RAIA 11 WA PAKISTANI NA BANGLADESHI KURUDISHWA MAKWAO
Na Stephano Mango ,Songea.
WATU kumi na moja ambao ni raia wa Pakstani na Bangladesh waliokuwa wamekamatwa katika kijiji cha Magwamila kilichopo wilayani Songea mkoani Ruvuma wakitokea Msumbiji ambako walifukuzwa na askari wa Nchi hiyo kwa kupigwa na mijeredi sehemu mbalimbali za miili yao na kujeruhiwa wanatarajiwa kurejeshwa kwenye Nchi zao kwa kupitia ofisi za balozi za Nchi hizo hapa nchini.
Afisa uhamiaji wa Mkoa wa Ruvuma Koku Rwebandiza akizungumza jana na mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ amesema kuwa raia hao wa Pakistan na Bangladesh kwa sasa hivi wanafanyiwa taratibu za kuwarejesha kwani walipokamatwa huko katika kijiji cha Magwamila walikutwa wakiwa na hati za kusafiria ambazo zilionekana kuwa na utata.
Rwebandiza alisema kuwa hati hizo za kusafiria ambazo walikutwa nazo watu hao ambao ni Raia wa Bangladesh na Pakstan hazioneshi ni lini waliingia Tanzania wakati wakitokea kwenye Nchi zao wala hazionyeshi ni lini waliondoka hapa Nchini na kuelekea Msumbiji ambako walikamatwa wakiwa katika eneo la Lichinga na askari wa Nchi ya Msumbiji.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo idara ya uhamiaji mkoani Ruvuma imelazimika kuwarejesha raia hao kwenye balozi za Nchi zao ambazo ndizo zitakazoangalia ni namna gani zitawarudisha kwenye nchi zao.
Rwebandiza alisema kuwa raia hao kumi na moja wa nchi za pakistan na Bangaladesh walikamatwa mwanzoni mwa wiki huko katika kijiji cha magwamila kilichopo mpakani mwa Tanzania na Msumbiji ambapo inadaiwa walifukuzwa toka msumbiji kwa kupigwa mijeredi sehemu mbalimbali za miili yao na kunyang'anywa mali zao zote walizokuwa nazo pamoja na fedha na askari wa nchi ya Msumbiji kisha waliletwa hadi mpakani na kufukuziwa kijijini hapo huku wakiwa na majeraha.
Hata hivyo afisa uhamiaji Rwebandiza alisema kuwa raia hao baada ya kuwahoji walieleza kuwa wao walitoka Pakstan kwa pamoja kwa usafiri wa Ndege hadi Tanzania kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa jijini Dar es salaamu na baadae walitafuta usafiri wa basi hadi Mtwara ambako nako walifanikiwa kupata usafiri wa malori hadi wakafanikiwa kuvuka msumbiji ambako walinaswa na askari wa Nchi hiyo.
Raia hao ambao walikamatwa ni wapakistan watano ambao ni Hassan Bilali (20), Fawad Yassin (20), Mohamed Hawadhi(20),Haftari Hussein (24) na Hassad Hawadh (45) na raia toka Bangladesh waliokamatwa ni sita ambao ni Shahed Alzani (29) ,Amar Hamad (25),Garuan Khalifa(40),Mohamed Parvaz(35) ,Shajar Meya (28) na Sao Meya (28) .
MWISHO.