About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Wednesday, November 30, 2011

WENGI WATEKETEA KWA UGONJWA WA MALARIA WILAYANI NYASA MKOANI RUVUMA

   Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Daniel Malekela
Na Thomas Lipuka,Songea
UGONJWA wa malaria katika vijiji  kumi vya tarafa ya Ruhuhu wilayani Nyasa mkoani Ruvuma,unatishia ustawi wa jamii kutokana na wananchi wengi kuugua na kupoteza maisha kila mwaka.
Mganga mkuu wa hospitali ya Lituhi Dk.Martin Ndunguru amesema  katika kipindi cha mwaka 2009/2010  jumla ya watu 130 walikufa kati yao watoto 93 wenye umri chini ya miaka mitano na watu wazima 37.
Amevitaja vijiji ambavyo vinakabiliwa na ugonjwa wa malaria katika tarafa ya Ruhuhu kuwa ni Lituhi, Litumbakuhamba, Ngingama,Tumbi,Mbaha,Lundu,Hinga,Mkili,Ngumbo,Yola,Liwundi, Mbuli,Liweta na Njomole.
Kwa mujibu wa Dk.Ndunguru  vifo vingi vinavyotokana na ugonjwa wa malaria vinasababisha na wagonjwa kupungukia damu na kuchelewesha kupelekwa kwenye vituo vya tiba,umbali kutoka katika kijiji husika hadi kituo cha tiba.
Mganga mkuu huyo wa hospitali ya Lituhi alisema tarafa hiyo ina vituo vichache vya tiba ambapo zahanati zipo katika vijiji vya Litumbakuhamba,Ngingama,Ndumbi,Lundo,Mbuli na Mkili ambako kuna kituo cha afya.
Hata alisema vituo hivyo vya tiba vinakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo ni upungufu wa madawa,watalaamu wa afya,miundombinu hafifu,vifaa hasa vya maabara na kituo cha afya cha Mkili  kukosa  benki ya damu hali ambayo inaleta usumbufu kwa wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu.
Wakazi wa vijiji vya Ngingama na Litumbakuhamba ambao ni Helumina Chawala,Martina Haule,Sophia Kayombo na Kalistus Mapunda wamedai kuwa  malaria ni ugonjwa ambao unawatesa siku hadi siku  na kwamba upungufu wa dawa kwenye zahanati na bei kubwa ya dawa za malaria kwenye maduka yamadawa  ni kikwazo.
Mganga wa zahanati ya kijiji cha Ndumbi Yohana Kanyanja amekiri malaria ni tishio kwa wakazi wa mwambao mwa ziwa Nyasa ambapo katika zahanati ya kijiji cha Ndumbi pekee kwa mwezi  hupokea zaidi ya wagonjwa  356 wengi wao wakiwa ni watoto chini ya miaka mitano.
Anabainisha kuwa katika kipindi cha mwaka 2009/2010 watoto chini ya umri wa miaka mitano wapatao 2460 waliugua malaria katika kijiji cha Ndumbi na watu wazima katika kipindi hicho walikuwa ni 1200.
Mganga wa kituo cha afya Mkili Thomas Magulilo anazitaja changamoto ambazo zinakikabili kituo hicho kuwa ni  kituo kukosa gari la wagonjwa, upungufu mkubwa wa watumishi ambapo kituo kina watumishi wane tu kati ya mahitaji ya watumishi 25 na kwamba kituo hakina vitendea kazi vya kutosha katika maabara.
“Kituo chetu hakina gari la wagonjwa ili kuwasafirisha wagonjwa wanaozidiwa  na kuwapeleka katika hospitali za Litembo,Liuli na Mbinga ambazo zipo zaidi ya kilometa 64 kutoka hapa,hivyo inawalazimu wananchi kuwabeba wagonjwa waliozidiwa kwenye machela au kwenye mtumbwi hali inayosababisha baadhi yao kufia njiani’’,alisema.
Hata hivyo amesema hatua mbalimbali kituo kinachukua ili kukabiliana na tatizo la ugonjwa wa malaria ikiwemo kutoa elimu ya kupambana na ugonjwa huo,kugawa vyandarua na kuwahamasisha wananchi kuua mazalia ya mbu  na kuhakikisha wagonjwa  wanamaliza dozi  ya malaria.
Andrew Niliwani ni mkazi wa kijiji cha Mkili anatoa ushuhuda kuwa kuna wagonjwa watatu wa malaria waliobebwa kwenye machela walifia njiani wakati wanapelekwa katika hospitali ya Litembo,wagonjwa hao walifia katika maeneo ya Ndandaghala,Nahande na Mbugu.
Mganga mkuu wa hopsitali ya Liuli Dk.Daniel Ndimbo anazitaja changamoto zinazoikabili hospitali hiyo kuwa ni upungufu wa mashine za kuchunguza damu ya malaria,upungufu wa vitanda 50 na upungufu mkubwa wa wauguzi.
 Mganga mkuu wa kituo cha afya Mbambabay Wenceslaus Socky  anaeleza kuwa dawa za malaria huwa hazifiki kwa wakati katika kituo hicho na kwamba hata kiwango kinachofika hakilingani na mahitaji ya maombi yao  hali inayosababisha upungufu wa dawa hizo kila mwezi
 Mganga mkuu wa mkoa wa Ruvuma Dk.Daniel Malecela amesema katika kukabiliana na ugonjwa wa malaria mwaka 2010 jumla ya watoto 246,927 walio chini ya umri wa miaka mitano wamepewa bure vyandarua vyenye dawa.
Dk. Malekela alisema kuwa walifanya sensa ya kutambua idadi ya kaya zinazohitaji vyandarau ambapo jumla ya vyandarua 274,687 vimeshasambazwa katika vijiji na mitaa 539 ya mkoa wa Ruvuma
Licha ya kugawa vyandarua vyenye dawa mkoa wa Ruvuma umeviwekea  dawa vyandarua vipatavyo 254,400 vinavyotumika katika kaya bila jamii kuchangia gharama zozote.
"Tumeamua kufanya kampeni hii kwani katika tafiti ya kitaifa iliyofanywa mwaka 2007/2008 inaonyesha kuwa ni kaya nne tu kati ya 10 zinatumia chandarua kimoja chenye dawa hii inaonyesha kuwa kaya nyingi katika jamii yetu hazitumii vyandarua vyenye dawa na hivyo kuwa katika hatari ya kuambukizwa ugonjwa wa malaria", alisema Dk. Malekela.
Aliendelea kusema kuwa takwimu za mkoa wa Ruvuma za mwaka 2008 zinaonyesha kuwa asilimia 55 ya wagonjwa wote waliopata huduma katika vituo vya kutolea huduma wenye umri chini ya miaka mitano waliugua ugonjwa wa malaria na vifo chini ya miaka mitano vilikuwa ni asilimia 56 ya vifo vyote vilivyotolewa taarifa.
Ugonjwa wa malaria unashika nafasi ya kwanza katika mkoa wa Ruvuma kwa kusababisha vifo  kwa kiwango cha asilimia 23.9. Takwimu za mwaka 2004  hadi 2008 zinaonyesha kuwa  asilimia 50.3 ya wagonjwa wote wa malaria walikuwa ni watoto chini ya umri wa miaka mitano na zaidi ya miaka mitano walikuwa ni asilimia 49.7.

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ugonjwa wa malaria ndio unaoongoza kwa mahudhurio ya wagonjwa wanaofika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya, na kwamba matukio takriban 12 milioni ya malaria hutolewa taarifa.
 Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa watu kati ya 60,000 hadi 80,000 hupoteza maisha kila mwaka kwa ugonjwa  malaria ambapo asilimia 80 ya wanaofariki ni watoto wadogo wenye umri chini ya miaka mitano na mama wajawazito.  Kwa wastani, malaria humuua mtu mmoja katika kila dakika tano.

 Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ugonjwa wa Malaria wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, unalenga kupunguza idadi ya wagonjwa na vifo kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2013.  Kwa maneno mengine, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ina lengo la kuwapunguza wagonjwa wa malaria hadi kufikia milioni 6 na idadi ya vifo hadi kufikia kati ya 30,000  hadi 40,000 kwa mwaka ifikapo
mwaka 2013.