About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Wednesday, September 21, 2011

MJUMBE WA BODI YA MIKOPO WA SERIKALI ZA MITAA ATEMBELEA SOKO LA SONGEA NA KUJIONEA CHANGAMOTO ZAKE

    Na Amon Mtega,Songea
 
SOKO kuu la Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma lililoungua moto mwaka 2003 na kuteketeza kabisa fedha na mali za wafanyabiashara wa soko hilo na kisha kujengwa upya na Manispaa  hiyo kwa fedha zilizotoka kwa wahisani na taasisi za mikopo na kisha kuendelea kutoa huduma hiyo lakini bado linakabiliwa na changamoto mbali mbali.
 
Akitoa taarifa ya uendeshaji wa soko hilo mkuu wa Masoko ya Manispaa ya Songea Salum Homera kwa Mjumbe wa bodi ya mikopo ya Serikali za Mitaa George Mallima Lubeleje alisema kuwa baada ya soko hilo kujengwa upya likiwa na meza 308 na maduka 161 na kwamba linatoa huduma kwa wananchi wa ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma.
 
 Alisema kuwa pamoja na huduma hizo halmashauri hukusanya kiasi cha shilingi milioni 9.4 kwa mwezi ambazo hutumika kuisaidia halmashauri kugharamia shughuli mbambali za kiutawala na utoaji huduma kwa wananchi pia serikali kuu hukusanya kodi ya mapato kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wa soko hilo ambayo huisaidia serikali kutoa huduma boraa kwa wananchi.
 
 Aidha pamoja na mafanikio hayo Homera alisema kuwa zipo changamoto ambazo zinahitaji kutatuliwa ili kuboresha mapato zaidi ikiwemo mahitaji ya ukarabati ambayo ni makubwa kuliko kiasi kinacho kusanywa na soko hilo,baadhi ya wafanyabiashara kuendesha biashara zao nje ya soko na kulikosesha soko mapato na kuchelewa kusainiwa kwa sheria ndogo za halmashauri ambazo huwa zina mapendekezo ya maboresho ya viwango vya kodi na ushuru mbali mbali.
 
 Kwa upande wao wafanyabiashara na wananchi wanaolitumia soko hilo walisema kuwa soko hilo bado linahitaji ukarabati mkubwa ili liweze kuwa na hadhi ya Manispaa na hasa katika maduka ya kuuzia nyama ambako kunahitaji usafi wa hali ya juu tofauti na hali ilivyo sasa.
 
Naye mjumbe wa bodi ya mikopo ya Serikali za Mitaa  George Malima Lubeleje akizungumza baada ya kukagua soko hilo mbali na kupongeza matumizi ya fedha ya mkopo iliyotolewa na bodi hiyo kwa ajili ya ujenzi huo alisema kuwa halmashauri inapaswa kusimamia sheria ndogo ambazo zitasaidia kuongeza kipato na kuweza kumaliza kulipa deni la mkopo huo ili iweze kupewa mkopo mwingine.
 mwisho





MAJAMBAZI WAUA,WAJERUHI,KUPORA SHILINGI MILIONI MBILI NA KUTOKOMEA ZAO

               Na Steven  Augustino,Tunduru

WATU wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wamemuua kwa kumpiga mapanga mkulima wa kitongoji cha Mkangwala kilichopo katika kijiji cha Mbatamila Wilayani Tunduru aliyefahamika kwa jina la Bibie Mtenje (25) na kumjeruhi vibaya mume wake Kasim Shaibu (35).

Taarifa kutoka katika kijiji hicho zinaeleza kuwa baada ya watu hao kutekeleza uharamia huo walifanikiwa kupora fedha taslimu zaidi ya shilingi milioni mbili pamoja na kuchoma moto nyumba ya jirani yake aliyetambulika kwa jina la Anafi Alifa aliyedaiwa kutoka na kupeleka taarifa kwa majirani wakati tukio hilo likiendelea.

Ndugu wa majeruhi Shaibu ,Bw.Sandali Shaibu na Kazembe Rajabu wanao muuguza majeruhi huyo aliyelazwa katika hospitali ya Wilaya ya Tunduru akiwa hajitambui walisema kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Septemba 21 mwaka huu.

Wakifafanua taarifa hiyo wanafamilia hao walidai kuwa fedha alizo porwa majeruhi na kusababisha kifo cha mkewe zilitokana na mauzo ya viroba 24 vya mpunga ambao walilima na kufanikiwa kuvuna msimu uliopita wakiwa na matumaini ya kujiletea maendeleo baada ya kuuza.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma  Michael Kamuhanda mbali na kukiri kuwepo kwa tukio hilo alisema kuwa jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na kwamba endapo watabainika watu kuhusika na tukio hilo sheria itafuata mkondo wake.

 Mganga wa hospitali ya Wilaya ya Tunduru Dkt. George Chiwangu ambaye alimpokea na kumshughulikia majeruhi Shaibu alisema kuwa, majeruhi huyo ameumizwa vibaya kichwani na sehemu za tumboni kutokana na kukatwa mara nyingi na mapanga.

Naye Mganga aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Mtenje, Dkt.Titus Tumbu alisema kuwa kifo chake kimesababishwa na kutokwa na damu nyigi zilizosababishwa na majeraha ya kukatwa na mapanga sehemu za kichwani.

Mwisho   

MANISPAA YA SONGEA WAFANIKIWA KUDHIBITI MIMBA KWA WANAFUNZI WA SHULE ZA MSINGI

               Na Thomas Lipuka,Songea

IDARA ya Elimu  na wadau wa Elimu katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma,wamefanikiwa kuondoa tatizo la mimba kwa wanafunzi wa Shule za Msingi kwa kipindi cha mwaka 2010 hadi 2011 ambapo hakuna mwanafunzi aliyepata mimba katika Shule zote za Msingi katika Manispaa hiyo.
Taarifa ya hali ya Elimu ya mwaka 2010/2011 iliyosomwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Zakaria Nachoa kwa wadau wa Elimu katika Ukumbi wa Songea Club hivi karibuni imebaini kuwa hakuna mimba iliyoripotiwa kwa wanafunzi wa Shule kwa Kata zote 21 za Manispaa hiyo.
Nachoa alisema mbinu iliyotumika katika kuzuia suala la mimba ni pamoja na ushirikiano wa karibĂș baina ya wazazi,walimu,wadau wa Elimu na Viongozi wa Elimu ngazi zote za Manispaa na hatimaye kufikia kufuta kabisa tatizo la mimba katika Shule za Msingi zote za Manispaa ya Songea.
Taarifa ya mandeleo ya Elimu katika Manispaa hiyo imetaja pia mafanikio zaidi yaliyojitokeza katika sekta ya Elimu ni pamoja na ufaulu kwa Wanafunzi waliomaliza Elimu ya Msingi 2010 ambapo Manispaa hiyo imekuwa ya kwanza Kimkoa, na kuzipita Wilaya za Songea,Mbinga,Namtumbo na Tunduru.
Hata hivyo changamoto kadha zimejitokeza katika tathmini elimu Manispaa ya Songea ambapo kuna uhaba wa vitabu vya kiada,jambo ambalo linapelekea kitabu kimoja cha kiada kutumiwa na wanafunzi 11 ama zaidi.
Changamoto zingine zilizotajwa katika tathmini hiyo ni uhaba wa walimu darasani, hivi sasa kuna walimu 820 wakati mahitaji ni walimu 1259 hivyo Manispaa ya Songea kuwa na upungufu wa walimu 439 darasani ,jambo ambalo linahitaji msaada toka Serikali kuu.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea amewaambia wadau wa Elimu kuwa kuna upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa,vyoo na nyumba za walimu,ameomba wadau wa Elimu kujipanga kwa hatua za awali za ujenzi wa maboma ili wanafunzi wote watakao faulu 2011 waweze kupata nafasi kidato cha kwanza.
Kuhusu changamoto ya upatikanaji wa madawati wadau wamesema ni vema kujipanga upya kwani suala la miti ya kutengenezea madawati lipo kwenye uwezo wao, isipokuwa Serikali iwezeshe Manispaa ya fedha kwa vifaa vya kiwandani ili kuondoa tatizo la madawati hatimaye wanafunzi wapate mazingira bora ya kujifunzia na kuleta usikivu,wanaposoma ili kuongeza ufaulu.
Mkurugenzi wa Manispaa pia alitoa taarifa ya maendeleo ya Elimu ya watu wazima mbele ya Mwenyekiti wa kikao cha tathmini Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Sabaya kuwa Manispaa ya Songea ina watu 2883 ambao hawajui kusoma kuhesabu na kuandika sawa na asilimia 40% ya watu wazima wote wa Manispaa hiyo ambapo Mkuu huyo wa Wilaya akatia mkazo kwa Kata zote kuendeleza kwa kasi Elimu ya watu wazima ili kufuta kabisa asilimia ya wasiojua kusoma,kuandika na kuhesabu katika Manispaa ya Songea.
“Naagiza kisomo sasa kipambe moto kata zote waratibu Kata,walimu wakuu,watendaji ngazi zote wajibikeni ipasavyo” alisisitiza Bwana Sabay.
Mwenyekiti huyo wa Kikao hicho ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Sabaya amewaagiza viongozi wa Elimu Manispaa,Waratibu Kata,walimu na wadau wa Elimu kusimamia kikamilifu malengo ya kukuza taaluma katika Manispaa kwa kuhimiza mahudhurio ya wanafunzi,walimu kufundisha kikamilifu,wakaguzi kufuatilia ufundishaji na viongozi kutekeleza wajibu wao kwa kutoa stahiki zote za walimu ikiwemo malipo ya likizo,matibabu na posho zao za kujikimu.

MWISHO