About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, May 11, 2012

WAANDISHI WAASWA KURIPOTI KIKAMILIFU ADHA YA UMEME MANISPAA YA SONGEA

                            
MAHINDI YAKIWA KWENYE KIWANDA CHA MTAZAMO KWA AJIRI YA KUSUBIRI UMEME ILI YAKOBOLEWE NA YASAGWE 




Na Stephano Mango, Songea
WAANDISHI wa Habari mkoani Ruvuma wametakiwa kutumia taaluma yao kikamilifu katika kuwaokoa wananchi wanaoteseka kutoka na adha wanazozipata kutokana na mgawo mkubwa wa umeme usiokuwa na kikomo unaoendelea kuwakabili katika Halmashauri ya Manspaa ya Songea
Wito huo umetolewa jana na Mkurugenzi wa kampuni ya Mtazamo Enterpress, Julius Mlawa wakati akizungumza na waandishi wa habari jana waliotembelea kiwanda cha kampuni hiyo kinachojishughulisha na ukoboaji nafaka, usagaji na uuzaji wa unga
Mlawa alisema kuwa waandishi wa habari ndio jukwaa la wananchi wanyonge ambao sauti zao hazisikiki vizuri kusemea licha ya kuendelea kuteseka na adha ya mgao mkubwa wa umeme unaowasababishia kupanda kwa gharama za maisha
Alisema kuwa mashine za kusaga nafaka ambazo zipo katika baadhi ya maeneo ya Manispaa hiyo zimeshindwa kutoa huduma kwa muda muafaka na kusababisha wananchi walio wengi kulazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma nje ya Manispaa ambako kuna mashine za kusaga nafaka zinazotumia mafuta ya Dizeli na kusababisha bei ya huduma hiyo kupanda mara mbili ikilinganishwa na awali
Alieleza kuwa kitendo cha shirika la umeme mkoani humu kushindwa kutoa huduma hiyo kwa wakati mbali ya kusababisha usumbufu kwao lakini kimekuwa kikiwakosesha mapato ambayo wanayatumia kulipa kodi kwenye mamlaka ya mapato Tanzania(TRA) kutokana na hasara zinazosababishwa na ukosefu wa umeme
Alifafanua zaidi katika kiwanda chake kuna wafanyakazi zaidi 30 ambao wanashinda kiwanda wakisubiri umeme ili waweze kufanya kazi bila mafanikio huku wakilipwa posho zao za kila siku bila kufanya kazi jambo linalosababisha hasara kubwa
Alieleza zaidi kuwa kutokana na ukosefu wa umeme ambao umekithiri katika manispaa ya Songea wafanyabiashara wengi wanashindwa kurejesha mikopo waliyokopa kwenye taasisi za fedha jambo ambalo ni hatari kwa biashara zao na jamii ambayo inanufaika na biashara hizo
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo huenda akalazimika kusitisha kwa muda kutoa huduma ya usagaji na ukoboaji wa nafaka kama hali hiyo ya ukosefu wa umeme wa uhakika haitafanyiwa kazi na shirika hilo la umeme mkoani humu kwa sababu mbali ya kukosa mapato lakini imekuwa ni usumbufu kwa wananchi ambao wanahitaji huduma hiyo.
Kwa upande wake Meneja wa shirika la umeme mkoa wa Ruvuma Mhandisi Monika Kebara alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na alisema hivi sasa huduma hiyo ya umeme inatolewa kwa mgawo kwa sababu uwezo wa ufuaji wa umeme umepungua sana kutokana na kuharibika kwa mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo Kibulang’oma mjini hapa.
Kebara alisema kituo hicho kina mashine saba za kuzalisha umeme lakini kwa hivi sasa ni mashine tatu ndizo zinazofanya kazi hiyo kwa kutoa Megawati 2.6 wakati mahitaji ni Megawati 5 hasa ikizingatiwa kuwa katika mji wa Songea shirika hilo lina wateja elfu kumi na mbili.
Alisema kuwa tayari jopo la mafundi kutoka Jijini Dar es Salaam limefika kwa ajiri ya ukarabati mkubwa wa mitambo hiyo na kwamba mwishoni mwa mwezi mei kutakuwa na umeme wa uhakika
MWISHO

KAGASHEKI:SIKUBALI KUNYONGWA

                           .MAIGE AKIRI KUPONZWA NA WATENDAJI



Na Asha Bani, Dar
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amesema hatokubali kuhukumiwa kufa kwa kunyongwa au kupigwa risasi kwa sababu ya madudu yatakayofanywa na watendaji wa wizara hiyo.

Kagasheki alisema wizara hiyo imechafuka kwa kiasi kikubwa na tuhuma za ubadhirifu wa hali ya juu umewafanya hata wabunge kupendekeza mtumishi wa serikali atakayebainika kuhujumu mali za nchi kuuawa kwa kunyongwa.

Akizungumza katika makabidhiano baina yake na aliyekuwa akishikilia wizara hiyo, Ezekiel Maige, waziri huyo mpya alisema wizara hiyo ina sura mbaya kwa nje kutokana na tuhuma za ufisadi wa kutisha unaofanywa na baadhi ya watendaji wake jambo lililosababisha katika kipindi cha utawala wa Rais Jakaya Kikwete kuongozwa na mawaziri watano.

Wizara hiyo imeongozwa na mawaziri Anthony Diallo, Prof. Jumanne Maghembe, Shamsa Mwangunga, Ezekiel Maige na sasa Kagasheki mwenyewe.

“Katika Bunge lililopita mbunge mmoja alitaka mawaziri wabadhirifu wanyongwe au wapigwe risasi mimi sitaki kufikia huko nitawanyonga wafanyakazi wabadhirifu kabla ya kunyongwa mimi; nasema hili kwa nia njema kabisa na sio kutisha watu,” alisema Kagasheki.

Alisema kutokana na uozo huo, wizara hiyo imebadilishwa jina na kuitwa ‘mali ya siri kubwa’ jambo ambalo si zuri kwa kuwa kila kitu kinatakiwa kufanyika kwa uwazi kwa maendeleo ya taifa.

Waziri huyo pia alisema Wizara ya Maliasili na Utalii inatakiwa kuchangia pato kubwa la taifa kupita wizara nyingine yoyote hata ile ya Nishati na Madini isingeweza kufikia lakini kwa sasa inachangia pato la taifa kwa asilimia 18 tu.

“Mimi nataka kufanya kazi kwa kushirikiana na sio kwa ugomvi: waziri haelewani na naibu wake; vurugu tupu. Hii inaondoa ufanisi katika kazi na kama naibu waziri na waziri wanashindwa kuelewana itasababisha hata watendaji wa ngazi ya chini kushindwa kuelewana pia,” alisema Kagasheki.

Alisema atafanya kazi kwa kuangalia pia changamoto mbalimbali katika sekta za wizara hiyo, ikiwa ni pamoja na kuangalia sekta ya wanyapori, misitu na sera nzima ya utalii na changamoto nyingine ikiwemo ya upungufu wa watumishi na kufuatilia kwa kina yanayozungumzwa katika hifadhi ya Ngorongoro.

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Lazaro Nyalandu, alisema kwa kushirikiana watahakikisha pato la wizara hiyo linakuwa kwa kasi, watalii wanaongezeka kwa kuutangaza utalii ndani na nje ya nchi.

Aidha alimtaka kila mfanyakazi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa moyo mmoja na kuhakikisha kuwa anaongeza uzalishaji wake.
Akikabidhi ofisi aliyekuwa waziri, Ezekiel Maige, aliwatahadharisha mawaziri hao kuwa macho kwa vile anajua aliondolewa kutokana na makosa ya baadhi ya watendaji wake wa chini.

Maige alidai kuwa katika wakati wake wa utendaji, alijitahidi sana kutumia akili na nguvu zake nyingi kuimarisha wizara hiyo, na kukiri kuwa kuna tuhuma za baadhi ya wafanyakazi wanaojihusisha na biashara za utalii.

Alidai kuwa baadhi ya wafanyakazi, akiwemo mtumishi mmoja mwandamizi ambaye kesi yake iko mahakamani, wamejitumbukiza katika biashara hizo, na kumtaka Kagasheni kupambana nalo.

Maige alidai wizara hiyo katika kutekeleza majukumu yake inakabiliwa na upungufu wa watumishi, ujangili, uvujaji wa mapato, ukosefu wa vitendea kazi na uchakavu wa miundombinu.

Nyingine ni utoroshwaji wa wanyamapori hai kupitia uwanja wa ndege wa Kilimanjaro, ambapo wizara ilisitisha biashara ya wanyapori hai sambamba na kuunda tume mbalimbali za kufanya uchunguzi kwa maofisa walioshiriki.

Waziri Maige aliahidi kushirikiana nao bega kwa bega katika kuendeleza yale aliyoanza kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na suala la uchimbaji urani katika pori la akiba la Selous.