Mhashamu Askufu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea Dkt Norbert Wendelin Mtega akizungumza na Wanahabari mara baada ya KUJIUDHURU |
Na, Stephano Mango, Songea
JUMATANO Mei 15, mwaka 2013 ni siku ya historia kubwa
na ilioyo dhahiri kwa Kanisa Katoliki
Jimbo Kuu la Songea na kwa Waamini wote wa Yesu Kristo na wote wenye mapenzi
mema
Ni siku pekee ambayo haikutarajiwa na Wateule, Watakatifu na
Wanakanisa pale Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Songea Dkt
Norbert Wendelin Mtega alipoamua kuwatangazia Taifa la Mungu kustaafu (
Kujiudhuru) nafasi yake hiyo
Aliamua kuwatangazia uamuzi wake huo Viongozi mbalimbali wa
Kanisa Majira ya saa saba Mchana Hanga Monasteri iliyopo Wilaya ya Namtumbo
Mkoa wa Ruvuma nje kidogo ya Wilaya ya Songea,
siku ya Jumatano Mei 15, 2013
“…kwa kuzingatia hali yangu ya afya , kwa kuzingatia jinsi
nilivyoonja utendaji wangu unavyoonyesha dalili za kuchoka na pengine kuzorota nikiwa katika mwaka wangu wa
28 wa Uaskofu kwa hiari yangu kabisa niliamua kumuandikia barua Baba Mtakatifu
ili aniruhusu kustaafu kabla ya kufikia umri wa sheria na kanuni za kustaafu
rasmi” alisema Mtega
Alisema kuwa nafurahi kwa kuwa Baba Mtakatifu leo amenijibu
na kunikubalia ombi langu na dakika hii mbele yenu natua jukumu lote la Uongozi
juu ya Jimbo Kuu la Songea
Kwa hiari yangu na kwa kuashiriwa na hali ya afya yangu na
jinsi kazi inavyonielemea kupita uwezo wangu wa awali, nafanya hivyo kwa ajili
ya ustawi wa Taifa la Mungu, na hasa Kanisa lililoko Songea kwa hiyo mimi staki
niwe kikwazo na hoja ya Jimbo kuzorota katika siku za mbele
Alisema kuwa kuanzia sasa Msimamizi wa kitume wa Jimbo kuu
la Songea katika kipindi ambacho ambaye ameteuliwa na Baba Mtakatifu ni
Mhashamu Baba Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa
Ni msimamizi kwa kuwa ataliongoza Jimbo kuu la Songea katika
kipindi ambacho Baba Mtakatifu anapitia mchakato wake wa kumteua na kumtuma
rasmi Askofu Mkuu mwingine wa Songea
Hakuna shaka kuwa yeye ni msimamizi kwa kuwa yeye anaendelea
kuwa Askofu halali kabisa na mwenye mamlaka kamili bado juu ya Jimbo la Iringa,
hivyo yeye ni wa kitume kwa sababu ameteuliwa na Baba Mtakatifu.
“Kwa hiyo tangu sasa mamlaka yote ya Uongozi wa , Usimamizi
na maamuzi ninajivua kikamilifu kabisa naye Askofu Taricisius Ngalalekumtwa na
achukue sasa nafasi yake kikamilifu kabisa” Alisema Dkt Mtega
Alisema kuwa kuanzia sasa saa saba mchana ya mei 15, mwaka
2013 nikiwa mbele yenu kwa moyo wa dhati kabisa na kwa upendo mkubwa
kuwashukuru ninyi nyote wakiwemo Mapadre na Watawa na kwa kupitia kwenu nawaaga
wale wote mnaowaongoza, waamini na wafadhiri na marafiki wote wa Jimbo kuu la
Songea
Mhashamu Askofu Mkuu Dkt Norbert Wendel Mtega ni Askofu wa
pili wa Jimbo Kuu la Songea ambaye alishika nafasi hiyo baada ya Askofu Mkuu
Hayati Yakob Yafunani Komba
Dkt Mtega kiasili alizaliwa tarehe 17 Agosti 1945 katika
Kijiji cha Kinyika, Parokia ya Lupanga , Wilaya ya Ludewa, Jimbo la Njombe,
ambapo Jina la Baba yake ni Wendelin Mbwatilo Paulo Mtega
Jina la Mama yake ni Martha Msafiri Petro Mtweve na katika
familia yao
walizaliwa watoto kumi wakiwemo wavulana sita na wasichana wanne ambapo
wavulana wawili walikufa, mmoja ni kaka yake na mmoja ni mdogo wake.
Askofu Mtega aliwapa jina moja Marehemu hao ambalo
lilifahamika kwa Boniventura sababu ambazo yeye alizipenda, Yeye alikuwa ni
mtoto wa nne katika familia yake hiyo yenye watoto kumi waliozaliwa pamoja naye,
na yeye ni wanne katika nane walio hai.
Alibatizwa tarehe 9 Septemba 1945 na Padre Leonhard Wuesst
OSB Mmisionari Mbenedikitine Mswisi, ambapo Septemba 10, mwaka 1955 akiwa
darasa la Tatu, aliungama kwa mara ya kwanza na kupokea Komunyio ya Kwanza katika
Kigango cha Lupanga akiwa na umri wa miaka kumi.
Tarehe 2 Octoba 1956 akiwa darasa la nne alipata Sakramenti
ya Kipaimara ( LC 3034) Parokiani Madunda kwa Askofu Eberhard Spiess OSB.
Alisoma Darasa la kwanza hadi la nne katika Shule ya Msingi
ya Lupanga Wilayani Ludewa tangu Mwaka 1953 hadi 1957 na kwa kuwa Shule haikuwa
mbali sana na
nyumbani kwake, alikuwa ni mwanafunzi wa kutwa.
Jumamosi na Jumapili alikuwa anashinda nyumbani na kuchunga
mbuzi na ng’ombe za Baba yake , kazi ambayo alikuwa anaipenda sana, hata hivyo
mwaka 1956 alishinda mtihani wake wa darasa la nne ingawa alilalia darasa hilo.
Elimu ya Sekondari alisoma katika Seminari ya Kigonsera na
baadaye Seminari ya Likonde mwaka 1962 , ambapo alimaliza kidato cha nne
Novemba, mwaka 1964 na kuchaguliwa kwenda kidato cha tano Sekondari ya Serikali
ya Tosamaganga Mkoani Iringa na kumaliza kidato cha sita mwaka 1967.
Mwishoni mwa mwaka 1967 alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa
katika Kambi la Kitai Wilayani Mbinga na baadae Kambi ya Mafinga na kupata
namba ya kijeshi A0468 ambapo alifuzu mafunzo na kutunukiwa cheti
kinachotambulika kwa Best Trainee katika Kombania yake D.
Julai 1968 alijiunga na Seminari Kuu ya Peramiho kwa ajili
ya Mafunzo ya Falsafa kwa miaka miwili
ambapo alimaliza Novemba mwaka 1969 na Januari 1970 hadi Novemba 1973
aliendelea na masomo ya Teolojia hapo Seminari Kuu ya Peramiho
Alijipatia Stahashahada ( Diploma) ya Teolojia kutoka Chuo
Kikuu cha Makerere- Uganda
na mara baada ya kutoka huko alipata madaraja mbalimbali katika Kanisa kama vile kuwa Mkleri mwaka 1970 katika Parokia ya
Madunda , ambapo mwaka aliingizwa katika huduma ya Ungojezi Mlango na Uzinguaji
na baadaye Ushemasi mdogo
Mwaka 1973 alipewa Daraja la Ushemasi Seminari ya Peramiho
na Novemba 1973 alipewa Daraja Takatifu la Upadre Parokiani Lupanga ambapo
madaraja yote mawili alipewa na aliyekuwa Askofu wa Jimbo la Njombe Raymond
Mwanyika
Novemba 1973 alitolea misa Takatifu ya kwanza katika Parokia
ya Lupanga, na kwamba kazi yake ya Uchungaji mara baada ya Upadrisho wake
alitumwa Uaskofuni Njombe kuwa Mkurugenzi wa Caritas, Mkurugenzi wa Miito,
Mwalimu wa Dini katika shule ya Sekondari ya Njombe, Mlezi wa YCS Jimbo na
Paroko Msaidizi wa Pili wa Njombe
Septemba 1976 alijiunga na Chuo cha Kipapa Jijini Roma
(Pontificia Universita Urbaniana), Septemba 9 mwaka huo alianza kozi ya lugha
ya Kiitaliano ambapo Octoba 10, 1976 masomo ya Chuo Kikuu yalianza nay eye
alichukua masomo ya Falsafa
Mwaka 1978 alijipatia Shahada ya kwanza nay a pili ya masomo
ya Falsafa na kupewa Magna Cum na Januari 1981 alihitimu Shahada ya Tatu na
kupewa Summa Cum Laude, baada ya kurejea Tanzania alifundisha Seminari Kuu
ya Peramiho akifundisha masomo ya Falsafa , Historian a Kilatini
Novemba 28, 1985 aliteuliwa kuwa Askofu wa Tatu Jimbo la Iringa
na kupewa daraja hilo la Uaskofu Januari 6, 1986 mjini Roma na Baba Mtakatifu
John Paulo II, ambapo Julai 6, 1992 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la
Songea kuchukua nafasi ya Hayati Askofu Mkuu Yakobo Yafunani Komba
Tarehe 20 Septemba 1992 alisimikwa kuwa Askofu Mkuu wa Pili
wa Jimbo Kuu la Songea ambapo 2013 anatimiza miaka 27 ya Uaskofu na miaka 21 ya
Uaskofu Mkuu na 40 ya Upadre na 68 ya umri
Mei 19, 2013 amewaaga rasmi Waamini katika Kanisa Kuu la
Kiaskofu Songea na kuongoza misa maalumu akiwa Askofu Mkuu Mstaafu na kuwataka
waumini wamuombee kwani Mei 31, 2013 anaenda nje ya nchi kwa matibabu
“ Mwenyezi Mungu awabariki sana, na awaneemeshe, Niombeeni kama vile
nami nitakavyokuwa nawaombeeni, Amina” Alimalizia kwa kusema Askofu Mtega
Ni dhahiri kuwa Mhashamu Askofu Mtega amejiudhuru nafasi
yake hiyo kubwa ndani ya kanisa na kusababisha sintofahamu miongoni mwa Taifa
la Mungu, kila mmoja katika fikra zake anawaza kilichosababisha ang’atuke
Safari yake ya kiuchungaji ni ndefu inatupasa tuielewe na
kuitathimini kwa dhati ili tuweze kuliimarisha Taifa la Mungu kwani sote tu
mashahidi wa safari yake hiyo kwa ubora na udhaifu wake katika misingi ya
Imani, Upendo, Amani na Mshikamano miongoni mwa jamii ya Kanisa, yatosha kusema
Askofu Mtega asante na kwaheri Jimbo kuu la Songea
MWISHO
Mwandishi wa Makala
Anapatikana 0715-335051
www.stephanomango.blogspot.com
No comments:
Post a Comment