Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma michael Kamuhanda
Na Gideon Mwakanosya, Songea
MTU mmoja amefariki dunia na wengine kumi wamejeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Dar Pori kwenda Mbinga kuacha njia na kupinduka katika eneo la barabara ya Mpepo maarufu kwa jina la babu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda amesema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 9 alasiri kwenye eneo hilo ambako gari lenye namba za usajili T537AUQ Aina ya Toyota Landcruser ambayo ilikuwa ikiendeshwa na Prosper Ndunguru ikiwa imesheheni mizigo pamoja an abiria iliacha njia na kupinduka.
Kamuhanda amemtaja aliyekufa kuwa ni Nikodem Ndunguru (45) Mkazi wa Mbinga Mjini na amewataja waliojeruhiwa vibaya kuwa ni dereva wa gari hilo Prosper Ndunguru Mkazi wa Mbinga, Immaculata Ndomba (19) Mkazi wa Songea Mjini na Lucy Martin Mkazi wa Furaha Store Mbinga ambao kwasasa wamelazwa katika hospitali ya Misheni ya Mbinga wakiendelea kupata matibabu.
Amewataja majeruhi wengine ambao kwasasa wamepelekwa katika hospitali ya Misheni Peramiho Wilaya ya Songea kuwa ni Rukia Jofrey (47) Mkazi wa Jijini Dar es Salaam,Rukia Myovela (50) Mkazi wa Songea Mjini,Magreth Ndomba (27) Mkazi wa Mbinga mjini,Peter John (84) Mkazi wa Manispaa ya Morogoro,Sara Mkinga ambaye ni mfanyabiashara kati ya Mbinga na Dar Pori,Asha Katau (37) Mkazi wa Mfaranyaki Songea na Simon Komba Mkazi wa Tanki la Maji Mbinga Mjini.
Kamuhanda amefafanua kuwa Nikodem alifariki dunia baada ya ajali hiyo kutokea wakati alipokuwa akipelekwa kwenye Zahanati ya Mpepo na majeruhi wengine walikimbizwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mbinga na Hospitali ya Misheni Peramiho ambako bado wanaendelea kupata matibabu na hali zao bado ni mbaya .
Ameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kwamba gari ilikuwa kwenye mwendo kasi ambao ulimsababishia dereva kushindwa kuumudu usukani kisha gari ikaacha njia na kupinduka.
MWISHO