WAKATI watuhumiwa wanne zaidi wakiongezwa katika kesi ya mauaji
ya mfanyabiashara wa madini ya tanzanite mkoani Arusha, Erasto Msuya,
waandishi wanaoiripoti jana walionja joto ya jiwe kwa kukwidwa na
kutaka kunyang’anywa vitendea kazi vyao.
Tafrani hiyo ilitokea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi
saa 5:30 wakati kesi hiyo inayowakabili washtakiwa saba wanaodaiwa
kushiriki kupanga na kutekeleza mauaji ya Msuya ilipofikishwa mbele ya
mahakama kwa ajili ya kutajwa.
Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa waandishi hao, Fadhili Athuman
alisema kuwa walipata wakati mgumu walipojaribu kuchukua picha za ndugu
wa Msuya.
Athuman alisema kuwa baada ya kupiga picha kadhaa, alikwidwa na
wanafamilia hao, wakitaka kumpora kamera huku mwandishi mwenzake
akishikwa na kupigwa kibao.
“Baada ya kesi kuahirishwa iliibuka tafrani, walitaka kuninyang’anya
kamera ili wafute picha nilizokuwa nimepiga. Mwenzangu yeye alikamatwa
na kupigwa vibao kabla askari wa kikosi cha FFU kumuokoa,” alisema.
Kwa mujibu wa mmoja wa watu wa karibu na familia ya Msuya ambaye
aliomba kuhifadhiwa jina, wamechukizwa na hatua ya baadhi ya waandishi
kutochapisha picha za watuhumiwa, na badala yake zinatolewa za
wanafamilia hiyo.
Hali ya taharuki ilianza mapema baada ya chumba kilichozoeleka
kuendeshea kesi hiyo kubadilishwa kwenda kwenye chemba kutokana umati
wa watu uliohudhuria kuwa mkubwa.
Wakati huo huo, vilio viliendelea kutawala mahakamani hapo baada ya
kesi hiyo kuahirishwa. Mama mzazi wa Msuya, Marry Msuya alipoteza
fahamu na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Awali mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Ruthi Mkisi, mawakili
wa serikali, Stella Majaliwa akisaidiwa na Janeth Sipule waliieleza
mahakama kuwa washitakiwa wanne wameunganishwa katika kesi hiyo na
kufikia saba.
Majaliwa aliwataja waliounganishwa kuwa ni mshitakiwa wa nne hadi
saba ambao ni Jalila Zuberi, Karimu Kihundrwa, Sadiki Jabiri (Chusa) na
Joseph Mwakipasile ambao wote walifika mahakamani hapo.
Hakimu Mkisi alisema kesi hiyo imeahirishwa kutokana na upelelezi
kutokamilika na hivyo kutaka washitakiwa hao kurudi rumande hadi Oktoba
2, mwaka huu.
Agosti 21, mwaka huu, washitakiwa watatu; Sharifu Mohammed, mkazi wa
Kimandolu Arusha, Shaibu Mpungi, mkazi wa Kijiji cha Songambele
wilayani Mererani na Musa Mangu mkazi wa Shangarai kwa Mrefu Arusha,
walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.
Washitakiwa wote saba waliondolewa mahakamani hapo chini ya ulinzi
mkali wa askari wenye silaha za moto wakiwa ndani ya gari lenye namba
za usajili T 743 ADC lenye vioo vyeusi.
Msuya aliuawa Agosti 7 mwaka huu saa 6:30 mchana kwa kupigwa risasi
13 kifuani, kando ya barabara kuu ya Arusha – Moshi katika eneo la
Mjohoroni wilayani Hai.
|