About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, August 26, 2011

Mwenyekiti wa mtaa wa Mshangano Paulo Mangwe akisoma tamko la Wenyeviti wa mitaa mitatu ya kata ya Mshangano mbele ya waandishi wa habari la kumtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda awachukulie hatua za kuwafukuza kazi Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Zakaria Nachoa na Afisa Mipango Miji wa Manispaa hiyo Kastori Msigara kwa vitendo vyao vya kukwamisha maendeleo ya wananchi wa kata ya Mshangano,kushoto ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Mitendewala Bernado Mahinya




WANANCHI KUANDAMANA KUSHINIKIZA KUPIMIWA ARDHI, KUNG’OLEWA MKURUGENZI SONGEA

Na Stephano Mango,Songea

WANANCHI wa Kata ya Mshangano, Halmashauri ya Manispaa ya Songea wanatarajia kufanya maandamano makubwa  ya amani ya kumtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwang’oa  kazi Mkurungezi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria na , Afisa Mipango Miji wake Castory Msigala kwajili yakuwa kikwazo cha maendeleo ya wananchi.

Akisoma tamko la wenyeviti wa serikaili za mitaa wa kata ya Mshangano ambayo imekumbwa na mgogoro mzito wa ardhi, Mwenyekiti wa  serikali ya Mtaa wa Mshangano, Paul Mangwe alisema kuwa (kesho) leo wanataria kufqanya maandamano ya amani yatakayo anzia kwenye ofisi ya kata hiyo hadi kwa mkuu wa wilaya ya Songea Thomas ole Sabaya kumfikishia ujumbe wa kutaka kupewa kibali cha kupimiwa ardhi yao na kumuomba Waziri Mkuu kuwang’oa viongozi hao wawili ambao wamekuwa kikwazo kwa zoezi hilo.

“ Sisi wenyeviti wa serikali za mitaa ya Mitendewawa, Namanyigu na Mshangano tulishaomba kibali kwa OCD  wa Songea kumjulisha kuhusu maandamano ya amani, kibali tutapata na hata kama hakitapatikana wananchi wamedai lazima waandamane kesho(Leo),” alisema Mangwe.

Alisema ifahamike kuwa wananchi wa kata ya mshangano tangu walipo kutana Agosti 13 mwaka huu walimtaka  Mkurugenzi huyo awe amesaini michoro na kibali cha kuiruhusu Kampuni ya Ardhi Plan ltd  yenye Makao makuu Dar es Salaam ambayo imekwisha wahi kufanya kazi kama hiyo kwenye Kata ya Mwenge Mshindo mjini hapa iweze kuwapimia wananchi maeneo yao ambayo wamesitisha shughuli ya kuyaendeleza tangu Disemba 2010.

Katika taarifa hiyo Wenyeviti wa Mitaa wa Kata hiyo walisema kwakuwa Mkurugenzi Nachoa na Afisa Mipango Miji wake Msigala wamekaidi matakwa ya wananchi wenye ardhi wa kata ya Mshangano kushindwa kujibu barua ambazo walizipeleka za kutaka kupimiwa ardhi takribani miezi tisa sasa wameshindwa kumuelewa ni kitu gain anachotaka kutoka kwa wakazi wa kata hiyo.

“Tunapata mashaka makubwa na kukosa imani na Viongozi hao wawili(Nachoa na Msigala) kwani pamoja na kutokujibu barua zetu lakini mazingira yamejionyesha kuwa wao wana maslahi binafsi,” walisema wenyeviti hao katika mkutano na waandishi wa habari.

Hata hivyo, walisema wao wapo tayari kufa kuliko kuiachia ardhi ya wapiga kura wao waliowachagua mwaka 2009 katika uchaguzi wa serikali za mitaa kuwaletea maendeleo.

Walisema kuwa hawaoni mtu mwingine atakaye suluhisha mgogoro huu mkubwa uliodumu kipindi kirefu zaidi ya mtoto wa mkulima  Waziri Mkuu Mizengo Pinda mwenye uchungu na watu wanyonge hapa nchini.

Walisema wameshangazwa sana na viongozi wa serikali ya mkoa wa Ruvuma kulifumbia macho swala zito kama hili  na hivi sasa wameona wana mtu mmoja tu ambaye wanaamini ana ujasiri wa kumfikishia ujumbe waziri Mkuu na si mwingine bali ni DC wa Songea Thomas Ole Sabaya ambaye hata kama atasema hana mafuta ya kwenda na kurudi Dodoma wao wako tayari kuchanga nauli hiyo ilimradi Waziri Mkuu Pinda apate ujumbe huo wa kutaka kurasmishiwa makazi yao badala ya kujenga kiholela kwenye eneo la Manispaa.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamuhanda, alisema kibali cha maandamano hayo hakijakamilika kwakuwa hakijakidhi matakwa kama yale ya kuonyesha njia, muda na tarehe ya maandamano.

Kamuhanda amefafanua kuwa tatizo hilo ni kubwa na tayari linatarajiwa kupelekwa kwenye kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa ili kuangalia wapi chanzo cha kuendeleza mgogoro huo hadi watu wafikie hatua ya kutaka kuandamana.
Mwisho

Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Oley Sabaya


MADEREVA TAKSI SONGEA WAMCHARUKIA MKURUGENZI
Na Stephano Mango,Songea
MADEREVA taksi wanaoegesha gari zao kwenye eneo la soko kuu katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma wameiomba Serikali ione umuhimu wa kusikiliza kilio chao baada ya Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo kushindwa kuwasikiliza wala kuwajibu kuhusiana na pingamizi walilotoa la kufukuzwa kwenye eneo la Soko kuu kwa madai kuwa eneo hilo ni jirani na Benki ya Nmb tawi la Songea.
Wakizungumza na mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com hapa jana Wawakilishi wa madereva hao Peter Vicent,Pashens Mkinga,Christopher Komba na Hussein Mhagama wameeleza kuwa kitendo cha Halmashauri ya Manispaa ya Songea cha kuwakataza kuegesha magari yao kwenye eneo la Soko kuu ni cha unyanyasaji kwani wao ni madereva wa magari madogo(taksi) ambayo yamekuwa yakiegeshwa kwenye eneo hilo kwa ajili ya kusubiri wateja wanaotoka Sokoni na wengine kwenye Taasisi za fedha ambazo zipo jirani na eneo hilo.
Walisema kuwa pamoja gari hizo kuegeshwa kwenye eneo hilo zimekuwa zikilipiwa stika shilingi 35,000 kila baada ya miezi sita kwa kila gari moja fedha ambazo zimekuwa zikipokelewa na Halmashauri hiyo.
Walieleza zaidi kuwa pia wamekuwa wakilipa ushuru wa kuegesha taksi hizo kwenye eneo hilo shilingi 250 kwa kila gari kila siku na Manispaa hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Ruvuma imekuwa ikiwatoza shilingi laki 291,000 kwa kila gari dogo (taksi) kwa mwaka.
Walifafanua zaidi kuwa wao ni wadau wakubwa kwa kuchangia maendeleo ya Manispaa hiyo pamoja na Serikali kuu lakini wanashangaa kuona kuwa uongozi wa Halmashauri hiyo umechukua uamuzi mkubwa wa kuwafukuza kwenye eneo la Soko kuu kwa kuwatumia askari wa kikosi cha usalama barabarani bila kuwapa taarifa ya maandishi ya kuwahamisha kwenye eneo hilo.
Waliongeza kusema kuwa baada ya kuona wamefukuzwa kwenye eneo hilo walimwandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songea ya kupinga kufukuzwa kwenye eneo la Soko kuu tangu Julai 20 mwaka huu lakini mpaka leo hawajapewa jibu la aina yeyote na juzi mchana walikwenda kufuatilia barua yao ya pingamizi kwa Mkurugenzi ambaye aliwajibu kuwa barua yao ya pingamizi alishaipata na anaamini kuwa tayari walishajibiwa jambo ambalo lilianza kuonyesha kuwa lina utata kwa vile wao walikuwa bado wanasubiri majibu toka Manispaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria alipohojiwa na mtandao huu jana kwa njia ya simu kuhusiana na madereva taksi hao kufukuzwa kwenye eneo walilokuwa wakiegesha magari yao na kuto kuwajibu barua ya pingamizi waliyomuandikia alieleza kuwa ana kiri kuwa ofisi yake ilipokea barua ya pingamizi ambayo walikuwa wameiandika madereva taksi ambao wanaegesha kwenye Soko kuu na kwamba zipo sababu za kiusalama zilizofanya waondolewe kwenye eneo hilo .
Zakaria alieleza zaidi kuwa eneo hilo la Soko kuu lipo karibu na benki ya NMB hivyo kwa kuweka usalama kamati ya ulinzi na usalama iliamua gari hizo ndogo (taksi) zinazoegeshwa kwenye eneo hilo ziondolewe na badala yake zipangiwe eneo jingine ambalo alilitaja kuwa eneo la wazi kwenye barabara inayotoka TTCL kwenda Hospital ya Serikali ya Songea ambapo wao wameamua kupinga maamuzi hayo kwa madai kuwa eneo hilo halina miundo mbinu mizuri ya vyoo na maji
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo alisema kuwa Halmashauri yake inafanya utaratibu wa kuweka miundo mbinu wanayodai madereva hao hivyo wanapaswa kukubali kuhamia kwenye eneo hilo na kwamba barua yao waliyoandika ya kupinga pingamizi ofisi yake ilisha wajibu kwamba ni lazima wahamie kwenye eneo lililopangwa na si vingenevyo.
 MWISHO

Aliyekuwa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Ally Said Manya


MADIWANI NANE WA CCM KUCHUANA KUGOMBEA UMEYA SONGEA
Na Stephano Mango,Songea.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM ) Wilaya ya Songea mjini Mkoa wa Ruvuma kimeanza mchakato wa uchaguzi wa kura za maoni kujaza nafasi ya aliyekuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Ally Said Manya aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa kisukari Julai 29 mwaka huu katika Hospitali ya Misheni ya Peramiho iliyopo wilaya ya Songea vijijini ambapo madiwani wanane na mgombea mmoja binafsi wamechukuwa fomu ya kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza na mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ jana ofisini kwake Katibu wa CCM wilaya ya Songea mjini  Alfonsi Siwale alisema kuwa wagombea wa kiti cha Umeya kupitia CCM tayari wamechukua  fomu na kuzirudisha ofisini hapo mapema jana majira ya saa 10.30 jioni.
Siwale amewataja Madiwani waliojitokeza kuchukuwa za kuwania nafasi hiyo kuwa ni  Charles Mhagama diwani wa kata ya matogoro,Merius Ponera Diwani wa kata ya Tanga, Jemes Makene diwani wa kata ya Matarawe, Victor Ngongi diwani wa kata ya Ruvuma,Faustin Mhagama diwani wa kata ya Mshangano, Mariam Dizumba diwani viti maalumu, Genrida Haule diwani viti maalum, Christian Matembo diwani wa kata ya Seedfam pamoja na Willy kayombo ambaye ni Mwenyekiti wa jumuia ya wazazi Mkoa wa Ruvuma ambaye ndiye mgombea pekee binafsi aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo.
Alisema kuwa ofisi yake ilipata barua toka kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo ya kumtaka aanze mchakato wa kumuandaa mgombea kwa nafasi ya umeya kupitia CCM na chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) ambacho kinamadiwani kwenye halmashauri hiyo kwa lengo la kutaka kujaza nafasi ya meya ambayo iliachwa wazi baada ya Manya kufariki dunia.
Alieleza zaidi kuwa kwa sasa chama cha CCM wilayani humo kimepokea majina nane ya madiwani pamoja na mgombea mmoja binafsi ambao wote wamerudisha fomu za kutaka kugombea nafasi hiyo na baada ya hapo majina yatapendekezwa katika vikao mbalimbali vya chama wilaya na mkoani na kutoa maoni kwa kamati kuu ya CCM Taifa ambayo ndio itakayofanya uteuzi wa mwisho na kurudisha majina ambayo ndio yatapaswa kupigiwa kura na madiwani ndani ya baraza la madiwani wa CCM.
Siwale alifafanuwa kuwa baada ya madiwani hao kumpata mgombea ndipo jina la mshindi litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo ambaye ndie atakayepanga tarehe ya uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo kwa kumkutanisha na mgombea mwingine wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) endapo nao watampendekeza mgombea.
Ally Manya alikuwa diwani wa kata ya Lizaboni na alichaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo Novemba mwaka jana na alifariki dunia baada ya kuuguwa kwa muda mrefu ugonjwa wa kisukari.
 MWISHO.