Friday, April 19, 2013
ZAO LA UFUTA KUBADILI MAISHA YA WAKULIMA MKOA WA PWANI
Miongoni mwa wakulima wa ZAO la ufuta waliopo mkoani Ruvuma wakiwa kwenye Picha ya Pamoja
Na Stephano Mango
UFUTA ni zao lisilotiliwa maanani na wakulima wengi nchini kwa miaka mingi pamoja na uwingi wa faida zake kwa binadamu, lakini kwa miaka ya hivi karibuni, takribani sehamu zote ambako hali ya hewa imekuwa rafiki wa kulistawisha zao hilo, wakulima wameligeukia na kuanza kulima kwa kasi.
Zao la ufuta linatabiriwa kuwa zao kuu mbadala la kibiashara mkoani Pwani kutokana na mahitaji ya soko kuwa makubwa kwa sasa likifuatiwa na Muhogo pamoja na Embe.
Wilaya ya Rufiji ni mojawapo ya wilaya ambazo zinastawisha zao la ufuta kwa siku nyingi na siku za hivi karibuni kasi ya uzalishaji imeongezeka kutokana na upatikanaji wa uhakika wa soko la ufuta.
Katika msimu wa mwaka 2010 mpaka 2011, kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya hiyo Nurdin Babu. zao la ufuta liliiingizia mapato halimashauri ya wilaya ya Rufiji kiasi cha shilingi milioni sitini (60,000,000/=), hivyo kuongoza katika kuiingizia halimashauri mapato kupitia vyanzo vyake vya mapato
Hata hivyo, Mkuu wa wilaya hiyo alisema kuwa ni lazima kujiwekea malengo ya kuzalisha walau kwa kuanzia tani elfu tano (5000) katika msimu ujao wa kilimo 2012/2013 kutoka tani za sasa 400 kwa mwaka na tani 280 mwaka 2005/06.
Utafiti uliofanywa na jarida la “MUVI – Nuru ya Mafanikio” umebaini kuwa tofauti na mazao mengine ya kibiashara yanayolimwa mkoa wa Pwani kama vile Embe, Nanasi na Muhogo ni kuwa zao la ufuta hususani wilayani Rufiji wanunuzi hununua likiwa bado shambani na kulipa pesa pale linapoanza kuvunwa na mteja ndiye anayepanga bei na sio mnunuzi.
Hali ya soko kwa zao la ufuta ni kuwa bei ya kilo moja ya ufuta imepanda toka Tshs500/= mwaka 2000 hadi Tshs 1500/= mwaka huu 2012 kwa kilo, na hivyo kuchochea uzalishaji wa zao la ufuta kwa wakulima, anaeleza mkufunzi wa mafunzo na Afisa Mazao wa Wilaya ya Rufiji Ndugu Bahinga.
Kwa mujibu wa tafiti iliyofanywa na Dkt.Elly Kafriti, kutoka katika kituo cha utafiti Naliendele mkoani Mtwara katika mazao ya mbegu za mafuta,zao la ufuta linaongoza kwa kulipatia taifa fedha nyingi za kigeni.Mwaka 2005 taifa lilipata zaidi ya shilingi bilioni 20 kutokana na mauzo ya tani 32,000 za ufuta nje ya nchi.
Nchini Tanzania zaidi ya asilimia 75% ya ufuta hulimwa katika mikoa ya kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma na katika mikoa hiyo ufuta ni zao la Pili la biashara baada ya Korosho. Mikoa mingine ni Tanga,Pwani na Morogoro.
Katika wilaya ya Rufiji Ufuta hulimwa ukanda wa juu yaani tarafa za kibiti,Kikale,Mohoro na Ukanda wa tambalale tarafa za Mkongo na Ikwiriri.
Inafahamika wazi kuwa mradi wa MUVI ni wa miaka saba (7) uliibuliwa na Serikali kupitia wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ambao unatekelezwa kwa mkopo wa Serikali toka Shirika la IFAD ambapo SIDO inatekeleza mradi huu kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.
Madhumuni ya mradi ni kumwezesha mjasiriamali mdogo wa kijijini awe mkulima, mfanyabiashara, msindikaji vyakula n.k ili aweze kujiongezea kipato katika shughuli zake na kupunguza umasikini. Hivyo basi mradi wa MUVI unalenga kutoa ajira kwa vijana toka familia masikini vijijini.
Ili kufanikisha hilo Afrikan Image imepewa jukumu la kusimamia utoaji huduma ya mawasiliano ya kibiashara vijijini kwa wajasiriamali wadogowadogo katika mikoa sita na Pwani ikiwemo.
Njia mbalimbali zimekuwa zikitumika kama kutengeneza na kurusha vipindi mbalimbali vya radio, kutengeneza machapisho mbalimbali, mbao za matangazo vijijini, taarifa za bei za mazao kwa njia ya simu na mtandao wa MUVI kwa lugha ya Kiswahili ili kuwezesha mawasiliano ya kibiashara kufanikiwa vijijini.
Hadi robo ya pili ya mwaka wa tatu wa uhai wa mradi, jumla ya vikundi 90 vya wajasiriamali vimefikiwa, wanaume wakiwa 803 na wanawake 775, machapisho mbalimbali yanayofikia zaidi ya 50 elfu yakiwemo ya maembe, mananasi, jarida la muvi, kalenda, alizeti, muhogo na mwongozo wa namna ya kutumia ubao wa matangazo kwa wajasiriamali vijijini,
Kwa kipindi cha miaka miwili ya uhai wa mradi katika wilaya tatu za mkoa wa Pwani, Mkuranga, Bagamoyo na Rufiji yamesambazwa vijijini na kutoa mchango mkubwa katika kubadili mazoea ya wakulima na hivyo kuongeza tija katika kilimo.
Afrikan Image wanatarajia kuzindua huduma ya mawasiliano kwa njia ya ujumbe mfupi ili kupata taarifa za masoko kwa mazao mbalimbali pamoja na kuanza kurusha vipindi vya radio ifikapo katika ya mwezi machi mwaka huu.
Ili kuweza kuongeza chachu ya ustawishaji wa zao hilo Serikali kupitia wizara ya viwanda, biashara na masoko, chini ya mradi wa MUVI mkoa wa Pwani, hivi karibuni waliendesha mafunzo kwa maafisa ugani ishirini (20) kutoka Kata mbali mbali za Wilaya ya Rufiji ambapo wamepatiwa mafunzo maalum ya kilimo bora cha zao la ufuta.
Mafunzo kwa maafisa ugani wa Kata na Vijiji ni muhimu katika kuleta ufanisi katika utekelzaji wa shughuli za kitaaluma kwa walengwa. Mradi umebaini ya kwamba kutoa mafunzo ya namna hii kutasaidia kueneza taaaluma ya kilimo bora kwa wakulima wadogo wadogo kwa urahisi kwa sababu maafisa ugani wanaishi pamoja na walengwa kila siku.
Ni rahisi kufikisha ujumbe kuliko kungoja taarifa za taaluma kuletwa na maafisa mradi walioko mbali na wakulima hao. Kwa kuzingatia fursa iliyopo sasa ya zao hilo, Elimu waliyoipata wataipeleka moja kwa moja kwa walengwa, ambao ni wakulima wadogowadogo walioko kwenye kata na vijiji husika.
Mafunzo hayo yamelenga kumuwezesha mkulima kupata taaluma na uelewa mzuri zaidi katika kilimo cha zao hili tofauti na wanavvoelewa sasa ili kuboresha uzalishaji kwa lengo la kuongeza mazao yaliyo bora yatakayowezesha kupata bei nzuri kwenye soko.
Nurdini Babu ni mkuu wa wilaya ya Rufiji na hapa anasisitiza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika mji mdogo wa Ikwiriri wilayani Rufiji, “Hili ni zao lenye faida kubwa kama utekelezaji wa taaluma ya uzalishaji utafuatwa kwa makini, ambalo ndiyo lengo kuu la mafunzo haya”, anasisitiza Babu.
Katika ziara ya kutathmini shughuli za mradi iliyofanywa na wafadhili wa mradi,yaani IFAD, ilipendekezwa kwamba zao lenye mzunguko mfupi linaloweza kuleta mafanikio ya kuongeza kipato kwa mkulima liongezwe kwenye mchakato wa uendelezaji wa mnyororo wa thamani sambamba na mazao ya muhogo na matunda yaliyopo sasa.
Ufuta ulichaguliwa katika ushindani na mazao mengine kama, mahindi, mpunga na mtama mweupe. Mafunzo yanatolewa ili kilimo cha ufuta kianze mara moja katika msimu huu.
Zao la ufuta sio zao geni machoni mwa wakulima waliowengi mkoani Pwani, kwa vile uzalishaji wake hautakuwa mgumu hasa ikizingatiwa kwamba soko la kueleweka lipo na pia ni endelevu.
Pendekezo la kujumuisha zao hili pamoja na mazao ya muhogo na matunda unatokana na faida yake kuwa kubwa katika kuongeza kipato kwa mkulima kwa muda mfupi tofauti na mazao ya muhogo na matunda.
Mjadala mkali wa jinsi zao la ufuta linavyoweza kuendelezwa na kumkomboa mkulima sambamba na fursa za soko zinazolizunguka zao hilo ulitawala kwa muda wa siku tano za mafunzo maalumu kuhusu kilimo bora cha ufuta, uliowashirikisha maafisa ugani zaidi ya ishirini na wadau mbalimbali wa zao la ufuta wilayani Rufiji.
Katika mafunzo hayo ya maafisa ugani, wamejifunza kanuni za kilimo bora cha zao la ufuta, kuanzia uchaguzi wa mbegu bora, utayarishaji wa shamba, udhiti wa mgonjwa na wadudu, utunzaji wa shamba na uhifadhi wa mazao baada ya kuvuna pia na usafirishaji.
Nchini Tanzania zaidi ya asilimia 75% ya ufuta hulimwa katika mikoa ya kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma na katika mikoa hiyo ufuta ni zao la Pili la biashara baada ya Korosho.
Mikoa mingine ni Tanga,Pwani na Morogoro. Katika wilaya ya Rufiji Ufuta hulimwa ukanda wa juu yaani tarafa za kibiti,Kikale,Mohoro na Ukanda wa tambalale tarafa za Mkongo na Ikwiriri.
Subscribe to:
Posts (Atom)