Na Gideon Mwakanosya, Songea
MTAMBO wa kufulia umeme jua (Sola) uliokuwa umefungwa kwenye Ofisi ya Shirika la Posta Tanzania ya Wilayani Mbinga wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni nne Mkoa wa Ruvuma inahofiwa kuwa umeondolewa katika mazingira tatanishi kwa madai kuwa kigogo mmoja mwandamizi wa Shirika hilo ameuhitaji kwa matumizi yake binafsi.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Shirika la Posta Mkoani Ruvuma ambao wameomba majina yao yahifadhiwe wameuambia mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com kuwa Mtambo huo wa kufulia umeme jua ulikuwa umefungwa kwenye Ofisi za Shirika hilo iliyopo Mbinga Mjini ambao ulikuwa ukisaidia kwa kiasi kikubwa shughuli mbalimbali ofisini hapo zikiwemo za mawasiliano pamoja na matumizi mengine ya kazi za kila siku ofisini hapo.
Wamesema kuwa jambo la kushangaza ni kuwa Meneja wa Shirika hilo la Posta Mkoani Ruvuma Rochus Asenga mwezi machi mwaka huu alikwenda Mbinga na kuung’oa mtambo huo ambao ulikuwa umefungwa kwenye ofisi za Posta Mbinga na kudai kuwa kwa vile Mbinga kuna Shirika la umeme Tanzania Tanesco mtambo huo unatarajiwa kuondolewa Mbinga na Kupelekwa Jijini Dar es Salaam ambako kuna kiongozi mmoja anauhitaji.
Wameeleza zaidi kuwa Mtambo huo wa kufulia umeme jua inadaiwa kuwa uliondolewa Mbinga bila kuwepo na maandishi ya aina yeyote na badala yake Asenga alieleza kwa mdomo kuwa Sola hiyo inahitajika mahali pengine Jijini Dar es Salaam kwa bosi wake.
Akizungumza na www.stephanomango.blogspot.com Meneja wa Shirika hilo Mkoani Ruvuma Rochus Asenga kuhusiana na kuuhamisha mtambo wa kufulia umeme (Sola) katika mazingira tatanishi alisema kuwa yeye siyo msemaji wa Shirika la Posta Tanzania ila alikiri kuwa Mbinga kulikuwa na mtambo wa umeme jua (Sola) ambao uliondolewa lakini kwasasa hawezi kusema lolote kwa vile yeye siyo msemaji wa Shirika hilo.
Naye Afisa Mwandamizi wa Shirika la Posta Tanzania Wilayani Mbinga Mbutolwe Mwakitalima alipohojiwa na mtandao huu kwa njia ya simu kuhusiana na mtambo wa umeme jua uliokuwa umefungwa kwenye Ofisi yake kwaajili ya matumizi mbalimbali ambao unadaiwa kuondolewa katika Mazingira tatanishi na kupelekwa kusikojulikana alisema kuwa ni kweli Meneja wake wa Mkoa Asenga mwezi machi mwaka huu majira ya saa za kazi alifika Ofisini kwake na kudai kuwa mtambo huo anauondoa na kuupeleka Makao makuu ya Shirika hilo Mkoani Ruvuma ambako baadae wataangalia ni wapi wataupeleka ukaendelee kutumika.
Mwakitalima alifafanua kuwa kwasasa hivi hawezi kufahamu mtambo huo wa kufulia umeme upo wapi wala hana sababu yeyote ya msingi kuulizia kwa vile Bosi wake aliuchukua na Wafanyakazi wengine wa Shirika hilo wakiwepo ila aliuchukua bila kuandikiana.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania Kanda ya Mbeya inayohusisha Mikoa ya Rukwa,Mbeya,Iringa na Ruvuma ambaye alijitambulisha kwa jina moja la Mlay aliuambia mtandao huu kwa njia ya simu kuwa Wafanyakazi wa Posta Songea kwa muda mrefu wamekuwa na malalamiko mengi kati yao na Menejimenti lakini suala la upotevu wa Sola iliyokuwa ikitumika Posta Mbinga Ofisi yake ilikuwa bado haijapata taarifa hizo lakini ameeleza kuwa atawasiliana na Menejimenti ya Mkoa huo ili afahamu zaidi juu ya taarifa ya Sola iliyokuwa imefungwa Mbinga kuwa imepelekwa wapi.
Hata hivyo www.stephanomango.blogspot.com iliwasiliana na Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Deus Mndeme na kumtaka atoe ufafanuzi juu ya Mtambo wa kufulia umeme jua uliokuwa umefungwa kwenye Ofisi ya Mbinga alieleza kuwa yeye mpaka sasa hafahamu lolote isipokuwa anachojua kuwa kwenye Ofisi ya Posta hakuna Sola iliyokuwa imenunuliwa na Shirika na kwamba amekanusha vikali uvumi unaodai kuwa mtambo huo umechukuliwa na baadhi ya vigogo Jijini Dare s Salaam kwa matumizi yao binafsi.
Mndeme amefafanua kuwa Shirika la Posta lina utaratibu maalumu ambao unafahamika kwa kila Mfanyakazi kuwa anapohamisha mali ya Shirika kutoka Ofisi fulani kwenda Ofisi nyingine ni lazima kuna taratibu zinazotakiwa kufanywa kwa kujaza fomu maalumu ambazo zinaonyesha mali hiyo inahamishwa na mahali inakopelekwa lakini kama utaratibu huo haukufuatwa basi hapo kuna utata.
Amesema kuwa kwa vile Shirika la Posta lina kitengo cha usalama hivyo suala hilo ataliwakilisha kwa Mkuu wa Idara ya usalama ili nao waweze kulifanyia kazi na kuweza kubaini mtambo huo wa umeme umehamishwa Mbinga na umepelekwa wapi au ni nani anayeutumia kwa hivi sasa na kwamba kama kweli kuna kigogo mmoja ameamua kuuchukua basi hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
MWISHO.