Mganga Mkuu wa Mkoa Ruvuma Daniel Malekela
Na, Augustino Chindiye Tunduru
SERIKALI imeombwa kuvifuta vyuo ambavyo vimekuwa vikitoa elimu ya Uuguzi na Ukunga bila kuwa na usajili na kupelekea fani hiyo kuvamiwa na watu wasioiva kitaaluma ( Makanjanja) na kusababisha utoaji wa huduma kushuka.
Rai hiyo imetolewa na Wanachama wa Mkutano Mkuu wa 39 wa Chama cha Wauguzi na Wakunga (TANNA) wa Mkoa wa Ruvuma uliofanyika katika Ukumbi wa Kanisa la Bibilia mjini hapa.
Akifafanua taarifa hiyo Mwenyekiti wa Chama hicho Jordan Nchimbi alisema kuwa pamoja na vyuo hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza idadi ya watumishi wa kada hiyo, lakini pia kada hiyo imeonekana kutokuwa na maadili kutokana na kuvamiwa na kundi hilo ambalo uchunguzi unaonesha kutokuwa na maadili kutokana na kutosoma masomo yenye maelekezo ya kufuta mitaala wakati wa utumishi wao.
Sambamba na maombi hayo pia Wajumbe hao walibainisha baadhi ya vikwazo ambavyo vimekuwa vikiwakatisha tamaa wakati wa utendaji wao kuwa ni pamoja na ucheleweshaji wa upatikanaji wa haki zao kutoka hazina, makato ambayo hufanyika bila taarifa wala kupata ridhaa yao na kutokuwepo kwa usafiri kwa watumishi wa kada ya chini hasa wanaofanya kazi vijijini huku kukiwa na matishio ya kujeruhiwa na wanyama wakali.
Akiongea kwa niaba ya Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Dkt. Alex Kazula. Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya hiyo Dkt. Goerge Chiwango alitumia nafasi hiyo kuwaasa wanachama hao kutumia nafasi hiyo vizuri hasa wakati wa kujikumbusha Masomo mbalimbali pamoja na muda wa kubadilishana uzoefu kupitia mijadala.
Nao Muuguzi Mkuu wa Mkoa huo Nenedikter Ndumbaro, Katibu mwenezi wa TANNA Norbart Haule na Katibu wa Chama hicho Mkoa wa Ruvuma Paul Mtimba pamoja na mambo mengine waliwahiza wauguzi wote wa mkoa huo kujiunga na chama hicho ili waweze kupaza sauti zao kwa pamoja,
Walisema Chama hicho chenye wanachama 662 lakini takwimu za wanachama hai zinaonesha kuwa ni 490 tu, hali inayotishia uwepo utengano miongoni mwao na wakatumia nafasi hiyo kukemea tabia za wauguzi kutumia lugha za matusi kwa wateja ili kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza.
Akijibu kero za Wauguzi hao wakati akifungua Mkutano huo Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini Alhaji Mtutura Abdalah Mtutura, pamoja na mambo mengine aliwataka wakuu wa idara na viongozi waliopewa mamlaka ya kusimamia utendaji wa Shughuli za Serikali kutekeleza wajibu wao kwa haki ili kuondoa manung`uniko ya watumishi waliopo chini yao .
Aidha Mtutura pia alikemea tabia za viongozi na wakuu wa idara kuchukua hatua za kuwahamisha watumishi waliopo chini yao bila malipo hali ambayo imekuwa ikilisanbabishia Taifa Kero kubwa ya kudaiwa huku hali ikionesha kuwa hamisho nyingi hufanyika kwa hira za viongozi hao kutaka waabudiwe.
Kuhusu kero ya Malalamiko ya wauguzi hao kutolipwa malipo yao mbalimbali Alhaji Mtutura aliahidi kulifikisha suala hilo kwa Waziri mwenye dhamamna ili kulitafutia ufumbuzi wa kudumu zikiwa ni juhudi za kuboresha utoaji wa huduma.
Mwisho