Na Stephano Mango, Songea
TIMU ya soka ya Mlale JKT ya Songea imesajili kinda kutoka Kahama United ya Shinyanga katika nafasi ya kiungo katika usajili wa dirisha dogo kabla ya kuanza kwa ligi ya Daraja la kwanza mzunguko wa pili, ligi hiyo ambayo inatarajiwa kuanza Februari, 4 mwaka huu.
Akizungumza mjini hapa jana kocha msaidizi wa Maafande hao, Edger Msabaila alimtaja kinda hilo kuwa Dotto Mrisho ambaye alikuwa akichezea nafasi ya kiungo katika timu yake ya Kahama United na kuwa tishio kwa timu nyingine za mkoa huo.
Alisema wamechukua uhamuzi huo wa kusajili nafasi hiyo moja ya kiungo baada ya kukaa chini na kamati ya ufundi wa timu hiyo na kuweza kubaini kulikuwepo na pengo katika mechi zake za mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo kutokana na mchezaji anayechezea nafasi hiyo, Patrick Batweri kusumbuliwa na maumivu ya mara kwa mara ya kifundo cha mguu.
Alieleza usajili huo wa kinda hilo umepelekea timu yao kukamilika kila idara zake na kuwataka wapenzi wa soka wa mkoa wa Ruvuma wawe na matumaini ya kuvuka ungwe hiyo na kucheza tisa bora na hatimaye kucheza ligi kuu ya Bara msimu ujao
Alisema moyo wa matumaini hayo yamekuja kufuatia uwezo mkubwa aliouonyesha kinda huyo wa kuweza kumiliki nafasi hiyo ya kiungo ambao anauonyesha katika mazoezi na kuwa kivutio kwa watazamaji wanaofurika kushuhudia mazoezi yao yanaendelea kwenye uwanja wa Majimaji mjini hapa.
Mlale JKT katika mchezo wake wa kwanza duru la mzunguko wa pili wamepangwa kukutana na ndugu zao Majimaji kabla ya kucheza na Small Boys ya Rukwa na mchezo wake wa tatu itasafiri na kwenda kukutana na Maafande a Polisi Iringa, kabla ya kurudi nyumbani na kuzisubili timu za Mbeya City na Prisons ya Mbeya.
MWISHO.