About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, March 28, 2013

ZITTO: CHADEMA SI PANGO LA WAUAJI, ASEMA HAAMINI KAMA DK.SLAA ANAWEZA KUMUUA

Na Waandishi wetu
 
SIKU moja baada ya gazeti la Mtanzania kuandika habari likidai kuwa siri ya kumuua Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) imefichuka, kiongozi huyo amejitokeza akisema ni uzushi.
 
Habari hiyo ilidai kuwa ilipangwa Zitto anyweshwe sumu hotelini na kumtaja Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kuwa ndiye alimtuma kijana Ben Saanane kutimiza mkakati huo.
 
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa kisiasa walisema habari hiyo inayodai tukio hilo lilitokea Mei mwaka jana jijini Dar es Salaam, ilikuwa ni propaganda ya kuhamisha mjadala wa sakata la kuteswa na kuumizwa kwa
 
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Absalom Kibanda.
Kibanda alitendewa unyama huo Machi 6 mwaka huu, lakini hadi leo vyombo vya dola vimeshindwa kuwakamata wahusika na badala yake yamekuwa yakiibuliwa matukio mbalimbali ili kupoteza ajenda hiyo inayoonesha udhaifu wa kiutendaji wa vyombo hivyo.
 
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Zitto alisema habari hiyo imemletea usumbufu mkubwa kwani ndugu, jamaa, marafiki na wapiga kura wake wamejawa na wasiwasi kwamba anaweza kuuawa.
 
“Moja, sijawahi katika maisha yangu yote kukutana na mtu anayeitwa Ben Saanane na hivyo hicho kikao ambacho inasemekana nilikuwa naye na akajaribu kunipa sumu hakijawahi kutokea. Imetajwa Hoteli ya Lunch Time ambayo sio tu sijawahi kufika, pia hata siijui ipo wapi,” alisema.
 
Alifafanua kuwa haijawahi kutokea yeye kufanya kikao cha pamoja na Ben Saanane, Juliana Shonza na Mtela Mwampamba. Hivyo habari iliyoandikwa ni ya kufikirika.
 
“Pili, siamini kamwe kuwa Katibu Mkuu wa chama changu (Dk. Slaa) anaweza kupanga kuniua maana hana sababu ya kufanya hivyo. Napenda kurudia kusema kwamba mimi ninaamini kuwa kila nafsi itaonja mauti.
 
“Kila mtu atakufa. Kama nitakufa kwa kuuawa na mtu mwingine ndiyo itakuwa nimeandikiwa hivyo na Mungu. Ndiyo maana hata siku moja silalamiki kuhusu vitisho vya kuuawa. Kama kuna mtu anafikiria kuwa kumuua Zitto ndiyo furaha ya maisha yake atakuwa anajidanganya tu maana Zitto anaweza kufa kimwili, lakini mawazo, fikra na maono yake yataishi tu,” alisema.
 
Aliongeza kuwa haogopi kufa maana maisha aliyoyachagua ndiyo haya ambayo yamejaa vitisho, kwamba muhimu kwake ni kufanya kazi zake kwa bidii, uhodari na uaminifu.
 
“Tatu, nawashauri watu ambao wamehama CHADEMA na kuhamia vyama vingine watumie muda wao kujenga vyama vyao badala ya kila siku kuzungumzia masuala ya chama ambacho wao sio wanachama tena.
 
“Kama mtu kaamua kuhama CHADEMA anapoteza haki ya kujadili masuala ya CHADEMA, maana kama angekuwa anapenda kuyajadili asingehama. Naonya mtu yeyote ambaye anatumia jina langu ili kufanikisha malengo yake ya kisiasa,” alionya Zitto.
 
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA (Bara), alisema chama hicho si pango la watesaji wala wauaji, kwamba kuna mwanachama wa chama kingine cha siasa anayedhani kuna mtu ndani ya CHADEMA anapanga mipango ovu aende kwenye vyombo vya sheria kumshtaki.
 
“Matendo ya mtu mmoja yasifanyiwe propaganda kama ni malengo ya taasisi. Nne, Nawashauri viongozi wa CHADEMA na hasa wanachama tutumie muda wetu kujenga mshikamano ndani ya chama. Fitna, majungu, uongo, uzandiki nk kamwe havijengi chama,” alisema.
 
Saanane ang’aka
Naye Saanane aliyedaiwa na gezeti hilo kuwa ndiye alikuwa ametumwa kumdhuru Zitto, alisema amesikitishwa jinsi lilivyoshiriki katika dhamira nzima ya kumchafua.
 
Akizungumza katika ofisi za Tanzania Daima jana, Saanane ambaye ni mjumbe wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) alisema kutokana na habari hiyo ameamua kukutana na wanasheria wake kuangalia hatua za kuchukua ili ukweli ubainike.
 
“Nasisitiza sijawahi kupanga kumuua mtu yeyote, sijawahi kutumwa kumuua Zitto Kabwe. Nimesikitishwa kuona chombo cha habari kikitumika kwa maslahi binafsi ya kuchafua watu kisiasa,” alisema.
Aliongeza kuwa mara zote alizokutana na Zitto, hawajawahi kufika katika Hoteli ya Lunch Time wakiwa pamoja kama ilivyoelezwa katika gazeti hilo.
 
Bashe anena
Alipoulizwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd wachapishaji wa gazeti hilo, Hussein Bashe juu ya tetesi za kutumiwa kuyeyusha sakata la kuteswa kwa Kibanda kwenye vyombo vya habari, alisema hawawezi kutumiwa na taasisi yoyote kuzima suala hilo.
 
“Hilo la namna habari ilivyotoka mimi si mwandishi wa habari, ninachoweza kukuambia ni kwamba magazeti ya New Habari hayawezi kutumiwa na mtu yeyote kuzima au kufifisha suala la Kibanda,” alisisitiza.
 
Alisema kama kuna watu wanafanya siasa rahisi za kuyahusisha magazeti yao na mkakati wa kuzima suala la Kibanda watakuwa wamekosea kwa kile alichoeleza hawezi kuruhusu hali hiyo.
 
Alipoulizwa atachukua hatua gani kwa mhariri endapo itabainika gazeti hilo kutumika kwa lengo la kuwatoa watu katika kujadili madhila yaliyompata Kibanda, alisema hayo ni masuala ya ndani ambayo hayawezi kuwekwa hadharani pasipo kufuata taratibu.

Thursday, March 7, 2013

LA KIBANDA NALO LINAKUMBUSHA HAYA



Watanzania wenzangu,

Tumeshashughudia utekwaji wa watu kadhaa mara kwa mara. Tumeshashuhudia matukio mbalimbali ya ajabu, ambayo hata hivyo yalifanywa kwa namna ya kuwasingizia majambazi.

Leo, tunamwona tena Mwanahabari mahiri, Absalom Kibanda, akipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu, si ya ugonjwa, bali ya kipigo kutoka kwa watu wasiofahamika, watu waitwao majambazi.

Hili linatokea muda wa miezi takribani minne baada ya Mnaku Mbani, Mhariri wa gazeti la Business Times kupigwa risasi mdomoni na kupoteza meno matatu.

Hili linakuja baada ya Mwandishi mwingine wa Tanzania Daima, Shaaban Mtutu kupigwa risasi na Polisi eti akidhaniwa ni jambazi. Huyu alipigwa risasi akiwa nyumbani kwake mnamo tarehe 4 Disemba, 2012, eti polisi walimdhania ni jambazi, AKIWA NYUMBANI KWAKE.

Tukio la Kibanda, linatokea ikiwa ni miezi michache tangu Mwangosi Daudi, mwandishi wa Channel Ten kuuawa na jeshi la polisi tarehe 2 Septemba 2012.

Hili linakuja miaka michache baada ya mapema mwaka 2008 Saed Kubenea, Mkurugenzi wa kampuni ichapayo gazeti la Mwanahalisi (ambalo nalo limefungiwa), kumwagiwa tindikali machoni pamoja na Mhariri Mshauri wa gazeti hilo Ndimara Tegambwage kucharangwa kwa mapanga.

Linatokea miezi michache baada ya Dk. Ulimboka kutekwa na kupigwa nusu kifo, na kutupiwa msitu wa Mabwepande. Haya yote yanatokea Tanzania, na asilimia kubwa ya haya yote yamehusishwa na ujambazi.

Huwa najiuliza, ujambazi ni nini? Kwa nini hao majambazi hawaibi chochote zaidi ya kuwajeruhi na kunuia kuwaua hawa makamanda? Kwa nini wawavamie tu watu wenye kuikosoa serikali?

Hao majambazi kwa nini hawapatikani? Ikiwa juzi tu ameuawa kwa risasi Padre kule Zanzibar, na serikali imewaleta FBI kwa ajili ya uchunguzi wa tukio hilo, kwa nini serikali isione haja ya kuwatumia FBI na taasisi nyingine za ukachero kutoka mataifa yaliyoendelea ili tuwapate hawa wahalifu wawavamiao wanahabari na wanaharakati wetu? Watanzania, tutanyamaza hadi lini ikiwa sauti zetu zinanyamazishwa?

Bwana Kibanda, hadi sasa, ana kesi mahakamani. Kesi ya uchochezi baada ya gazeti la Tanzania Daima (Wakati Kibanda akiwa Mhariri) kuchapa makala iliyoandikwa na Mwandishi na Mwanaharakati Samson Mwigamba. Kesi hii ingali ikisikilizwa, leo tunasikia kuwa amevamiwa na majambazi! Kweli? Latuingia akilini kweli? Latushawishi hili kweli?

Tanzania, serikali imetengeneza mtandao wa Kimafia (kama alivyoeleza Mh. Joseph Mbilinyi Bungeni Mwaka jana). Kumekuwa na mtandao wa kimafia unaowawinda makamanda, wanaharakati.

Habari/tetesi zilishawekwa wazi kuwa kuna kundi la watu limeundwa, linalojishughulisha na utekaji, utesaji, na uuaji wa watu wenye ushawishi katika jamii, wanaoikosoa serikali kwa uwazi. Yamkini kundi hili ndilo lililoripotiwa kuwafuatilia Mh. John Myinka, Mh. Godbless Lema, na Mh. Dk. Wilbroad Slaa.

Yamkini hilo ndilo kundi lililomwekea sumu Mwanaharakati mwingine Dk. Harryson Mwakyembe. Hili ndilo kundi lililoripotiwa kufuatilia maisha ya Mh. Samwel Sitta. Hili ndilo kundi, ndilo hasa!

Kundi hili la kimafia limeamua kuwanyamazisha Watanzania, na kuiacha serikali iendelee kutuibia, kutunyonya na kutufanya mafukara.

Kundi hili limenuia kuifanya serikali iendelee kutawala na kujinawirisha. Vigogo wa serikali na watoto wao waendelee kufurahia nchi, kwa kodi zetu wananchi.

Kundi hili limenuia kuhakikisha viongozi waovu na wabadhirifu wa mali za umma wanaendelea kututawala kwa mabavu, kwa matisho na kwa dhuluma.

Kwa mtindo huu, lazima tuhoji waziwazi kuwa kwa nini watu hawa hawakamatwi na kutiwa nguvuni, iwapo kweli serikali haina uhusiano nao?

Si ndio hawa wafanyao kazi kama Ramadhani Ighondu? Hapa tusidanganyane, serikali inawafahamu watu wote wa kundi hili... Serikali inafahamu A hadi Z ya kundi hili, na yamkini serikali ndiyo iliyowapa kazi hii maalum.

Kufunika kombe ili mwanaharamu apite, tunaiona serikali ikienda kuwajulia hali wahanga wa uonevu huu. Serikali inamtuma Makamu wa Rais kwenda kumtazama Kibanda hospitalini, Rais Kikwete pia alikwenda kumjulia hali Saed Kubenea... Yote haya ni kujaribu kutudanganya (elude) kuwa hawajui kiendeleacho..

Serikali inafahamu kundi lake hili la kimafia. Kundi la uovu, inalifahamu vyema..

Sasa, kwa nini serikali ifanye hivi? Kwa nini wanaharakati wateswe, wakamatwe, wauawe? Ukweli wenyewe ndio huu:

Lengo kuu la serikali, ni kunyamazisha sauti zote zinazoikosoa bila kujali sauti hizo zinatokea wapi. Serikali inahitaji kunyamazisha sauti za watu binafsi, inahitaji kunyamazisha sauti za vikundi, vyama au jumuiya zinazoikosoa.

Sasa kwa sababu tasnia ya habari huwafikia wengi, na kwa sababu watu wengi huamini habari za vyombo vya habari, serikali imenuia kuinyamazisha kabisa tasnia ya habari kwa kushughulika na wakosoaji wakubwa katika vyombo vya habari.

Ndio maana hata waandishi wa makala kama hizi wanatafutiwa visa hata vya kufungwa gerezani. Mfano mzuri wa hili ni kesi ambayo inaendelea mahakamani dhidi ya Kibanda mwenyewe, na Samson Mwigamba, eti kwa sababu ya makala iliyochapwa kwenye gazeti la Tanzania Daima.

Pengine wengi wetu mnamkumbuka Sam Shollei. Huyu alikuwa ni Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti la Mwananchi, kabla ya Tido Mhando wa sasa.

Huyu si Mtanzania bali ni Mkenya. Shollei aliibadilisha taswira ya gaeti la Mwananchi na kulifikisha katika taswira lililokuwa nayo sasa.

Alifanya kazi kubwa sana. Lakini, mwisho wake alinyimwa kibali cha kuendelea kufanya kazi nchini Tanzania baada ya kibali chake cha awali kwisha muda.

Serikali, kupitia uhamiaji, ilimnyima Shollei kibali bila kuweka bayana sababu za kufanya hivyo. Zitto Kabwe alipiga kelele kidogo kuikosoa serikali kwa swala hilo lakini kelele zake hazikufua dafu.

Shollei, aliyelipa gazeti la Mwananchi umaarufu mkubwa na maendeleo makubwa akalazimika kuacha kazi.

Baada ya Shollei kulazimika kuondoka Tanzania, nafasi yake ikachukuliwa na Tido Mhando. Hapa tukumbuke kuwa, Tido Mhando alifuatwa na Rais Kikwete London mwaka 2007, akiwa Mkurugenzi wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC, na Kikwete akamwomba aje aiongoze TBC.

Hata hivyo naye alipoiongoza TBC na kuwa chombo cha uwazi na ukweli, na pale aliporuhusu kuonyeshwa kwa mikutano ya kampezi ya vyama vyote vya siasa katika uchaguzi Mkuu wa 2010, bila upendeleo, Tido alinyimwa mkataba mpya mwaka 2011.

Tido, akiwa amebadilisha taswira ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), akanyimwa mkataba wa kuendelea kuiongoza. Sasa ni nani asiyejua kuwa TBC imeshapoteza ule umahiri wake ambao Tido aliisaidia kuwa nao? TBC sasa imerejea ilipotoka, imeanza kulichungulia kaburi tena...

Baada ya Tido kunyimwa mkataba na serikali, licha ya kwamba watu wengi walilaumu sana, Tido akachukuliwa na Mwananchi, kuziba nafasi ya Shollei.

Sasa, pengine kwa weledi wa Absalom Kibanda, kwa kazi ambayo ameifanya tangu akiwa Mhariri Mtendaji wa Tanzania Daima, naye ameanza kutafutwa roho yake na hao wanaoitwa "majambazi". Majambazi wasioiba chochote, majambazi watafutao roho za wanahabari mahiri na wanaharakati.

Nirudie tena, lengo la serikali ni kuifunga mdomo tasnia ya habari Tanzania. Lengo lake ni kuwa na vyombo vya habari kama Radio Uhuru na Gazeti la Mzalendo ambayo kazi yao ni kuitukuza serikali ya CCM hata pale pasipostahili.

Lengo la serikali, ni kuwanyamazisha makamanda wote waonekanao kuikosoa serikali kwa uwazi. Na hili linaonekana kufanikiwa kwa kiasi fulani.. Kwani gazeti la Mwanahalisi liko wapi leo? Mwangosi yuko wapi? Kubenea anasikika tena? Je ulimboka mmemsikia tena? Wote hawa wameshanyamazishwa kwa kiasi fualani, sauti zao zimefifia.

Watanzania wenzangu, Tanzania ya sasa si mahala salama kwa Wanahabari makini, na wanaharakati. Nawaomba na kuwasihi tuwe macho na tuamke tuungane na wenzetu hawa waliojitoa mhanga.

Tusimameni imara kuitetea nchi yetu, haijalishi watuue sote. Kwa hakika, tusiposimama imara, nchi hii tutaitumbukiza korongoni.

Tupazeni sauti zetu pale tuwapo na nafasi. Kwa wale tusioweza kuchapa makala kwenye magazeti mbalimbali, mitandao ya kijamii ndio silaha yetu iliyosalia.

Tusiandike jumbe za mapenzi kwenye kuta zetu za Facebook, Tiwitter, blogu zetu. Tuandikeni jumbe za kutafuta haki na usawa nchini.

Tuandikeni jumbe za kuikosoa serikali na kuilalamikia kila uchwao uchao. Tusiishie hapo; tuwaamsheni Watanzia wenzetu; tuwaamsheni waliolala... Tuwaelezeni kumepambazuka.... Tusipofanya hivyo, tutakapoacha kazi hii mikononi mwa wenzetu wachache, kwa hakika tutashiriki kiliangamiza taifa letu. Mwisho tutalia na kusaga meno.

WANAKONGANO WATAKIWA KUJITUMA KATIKA UZALISHAJI WA UYOGA



Na,Mwandishi Wetu , Songea
WANAKONGANO wa Uyoga Songea wametakiwa kujishughulisha kwa kasi na kujituma katika kilimo cha uyoga ili kuweza kuongeza uzalishaji wa zao hilo ili walaji waupate kwa wingi kwa mahitaji mbalimbali katika Jamii

Wito huo umetolewa jana na  Mkuu wa Wilaya ya Songea Joseph Mkirikiti kwenye ukumbi wa Saccos ya Walimu Songea Mjini wakati akiwahutubia Wanakongano na wageni waalikwa kwenye hafla fupi ya kuikabidhi hundi ya shilingi milioni nane Kongano la Uyoga Songea

Mkirikiti alisema kuwa  Kongano la Uyoga Songea  linapaswa kuwa chachu ya kujiimarisha katika uzalishaji wa zao la Uyoga  kwa lengo la kuongeza lishe na kipato miongoni mwa Jamii kama vile malengo yake ya kuanzishwa yanavyosema

Alisema kuwa hadi sasa Kongano hili limethubutu kufanya jambo  la kimaendeleo ambalo leo limetukutanisha katika ukumbi huu likiwa na malengo ya kuiwezesha jamii kupata lishe bora na kipato miongoni mwao

Awali akizungumza na Wanakongano hao Mratibu wa Kongano Nchini kutoka Tume ya Sayansi na Teknologia Omary Bakari alisema kuwa (Songea Mushroom Cluster ) Kongano la Uyoga Songea limeonyesha mfano wa kuigwa kwani mara baada ya kupata mafunzo ya uwezeshaji waliweka mpango kazi ambao leo umezaa matunda stahiki

Bakari alisema kuwa mpango huo umeletewa fedha ya shilingi milioni nane kutoka Tume ya Sayansi na Tecknologia ili uweze kutekelezwa na kufikia mafanikio yaliyokusudiwa kadri ya shughuli zilizopangwa kwenye mpango kazi

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo Katibu Mtendaji wa Kongano la Uyoga Songea Stephano Mango alisema kuwa haikuwa gazi rahisi kutengeneza mpango huo wa kuiwezesha Kongano ili liweze kusonga mbele

Alisema kuwa mpango huo utaiwezesha Kongano kuimarika na kuongeza uzalishaji wa uyoga kwa sababu fedha iliyofika itasaidia kutatua vikwazo ambavyo vinaisumbua Kongano vikiwemo vya uharibifu wa Vimeng’enya, wadudu waharibifu,zana duni za kilimo na kuhifadhia uyoga, elimu duni ya kumbukumbu

Mango alisema kuwa mpango huo ni wa miezi 18 na kwamba umegawanyika katika vipengele vitatu vya  uhamasishaji ,muda mfupi na muda mrefu ili malengo yatimie
MWISHO

Wednesday, March 6, 2013

MAAFISA UGANI WAPATIWA MAFUNZO YA ZAO LA UFUTA



Na, Stephano Mango,Pwani
MAAFISA Ugani nchini wametakiwa kukithamini na kukiendeleza kilimo cha zao la Ufuta ili kiweze kubadilisha maisha ya watanzania kutokana na mahitaji ya soko kuwa makubwa kwa sasa na kufanya zao hilo kwa baadhi ya maeneo kuwa zao kubwa la kibiashara

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Nurdin Babu kwenye ufunguzi wa mafunzo maalumu kuhusu kilimo bora cha ufuta, uliowashirikisha maafisa ishirini na wadau mbalimbali wa zao la ufuta wilayani Rufiji Mkoani Pwani yaliyofanyika  Mji mdogo wa Ikwiriri Wilayani Rufiji

Babu alisema kuwa Ufuta ni zao lisilotiliwa maanani na wakulima wengi nchini kwa miaka mingi pamoja na uwingi wa faida zake kwa binadamu, lakini kwa miaka ya hivi karibuni, takribani sehamu zote ambako hali ya hewa imekuwa rafiki wa kulistawisha zao hilo, wakulima wengi wameligeukia na kuanza kulima kwa kasi.

Alisema kuwa Wilaya ya Rufiji ni mojawapo ya wilaya ambazo zinastawisha zao la ufuta kwa siku nyingi na siku za hivi karibuni kasi ya uzalishaji imeongezeka kutokana na upatikanaji wa uhakika wa soko la ufuta.

“Hili ni zao lenye faida kubwa kama utekelezaji wa taaluma ya uzalishaji utafuatwa kwa makini, ambalo ndiyo lengo kuu la mafunzo haya na ni lazima walau kwa kuanzia tani elfu tano (5000) katika msimu ujao wa kilimo 2012/2013 kutoka tani za sasa 400 kwa mwaka na tani 280 mwaka 2005/06., anasisitiza Babu.

Akizungumza kwenye Mafunzo hayo Afisa Habari Mshauri Mkoa wa Pwani Silas Bwena alisema kuwa Serikari kupitia wizara ya viwanda, biashara na masoko, chini ya mradi wa MUVI mkoa wa Pwani imetoa mafunzo hayo kwa maafisa ugani ili waweze kuifikisha Elimu waliyoipata moja kwa moja kwa walengwa, ambao ni wakulima wadogowadogo walioko kwenye kata na vijiji husika.
Bwena alisema kuwa Mafunzo hayo yamelenga kumuwezesha mkulima kupata taaluma na uelewa mzuri zaidi katika kilimo cha zao hili tofauti na wanavvoelewa sasa ili kuboresha uzalishaji kwa lengo la kuongeza mazao yaliyo bora yatakayowezesha kupata bei nzuri kwenye soko
MWISHO