About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, June 8, 2012

UJIO WA FILAMU YA ADELAHIDA NI NGUZO MUHIMU KATIKA KUINUA TASNIA YA FILAMU MKOANI RUVUMA

 

Kaa tayari kwa Filamu ya Adelahida iliyotayarishwa na Mtayarishaji anayechipukia Shukrani K.Faraji.
 
Ni ndugu wa mapacha watatu Ade,Lah na Ida wanakuja kukutana tena baada ya kupoteana kwa muda wa miaka ishirini.
 
Kujua kilichosababisha utakiona ndani ya Filamu hii kwani ipo mitaani.
 
Ni filamu iliyotengenezwa kwenye mazingira ya asili katikati ya Misitu ya maeneo ya milima ya Matogoro-Songea.
 
Filamu hiyo itazinduliwa rasmi katika Ukumbi wa Songea Club Tarehe 1,7,2012 majira ya alasiri

MWAKYEMBE ALIPUKA TENA NA AANIKA MADUDU YALIYOMNG'OA MKURUGENZI ATC



Na Nasra Abdallah

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harison Mwakyembe, ameendelea kuwasha moto ndani ya Shirika la Ndege (ATCL) ambapo jana aliweka bayana sababu kadhaa za kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Paul Chizi.

Akizungumza na wafanyakazi wa shirika hilo katika karakana ya uwanja wa ndege jijini Dar es Salaam, Mwakyembe alisema kamwe hawezi kufanya kazi na watendaji wabovu na kuwataka wale walioumizwa na maamuzi yake kuacha kazi mara moja.

Huku akionyesha kukasirika, waziri huyo aliapa kuendelea kufukuza watendaji wengine zaidi watakaobainika kwenda kinyume na sheria.
Akitaja sababu zilizomwondoa Chizi, alisema kuwa uteuzi wake haukuzingatia tarartibu za utumishi wa umma.

“Chizi katika ripoti yake ya uzoefu wa kazi inaonekana kuwa alishastaafu kwa mujibu wa sheria ambapo kwa wafanyakazi wa aina yake kuna taratibu za kuwaajiri, hivyo anatakiwa azifuate ili kuajiriwa tena,” alisema.

Mbali na hilo, sababu nyingine iliyomponza mkurugenzi huyo ni kuingia mkataba wa kukodi ndege bila ridhaa ya serikali wala wizara husika.
Hata hivyo, Dk. Mwakyembe alipotakiwa aeleze kwa nini mkurugenzi huyo alifanya hivyo, alisema anaogopa kusema kwani huenda akazidi kuibua mjadala zaidi katika taifa.

“Inasikitisha sana kuona kuwa ilifika mahali watu wakaona shirika ni mali yao na kufanya maamuzi vile wanavyotaka huku wakisahau kwamba wananchi wanaliangalia shirika hilo linavyouawa,” alisema.

Alisema kuwa serikali mbali na kutoridhia pia ukodishwaji huo haukufuata taratibu za manunuzi ya umma kwani ndege hiyo ilinunuliwa nchini Liberia ambako bidhaa zote chakavu ‘mikweche’ kama baiskeli, pikipiki na ndege zimekuwa zikipelekwa huko na nchi zilizoendelea.

Alieleza kukerwa na kitendo cha watendaji wa shirika hilo kujinunulia magari ya kifahari wakati serikali ilitoa fedha ili shirika lifufuke.

“Maana inashangaza iweje idara na kampuni ndogo zinaweza kujiendesha na kusimama zenyewe lakini ATCL imekuwa ikibebwa hadi leo pamoja na kuwa na wafanyakazi wazuri ambao wakienda kufanya kazi katika makampuni mengine wanafanya vizuri,” alihoji.

Alisema kuwa serikali inajua wako mawakala wa makampuni ya ndege binafsi, wanaodhani wataiua ATCL kumbe wanajiua wenyewe, na hivyo kuwaonya akisema kama bado wapo ni bora waondoke wenyewe kabla hajawaondosha.

Alisema yuko tayari kufikishwa mahakamani kwa ajili ya suala hilo kwani wanaofanya hivyo ni sawa na kuchezea sebuleni kwake.
Akifafanua zaidi madudu ndani ya ATCL,

 Mwakyembe alisema kuwa fedha za bima ya ndege iliyodondoka mkoani Kigoma takriban dola bilioni saba, tatu za awali zililipwa na iliagizwa ziingizwe katika akaunti ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma(CHC) lakini watendaji wakafanya kinyume.

“Watendaji hao hawakufanya hivyo na kuamua kuziingiza katika akaunti ya ATCL, ambapo kati ya fedha hizo tumekuta dola bilioni mbili na dola bilioni moja zilizosalia hazijulikani zilipopelekwa,” aliongeza.

Waziri huyo aligusia pia hatua ya baadhi ya maafisa kwenda nchini China na kukaa huko takriban siku 45 kwa ajili ya kusimamia sare za wafanyakazi, jambo ambalo alidai ni ufujaji wa fedha za umma kwa kugharamia sare moja dola 49,900.

Kuhusu ajira ndani ya ATCL, Dk. Mwakyembe alisema kuna waajiriwa wengi waliokwishastaafu na pia ajira mpya zilitolewa bila kufuata tararibu ikiwemo kutangaza nafasi zilizopo ili wenye sifa washindane.

Alisema kuwa badala yake watu wamekuwa wakipeana ajira hizo kwa kufahamina na kuacha wale walio na sifa, jambo alilodai kuwa walikuwa wameamua kufukuza menejimenti yote, lakini wakahisi wangekosa kumbukumbu za urushwaji ndege.

“Baada ya kupitia baadhi ya mafaili ya watendaji hao tulikuta mwenye afadhali ni Kaimu Mkurugenzi huyu niliyemteua, Kapteni Lusajo Lazaro,” alisema.
Aliwaonya wanaozusha kuwa ametumia ukabila kumteua mkurugenzi huyo, akidai kuwa amebebwa na sifa pamoja na uwezo wake kiutendaji.

Waziri huyo alisema kuwa wameunda tume ambayo anaamini itakuja na majibu mazuri yatakayoliwezesha shirika hilo kusonga mbele.
Aliwataka wafanyakazi waliobaki, kuchapa kazi ili kumrahisishia pale anapoomba fedha serikalini aeleweke na kuongeza kwamba tayari wameshakabidhiwa sh bilioni 4.9 kutoka hazina kwa ajili ya matengenezo ya ndege.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Shirika hilo aliahidi kuyafanyia kazi yale yote waziri huyo aliyowaagiza, na kutimiza malengo ndani ya miezi mitatu waliyopewa.

Kwa niaba ya wanafanyakazi hao, Nelson Kalinga, alisema kusuasua kwa ATCL kumechangiwa na serikali kutowasikiliza wafanyakazi, kwani tangu awali walipinga kununuliwa kwa ndege hiyo ya Air Bus, ambapo waliandamana na kuandika barua wizarani lakini hawakusikilizwa.