WANANCHI WATANGAZA MGOGORO MKUBWA WA ARDHI SONGEA
Na Stephano Mango,Songea
WANANCHI zaidi ya 1200 wa Kata ya Mshangano Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Songea kurasimisha mali zao kwa kuiruhusu Kampuni ya Ardhi Plan iwapimie viwanja na makazi walioanza kuyaendeleza kiholela.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi wa kata hiyo ambao chini ya uenyekiti wa Diwani wa Kata hiyo Faustine Mhagama walisema kuwa kata yao imekumbwa na mgogoro mkubwa wa ardhi baina ya wananchi wa eneo hilo na Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na madiwani mbalimbali na viongozi wa serikali uliofanyika jana kwenye viwanja vya ofisi ya kata waliohudhuria wengi wao wakiwa wanawake walisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa kurasimisha mali zao na kupata hati miliki za maeneo yao ili waweze kufanya kazi za kujipatia kipato na kukuza uchumi wao kutokana na urasimu wanaofanyiwa na Idara ya mipango miji ya Manispaa hiyo
Walisema kuwa maeneo yao wanataka kuyaendeleza kwa kuyafanyia shughuli mbalimbali za kiuchumi lakini hawajapimiwa na wala hayana hati hivyo wananchi kwa kushirikisha serikali zao za mitaa na kata hiyo kwa mamlaka iliyokuwa nazo ziliamua kuitafuta kampuni na kuweka michoro stahiki ya eneo hilo na kuiwasilisha kwenye Halmashauri hiyo ili waweze kupimiwa ardhi yao.
Anastasia Ndumbaro mkazi wa kata hiyo alisema kwa uchungu mkubwa huku akidondosha machozi kuwa wanasikitika kwa kitendo cha Manispaa ya songea kukwamisha zoezi hilo .
“tunasikitika kwa kitendo cha kuizuia kampuni kutupimia viwanja vyetu kwani tumekuwa tukihitaji sana kurasimishiwa maeneo yetu ili tuyaendeleze,”alisema Ndumbaro.
Ndumbaro alisema kuwa familia yake ina mashamba ya ekari 10 katika eneo hilo na Baba yake alifariki toka mwaka 1992 ambako amekuwa akifuatilia idara ya mipango miji ili iweze kumpimia viwanja hivyo na kugawana na ndugu zake mirathi lakini amekuwa akiyumbishwa hadi leo hii.
Naye Mwenyekiti wa mkutano huo Diwani Faustine Mhagama akifunga mkutano huo alisema kuwa amesikiliza kwa umakini kilio cha wapiga kura wake na matamko mbalimbali waliyoyatoa na kwamba anawaunga mkono.
Mhagama alisema atayawakilisha maazimio ya mkutano huo kwa maandishi kumtaka Mgurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Zakaria Nachoa kukaa na kuutazama mpango huo mzuri wa wananchi wa kata hiyo na kuiruhusu kampuni hiyo iwapimie wananchi maeneo yao .
Alifafanua zaidi kuwa ardhi hiyo ni mali ya wananchi wa kata hiyo na wao wameitaka kampuni iwapimie maeneo yao ili waweze kufanya shughuli zao za kukuza uchumi na kwamba kampuni kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa yote ya kata hiyo walifanya mikutano na wananchi walipeleka taarifa kwenye mamlaka husika bila kupata majibu kwa wakati ambapo sheria inatamka muda wa majibu ukichelewa ina maanisha mpango umekubaliwa
Alieleza zaidi kuwa Kampuni hiyo imekubali kuwapimia wananchi maeneo yao ili kurasmisha mali zao na kuendeleza makazi holela waliyonayo, kuweka alama maeneo hayo, kuwatafutia wananchi hati za kumiliki maeneo yao,kuchonga barabara za eneo hilo kwa gharama nafuu kwa lengo la kuharakisha maendeleo kama masterplan inavyoelekeza.
“Tunamtaka Mkurugenzi ndani ya siku saba airuhusu kampuni kuendelea na kazi iliyoelekezwa na wananchi endapo atakaidi agizo hilo wananchi wataamua vinginevyo ikiwa ni pamoja na kufanya maandamano ya amani ili kushinikiza Mgurugenzi na Afisa Mipango miji waondolewe kwenye nafasi zao na kumpeleka mahakamani,” lilisema azimio hilo.
Mwisho.