NA AUGUSTINO CHINDIYE,SONGEA
WATU wasiojulikana wamevunja nyumba na kuiba mali mbalimbali zenye thamani ya Sh laki 9.5 kwenye nyumba inayomilikiwa na Dainess Mgumba (17) mkazi wa eneo la Mahenge B katika halmashauri ya manispaa ya Songea mkoani Ruvuma .
Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma Michael Kamhanda alisema kuwa tukio hilo lilitokea aprili 3 mwaka huu majira ya saa 8 mchana huko katika eneo la Mahenge ambako Dainess ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha 3 katika shule ya sekondari ya kutwa ya Msamala aligundua kuvunjiwa nyumba yake na kuibiwa mali mbalimbali zilizokuwemo ndani .
Kamanda Kamhanda alizitaja mali zilizoibiwa kuwa ni keyboard ,DVD deck,Radio aina ya Aiwa,simu moja ya mkononi aina ya sumsung na receiver aina ya media com vyote vikiwa na thamani ya Sh laki 9.5 na alidai kuwa watuhumiwa bado hawajakamatwa na upelelezi wa tukio hilo unaendelea kufanywa ili kuwabaini wale wote waliohusika katika kutenda kosa hilo .
Alieleza zaidi kuwa kutokana na polisi kwa kushirikiana na sungusungu kuweka ulinzi mkali nyakati za usiku kwa hivi sasa waharifu wamebadilisha mbinu za utendaji wa makosa hivyo kwa sasa wamekuwa wakifanya uharifu huo nyakati za mchana ambapo alitoa mfano wa tukio hilo kuwa lilitokea wakati Dainess akiwa shuleni na aliporudi alikuta nyumba yake imevunjwa kufuli na alipoingia ndani alikuta mali zake zimeibiwa .
Alisema kuwa kwa hivi sasa polisi inaendelea kuwasaka waharifu wa tukio hilo lakini amewataka wananchi mkoani Ruvuma waone umuhimu wa kufanya dhana ya ulinzi jirani ambao utaweza kudhibiti kwa kiasi kikubwa hali hiyo ya uharifu unaofanywa na watu wanaodaiwa kuwa ni vibaka nyakati za machana .
Amewashauri viongozi wa serikari za mitaa kwenye maeneo yao wawe na mikakati ya kuwa na dhana ya ulinzi jirani ambayo itaweza kuwakimbiza waharifu ambao walikuwa wamezoea kuiba nyakati za usiku na hivi sasa wameamua kuiba mchana baada ya kugundua kuwa zoezi la ulinzi shirikishi linalofanywa na polisi kwa kushirikiana na wananchi nyakati za usiku zimepamba moto mkoani Ruvuma.
MWISHO