Na Gideon Mwakanosya, Songea
AFISA Mtendaji wa Kijiji cha Ngahokola kilichopo katika Kata ya Magagula Wilaya ya Songea Vijijini Mkoa wa Ruvuma Cremence Mbogoro (48) amekutwa amekufa kwa kujinyonga kwa kutumia shuka ambalo alikuwa amelifunga shingoni na kujining’iniza kwenye mti wa boriti wa paa la choo cha nyumba yake.
Akizungumza na Mwandishi wa mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ Gideon Mwakanosya Ofisini kwake kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Naftari Mantamba amesema kuwa tukio hilo limetokea octoba 18 majira ya saa nne asubuhi huko kwenye eneo la Choo cha nyumba yake.
Amesema kuwa inadaiwa siku hiyo ya tukio Mbogoro alikutwa akiwa ananing’inia juu kwenye paa la choo na mtu mmoja ambaye alikwenda kutaka kujisaidia akiwa amejinyonga kwa kutumia shuka ambalo alijifunga shingoni.
Amefafanua zaidi kuwa mtu huyo aliyekuwa ameomba kwenda kujisaidia baada ya kugundua tukio hilo alitoa taarifa kwa majirani ambao walifika kwenye eneo la tukio na kumkuta Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho Mbogoro akiwa ananing’inia chooni baada ya kujinyonga.
Ameelezwa zaidi kuwa baada ya tukio hilo kufahamika kwa majirani uongozi wa Serikali ya Kijiji cha Ngahokola ulitoa taarifa polisi juu ya tukio hilo ambapo askari polisi pamoja na daktari walifika kwenye eneo la tukio na kuukuta mwili wa Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho Mbogoro ukiwa unaning’inia baada ya kujinyonga kwa kutumia shuka ambalo alikuwa amejifunga shingoni na kujining’iniza kwenye boriti ya mti wa choo ambao ulikuwa umewekwa kwenye paa.
Mantamba ameeleza zaidi kuwa chanzo cha tukio hilo bado kinachunguzwa licha ya kuwa uchunguzi wa awali wa polisi umebaini kuwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ngahokola Mbogoro kabla hajafikia uamuzi wa kujiua kwa kujinyonga alikuwa akimlalamikia mwajiri wake kuwa kwanini anashindwa kumuhamisha kwenye Kijiji hicho kwakuwa hapo awali alikuwa ameomba kuhamia Kijiji cha Igawisenga ambako ndiyo nyumbani kwake alikozaliwa.
Hata hivyo uchunguzi huo pia umebaini kuwa Mbogoro akiwa kama Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho anadaiwa kuwa alikuwa amewachangisha wananchi fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja fedha ambazo idadi yake haifahamiki na zinasadikiwa kuwa zimeliwa jambo ambalo lilimfanya alazimike kumuomba mwajiri wake kuhama kwenye Kijiji hicho bila kuwa na mafanikio na polisi bado inaendelea kufanya upelelezi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
MWISHO