RAIS Jakaya Kikwete amevunja ukimya kwa kusema kwamba hakuna rushwa kwenye kashfa ya ununuzi wa rada kutoka nchini Uingereza. Ingawa Rais Kikwete hakutaja jina, lakini kwa kauli hiyo ni dhahiri kwamba amemsafisha Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitajwa ndani na nje ya chama chake kuhusika na kashfa ya ununuzi wa rada kutoka Kampuni ya BAE- System. Chenge, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi, anatajwa kuhusika kutoa ushauri wa kisheria wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ushauri ambao unatajwa kuzingatiwa katika hatua za uamuzi. Mwingine anayehusishwa na kashfa hiyo ni aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT) Dk. Idriss Rashid. Pamoja na hao, wanatajwa wafanyabiashara wenye asili ya India, lakini ambao wanaishi/walipata kuishi Tanzania, Tanil Somaiya, ambaye alikuwa akimiliki kampuni ya uwakala wa simu ya Shivacom na Sailesh (Shailesh) Vithlani kuwa watu wa kati wa biashara hiyo. Akijibu swali kutoka kwa mmoja wa wahariri aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa kwa waliohusika na ununuzi wa rada wakati chenji yake imesharejeshwa, Rais Kikwete alisema Serikali ya Uingereza iliyokuwa ikichunguza kashfa hiyo imebaini kuwa hakukuwa na rushwa katika ununuzi wa rushwa. Kwa mujibu wa Rais Kikwete, uchunguzi wa Serikali ya Uingereza ulibaini kuwa kulikuwa na makosa ya uchapaji, lakini hakuna mtu aliyehusika kutoa wala kupokea rushwa. “Kama Uingereza waliochunguza kashfa hiyo wamefika mahala wanasema kulikuwa na makosa ya uchapaji tu, mtu wenu mnamfikisha mahakamani kwa ushahidi upi?” alihoji Rais Kikwete. Mchakato wa ununuzi wa rada, uliwahusisha watu wa madaraka na kada mbalimbali ambao ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair. Blair anatajwa kuwa ndiye aliyemshawishi aliyekuwa Rais wa Tanzania wakati huo, Benjamin Mkapa, kununua rada hiyo kutoka Kampuni ya kutengeneza silaha ya Uingereza BAE-Systems. Wakati huo aliyekuwa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa, Clare Short, alikataa katakata Tanzania, moja kati ya nchi masikini kabisa duniani, kutumia sh bilioni 40 kununua rada katikati ya umasikini unaonuka. Hata hivyo chenji hiyo ya rada, zaidi ya sh bilioni 75 zimerejeshwa nchini baada ya hati ya makubaliano baina ya pande zinazohusika kusainiwa. Hati hiyo ilisainiwa kati ya Serikali ya Tanzania, Kampuni ya Uuzaji wa Silaha ya Uingereza (BAE - System), Ofisi ya Uingereza ya Kupambana na Ufisadi (SFO) na Idara ya Kimataifa ya Misaada ya Maendeleo (DFID). Chenge mwenyewe huko nyuma alipata kuzungumzia suala hilo na hasa, kumiliki kwake kwa akaunti ya fedha nyingi nje ya nchi inayohusishwa na mlungula wa ununuzi wa rada. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Edward Hosea, alipata mara mbili kunukuliwa akisema Chenge hakuwa na kesi ya kujibu katika kashfa hiyo ya rada. Kuhusu sakata la wizi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), iliyohusisha Kampuni ya Kagoda iliyochota sh bilioni 40, Rais Kikwete alisema suala haliko kwake bali mikononi mwa vyombo vya dola. “Hili la Kagoda liko mikononi mwa vyombo vya dola, wanaendelee nalo,” alisema Rais Kikwete. Hata hivyo Rais Kikwete alitamba kuwa serikali yake imejitahidi sana kupambana na rushwa kwa kuimarisha uwezo wa TAKUKURU.
Chanzo Tanzania Daima
|
No comments:
Post a Comment