About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Sunday, June 16, 2013

KITUO CHA SAUTI YA JAMII SONGEA CHAPEWA MSAADA WA KOMPYUTA NA TGNP



Na, Stephano Mango, Songea

WANAWAKE waliopo pembezoni wametakiwa kukithamini na kukitumia Kituo cha taarifa na maarifa ili kuweza kupaza sauti zao kikamilifu katika changamoto zinazowakabili kwenye ujenzi wa tapo la ukombozi wa wanawake kimapinduzi

Wito huo umetolewa jana na Afisa Habari na Mawasiliano wa Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TGNP) Lilian Kitunga alipokuwa akikabidhi msaada wa Kompyuta,printer, moderm na muda wa maongezi vyenye thamani ya shilingi milioni 1.9 kweny Ofisi ya Sauti ya Jamii Kituo cha Taarifa na Maarifa Songea

Kitunga alisema kuwa msaada huo unapaswa kutumiwa kwa malengo kusudiwa ya mawasiliano kwa kuwafikia watu mbalimbali, kujenga nguvu ya pamoja katika kuleta mabadiliko chanya kwa kutumia ujumbe mfupi wa simu (sms) kwa gharama za Tgnp ili kuweza kuunganisha nguvu katika kuhabarishana na kuchukua hatua za kuwajibisha mamlaka na kuleta mabadiliko chanya

“Sauti ya Jamii itatumia teknolojia ya bulk sms kwa kutuma ujumbe kwenye simu kwa kutumia Kompyuta kwa zaidi ya watu 10,000 kwa wakati mmoja kwa lengo la kupashana habari za ujenzi wa vuguvugu la kimapinduzi” alisema Kitunga

Alifafanua kuwa kwa zaidi ya miaka 18 sasa, Tgnp imejikita katika harakati za kupigania haki za binadamu hasa wanawake na makundi yaliyopo pembezoni, usawa wa kijinsia, pamoja na ujenzi wa vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi katika ngazi zote za kijamii

Alisema kuwa Tgnp kwa kushirikiana na wada wengine ilibaini kuwa mbinu za kupeana taarifa kwa wakati baina ya vikundi na asasi za kimataifa ni tatizo kubwa ambalo linakwamisha jitihada za ujenzi bora wa tapo la ukombozi wa wanawake wa kimapinduzi

Alieleza kuwa ili kukabiliana na tatizo hilo moja ya mikakati iliyowekwa ni kuanzisha na kuviendeleza vituo vya Taarifa na Maarifa kwa kushirikiana na jamii ambavyo vitakuwa vitovu vya harakati katika ngazi ya jamii

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Sauti ya Jamii Kituo cha Taarifa na Maarifa Songea Fatuma Misango alisema kuwa mradi huo ulibuniwa na Tgnp utaongeza chachu ya kuleta mabadiliko katika jamii na kuboresha mahusiano na mitandao ya kupashana habari kati ya Wanaharakati, Vikundi na Mitandao katika ngazi ya Jamii hadi Taifa ili kupunguza pengo kati ya wanao faidi taarifa muhimu na wale ambao hawapati taarifa hizo

Misango alisema kuwa kuanzishwa kwa Kituo hicho kutasaidia kunoa uelewa wa wanawake waliopo pembezoni wa uchambuzi wa masuala ya kimfumo, Kisera na kimuundo na kutumia chambuzi hizo katika kudai uwajibikaji na mabadiliko yenye mrengo wa ukombozi wa wanawake wa kimapinduzi

MWISHO

TGNP NA MPANGO WA UTAFITI SHIRIKISHI WA URAGHABISHI



Miongoni mwa Wanawake walipo Pembezoni wakipepeta pumba za Mchele ili waweze kupata punje za mchele ambazo zinawasaidia kwenda kutengeneza chakula chao au vitumbua ambavyo wanaviuza na kujikimu na maisha, hapo ni Songea
Bibi mkazi wa Bombambili Songea ambaye anakadiliwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka 70, akitengeneza udongo ambao unapendwa sana na kina mama(Picha zote na Stephano Mango, Songea)

Na, Privatus Karugendo

KATIKA jitihada zake za kupambana na mfumo dume, uliberali mamboleo na mifumo yote kandamizi na kupambana ili rasilmali ziwanufaishe wanawake walioko pembezoni, TGNP imeanzisha mpango wa utafiti shirikishi wa uraghabishi.

TGNP, imeamua kuukumbatia mpango huu kwa vile unatoa nafasi pana ya ushirikishwaji hadi ngazi ya vijijini na kuchochea kuibua kero na changamoto nyingi ambazo zinahitaji majibu ya jamii nzima.

Mpango huu unatumika kama mbinu muhimu ya kujifunza, kutafakari, kuchambua na kutekeleza mikakati mbalimbali ya ujenzi wa Tapo la ukombozi wa wanawake kimapinduzi lililokita katika ngazi za msingi ya kijamii na lenye uwezo kwa kudai uwajibikaji katika kutoa huduma bora, kusimamia rasilimali za taifa ili ziwanufaishe makundi yaliyoko pembezoni hususan wanawake.



Lengo kuu na mpango huu wa utafiti shirikishi wa uraghabishi ni kuwezesha ushiriki wa wanawake, wanaume, makundi na mitandao katika ngazi ya jamii kufanya uchambuzi wa hali halisi kwa mrengo wa ukombozi wa wanawake kimapinduzi; kuibua kero na changamoto zinazokabili makundi husika na za pamoja.

Mpango huu pia unalenga katika kukuza uwezo na uelewa wa uchambuzi wa kero zinazoikabili jamii.

Tamko la TGNP kwa vyombo vya habari lilitolewa tarehe 9. 6. 2013, ni la mpango huu ulioendeshwa kwenye wilaya tatu za Mbeya Vijijini, Kata ya Mshewe, Morogoro Vijijini Kisaki na Kishapu – Shinyanga. Katika makala hii tutajadili mrejesho wa utafiti huu ambao ni wa aina yake.

Changamoto za uwekezaji na mgawanyo mbaya wa ardhi kwa wananchi, ilijitokeza katika utafiti huu na mfano mzuri ni Kata ya Mshewe, Mbeya Vijijini. Katika kata hii utafiti ulibaini mgawanyo mbaya wa ardhi kwa wawekezaji; ardhi nzuri na yenye rutuba imetolewa kwa wawekezaji kiasi kwamba wenyeji hawana mashamba na wanalazimika kuwa vibarua kwenye mashamba ya wawekezaji.

Mbaya zaidi ni kwamba wawekezaji wenyewe wanawalipa kidogo. Mfano wanawake wanalipwa kati ya shilingi 2,500 hadi 3,000 kwa siku.

Pamoja na kulipwa kidogo, wanakumbana na rushwa ya ngono na manyanyaso mengine hali inayosababisha ongezeko la magonjwa ambukizi yakiwamo VVU na ukimwi.

Changamoto hii ya mgawanyo mbaya wa ardhi imejitokeza pia katika Kata ya Kisaki, Morogoro mjini, ambapo wakulima wadogo wadogo wanapambana na wafugaji.

Kwa vile wafugaji hawana maeneo ya kutosha kwa mifugo yao, wanaingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kuleta vita mbaya. Kwa upande mwingine wafugaji wanatumia fedha kuwahonga viongozi ili wasisumbuliwe wanapoingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima.

Matumizi ya fedha ni kupokonya wanyonge haki zao, ni tatizo sugu kwa wananchi waishio pembezoni.

Suala jingine muhimu lililojitokeza kwenye utafiti huu wa TGNP kwenye wilaya tatu, ni upatikanaji wa maji safi na salama.

Pamoja na sera ya taifa kwamba maji yawe umbali wa mita 400 kutoka kwa makazi ya watu, bado maeneo mengi hapa Tanzania yana tatizo kubwa la kupata maji safi na salama. Watu wa Kishapu na Mshewe, ni miongoni mwa wananchi wa Tanzania ambao bado wana tatizo hili kubwa. Kijiji cha Ilota- Mshewe, wananchi wanalazimika kuchangia maji machafu na mifugo.

Tatizo hili la maji safi na salama ni kubwa sana katika vijiji vya Isoso na Lubaga katika Kata ya Kishapu, wanawake wanatembea mwendo mrefu na katika mazingira hatarishi kutafuta maji; mazingira haya yanasababisha mimba za utotoni, ubakaji na vipigo kwa wanawake wakichelewa kutoka kuchota maji.

Na nyongeza ni kwamba muda mwingi na rasilmali vinatumika kusaka maji kitu kinachoongeza hali ya umaskini katika jamii ya watu hawa wa Kishapu.

Ukosefu wa huduma bora za afya ni suala jingine lililoibuliwa na mpango wa utafiti shirikishi wa uraghabishi. Mfano kati ya wanawake 20 walihojiwa katika Kijiji cha Ilota, Mbeya Vijijini ni mwanamke mmoja tu ndiye aliyetaja kujifungulia hospitali.

Umbali wa hospitali na vituo vya afya unawalazimisha wanawake wengi kuzalia nyumbani kwa wakunga wa jadi.

Hii ni hatari kwa mama na mtoto na kuna ukweli wa wanawake wengi kupoteza maisha wakati wa kujifungua na watoto kutopata huduma muhimu za chanjo wakiwa na umri chini ya miaka mitano.

Kata ya Kisaki, Morogoro Vijijini, tatizo si hospitali wala kituo cha afya, tatizo ni dawa na wahudumu wa afya katika vijijini vya Gomero, Stesheni na Nyarutanga. Vijiji hivi vina majengo mazuri, lakini hakuna dawa na wahudumu.

Mbali na tatizo hilo, pia inapobidi wananchi wanachangia gari la wagonjwa shilingi 70,000, ili kumpeleka mama mja mzito kwenye Hospitali ya Mkoa wa Morogoro. Hali hii ni hatari, maana wanawake wengi wanaweza kupoteza maisha yao kwa kushindwa kulipia hizo shilingi 70,000.

Ukiachia masuala hayo yaliyotajwa hapo juu, utafiti huu wa TGNP, ulibaini kwamba lipo tatizo la msingi ni uongozi mbovu na rushwa. Hili lilitajwa kila sehemu iliyofanyiwa utafiti.

Kwamba uongozi mbovu na rushwa vinasababisha ukosefu wa huduma za msingi kwa wanawake na wanaume walioko pembezoni.

Na kwamba kuna usiri wa taarifa za mapato na matumizi, viongozi kutowashirikisha wananchi katika masuala ya maendeleo, viongozi ngazi za vijiji kuruhusu video za ngono na viongozi kutotekeleza ahadi zao kwa wananchi.

Ni mengi yaliyojitokeza kwenye utafiti huu, ila yametajwa machache ili kufikisha ujumbe kwa wahusika, ili wajaribu kutafuta majibu ya kuondoa unyanyasaji wa wanawake na wasichana katika wilaya hizi zilizotembelewa na watafiti wa TGNP pamoja na maeneo mengine ndani ya taifa letu.

Mfano tatizo la maji linasababisha vipigo kwa wanawake, ubakaji, elimu duni kwa wasichana, mimba za utotoni na ukosefu wa kipato.

Serikali kuu na serikali za mitaa zinaweza kuyatumia matokeo ya utafiti huu kurekebisha matatizo yaliyoorodheshwa hapo juu: Mfano serikali kuirejesha ardhi ya Kata ya Mshewe inayomilikiwa na wawekezaji wa nje na ndani ya nchi, kwa manufaa ya wananchi sasa na vizazi vijavyo.

Pia serikali itenge maeneo ya wafugaji katika Kata ya Kisaki, ili kuepusha mapigano kati ya wakulima na wafugaji.

Huduma ya kupatikana maji safi na salama ishughulikiwe katika vijiji vilivyotajwa na ambavyo havikutajwa.

Utafiti huu umeonesha wazi kwamba maji safi na salama ni muhimu kwa Watanzania wote. Huduma ya hospitali pia iboreshwe. Pia ni muhimu kuwapo na mfumo wa kuwawajibisha viongozi wote wanaokiuka maadili ya kazi zao ili kuondokana na aina zote za rushwa na ukatili wa kijinsia hasa ukatili kwa wanawake na wasichana.

Lakini pia viongozi wawakilishi hususan madiwani na wabunge wanaweza kutumia matokeo ya utafiti kudai uwajibikaji wa serikali kwa wananchi katika ngazi zote kupita bajeti, ripoti ya mkaguzi wa serikali, kudai sera ya haki ya uhuru wa wananchi na mikakati mbali mbali ya maendeleo.

Vyombo vya habari, taasisi za utafiti na makundi ya kiraia yanaweza pia kuutumia mpango huu wa utafiti shirikishi wa uraghabishi kuibua masuala ya wanajamii na kujenga uwezo wa wanajamii kuhoji na kudai uwajibikaji.

Hapana shaka kwamba mpango huu wa utafiti shirikishi na uraghabishi ndio unafaa kabisa kubainisha chanzo cha vurugu za Mtwara. Mpango huu unamruhusu kila mshiriki kuzungumza bila kuogopa na kwa njia hii ya uraghabishi, watu wanajifunua na kujiweka wazi.


+255 754 633122 www.karugendo.net