About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Monday, November 14, 2011

NBC WATAMBA KUICHARAZA BAKORA CRDB KATIKA MECHI YA KIRAFIKI

             Nahodha wa Timu ya NBC Emmanuel Ntobi akizungumza na waandishi wa habari
Na Stephano Mango,Songea
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) tawi la Songea wametamba kuwanyeshea mvua ya magori watani wao wa jadi Benki CRDB katika mechi ya kirafiki inayotarajiwa kuchezwa Novemba 20 mwaka huu katika uwanja wa Majimaji
Akizungumza na Waandishi wa habari jana kwenye viwanja vya Makumbusho ya Taifa ya Majiamaji Songea Nahodha wa timu ya NBC Songea  Emmanuel  Ntobi alisema maandalizi ya mechi hiyo yamekamilika kwani wachezaji wote wana ari nzuri wanaendelea na mazoezi  kwa ajili ya mechi hiyo ya aina yake
Ntobi alisema kuwa lengo mechi hiyo ni kukuza urafiki,ujirani na undugu kati ya taasisi za kifedha na wateja wao kiujumla kwani muda mwingi wamekuwa wakikutana katika shuguli za kibenki tu na kufanya wateja wasifurahi  pamoja na wafanyakazi wa taasisi za kibenki
Alisema kuwa lengo jingine ni kujenga afya njema za wafanyakazi wa taasisi hizo za kifedha kwani michezo licha ya kuwaweka watu pamoja pia ni nguzo muhimu ya kujenga afya stahiki kwa binadamu yoyote
Alisema kuwa siku hiyo ni muhimu sana kwa kutengeneza na kudumisha mtandao baina ya wateja na maafisa wa taasisi hizo za benki na kwamba kutakuwa na burudani mbalimbali zitakazoporomoshwa na maafisa wa benki hizo muhimu kibiashara nchini
Alifafanua kuwa mechi hiyo ya kirafiki ni hatua muhimu ya kuendelea na mipango stahiki ya kuboresha shughuli za kibenki na wateja wa taasisi za kifedha ndani ya mkoa na nje ya mkoa ili waweze kufaidi huduma za taasisi hizo kikamilifu na kukuza mahusiano
Nahodha huyo Ntobi alisema kuwa baada ya mechi hiyo kukamilika kutakuwa na programu nyingine mbalimbali za ujrlani mwema ikiwa pamoja na midaharo kuhusu thamani ya shilingi ya Tanzania na kudorora kwa uchumi wake
Alieleza zaidi kuwa katika mechi hiyo ya aina yake mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Meneja wa Kampuni ya Tigo Mkoa wa Ruvuma  Wilfred Nestory na kwamba wateja wa taasisi za fedha na wapenzi wa soka wanapaswa kuhudhuria mechi hiyo muhimu
MWISHO

HAYA NDIYO YALIYOJIRI KATIKA UZINDUZI WA MRADI WA KISASA NA WA AINA YAKE WA UPIMAJI WA VIWANJA 18000 KATIKA KATA YA MSHANGANO

 Afisa Mtendaji wa kata ya Mshangano Stan Kibiki akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa upimaji wa viwanja 18000 wakati wa uzinduzi
 Diwani wa Kata ya Mshangano Faustine Mhagama akizungumza siku ya uzinduzi
 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ardhi Plan Gombo Samandito akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa mradi wa upimaji wa viwanja 18000 katika kata ya Mshangano
Sehemu ya mradi wa upimaji viwanja 18000 linavyoonekana katika eneo la Beroya kata ya Mshangano

MRADI WA UPIMAJI VIWANJA 18000 WAZINDURIWA KWA MBWEMBWE MBALIMBALI KATIKA ENEO LA BEROYA KATA YA MSHANGANO

 Mgeni Rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati za Huduza za Uchumi na Jamii katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Genfrida Haule wa tatu toka kushoto ambaye alimwakilisha Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Charles Mhagama akizindua mradi wa upimaji wa viwanja 18000 katika eneo la kata ya Mshangano kwa kutumia Kampuni ya Ardhi Plan huku akishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali
Mgeni rasmi Genfrida Haule akikagua barabara iliyochimbwa na wananchi wa Kta ya Mshangano ndani ya eneo la mradi wa upimaji wa viwanja huku akisindikizwa na viongozi mbalimbali wa chama na Serikali katika Manispaa ya Songea
 Mgeni Rasmi Genfrida Haule akiwahutubia wananchi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa mradi wa kisasa na wa aina yake wa upimaji wa viwanja 18000
 Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali wakisikiliza hotuba ya ufunguzi wa mradi wa upimaji wa viwanja iliyokuwa ikitolewa na mgeni rasmi Genfrida Haule
Sehemu ya barabara iliyochongwa na wananchi kwa kupata ujira wa kulipwa Tshs 5000 kwa kila mmoja kwenye eneo la mradi

MRADI WA UPIMAJI VIWANJA 18000 SONGEA KUWAKOMBOA WANANCHI KIUCHUMI
Na Stephano Mango,Songea
IMEDHIHIRIKA kuwa tatizo la makazi holela ambalo limeshamiri nchini limetokana na kutokuwa makini katika mipango miji na ukosefu wa wataalamu wa mipango miji wenye ubunifu na kusababisha adha kubwa kwa wananchi kutokana na wananchi kuvamia maeneo mengi na kujenga holela
Na kusababisha maeneo hayo  mengi ya aina hiyo kukosa miundombinu ya maji safi na maji taka,barabara na nishati ya umeme na kufanya mikakati mbalimbali ya maendeleo  kutofikiwa kikamilifu,jambo ambalo linawezekana kuepukwa ikiwa kila mtu atatimiza wajibu wake kwa kukomesha ujenzi wa makazi holela
Novemba  19 mwaka 2011 nilibahatika kuhudhuria uzinduzi wa mradi wa kisasa  na wa aina yake ambao haujawahi kutokea tangu nchi ipate uhuru wake mwaka 1961 wa upimaji wa viwanja 18,000 katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Mradi huo umezinduriwa katika kata ya Mshangano yenye mitaa  mitano ya Namanyigu,Mitendewawa,Mhumbezi,Chandarua na Mshangano yenye jumla ya kaya 1508 zenye wakazi 7540 ikiwa wanaume 3196 na wanawake 4344
Ambapo wakazi wa kata hiyo kama walivyo wakazi wa kata zingine 20 zilizopo kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Songea wanajishughulisha na kilimo,ufugaji,na biashara ndogondogo katika  kujitafutia kipato cha maisha yao,
Mgeni rasmi katika uzinduzi wa upimaji wa viwanja hivyo alikuwa Mshahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Charles Mhagama ambaye aliwakilishwa na Mwenyekiti wa Kamati za Huduma za Uchumi na Jamii wa Manispaa hiyo Genfrida Haule
Akizindua mradi huo wa upimaji viwanja hivyo  Haule alisema kuwa  Suala la upimaji viwanja ni hatua kubwa ya maendeleo kwa kuwa baada ya upimaji miundombinu ya maji na umeme itakuja na wananchi wameongeza kipato kwa kuweza kukopa  na kuendesha miradi kupitia viwanja  na nyumba zao huku viwanja vikipandishwa thamani
“Mradi huo utawainua kiuchumi wananchi wa Kata ya Mshangano kwa sababu wataweza kukopaa kupitia makazi yao  na kwamba wataweza kuishi katika makazi bora yaliyopimwa na kufanya mji wa Mshangano kuwa wa kisasa zaidi kuliko maeneo mengine ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea”alisema Haule
Akielezea historia ya Mradi huo Afisa Mtendaji wa Kata ya Mshangano Stan Kibiki alisema kuwa mradi huo wa upimaji wa viwanja kwa kutumia Kampuni uliibuliwa na wananchi wenyewe baada ya kuona wanakaa na kuishi katika makazi holela yasiyopimwa kwa muda mrefu
Kibiki alisema kuwa kwa muda wa miaka mingi wananchi wa kata hii wamekuwa wakipeleka maombi Halmashauri ya kuomba kupimiwa maeneo yao bila mafanikio kutokana na Halmashauri kukosa uwezo wa kifedha
“Mwaka 2010 kata yetu ilibahatika kupata mradi wa upimaji wa viwanja ilibahatika kupata mradi wa upimaji viwanja wa Halmashauri lakini bahati mbaya fedha yenyewe ilikuwa kidogo kwani waliweza  kupima viwanja 347 katika mtaa wa Namanyigu eneo dogo mashambani hivyo tatizo la wananchi kuishi katika makazi holela lilibaki palepale”alisema Kibiki
Alisema kuwa wananchi  kwa kushirikiana na viongozi wao katika kutatua tatizo hili waliamua kutafuta njia mbadala ambayo kwa kutumia sheria namba 8 ya Mipango Miji ya 2007 walitafuta Kampuni ya Ardhi Plan ya Jijini Dar Es Salaam ili iweze kuwapimia viwanja katika maeneo yao
Alieleza kuwa baada ya kuipata Kampuni hiyo makubaliano yakawa malipo ni ardhi kwa ardhi yaani wanapima ardhi wanalipwa ardhi kwa asilimia za kwamba mwananchi anapata 60% ya ardhi iliyopimwa na Kampuni inapata 40% ya ardhi iliyopimwa
Alifafanua kuwa asilimia 40% inayotolewa kwa Kampuni inatumika katika kuandaa michoro ya ubunifu wa mipango Miji (10%),kupima viwanja (10%)kuchonga barabara (10%) na faida ya Kampuni (10%) na kwamba mradi huu hauhusishi malipo ya fidia yoyote hii ni kwa makubaliano ya wananchi wenyewe na itakuwa kwa kusogezana
Afisa huyo alisema kuwa maeneo ya umma kama vile soko,shule,zahanati ,makaburi,stendi,msikiti,kanisa na maeneo ya wazi(open space)  yatatolewa bure katika mradi huo na kufanywa kuwa mradi wa kwanza kuibuliwa na wananchi wenyewe kwa kuitumia Kampuni ya Ardhi Plan kupanga mji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea
Alieleza kuwa gharama za mradi huo zinatolewa na wananchi wenyewe kwa kutoa ardhi badala ya kusubiri  Serikali mpaka ipate uwezo wa kifedha ambapo kwa wale wenye maeneo madogo yaani kiwanja kimoja mpaka viwili wanatozwa gharama ya fedha shilingi laki moja(100,000/=) kwa kiwanja kimoja na laki mbili(200,000) kwa viwanja viwili kama gharama za upimaji
Kibiki alisema kuwa mitaa ambayo  michoro yake imekamilika ni Mshangano,Namanyigu, na Mitendewawa yenye jumla ya viwanja elfu kumi na nane (18,000/=) ambapo mitaa mingine itafuata baadaye
“Mchoro ambao tayari mawe yameshapandwa ni mchoro namba 9 ujulikanao kama Beroya na sasa wananchi wanaendelea na uchongaji wa barabara mchoro ambao una jumla ya viwanja 800”alisema Kibiki
Alisema kuwa mradi huo umesifiwa na viongozi wengi na wanaharakati mbalimbali wa masuala ya ardhi na maendeleo ya wananchi wanyonge kwani wamefanikiwa kupata maeneo yaliyopimwa na kuthaminiwa kwa ajili ya makazi yao na kuondokana na makazi holela
“Tunaomba wananchi wa maeneo mengine wenye matatizo kama yetu watuunge mkono wafanye kama tulivyofanya sisi kwani watapata maisha bora kwani thamani ya ardhi yao itapanda na kuwa na thamani kubwa”alisema
Alieleza zaidi kuwa huduma za jamii kama maji ya bomba,umeme,barabara na miundombinu mingine itawafikia kama ambavyo wananchi wa kata ya Mshangano wanavyotegemea kupata mara baada ya mradi kukamilika
Kibiki alisema kuwa katika mradi huo wananchi watapata faida nyingi ikiwemo ya ajira kuanzia hatua ya kupima viwanja kwani mchoro mmoja umetoa ajira kwa watu 40 ambao wamekuwa wanalipwa  Tshs 4000/= kwa kutwa moja na kwamba kwa michoro 23 itatoa ajira kwa watu 920
Alifafanua kuwa kwenye uchongaji wa barabara mchoro mmoja umetoa ajira kwa watu 80 ambapo kila mmoja analipwa Tshs 5000/= kwa kutwa hivyo michoro 23 itatoa ajira kwa watu 1840 ambapo jumla ya michoro yote 23 wananchi watakao kuwa wamepata ajira kwenye upimaji na kuchonga barabara ni watu 2760 wanawake na wanaume
Alieleza jumla ya fedha watakayokuwa wanapata wananchi wa kata hiyo kwenye upimaji wa viwanja ni 920X4000=3680,000/= na kwenye uchongaji wa barabara 1840x5000=9,200,000/= na kufanya jumla ya fedha yote kuwa ni Tshs 12,880,000/= kwa siku
Alifafanua kuwa wafanyakazi hao watatoka ndani ya kata ya Mshangano ambapo mradi unatekelezwa kwani hiyo inaweza kuwasaidia sana wananchi kujikimu kimaisha na kumudu kununua pembejeo za kilimo katika msimu huu na hivyo kuzalisha mazao kwa wingi
Naye  Diwani wa Kata ya Mshangano Faustine Mhagama akizungumza kwenye uzinduzi huo alisema kuwa mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe hivyo kwa kuwa mradi huo una manufaa kwa wananchi wake umekuwa ukipigwa sana mawe,lakini hata hivyo anasema atasimamaimara kupigania haki za wananchi wake.
Anasema kuwa  kwa mradi huo wananchi wamenufaika kwa kuweza  kuuza viwanja vyao kwa bei kubwa lakini pia Halmashauri imepunguziwa gharama  ya kulipa fidia ambayo mara nyingi imekuwa ikichelewa kulipa au kushindwa kulipa na kuzua malalamiko na migogoro kwa wananchi
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Ardhi Plan inayopima viwanja hivyo Gombo Samandito anasema kuwa Mradi huo ni wa  aina yake hapa Nchini na kwamba hakujawahi kuwa na mradi kama ule wa kupima viwanja 18,000 kwa muda mfupi tangu nchi ipate uhuru na kwamba dhamira yao ni kuona wananchi wakiishi katika makazi bora.
Samandito alisema kuwa mradi huo umeisaidia sana Serikali  kwani umeipunguza tatizo la kushindwa kupanga mji kutokana na ukosefu wa fedha za kugharamia mipango stahiki ya makazi bora kwani wananchi wa Mshangano wamethubutu kupanga mji kwa gharama zao jambo ambalo halijawahi kutokea kwa wananchi kupima viwanja vingi kiasi hicho kwa gharama zao
Mwandishi wa Makala
Anapatikana Simu 0755-335051/0715-335051/0784-335051/0778-335051
Barua pepe;stephano12mango@yahoo.com

WANANCHI SONGEA KUPIMIWA VIWANJA 18,000 KUONDOKANA NA MAKAZI HOLELA

 Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ardhi Plan Gombo Samandito akiwaonyeshwa wananchi RAMANI zilizopitishwa na Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya upimaji wa viwanja kata ya Mshangano
Na Joseph Mwambije,Songea
HALMASHAURI ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma imezindua mradi wa upimaji viwanja zaidi ya 18,000 unaofanywa na Kampuni binafsi ya Ardhi Plan Limited  kwenye Kata ya Mshangano baada ya kuibuliwa na wananchi wenyewe baada ya kuona  wanaishi katika makazi holela kwa muda mrefu.
Mradi huo umezinduliwa juzi na Meya wa Manispaa ya Songea Charles Mhagama aliyewakilishwa na Mwenyekiti wa huduma za jamii na elimu wa Manispaa hiyo  Genifrida Haule aliyekata utepe kuzindua mradi huo.
Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo Haule alisema Mradi huo utawainua kiuchumi wananchi wa Kata ya Mshangano kwa sababu wataweza kukopaa kupitia makazi yao  na kwamba wataweza kuishi katika makazi bora,
‘Suala la upimaji viwanja ni hatua kubwa ya maendeleo kwa kuwa baada ya upimaji miundombinu ya maji na umeme itakuja na wananchi wameongeza kipato kwa kuweza kukopa  na kuendesha miradi kupitia viwanja vyao na nyumba zao huku viwanja vikipandishwa thamani’alisema.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa  Mradi huo Afisa Mtendaji wa Kata ya Mshangano Stan Kibiki alisema Kata hiyo ina Kaya 1508 zenye wakazi 7540  na mitaa mitano ya Mshangano,Namanyigu,Chandarua,Mitendewawa na  Muhumbezi.
Alisema kuwa wananchi baada ya kuona kwa muda mrefu wanakaa na kuishi katika makazi holela yasiyopimwa wakaamua kuibua Mradi wa upimaji viwanja hasa baada ya kupeleka maombi ya kupimiwa viwanja   Halmashauri lakini ilishindwa kuwapimia  kwa kile ilichodai kuwa haina fedha.
“Mwaka 2010 Kata yetu ilipata bahati ya kupata mradi wa upimaji viwanja  ulioendeshwa na Manispaa ya Songea lakini fedha ilikuwa kidogo na hivyo waliweza kupima viwanja 347 tu katika Mtaa mmoja wa Namanyigu katika eneo dogo na hivyo tatizo la wananchi kuishi katika makazi holela likabaki palepale’alisema katika taarifa hiyo.
Alisema kuwa wananchi katika kutatua tatizo hilo kwa kushirikiana na viongozi wao waliamua kutafuta njia mbadala kwa kutumia sheria namba 8 ya  ya mipango miji ya mwaka 2007 walitafuta Kampuni ya Ardhi Plan Limitedya Dares-salaam ili iweze kuwapimia viwanja katika maeneo yao.
Alisema Mitaa ambayo michoro yake imekamlika ni  Mshangano,Namanyigu, na Mitendewawa  yenye jumla ya viwanja 18,000 na mitaa mingine itafuata baadaye na kufafanua kuwa mchoro namba 9 wa Beroya wenye viwanja 800 umekamilika na kazi ya kuchonga barabara inaendelea.
Afisa Mtendaji huyo alisema  mradi huo umesaidia kutoa ajira kwa wananchi kwa kuwa mchoro mmoja umetoa ajira kwa wananchi 40 ambao walikuwa wanalipwa sh. 4000 kwa kutwa na kwamba michoro23 ya mradi huo itatoa ajira 920.
Alisema katika uchongajio barabara mchoro mmoja unatoa ajira kwa watu 80 ambapo kila mmoja analipwea sh. 5000 na kwamba wananchi 2760 wanawake na wanaume watakuwa wamepata ajira katika zoezi la uchongaji wa barabara.
Kwa upande wake  Mkurugenzi wa Kampuni hiyo inayopima viwanja hivyo Gombo Samandito anasema kuwa Mradi huo ni wa  aina yake hapa Nchini na kwamba hakujawahi kuwa na mradi kama ule wa kupima viwanja 18,000 kwa muda mfupi tangu nchi ipate uhuru na kwamba dhamira yao ni kuona wananchi wakiishi katika makazi bora.
Naye Diwani wa Kata hiyo  Faustin Mhagama anasema  mti wenye matunda ndio unaopigwa mawe hivyo kwa kuwa mradi huo una manufaa kwa wananchi wake umekuwa ukipigwa sana mawe,lakini hata hivyo anasema atasimamaimara kupigania haki za wananchi wake.
Anasema kuwa  kwa mradi huo wananchi wamenufaika kwa kuweza  kuuza viwanja vyao kwa bei kubwa lakini pia Halmashauri imepunguziwa gharama  ya kulipa fidia ambayo mara nyingi imekuwa ikichelewa kulipa au kushindwa kulipa na kuzua malalamiko na migogoro kwa wananchi.
MWISHO