NA STEPHANO MANGO,SONGEA
UONGOZI wa klabu ya Majimaji ya Songea imetoa pongezi ya kumshukuru Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu kwa kazi kubwa ya kuiwezesha timu hiyo kubakia ligi ya Daraja la kwanza kwa ngazi ya Taifa msimu huu.
Akizumgumza mjini hapa ,Katibu Msaidizi wa Wanalizombe hao, Zakaria Ndumbaro alisema kuwa uongozi wa Majimaji umeweza kumwandikia barua ya kumpongeza pamoja na kumshukuru juu ya mchango wa kifedha , fikra na busara zake ambazo ndizo zilizoiwezesha timu hiyo kubakia kucheza tena ligi hiyo msimu ujao.
Alisema kama siyo mkuu wa mkoa kuipiga jeki timu hiyo basi kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kushuka daraja na kucheza ligi ya mkoa kitu ambacho kingekuwa fedheha kwa timu kama hiyo yenye historia ya soka hapa nchini.
Alisema katika kipindi chote cha ligi hiyo ya Daraja la kwanza kwa ngazi ya Taifa hatua ya makundi, licha ya kukabiliwa na tatizo la uongozi na kupelekea wanachama kuwaengua baadhi ya viongozi na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Mohamed Gayo kujihuzuru timu hiyo ilifikia hatua ya kuyumba na hata kutiliwa shaka kushiriki ligi hiyo.
Alisema kutokana na busara za mkuu huyo aliweza kuunganisha nguvu ya pamoja baina ya viongozi waliokuwepo madarakani, wanachama na wale walioenguliwa na kuwa kitu kimoja na kufanikiwa kucheza na kubakia katika hatua hiyo licha ya matatizo ambayo waliweza kukumbana nayo katika kipindi hicho cha ligi.
Alisema kutokana na matatizo yote hayo ambayo waliweza kukabiliana nayo, tayari uongozi wa timu hiyo umeanza kujipanga kuhakikisha na timu hiyo itaendeshwa kwa mtindo wa mfumo wa kibiashara na kuachana na mfumo wa sasa wa timu kuendeshwa na wanachama kwa kutegemea mifuko yao.
Alisema katika kuhakikisha heshima ya timu hiyo inarejea kama ilivyo katika miaka ya nyuma tayari amedai wameandaa mazingira mazuri ikiwemo ya kufanya mkutano wa pamoja kati ya wadau na wanachama mada kuu kuelezea changamoto zinazoikabili pamoja na maendeleo yake kwa kipindi cha miaka mitatu ya nyuma na malengo wanayokusudia kwa miaka ya mbele.
Pia, Ndumbaro alisema katika kikao chao walichokutana hivi karibuni wameweza kumsimamisha kazi Ofisa Habari wa Klabu ya Majimaji, Osama Ulaya kwa kile alichokidai amekuwa akifanyakazi kinyume na maadili ya kazi yake na kupelekea timu hiyo kwa kipindi chote kuingia katika malumbano yaliyochangia na kuwepo kwa uvumi na habari za uchochezi ambazo zilikuwa zikitolewa na Ofisa huyo.
MWISHO.