MKUU WA WILAYA YA MBINGA KANALI EDMUND MJENGWA
Na Stephano Mango, Songea
KUNDI la wananchi wenye hasira kali katika Mji mdogo wa Mbambabay wilaya mpya ya Nyasa Mkoani Ruvuma wamevamia baadhi ya ofisi za serikali na CCM pamoja na baadhi ya nyumba za makazi ya watu na kuharibu samani za ofisi na za watu kisha kuchoma nyaraka za Serikali na CCM zilizokuwa zimeifadhiwa kwenye majengo hayo yaliyo kuwa yamevamiwa
Baadhi ya watu walioshuhudia tukio hilo walieleza kuwa lilitokea baada ya uongozi wa Serikali kata ya Mbambabay kukataa kutoa kibali cha kumruhusu Mganga wa Jadi aliyetoka Jijini Tanga kwa lengo la kufanya kazi ya kuwafichua baadhi ya watu wanaojishughulisha na imani za ushirikina kwenye mji mdogo wa Mbambabay .
Watu hao ambao hawakutaka majina yao yatajwe gazetini walieleza kuwa Mganga huyo anaitwa Fakii Yahaya maarufu kwa jina la Jongo ambaye alikuwa amefika wilayani humo kuja kufanya kazi hiyo kwenye kijiji cha Ndengele ambako tayari alikuwa amesha fanya kazi ya kuwabaini watu wanaofanya shughuli za ushirikina na wananchi wa kijiji hiko walitangaza kuwakataa, hadharani wale wote waliobainika kuwa ni wachawi .
Walisema kuwa kufuatia hali hiyo baadhi ya wananchi wa mji mdogo wa Mbamba-bay walimwomba Mganga huyo ili aende akawasaidie kuwafichua watu wanaojihusisha na mambo ya ushirikina katika mji huo,jambo ambalo lilipingwa na uongozi wa Serikali ya kata ambayo inadaiwa kuwa ilikataa kutoa kibali cha kumhidhinisha Mganga huyo kufanya kazi Mbamba bay .
Walieleza kuwa baada ya Serikali kutokubali kumruhusu Mganga huyo kutofanya kazi ndipo wananchi wenye hasira kali walikusanyika na kuanza kuvamia baadhi ya majengo ya Serikali na ofisi ya CCM ya kata hiyo kisha waliaribu samani za ofisi na kuchoma moto nyaraka zote na baadaye walitawanyika.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mbinga Kanali Mstaafu Edmundi Mjengwa alipoulizwa na mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwepo uharibifu wa mali lakini alikataa kuelezea zaidi kwa madai alikuwa safarini vijijini kwa shughuli za kikazi .
Naye Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo ambalo alidai limetokea February 9 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi huko Mbamba -bay ambako kundi kubwa la watu wenye hasira kali lilivamia majengo mbalimbali ya Serikali zikiwemo ofisi ya Afisa Mfawidhi wa bandari ya Mbambabay ambako waling’oa madirisha matatu ya jengo hilo ,ofisi ya Afisa tarafa ya Ruhekei ambako walibomoa mlango na kisha kuchoma moto nyaraka zilizokuwa zimehifadhiwa ndani ya ofisi hiyo na baadaye walikwenda ofisi ya CCM nako walivunja mlango na kuzichoma moto nyaraka zilizomo .
Alifafanua kuwa baadhi ya samani zilizo haribiwa na kundi la wananchi wenye hasira kali ni pamoja na pikipiki aliyokuwa akiitumia Afisa Tarafa ,umemejua (sola) , Radio pamoja na mashine ya kupigia chapa ambazo ni mali ya bandari na ofisi ya Tarafa .
Kamanda Kamuhanda alisema kuwa chanzo cha vurugu hizo ni baada ya Mganga wa Jadi Yahaya (Jongo) kunyimwa kibali cha kuwafichua na kuwatambua watu wanaodaiwa kuwa ni wachawi kataka mji huo,hata hivyo mpaka sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiriwa kuhusiana na tukio hilo na polisi inaendelea kufanya upelelezi wa kina .
MWISHO