Vitanda ambavyo amekabidhi kwenye Kituo cha Afya Mkili na Zahanati ya Mbuli vikiwa vinatengenezwa kwa fundi
Magodoro na Vitanda vikiwa kwenye uwanja wa Kituo cha afya Mkili wilayani Nyasa kabla havijakabidhiwa
Wananchi waliojitokeza wakati Mbunge Kapteni Komba alipokuwa anakabidhi msaada huo kwa ajili ya kuimalisha sekta ya afya
Na Stephano Mango,Songea
MBUNGE wa Jimbo la Mbinga Magharibi wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Kapteni Mstaafu John Komba ametoa msaada wa vitanda,mito,shuka,chandarua na magodoro wenye thamani ya shilingi 3 milioni kwenye kituo cha Afya Mkili na Zahanati ya Kijiji cha Mbuli ili kuondokana na tatizo la wagonjwa kulala chini kwa kutumia mikeka
Akitoa misaada hiyo kwenye viwanja vya Kituo cha Afya Mkili Komba alisema kuwa kwa muda mrefu nilikuwa nafahamu kero ya wananchi wa maeneo hayo kuwa ni afya,maji,barabara,elimu na mawasiliano lakini kwa miaka mitano iliyopita nilichagua kushughulikia suala la elimu ,mawasiliano na barabara ambapo kwa sasa nashughulikia afya na maji
“Natambua matatizo yaliyopo kwenye sekta ya afya katika Jimbo la Mbinga Maghalibi hivyo kwa kuanzia natoa msaada wa shuka 24,magodoro 14,vyandarua 14,mito 14,vitanda 14 kwa ajili ya kituo cha afya cha Mkili na pia Vitanda 6,shuka 12,magodoro 6,Vyandalua 6,mito 6,na mzani wa kupimia watoto na wajawazito 1 kwenye Zahanati ya Kijiji cha Mbuli”alisema Komba
Komba alisema kuwa vituo vya afya na Zahanati karibu zote katika Wilaya hiyo hazina wataalamu,Vifaa Tiba na usafiri wa wagonjwa lakini tatizo hilo limeanza kushughulikiwa kwa kasi kubwa na nguvu zaidi kwa kuanzia kutoa vitu hivyo
Alisema kuwa natambua kuwa wananchi wamelalamikia kwa muda mrefu matatizo hayo hasa ya ukosefu wa vitanda na shuka kwani wanapotakiwa kulazwa hulazimika kutafuta mikeka na vitenge kwa ajili ya kujifunika wakati wa kulala huku wakipata mwanga wa vibatali kutokana na kukosa umeme
Kwa upande wake Diwani wa Kata hiyo Emmanuel Nchimbi akipokea msaada huo alisema kuwa kwa muda mrefu kituo hicho kilikuwa kinakabiliwa na matatizo hayo hivyo kwa msaada huo wananchi wanaopata huduma za matibabu watakuwa wameondokana na matatizo yaliyokuwa sugu katika kituo hicho
Naye Mganga wa Kituo hicho cha Afya Thomas Magulilo alieleza kuwa kituo chake cha afya kwa sasa kinakabiliwa na tatizo la watumishi wa kada ya afya,usafiri kwa wagonjwa na ukosefu wa maji kwani wagonjwa wamekuwa wakichota maji Ziwa nyasa na kuyatumia kwa kunywa,kuoga na shughuli zingine na kusababisha kuongezeka kwa magonjwa ya matumbo
Magulilo alisema kuwa kituo hicho kinahudumia wagonjwa kutoka Vijiji vya Yola,Luhundi,Ndonga na Mkili na wengine kutoka maeneo jilani hivyo kituo kimekuwa kikitoa huduma kwa wagonjwa wengi kuliko uwezo wake kwani vifaa tiba vipo vichache,wataalamu wa kada ya afya wapo wachache na kusababisha huduma inayotolewa kuwa duni
Alisema kuwa magonjwa sugu yanayosumbua wananchi wa maeneo hayo kuwa ni Malaria,upungufu wa damu,Minyoo,magonjwa yatokanayo na hali ya hewa,kuhala na kutapika pamoja na ugonjwa hatari wa ukimwi
Mwisho