About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Monday, January 27, 2014

WAFANYABIASHARA MANZESE WAUCHARUKIA UONGOZI WAO



Na, Stephano Mango, Songea
WAFANYABIASHARA  wa Soko la Manzese B lililopo katika halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wameutaka Uongozi wao ujiudhuru mara moja kutokana na utawala mbovu wanaoufanya na kuendeleza vitendo vya hujuma katika soko hilo

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa Habari jana katika viwanja vya soko hilo walisema viongozi hao wamekuwa wakishirikiana na Viongozi wa Halmashauri ya Manispaa kukiuka maadili ya uongozi na kusababisha migogoro ya mara kwa mara inayopelekea uvunjifu wa amani

Walisema kuwa toka kuwepo kwa mpango wa ujenzi wa vibanda 68 vya Soko hilo, viongozi wamekuwa wakifanya vikao vya siri vya kuwahujumu wafanyabiashara waliopo sokoni hapo kwa kupanga mipango ya kuwanyang’anya ili vibanda hivyo wapewe wafanyabiashara  vigogo ambao hawafanyi biashara katika soko hilo

Walisema kuwa mipango hiyo ya siri imezua malalamiko makubwa sana miongoni mwa wafanyabiashara kwani makubaliano ya awali yalikuwa ni lazima wafanyabiashara waliopo wapewe kipaumbele katika ujazaji wa mikataba katika ujenzi huo

“ Tunashangaa kuona viongozi wa Soko na Viongozi wa Halmashauri wanatoa mikataba kwa siri kwa wafanyabiashara vigogo kutoka maeneo mengine kinyume na utaratibu kitendo ambacho kimetusikitisha sana kwani hakijawa na uhalali wa kidemokrasia zaidi ya ubabe”

Walisema hali hiyo inaonyesha wazi kabisa kuwa kuna vitendo vya rushwa, ukiukwaji wa haki za binadamu kwani mara kwa mara wafanyabiasha wakihoji uhal wa mambo ambayo yanafanywa na viongozi hao wanatishiwa kwa maneno ya kuudhi

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mwenyekiti wa Soko hilo Omary Masai alisema kuwa yeye sio msemaji wa jambo hilo kwani linafanywa Mstahiki Meya wa Halmashauri Charles Mhagama hivyo kwa maelezo zaidi atafutwe yeye

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Misufini ambako soko hilo lipo Salumu Mfamaji alisema kuwa ujenzi huo unafanywa kihuni kwani kuanzia viongozi wa Serikali ya Mtaa na Serikali ya Kata haijashirikishwa na kuwa jambo hilo linaonekana limegubikwa na rushwa

Mfamaji alisema kuwa amewasiliana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria na wataalamu wake kusitisha mara moja ujenzi huo mpaka pale mkutano wa wafanyabiashara utakapoitishwa ili waweze kutendewa haki ikiwemo ya kuonyeshwa ramani ya Soko hilo na mikataba

Naye Meya wa Manispaa hiyo Charles Mhagama alipohojiwa kuhusiana na malalamiko ya Wafanyabiashara alisema kuwa tatizo hilo lipo lakini alidai kuwa msababishaji mkubwa ni Diwani wa kata hiyo na ndio maana Halmashauri imeamua kusimamia yenyewe ujenzi huo

Hata hivyo juhudi za kumtafuta Mkurugenzi wa Halmashauri kupitia simu yake ya kiganzani Nachoa Zakaria ziligonga mwamba kwani simu yake ilikuwa inaita tu bila kupokelewa

MWISHO