About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Sunday, August 28, 2011

WANANCHI WAMTAKA MKURUGENZI KUITISHA UCHAGUZI WA SERIKALI YA KIJIJI CHA MKILI

                                         Na Thomas Lipuka,Songea

WANANCHI wa Kijiji cha Mkili Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma wamemtaka Mkurugezi wa Halmashauri Wilaya ya Mbinga kusimamia zoezi la kupata uongozi wa kijiji hicho kwani  kijiji hicho kwa muda mrefu kina uongozi wa mda ambapo shughuli zote huendeshwa na Mtendaji wa kijiji, baada ya aliyekuwa Mwenyeketi wa kijiji hicho   John Isdori Tilia kusimamishwa uongozi na Serikali yake yote .

Tuhuma zilizopelekea Mwenyekiti huyo na serikali yake yote  kusimamishwa uongozi ni pamoja na kutoitisha mikutano ya serikali ya kijiji kutosoma mapato na matumizi ya kijiji kushindwa kusimamia miradi mbalimbali ya kijiji na wakati mwingine kujishughulisha zaidi na mambo ya starehe na kuacha yale yanayohusu maendeleo ya wanakijiji .

Wanakijiji  wa Mkili baadhi yao wametaja miradi ambayo ameshindwa kusimamia ni ujenzi wa kibanio cha mfereji wa maji kwa kilimo cha umwagiliaji ambacho kipo katika mto Ndumbi kijijini hapo ,ujenzi unaendelea wakituo cha afya kwa kujenga nyumba nne za waganga na ukarabati wa barabara itokayo bandari ya Mkili hadi Hospitari ya Litembo .

Wakitoa kero zao kupitia mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ baadhi ya wanakijiji hao walisema  toka serikali ya kijiji hicho ichaguliwe hawajasomewa taarifa ya mapato na matumizi ambapo shughuli zote huendeshwa na mwenyekiti aliyesimamishwa uongozi na mtendaji bila wanakijiji kuhusishwa.

Wameongeza kuwa kijiji hicho kina bonde la kutosha kwa fursa ya kilimo cha umwagiliaji  wa mpunga ambapo tayari Halmashauri ya Mbinga ilishatoa mradi wa umwagiliaji  katika kijiji hicho lakini kwa kukosa uongozi bora wa kijiji,kibanio kilisombwa na maji mara mbili jambo ambalo mkandalasi hakufuatiliwa namna alivyojenga  kibanio hicho  na ubora wake .

Wamesema kilimo hicho cha umwagiliaji katika bonde lililopo kijijini hapo kingeweza   kuwanasua  wanakijiji kwa kupata zao la mpunga mara mbili kwa mwaka hivyo wamemwomba mkurugezi wa Wilaya ya Mbinga kuharakisha zoezi la kuwapata viongozi wa serikali ya kijiji ili kuharakisha maendeleo yao.

Walipoulizwa kuhusu tatizo la sumu inayotiwa katika mito inayozunguka kijijini hapo hasa toka eneo milimani walisema vitendo  hivyo vya uharibifu vinatendwa na baadhi ya watu kutoka vijiji vya Mahande ,Siasa ,Lundumato,Mkoha,kwa uroho wa kutafuta Samaki ambapo madhara yake huua madhalia yote ya viumbe hai katika mito hiyo ambayo ni Ndumbi ,Mnyamaji,Chipindi,na Luhorochi.

Wanakijiji hao wamempongeza mkurugezi mtendaji wa Halmashauri wa Wilaya ya Mbinga kwa kuwatia moyo ili wafyatue matofari ya nyumba nne za waganga kwa ajili ya kuimarisha na kupanua kituo cha afya cha Mkili pia kwa ahadi ya kupatiwa gari la kusafirisha wagonjwa siku za usoni toka kituo cha afya Mkili hadi Hospitari za Lihili, Mbinga ,Litembo ,Songea na Peramiho.

Aidha wanakijiji hao wameiomba serikali kuwaimarishia mawasiliano ya simu kwa kuwajengea minara ya Voda,Airtel,Tigo na TTCL,mawasiliano ambayo wanayapata kwa shida kwa kupanda juu ya miti ama kwenye vichuguu.

AFYA ZA WAFANYABIASHARA SOKO KUU SONGEA ZIPO HATARINI KWA KUKUBWA NA MAGONJWA YA MLIPUKO


                                           Na Gideon Mwakanosya,Songea.
WAFANYABIASHARA katika Soko kuu katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma wapo katika hatari kubwa ya kukumbwa na magonjwa ya milipuko kikiwemo Kipindupindu kutokana na miundo mbinu ya maji taka yanayo simamiwa na mamlaka ya Maji safi na Maji taka Songea (SOUWASA) kuwa mibovu pamoja na wauzaji wa  nyama ya ng’ombe kwenye mabucha kutiririsha maji machafu wanayosafishia utumbo wa ng’ombe hadi maeneo wanayouzia nyanya,vitunguu na mbogamboga wafanyabiashara wadogo.
Mwandishi wa mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ jana alifanya mazungumzo na baadhi ya wafanyabiashara sokoni hapo ambapo walieleza kuwa miundo mbinu ya maji taka imekuwa ikipasuka na kutiririsha maji kwenye maeneo wanayouzia bidhaa zao na kusababisha adha kubwa kwa wafanyabiashara hao ambao wamekuwa wakilazimika kufanya kazi katika mazingira magumu.
Walisema katika hali ya kushangaza  soko hilo lina maafisa afya ambao wamekuwa wakifanya kazi kila siku kwenye eneo hilo ambalo lina mazingira machafu lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
Issa Hussen ambaye ni mfanya biashara katika soko hilo alieleza kuwa wafanyabiashara wa mbogamboga ambao wamekuwa wakitandika magunia chini kisha kuweka bidhaa zao kama nyanya, vitunguu wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu kwani kwenye maeneo wanayofanyia biashara hiyo maji yanayotiririshwa toka kwenye ma bucha ya nyama za ng’ombe wanayooshea utumbo wa ng’ombe pamoja na maji taka ambayo yanayo tiririka toka kwenye mtandao wa Souwasa yamekuwa yakipita kwenye eneo hilo wanayofanyia biashara na kuwaletea adha kubwa kwani wanunuzi wamekuwa wakikataa kununua bidhaa zao kutokana na maji machafu kuwa jirani na biashara zao.
 Kwa upande wake Afisa masoko wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Salum Homera alipoulizwa na mtandao huu kuhusiana na malalamiko ya wafanyabiashara kuhusiana na kukithiri kwa uchafu kwenye soko kuu ambalo limekuwa likitiririsha maji machafu kwenye ambayo yamekuwa yakipita jirani kabisa na maeneo ya biashara zao alikiri kuwepo kwa tatizo hilo lakini alisema kuwa tatizo hilo lipo juu ya uwezo wake.
Homera alisema kuwa Ofisi yake ilisha toa taarifa kwa idara ya Afya na kwamba maafisa afya ndiyo walitakiwa kuona umuhimu wa kudhibiti hali hiyo iliyojitokeza sokoni na kwamba mamlaka ya maji safi na maji taka songea (SOUWASA) nao walishapewa taarifa na waliahidi kufika kufanyia matengenezo mtandao wa maji taka.
 Kwa upande wake Afisa afya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Mahundi alipohojiwa na nipashe kuhusiana na kukithiri kwa uchafu katika soko hilo, alieleza kuwa tatizo hilo Ofisi yake ilikuwa bado haijalipata lakini Afisa masoko ndiye alitakiwa kutoa taaarifa ki maandishi kwenye ofisi ya idara ya afya ili tatizo hilo liweze kufanyiwa kazi kirahisi kwani yeye ndiye msimamizi mkuu wa masoko yote ya halamashauri.
 Jitihada za mtandao huu za kumpata Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na maji taka (SOUWASA) Fransis Kapongo ziligonga mwamba baada ya kumpigia simu yake ya mkononi zaidi ya mara tatu bila kupatikana na nipashe ilifanya jitihada zaidi ya kuwasiliana na kaimu katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Dr.Anselmo Tarimo na kumuuliza juu ya uchafu uliokithiri sokoni Songea amabye alikiri na kudai kuwa tatizo hilo linalazimika kufanyiwa utaratibu wa haraka ili kulimaliza kuanzia mwanzoni mwa wiki hii ambapo wataalamu wote wa afya watalazimishwa wawepo kwenye soko hilo ili waone ni jins gani wataweka mazingira mazuri sokoni hapo ambayo yatawafanya wafanyabiashar wasikumbwe na magonjwa ya milipuko.

MWEKEZAJI ADAIWA KUPORA ARDHI YA EKARI 5000 KWA WANAKIJIJI LIPOKERA

            Wananchi wa kijiji cha Lipokera wakiwaonyesha waandishi wa Habari ardhi yao ambayo wanadai wameporwa na mwekezaji
 Wananchi wakionyesha mahindi yao baada ya kuvuna haraka haraka kwa kumuogopa mwekezaji asije akawanyang'anya
Na Thomas Lipuka,Songea.
WAKAZI wa kijiji cha Lipokela wilayani Songea mkoani Ruvuma wanamuomba Waziri wa ardhi,nyumba na Maendeleo ya Makazi  Profesa Anna Tibaijuka kuwasaidia kuirejea ardhi yao yenye ukubwa wa zaidi ya hekari 5000  iliyochukuliwa kinyemela na mwekezaji.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika kijiji hicho baadhi ya wananchi walidai kuwa  mwekezaji mwenye asili ya Asia anayefahamika kwa jina moja la Merali  tangu mwaka 1985 alipewa ardhi kinyemela bila baraka za wananchi na kusababisha ardhi hiyo kuingia kwenye mgogoro mkubwa.
Wananchi  wamedai kuwa mwekezaji huyo alipewa  ardhi hiyo katika mazingira ya kifisadi kupitia aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji hicho  Joseph Komba pamoja na aliyekuwa katibu wake Gervas Mbonde .
Hata hivyo walisema mwekezaji huyo alipewa ardhi  kwa maamuzi ya wananchi yenye ukubwa wa hekari 1000 mwaka 1984 na kwamba mwaka 1985 aliomba tena ardhi hekari zaidi ya 5000 ambazo alipewa bila baraka za wananchi na kuleta mgogoro ambao unaendelea hadi sasa.
``Kuanzia mwaka 1985 wananchi wa kijiji cha Lipokela hawakujua kama ardhi yao ya hekari 5000 amepewa mwekezaji hadi mwaka jana  takriban miaka 25 ndipo ilipofahamika na kusababisha wananchi zaidi ya 250 wanaolima mashamba pamoja na makazi kwenye  eneo hilo  kuambiwa kuwa eneo hilo ni mali ya mwekezaji wa kiasia’’,walidai wananchi hao.
Akizungumza kwa niaba ya wenzao Mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho Faustine Komba alibainisha  kuwa ardhi hiyo yenye  mgogoro ilianza kutumika na wananchi kuanzia mwaka 1993 ambao walipimiwa kihalali na uongozi wa kijiji na kuendelea kuitumia mwaka hadi mwaka bila kutambua kuwa amepewa mwekezaji kinyemela.
Komba alisema mwekezaji alipewa kisheria hekari 1000 tu upande wa kulia mwa barabara ya Songea - Mbinga na kwamba eneo lenye hekari zaidi ya 5000 upande wa kushoto ambazo mwekezaji huyo anadai kupewa kinyemera sio zake kwa kuwa ni mali ya wananchi ambazo walipewa kihalali na serikali ya kijiji.
Uchunguzi ambao umefanywa na wanakijiji wanadai wamebaini kuwa mwekezaji huyo kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa kijiji hivi sasa amekuwa dalali wa kuwauzia ardhi wawekezaji wengine kutoka nchini Afrika kusini na Marekani hivyo wameiomba serikali na hasa waziri wa ardhi kuingilia kati mgogoro huyo.
Wananchi hao wakiwemo  Gofrey Lupindu,Agustino Komba,Filbert Kinunda, Vestina Hyera, Bomba Nchimbi wakizungumza kwa uchungu mkubwa ,walidai kuwa hivi sasa pia hawana imani na mwenyekiti wa kijiji aliyopo madarakani John Nchimbi ambaye anadaiwa kumsaidia mwekezaji badala ya kuwasaidia wananchi waliomweka madarakani.
Uchunguzi umebaini kuwa iwapo serikali haitachukua hatua za makusudi katika kutatua mgogoro huo wa ardhi kuna hatari ya kutokea machafuko makubwa kutokana na ukweli kuwa  wananchi wa kijiji hicho  wamedai hawapo tayari kuona mwekezaji anapora ardhi yao  kinyemela na kusababisha wananchi kuwa wakimbizi katika ardhi yao.
Uchunguzi mwingine ambao umefanywa katika kijiji hicho umebaini kuwa  mwekezaji huyo ambaye alipewa hekari 1000 na wananchi  katika kipindi  cha miaka mitatu alifanikiwa kulima hekari 15 tu na kitendo cha kutaka kuchukua hekari nyingine zaidi ya 4000 kinawapa mashaka kuwa kijiji hicho kipo katika hatari ya kuuzwa kwa kisingizio cha uwekezaji.
Afisa ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Japhet Mungashwa amekiri kwamba  mwekezaji huyo amemilikishwa eneo la hekari 5000 kihalali kwa kipindi cha miaka 99 kwa sheria ya ardhi ya mwaka 1923 ambayo inawaruhusu wajumbe wa kijiji kupitisha maamuzi bila kushirikisha maamuzi ya wananchi wote kama ilivyo katika sheria mpya ya ardhi ya mwaka 1999.
 Wananchi hao wametoa mwito kwa serikali ya wilaya ya Songea,mkoa wa Ruvuma pamoja na Waziri  wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi kufika katika kijiji hicho  ili kujionea hali halisi ya ardhi ya mashamba na makazi ambayo wameporwa  na mwekezaji.
Sheria ya ardhi ya vijiji  namba tano kifungu cha tano ya mwaka 1999 inasema kuwa Halmashauri ya kijiji haitagawa ardhi au kutoa hakimiliki ya kimila bila ya kwanza kupata idhini ya mkutano  wa kijiji ambapo katika kifungu cha sita katika sheria hiyo kinaeleza  Halmashauri ya kijiji italazimika kutoa taarifa na kuzingatia maoni ya mkutano wa kijiji kuhusu uendeshaji na usimamizi wa ardhi ya kijiji.
Kwa mawasiliano andika lipukakomba@yahoo.com