MIAKA 50 YA UHURU UMASKINI WA KIPATO UMEONGEZEKA MARA DUFU
Na Stephano Mango,Songea
WATANZANIA wamebakiza siku chache kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa nchi
yao baada ya kuupata disemba 9,1961 wakati huo nchi ikijulikana kwa jina la
Tanganyika kabla ya kuungana na Visiwa vya
Zanzibar
Mwaka huu
Tanzania inasherehekea miaka hiyo baada ya waliokuwa viongozi wenye uzalendo stahiki wa taifa
hilo changa walipofanikiwa kuwaondoa wakoloni wa Kiingereza kwa njia ya mazungumzo na kuwaacha watanzania wajiendeleze wenyewe
Katika
hilo hatuwezi kumsahau muasisi wa mazungumzo ya amani na kiongozi mzalendo wa kwanza wa taifa hili,Baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyepigania haki za Watanzania kabla na baada ya uhuru bila ya kumwaga damu
Kwa mantiki hiyo kamusi ya Kiswahili sanifu,tolea la pili la mwaka 2004 iliyotolewa na Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili
Dar es Salaam inatafsiri neno uhuru
kama hali ya kutotawaliwa na mtu au nchi nyingine na pia inafafanua ni hali ya kufanya mambo bila kuingiliwa
Kupitia tafsiri hii waasisi wa taifa letu walipigana dhidi ya utawala wa kikoloni ili kutuondoa katika hali ya kutawaliwa na wazungu sehemu zote yaani kiuchumi,kisiasa na kiutamaduni ambapo jambo hili lilifanikiwa na kumdhihilishia aliyekuwa mtawala wetu kwamba tuko tayari kujitegemea
Licha ya kusherehekea miaka hiyo kuna haja ya kujihoji kwa kina kama neno uhuru lilivyotafsiriwa kwenye kamusi tajwa hapo kwani binafsi nafikiri kuwa maana ya uhuru inapoteza maana yake kwani hali ya maisha ya watanzania inadhihirisha jambo
hilo
Watanzania wanaamnini kuwa hawako huru kwani watawala wanakazana kuwarudisha kwenye mfumo rasmi wa ukoloni tuliokuwa nao awali kabla ya kukombolewa na waasisi wa taifa hili miaka 50 iliyopita
Iliamini kuwa Taifa letu lina rasilimali nyingi
sana ambazo zingetumika kuliendeleza taifa kiuchumi,kielimu,kisiasa na kiutamaduni ili wananchi wake wawe na maendeleo stahiki kutokana na kufaidi rasilimali zao
Badala yake nchi yetu kutokana na mipango mibaya inayotungwa na watawala wetu ambao kimsingi wanapaswa kuitwa wakoloni weusi imebaki ikiwa omba omba wa kila kitu kutoka kwa wakoloni weupe ambao ndio tuliowanyang’anya nchi ili tuweze kujitawala wenyewe
Wengi sasa tunaamini kuwa uhuru tulio nao ni ule wa kupandisha bendera ya taifa yenye rangi nne na kuimba wimbo wa taifa wa mungu ibariki Tanzania kutoka na viongozi wetu tulio wapa dhamana kutuongoza kuuza nchi vipande vipande na kutegemea misaada kutoka kwa wakoloni ambao walifukuzwa na waasisi wetu wakati wakidai uhuru
Jambo
hilo halihitaji kuomba muongozo kwa mtu yoyote yule kwani inajidhihirisha waziwazi kwa kila mtanzania ambaye anapumua vizuri kutokana na uhai alionao kwani ukitathimini uchumi wan chi yetu utagundua wazi kuwa unamilikiwa,kuendeshwa na mataifa ya nje
Watanzania wamebaki wakiduwaa kutokana na mifumo mibovu ya nchi inayowaacha wananchi wake wakishangaa na kushindwa kujinasua katika shughuli zao za uzalishaji
mali kutokana na sera mufilisi zinazowabana wananchi na kupelekea kuvipuuza vitu vinavyozalishwa na watanzania
Kutokana na mifumo hiyo mibovu wafanyabiasha kutoka nje ya nchi wanapewa fursa nyingi katika nchi yetu nasi tunakuwa watumwa katika shughuli zao huku za kwetu zikiendelea kudharauliwa kwa maneno kadha wa kadha
Ndio maana nchi yetu leo inategemea bidhaa nyingi kutoka nchi mbalimbali duniani kama vile mchele tunategemea kutoka Thailand,mafuta kutoka Kenya,nyama Afrika kusini,kijiko,sahani,nguo,viatu kutoka China na bidhaa zingine kutoka nchi nyingine nyingi
Jambo
hilo linaendelea kuwatesa wananchi katika lindi kubwa la umasikini wa kipato kutokana na bidhaa zao wanazozalisha zinakosa soko kunakosababisha na ukosefu wa masoko stahiki kwa sababu ya mifumo nyanyaji kwa watanzania iliyowekwa kwa makusudi na viongozi wetu
Licha ya kusherehekea miaka hiyo 50 ya uhuru bado watanzania wengi wanakabiliwa na umasikini wa kipato ingawa Serikali imekuwa na mipango na mikakati mingi mfu katika kukuza uchumi wa nchi na kupunguza umaskini
Kwani tafiti nyingi zinazoendelea kufanya na wadau mbalimbali zinaendelea kuonyesha wazi kuwa hali ya maisha ya mtanzania ni mbaya
sana kiuchumi kwani wapo baadhi
yao wanatumia chini ya shilingi mia 600 kwa siku kutokana na ugumu wa upatikanaji fedha
Rekodi zinaonyesha kuwa uchunguzi wa bajeti ya kaya wa mwaka 2007(2007 Household Budget Survey-HSB) unaonyesha kuwa umaskini umepungua kidogo sana toka asilimia 38.6 mwaka 1990,asilimia 35.7 mwaka 2001 mpaka asilimia 33.3 mwaka 2007
Kwa kuwa idadi ya watanzania inaongezeka kwa asilimia 2.9 kila mwaka na idadi ya watu maskini imeongezeka kwa milioni moja na nusu toka watu milioni 11.4 mwaka 2001 na kufikia watu milioni 12.9 mwaka 2007
Izingatiwe kuwa kigezo kilichotumiwa na HBS 2007 cha mtu mzima kutohesabiwa kuwa siyo maskini ni kutumia shilingi 641 au zaidi kwa siku akiwa Dar es Salaam,shilingi532 au zaidi kwa siku akiwa katika miji mingine na shilingi 469 au zaidi akiwa vijijini
Ni wazi kigezo ni cha chini mno na bado idadi ya watu maskini imeongezeka kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya kambi ya upinzani bungeni mwaka huu wa 2011 kwani kigezo kilichokubalika kimataifa kuwa matumizi ya chini kabisa kwa mtu mzima asihesabiwe kuwa ni maskini wa kutupwa ni dola moja kwa siku
Benki ya dunia inakadiliwa kwa kutumia kipimo hiki umaskini Tanzania umeongezeka toka asilimia 73 ya watanzania wote mwaka 1990 mpaka kufikia asilimia 89 mwaka 2000 na kwamba kwa kutumia kigezo hicho hicho takwimu za uchunguzi wa bajeti ya kaya wa mwaka 2007 zaidi ya watanzania 90 katika kila watanzania 100 ni maskini wa kutupwa
Katika
hilo ikumbukwe kuwa taifa letu mara baada ya kupata uhuru lilikuwa na ndoto kuu tatu ambazo ni kutokomeza ujinga,umaskini na maradhi jambo ambalo miaka 50 ya uhuru limeshindwa kutekeleza ndoto hizo kwani kutimizwa kwa ndoto hizo kungefanya kuwa taifa lililoendelea na linalojitegemea
Tunapokumbuka na kuthamini mchango wa wale wote waliotimiza wajibu wao wakati huo wa kupigania uhuru,tunapaswa kuamini kuwa nasi tunaweza kuutimiza wajibu wetu
kama funzo katika kukabiliana na changamoto za leo na kesho ili taifa letu lisitopee kwenye utumwa
Taifa tulilonalo leo si lile la wakati wa uhuru ni wazi kuwa limepiga hatua kijamii,kisiasa,kiuchumi,amani,umoja na mshikamo miongoni mwa wananchi ni vielelezo vya baadhi ya mafanikio ambayo taifa limepata na kuyadumisha tangu uhuru
Ingawa hatua tuliyopiga kimaendeleo
kama taifa haiwiiana hata kidogo na uhuru wetu wa miaka 50 kwani maendeleo yetu yamekuwa yakisuasua na maliasili za nchi zimekuwa zikipukutika kwa kasi kubwa kwa kiasi kikubwa tumeshindwa kuutumia uhuru wetu kupunguza umaskini
Kwani
Tanzania ni moja ya nchi 10 zilizo maskini kabisa duniani kwa kipimo cha kimataifa cha umaskini kwani asilimia 57.8 sawa na watu milioni 20.2 wanaishi chini ya dola moja kwa siku na asilimia 89.9 sawa na watu milioni 31.5 wanaishi chini ya dola mbili kwa siku
Hali hiyo inatisha kwani hatuwezi kuwa na mshikamano wa kweli wa kitaifa ikiwa ukuaji wa uchumi unawanufaisha watu wachache na kuwaacha zaidi ya watanzania milioni 36 wakiwa maskini wa kutupwa
Takwimu zinaonyesha kuwa watanzania wenye lishe duni na utapiamlo wameongezeka toka asilimia 28 ya watanzania wote mwaka 1990 na kufikia asilimia 41 mwaka 1995 na kupungua kiasi kufikia asilimia 35 mwaka 2007
Miaka 50 ya uhuru ni aibu kuona watu wanaolala na njaa wakiongezeka kila siku iendayo kwa mungu kwani wameongezeka toka milioni 7.4 mwaka 1990 na kufikia milioni 14.4 mwaka 2007 wakati rasilimali zao zikitumika ipasavyo wangeweza kuisha maisha mazuri na kufanya taifa kuwa na ustawi stahiki
Kutokana na kasi yetu ndogo ya maendeleo,tafiti zinakadilia kwamba kwa kasi ya sasa ya ukuaji wa uchumi kwa asilimia sita kwa mwaka,italichukua taifa miaka 18 zaidi kuweza kuwanyanyua wananchi kutoka kwenye wastani wa kipato cha chini ya dola moja kwa siku hadi kufikia dola mbili za Marekani kwa siku
Tunapaswa kuelewa kwamba
kama tutashindwa kuchukua maamuzi sahihi na hatua madhubuti katika kuchochea uwajibikaji na ufanisi hata baada ya miaka 18,bado watanzania watakuwa maskini kwani hawataweza kujikimu kikamilifu kutokana na mifumo mibovu ya utawala inayoachilia mfumuko wa bei katika bidhaa mbalimbali
Ili ndoto ya uhuru itimie kuna haja ya msingi ya kuutazama upya mfumo wetu wa utawala,kujua ni kwanini umeshindwa kutuwekea mazingira ya kutupatia maendeleo ya haraka
Licha ya kuwa na rasilimali za kutosha na uhuru wa miaka 50 kwani inaaminika wazi wazi kuwa
Tanzania huru yenye maendeleo na inayojitegemea
inawezekana endapo kila moja wetu akitimiza wajibu wake
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana simu 0755-335051
Barua pepe;stephano12mango@yahoo.com