao walifanikiwa kuwapora abiria fedha Shilingi 930,000 na baadaye walikimbia na kutokomea kusikojulikana.
Akizungumza na mtandao huu wa www.stephanomango.blogspot.com  Ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amesema kuwa tukio hilo lilitokea Octoba 3 mwaka huu majira ya saa 1.30 asubuhi  huko katika Kijiji cha Ng’ombo kilichopo katika Kata ya Kilosa Wilaya ya Nyasa .
Kamuhanda amesema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio Dereva wa gari lenye namba za usajili T 554 ASE Toyota Hilux Joseph Hamza (35) akiwa  anaendesha  gari  hilo lililokuwa na abiria 14 waliokuwa wanatoka Mbamba bay kuelekea Mbinga Mjini akiwa katikati ya daraja ghafla aliwaona watu wawili wakiwa wamefunga vitambaa usoni huku wakiwa na Bunduki mbili ambao walilivamia gari hilo kisha walianza kufyatua risasi hewani ambazo ziliwajeruhi abiria wawili .
Amefafanua kuwa watu hao wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi ambao walikuwa na siraha za SMG na SAR  waliwapiga risasi Rehema Haule (11) ambaye alijeruhiwa  vibaya kwenye mguu wa kushoto wakati akiwa amebebwa na mama yake mzazi na Castory Kinunda (31) Mkazi wa Mbamba bay alijeruhiwa vibaya kwa kupigwa risasi na majambazi hao kwenye mkono wa kushoto .
Amebainisha zaidi kuwa  majambazi hao baada ya kufyatua risasi hewani walianza kuwapekua abiria mmoja hadi mwingine ambapo baadae walifanikiwa kuwapora abiria hao shilingi 930,000 na baada ya kuwanyang’anya fedha hizo walikimbia na kutokomea porini .
Alieleza zaidi kuwa majeruhi Rehema baada ya kupigwa  risasi kwenye mguu wa kushoto alikimbizwa katika Hospitali ya Misheni ya Liuli ambako alifariki dunia muda mfupi wakati akiendelea kupata matibabu na majeruhi  Kinunda  kwasasa hivi amelazwa katika hospitali ya Serikali ya Mbinga akiendelea kupata matibabu na hali yake bado ni mbaya.
Kamanda Kamuhanda amesema kuwa Polisi baada ya kupata taarifa ya tukio hilo walienda kwenye eneo la tukio na kuwakuta baadhi ya  abiria ambao walielezea tukio hilo lilivyotokea na kwamba upelelezi wa awali umefanyika ambao umebaini kuwa majambazi hao wametokea Kyela Mkoani Mbeya kwa kupitia Ziwa Nyasa.
MWISHO

VIONGOZI WA DINI WAOMBWA KUWANUSURU WANAFUNZI WA MTONYA NA MAPEPO

Na Augustino Chindiye,Tunduru

SHULE ya Msingi Mtonya Wilayani Tunduru imefungwa kwa muda usiojulikana ili kuwapisha Wazee wa mila,Mapadre na  Mashehe ili wawasaidie kuomba na kuyaondoa Mapepo ambayo yamekuwa yakisababisha Wanafunzi wanaosoma katika Shule hiyo kupatwa na homa ya kuchanganyikiwa na kuanguka wakati wa masomo.

Amri ya kufungwa kwa Shule hiyo imetolewa na Afisa elimu wa Shule za Msingi Mwl. Rashid Mandoa baada ya juhudi za maafisa tabibu kutoka katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru kushindwa kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.

Mwl. Mandoa aliendelea kufafanua kuwa tatizo la kuanguka na kupoteza fahamu kwa wanafunzi hao limekuwa likiongezeka siku hadi siku ambapo awali idadi ya watoto waliokuwa wakianguka walikuwa ni kati na watoto mmoja na watano lakini hivi sasa tatizo hilo limefikia zaidi ya watoto hamsini kwa siku.

Alisema kufuatia hali hiyo wazazi wa watoto wanaosoma katika shule hiyo walikuwa wakilazimika kufuatana na watoto wao na kupiga kambi pembezoni mwa shule wakiwa na lengo la kuwasaida watoto watakao kumbwa na homa hiyo.

Alisema ingawa Serikali haiamini mambo ya ushirikina lakini idara yake imechukua maamuzi hayo baada ya kubaini kuongezeka kwa matukio hayo na kwamba endepo tatizo hilo litaachiliwa liendelee kuna
hatari ya kushusha kwa taaluma za wanafunzi kutakakosababishwa na kushuka kwa ari ya wanafunzi kutopenda masomo.
Mwisho.

BUNGE LATAKIWA KUHAKIKISHA SUALA LA PENSHENI KWA WAZEE LINAINGIZWA KWENYE BAJETI YA TAIFA

  Mzee huyu ni miongoni mwa watu wanaotakiwa kupewa matibabu bure na pensheni nchini ili aweze kujikimu na maisha yake

Na Augusino Chindiye, Tunduru
BUNGE la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania limeahidi kusimamia na kuhakikisha kuwa mpango wa kuanza kuwalipa pensheni  wazee hapa nchini unaingizwa katika Bajeti ya Bunge lijalo na kuanza kulipwa mapema 2012.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru  Juma Madaha akiwa ananukuu Hotuba iliyokuwa imeandaliwa na Mwenyekiti wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania  Jenista Mhagama ambaye alitakiwa kuwa mgeni Rasmi katika maadhimisho ya siku ya Wazee Duniani iliyofanyika katika viwanja vya Baraza la Iddi Mjini Tunduru.

Akifafanua taarifa hiyo Dc,Madaha alisema kuwa Mhagama kwa kushirikiana na Wabunge wenzake wakiwemo wabunge kutoka Mkoa wa Ruvuma ameahidi kutoa msukumo mkubwa na kuhakikisha kuwa mswada wa kuanza kuwalipa Pensheni unatungiwa sheria mapema iwezekanavyo ili wazee wa Tanzania waanze kunufaika na mafao hayo.

Hotuba hiyo iliendelea kueleza kuwa wakati Wabunge hao wakishughulikia tatizo hilo tayari Serikali imeanza kuweka msukumo wa kuendelea kuwahudumia Wazee kote nchini waanze kupata huduma za Matibabu bure kupitia mkakati wa kuwaagiza Waganga wakuu wa Hospitali zote nchini kutenga vyumba maalumu vya kutolea huduma hiyo kwa wazee zikiwa ni juhudi za kuwaondolea kero na foleni.

Alisema Sambamba na kuwepo kwa zoezi hilo pia Hotuba hiyo ilieleza kuwa tayari Serikali pia kupitia Wakuu wa Wilaya kote nchini wamewaagiza watenzaji wa Vijiji kutekeleza agizo la kuwaandikia Wazee barua zitakazo wafanya watambuliwe na kuanza kupatiwa huduma za matibabu bure kuanzia ngazi za Zahanati,Vituo vya afya na Hospitali.

Awali akisoma Risala ya Wazee katika madhimisho hayo Katibu wa Chama cha Wazee wa Wilaya ya Tunduru (HAWATU) Jafari Msonjele alisema kuwa pamoja na kundi hilo kukabiliwa na changamoto nyingi za kimaisha Wazee wengi kote nchini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kulea kundi kubwa la Watoto yatima ambao wengi wao wameachwa na ndugu,jamaa na Watoto wao waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Wazee hao pia katika taarifa yao wakagusia changamoto kubwa ya kitaifa inayo wakabiri wazee wenzao wastaafu ambao wamekuwa wakiyumbishwa kwa muda mrefu kulipwa pensheni zao na mashirika ya PPF,PSPF, na LPF na wakatumia nafasi hiyo kuyaomba mashirika hayo kuridhia maombi ya wanachama wake ya kuanza kuwalipa wanachama wake malipo ya mwezi mmoja, Mitatu na Sita bila kupitisha muda wake pamoja na kuangalia uwezekano wa kama kuna nyongeza basi iongezwe kwa wanachama wote  ili kuwapunguzia makali ya maisha.

Nae Mwenyekiti wa Chama hicho Said Kabora akitoa neno la shukurani wakati wa kufunga maadhimisho hayo pamoja na kulipongeza Bunge kwa kauli hiyo alisema kuwa Wazee bado wanayo imani na serikali yao na wana amini kuwa macho hayo yaliyo ahidiwa kwa vipofu na chombo kinacho wawakilisha katika utoaji wa maamuzi yatatekelezeka na kuwafanya wazee kote nchini kufurahia matunda ya nchi yao. 
  Mwisho