About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, June 21, 2013

WATOTO WALILIA HAKI ZAO ZA KUISHI, KULINDWA NA KUHESHIMIWA



                              Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Eng, Stella Martin Manyanya ambaye pia ni Mbunge wa Vitimaalum Mkoa wa Ruvuma akizungumza na Watoto wa Wilaya ya Nyasa alipotembelea wilayani humo hivi karibuni

Na Gideon Mwakanosya ,Namtumbo

WATOTO wa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kukomesha vitendo vya ubakaji vinavyofanywa kwa watoto wadogo wilayani humo kwani tatizo hilo limeonesha kuwa kubwa ambapo katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu jumla ya watoto 14 walibakwa na kesi zao kuripotiwa katika kituo kikubwa cha Polisi cha Wilaya hiyo.

Wakisoma Risala ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu jana iliyofanyika Kiwilaya katika kijiji cha Hanga wilayani Namtumbo walisema kuwa pamoja na jitihada za Serikali na wadau mbalimbali za kukomesha vitendo vya unyanyasaji kwa watoto wadogo bado tatizo hilo ni kubwa kwa Wilaya ya Namtumbo.

Walieleza kuwa katika takwimu za miaka miwili iliyopita zinaonesha kuwa mwaka 2012 wanafunzi 16 waliacha shule kutokana na mimba na wanafunzi 151 kati ya hao wavulana 88 na wasichana 63 waliacha shule kwa utoro na mwaka 2013 wanafunzi 12 wa kike walipata ujauzito na kuacha shule huku wanafunzi 34 walikuwa watoro mwaka 2012 na mwaka 2013 wanafunzi 18 ambao waliripotiwa kuwa watoro.

Walisema kuwa tatizo la watoto kutumikishwa kazi za majumbani kama vile kazi za ndani na mashambani,kutumiwa na watu wazima kufanya biashara ndogo ndogo hata kama wanatakiwa kuwepo mashuleni bado limekuwa ni tatizo hivyo ni vyema kila mzazi akatambua kuwa kila mtoto ni wake na anahitaji malezi bora hasa kuwapatia elimu iliyo bora na itasaidia kupunguza tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.

Kwa Upande wake mgeni rasmi wa maadhimisho hayo Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alisema kuwa kila wananchi wakiwemo wazazi na walezi wanawajibu wa kuhakikisha kuwa watoto wao hawatumikishwi kazi za hatari na kazi zinazowazidi umri ili kupunguza tatizo la watoto kukimbilia mitaani na kujiingiza katika mambo mabaya ikiwemo madawa ya kulevya.

Alisema kuwa kutowajibika kwa wazazi na walezi katika kulea familia kunasababisha mambo mengi yasiyofaa ndani ya jamii ikiwemo utoro,mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari hivyo ni wajibu wa kila mzazi katika kuwafichua waharifu wanaowapa mimba wanafunzi ili vitendo hivyo vikomeshwe kabisa ndani ya Mkoa huo.

Aidha alisema kuwa wazazi na walezi watambue kuwa watoto wanahaki ya kulindwa, kukua,kuendelea kuishi na kushiriki kutoa mawazo ndani ya jamii lakini kuna baadhi ya wazazi a walezi watoto wanapohitaji huduma hupewa karipio kali na wakati mwingine kipigo pasipo sababu.

MWISHO.