Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria
Na Mwandishi Wetu, Songea
WAKAZI wa Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma wakiwemo wamiliki wa mabasi yanayo safirisha abiria wameulalamikia uongozi wa Halmashauri ya Manspaa hiyo kutokana na kushindwa kuzifanyia ukarabati barabara pamoja na kituo kikuu cha mabasi ambacho kimekithili kuwa na ubovu ambao umesababisha kuwepo na mashimo mengi katikati ya kituo hicho na kupelekea magari kukwama wakati mvua zinaendelea kunyesha
Mtandao huu wa stephanomango.blogspot.com ulitembelea kituo hicho cha mabasi kwa lengo la kujionea hali halisi ya ubovu wa miundo mbinu kwenye eneo hilo ambalo lilikuwa limejaa tope wakati mvua zinaendelea kunyesha huku mabasi yaliyosheheni abiria yakiwa yametitia kwenye tope hilo.
Uharibifu huo ambao umechangia kwa kiasi kikubwa kujaa kwa tope na kusababisha wananchi na magari kupita kwa tabu na mengine kukwama kabisa kutokana na utelezi uliotokana na uongozi wa Halmashauri hiyo kuridhia kumwaga kifusi cha udongo wa mfinyaji katikati ya kituo hicho kwa madai kuwa wanafukia mashimo yaliyokithili kwenye eneo hilo jambo ambalo limeonekana kuwa ni kero kubwa kwa wakazi wa Songea wakiwemo abiria na wamiliki wa mabasi .
Hali hiyo ndiyo iliyopelekea watumiaji wa kituo hicho kutoa malalamiko yao kwa Halmashauri ya Manispaa ya Songea wakidai kilio chao cha kutengenezewa stendi hiyo kimekuwa ni cha muda mrefu na kitu cha kushangaza hakuna hatua zozote zinazo chukuliwa kwa ajiri ya kukinusuru kituo hicho ambacho kipo katikati ya Manispaa hiyo
Mmoja wa wakazi wa Manispaa ya Songea Lucas Haule alisema inashangaza kuona kituo hicho ambacho kimekuwa kikilalamikiwa kwa muda mrefu kutokana na miundo mbinu yake kuwa mibovu huku Halmashauri ikitoza ushuru mkubwa kwa magari yanayo ingia kwenye kituo hicho yakiwemo mabasi ya kusafirishia abiria .
Nae mmoja wa watumiaji wa kituo hicho cha mabasi Paulo Ndunguru alisema kuwa anashangazwa kuona kituo hicho kilicho kithiri mashimo kinatengenezwa kiholela bila kufuata utaalamu na kudai kwamba endapo kama ungetumika utaalamu yakinifu tatizo hilo la kukwama kwa magari katikati ya kituo lisingeweza kujitokeza .
Hata hivyo jitihada zilizofanywa na mtandao huu za kumpata mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Nachoa Zakaria ziligonga mwamba baada ya kutopatikana ofsini kwake ambapo Katibu muhutasi wake alieleza kuwa Mkurugenzi alikuwa kwenye vikao vya maandalizi ya mapokezi ya mwenge na maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru na kwamba simu yake ya kiganjani alipopigiwa mara tatu iliita bila kupokelewa.
MWISHO