About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, October 3, 2013

MASHINE ZA TRA ZAZUA BALAA, WENGINE WASHUSHIANA MKON'GOTO



Na Kenneth Ngelesi

WAFANYABIASHARA mkoani Mbeya wamezua kizaazaa wakigoma kufungua maduka wakipinga agizo la Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) linalowataka kununua mashine za kielektroniki kwa ajili ya kukatia risiti za wateja pindi wanapowauzia bidhaa.

Katika sokomoko hilo lililotokea jana na kusababisha taharuki kwa muda kadhaa, wafanyabiashara hao wanadai kuwa gharama za mashine zitolewe na serikali.

Eneo la Soko la Sido ambalo lina wafanyabiashara wengi na tegemeo katika uchumi wa Jiji la Mbeya, walifunga biashara zao kwa muda usiojulikana.

Kadhia hiyo inakuja siku moja tangu Mkuu wa Mkoa huu, Abbas Kandoro, akutane na viongozi wa wafanyabiashara kutoka Soko la Sido na kuwataka viongozi kuwataarifu wenzao wasitishe mkutano ambao walitaka kuufanya jana katika uwanja wa Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe.

Kandoro alifikia uamuzi wa kukutana na viongozi hao baada ya kupata taarifa kupitia gari la matangazo ambalo lilikuwa likipita na kuzunguka katikati ya jiji na kuwataka wafanyabiashara hao kufunga maduka na kufika mkutanoni ili kujadili suala zima la mashine hizo.

Taarifa zinadai kuwa baada ya Kandoro kusikia matanagzo hayo, aliliagiza Jeshi la Polisi kumkamata dereva wa gari hilo pamoja na Mwenyekiti wa Soko la Sido na kuwaweka rumande kwa muda usiojulikana.

Baada ya wawili hao kuwekwa ndani, lilitolewa agizo la kuzunguka tena mitaani kwa kutumia gari hilo ili kuwatangazia wafanyabiashara hao kuwa mkutano huo umesitishwa.

Uamuzi wa kusitisha mkutano huo ulipuuzwa na wafanyabiashara hao ambao jana waliendelea na maandilizi ikiwa ni kukodi gari jingine la matangazo kupita mitaani kuwahimiza wenzao kujitokeza kwa wingi. 

Hatua hiyo iliufanya uongozi wa mkoa kuwasambaza polisi mitaani kuzuia mkutano huo. Mabomu ya machozi na maji ya kuwasha vilitembezwa kwa wafanyabiashara hao ambao walikuwa wamekusanyika huku maduka yao yakiwa yamefungwa.

Mabomu hayo ya polisi yaliwaathiri wanafunzi wa Shule ya Msingi Kagera na kuwafanya wataharuki na kuanza kukimbia hovyo huku wengine wakizirai.

Kufuatia hali hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Ayoub Kiwanga, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilomba, Erasto Mwakaponda na Diwani wa kata hiyo, Dickson Mwakilasa, walikubaliana kuwakabidhi wanafunzi hao kwa wazazi wao waliofika shuleni hapo kuwajulia hali baada ya kupokea taarifa za kupigwa mabomu.

Wakizungumza na Tanzania Daima, wafanyabiashara hao walisema kuwa wanashindwa kuelewa nguvu kubwa ambayo inatumiwa na polisi wakati hakuna vurugu zozote katika eneo hilo.

Alex Oswald, kwa niaba ya wenzake alisema kuwa wao waliamua kufunga maduka kwa hiari yao na kwamba lengo la mkutano lilikuwa kutoa msimamo wa kuiomba serikali itoe mashine hizo bure.

Naye Peter Tweve, alisema kuwa kimsingi wao hawajagoma kutumia mashine hizo bali wanataka wawekewe bure, kwani si kila mfanyabiashara anaweza kuinunua mashine hiyo ambayo kwa sasa inauzwa kwa sh 800,000.

Alipotafutwa Kandoro kuelezea tukio hilo, aligoma akisema kuwa yupo katika kikao, pia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani, simu yake iliita bila kupokewa.

Wiki moja iliyopita, Mkurugenzi wa Elimu ya Kodi wa TRA, Richard Kayombo, alitoa taarifa kuwa wafanyabiashara wenye mapato ya zaidi ya sh 45,000 kwa siku wanapewa hadi Oktoba 14, mwaka huu wawe wamenunua mashine hizo.