About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Wednesday, August 31, 2011

BIASHARA YA VIUNGO VYA BINADAMU YAHOFIWA KUANZA RUVUMA

                                                     Na Stephano Mango,Songea.

JESHI la polisi mkoani Ruvuma limebaini kuwa mabaki ya mwili wa binadamu yaliyokutwa yamehifadhiwa kwenye mfuko na  kutupwa kati kati ya mto Nakawale wilayani Songea hivi karibuni ulikuwa tayari umeshachunwa ngozi na kuchukuliwa mifupa pamoja na kichwa kitendo kilichofanywa na watu wasiojulikana na kisha kutokomea navyo kusikojulikana.

Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda akizungumza na mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 24 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi katika eneo la Nakawale wilayani Songea ambako Afisa mtendaji wa kijiji hicho alipewa taarifa na wananchi kuwa kuna mwili wa binadamu ukiwa umehifadhiwa kwenye kiloba umeonekana upo kati kati ya mto.
Alisema kuwa Afisa mtendaji huyo ambaye jina lake halikuweza kupatikana baada ya kupata taarifa hiyo alikwenda kwenye eneo la tukio ambako aliwakuta wananchi wamekusanyika kisha alifanya mawasiliano na polisi ambao baadaye walifika kwenye eneo la tukio wakiwa wameongozana na daktari wa serikali kwa ajiri ya uchunguzi.
Aidha alisema kuwa baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa mwili huo ilibainika kuwa mwili huo ulikuwa ni wa marehemu Jafar Shabani mkazi wa kijiji hicho huku ukiwa umechunwa ngozi ,mifupa pamoja na kichwa na kubaki nyama na  nguo za marehemu huyo zikiwa kando kando ya mto huo ambazo ndizo zilizopelekea wananchi kugundua kuwa aliyeuawa kuwa ni Shaban.
Kamuhanda ameeleza zaidi kuwa polisi baada ya kufanya uchunguzi zaidi walibaini kuwa siku chache kabla ya tukio hilo marehemu huyo alikuwa amegombana na Said Kandemanje(37) ambaye tayari amekamatwa na anahojiwa na polisi kuhusiana na tukio hilo.
Aidha kamuhanda alisema kuwa uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwepo kwa vitendo vya ufukuaji wa makaburi yaliyoko kwenye vijiji vya nchi jirani ya Msumbiji ambako karibu na mpaka wa Tanzania na kuchukua viungo mbali mbali vya binadamu vinavyodaiwa kupelekwa nchi nyingine kwa uuzaji wa mifupa hiyo ya binadamu.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusiana na matukio hayo ili kuweza kubaini mtandao wa watu wanaofanya vitendo hivyo viovu na kuwafikisha kwenye vyombo vya kisheria kwa hatua zaidi
MWISHO

MWANAFUNZI ASAKWA KWA KUMUUA MJOMBA WAKE TUNDURU

Na Gideon Mwakanosya,Songea.

JESHI la polisi mkoani Ruvuma linamsaka mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Mtonya iliyopo katika Tarafa ya Nakapanya wilayani ya Tunduru mkoani humo kwa tuhuma za kumuua mjomba wake ambaye alikuwa anaenda kumsaidia mama yake ambaye alikuwa anapigwa na kaka yake.
 
Akizungumza mwandishi wa mtandao huu wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ ofisini kwake kamanda wa polisi wa Mkoa wa Ruvuma Bw.Michael Kamuhanda alisema kuwa tukio hilo la mauaji limetokea jana majira ya saa 8 usiku wakati wa ugomvi baina ya marehemu ambaye jina lake ni Michael Gabriel(23) mkazi wa kijiji hicho na dada yake Marisela Jamadin(27).


Kamanda Kamuhanda alisema kuwa inadaiwa siku ya tukio hilo katika kijiji hicho cha Mtonya Gabriel aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na mtoto wa dada yake huyo Agrey Emmanuel(14) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba katika shule ya msingi Mtonya wilayani humo na baada ya kugundua kuwa ameua alikimbia na kutokomea kusikojulikana.
Kamanda Kamuhanda alisema kuwa mwanafunzi huyo Agrey anatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi  utakaofanyika nchini kote mwezi ujao na hivyo jeshi la polisi mkoani humu linaendelea kumsaka kuhusiana na tuhuma hizo na uchunguzi unaendelea kuhusiana na tukio hilo na hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa.
Hata hivyo kamada Kamuhanda alisema kuwa chanzo cha ugomvi huo ambao umepelekea  Gabriel kuhuwawa na mpwa wake bado hakijajulikana licha ya kwamba polisi wanaendelea na uchunguzi.
Mwisho.

Tuesday, August 30, 2011

KAMPUNI YA SONGEA NETWORK YAPANIA MAKUBWA KATIKA KILIMO NA ELIMU


                                     Na Thomas Lipuka,Songea
KAMPUNI ya Songea Network Centre na Valongo Network Centre za Mkoani Ruvuma zimeazimia kuimarisha kilimo cha Kahawa,ulezi na Jetropa katika Mkoa wa Ruvuma ili kuwakomboa wananchi wa kipato cha chini kwa kilimo hicho.
Kampuni hizo zimetambulishwa jana rasmi mbele ya Serikali ya Mkoa na kutaja malengo yao katika kuendeleza mazao hayo matatu kwa ustawi wa jamii za watanzania ambao zaidi ya asilimia 80 wanategemea kilimo.
Mkurugenzi wa Kampuni hizo Xaveri Kazimoto Komba ameyataja malengo yao kuwa ni kuendeleza elimu katika Mkoa,kuimarisha kilimo cha ulezi,kahawa na Jetropa,kukuza utamaduni na kuimarisha hali ya Mkoa kwa mazingira ili uoto wa asili usitoweke.
Komba alisema katika kuimarisha kilimo cha kahawa Mkoani Ruvuma tayari ameisha unganisha Mkoa na watafiti wa zao hilo toka Ujerumani ambao kwa kutumia teknolojia za kisasa wataliendeleza zao hilo na kuleta uzalishaji wenye tija ili kukuza kipato cha wakulima wa kahawa Mkoani Ruvuma.
Akiongelea hatua zingine za kuboresha uzalishaji wa zao hilo na mazao mengine yaliyo tajwa amesema hapata kuwepo na tatizo la soko kwani utaratibu umeisha andaliwa wa kununua mazao hayo iwapo yatazalishwa kwa kasi na kutunza ubora wake na soko limeandaliwa.
Akitambulisha mradi wa kuboresha elimu Kazimoto amesema tayari wameisha anzisha Sekondari ya St.Sapiensia ambayo ina kidato cha nne sasa na kuchukua wanafunzi wa dini zote wa kike na wa kiume,shule ambayo iko Parokia ya Mjimwema manispaa ya Songea.
Katika hatua nyingine tayari Songea Network Centre imeisha panda miti zaidi ya 500 ya kivuli matunda na mbao kwa hatua ya kulinda na kuboresha mazingira,miti ambayo imepandwa Songea mjini na Kijiji cha Mbinga Mhalule Tarafa ya Muhukuru.
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Vestina Nguruse ambaye kwa cheo chake ni mshauri wa mipango Mkoa amesema mradi wa kilimo kinachojali watu unaoanzishwa na Songea Network Centre uwe endelevu kwa kuwa mipango yake ni ukombozi kwa watu wa Ruvuma.
Amesema shida kubwa ni soko kwa mazao ya wakulima na bei zisizo za uhakika ambazo hubadilishwa mara kwa mara kutokana na soko la dunia linavyoendelea lakini kutokana na utafiti wa kina uliofanywa na Songea Network Centre bila wasiwasi suala la soko litadhibitiwa kikamilifu.
Nguruse amefafanua kuwa fursa za kuendeleza mazao haya katika Mkoa zipo za kutosha akataja uwepo wa ardhi safi kwa kilimo cha kahawa,ulezi na Jetropa  ni nguvu kazi ya kutosha yaani wakulima uwepo wa Bandari ya Mtwara na ujenzi wa barabara inayoendelea toka Mtwara Mbamba bay pia mito na mabonde yenye maji wakati wote kwa kilimo cha umwagiliaji.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa Nguruse aliwaasa viongozi wa mradi kusimamia mradi huo uwe endelevu na utimize azima yake ya kumkomboa mkulima wa Mkoa wa Ruvuma
Wakati huo huo imefahamika kuwa jitihada za kupata soko la uhakika kwa mazao hayo matatu zimeletwa na Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani Ahamad Ngemara ambaye amefanya jitihada kubwa kwa suala la masoko nchini Ujerumani.

KAIMU MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA SONGEA ANNA MBOGO

                                  

                                         WANANCHI SONGEA WAIFYATUKIA WIZARA YA AFYA
                                     Na Stephano Mango,Songea
 
WANANCHI wa Vijiji vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuona umuhimu wa kuwaletea watumishi wenye taaluma wakiwemo wauguzi na Waganga kwenye Zahanati na vituo vya Afya ambako kuna Upungufu wa Wataalamu.
 
Wakizungumza kwa Nyakati tofauti na mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ wananchi hao wameeleza kuwa kwenye baadhi ya Zahanati na Vituo vya Afya vilivyopo Wilayani Songea kuna tatizo kubwa la upungufu wa Wauguzi na Waganga ambao umekuwa ukisababisha kuwepo kero kubwa kwa Wakazi wa Vijiji hivyo.
 
Hebron Mbilinyi Mkazi wa Kijiji cha Madaba alisema kuwa katika Kituo cha Afya cha Madaba kina wauguzi na waganga wachache na kusababisha kuwepo msongamano mkubwa wa wagonjwa wanaofika kupata tiba kwenye Kituo hicho.
 
Alisema kuwa huduma inayotolewa kwenye Kituo hicho cha Afya ni duni kwani wakati mwingine wagonjwa ambao wana uwezo kifedha hulazimika kutafuta Hospitali za kulipia ambako hupatiwa matibabu.
 
Said Hussein Mkazi wa Kijiji cha Muhukuru alisema kuwa Kituo cha Afya cha Muhukuru kimekuwa na tatizo kubwa la kutokuwa na Waganga hasa ikizingatia kuwa kina Mganga mmoja tu ambaye hulazimika kutoa huduma tangu asubuhi na wauguzi waliopo ni wachache hivyo anaiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ione umuhimu wa kuwakumbuka wakazi wa Muhukuru kwa kuwapelekea Wataalamu wenye sifa ambazo zitapunguza kero zilizopo Kijijini hapo ambako kuna umbali wa Kilomita 80 tokea Songea Mjini ambako kuna Hospitali ya Serikali ya Mkoa.
 
Fadhili Ngonyani Mkazi wa Kijiji cha Liyangweni alieleza zaidi kuwa Huduma inayotolewa katika Zahanati ya Kijiji hicho siyo ya kuridhisha kwasababu Zahanati hiyo ina Wauguzi wachache ambao ndiyo wamekuwa wakitoa huduma badala ya Mganga ambaye hajaletwa tangu muda mrefu hivyo ameitaka Halmashauri ya Wilaya hiyo kuchukua hatua za haraka kutafuta Waganga pamoja na Wauguzi kwenye Zahanati hiyo ili kupunguza kero iliyopo Kijijini hapo.
 
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea Anna Mbogo aliuambia mtandao huu kuhusiana na kuwepo kwa malalamiko toka kwa Wananchi ya upungufu wa wataalamu kwenye Zahanati na Vituo vya Afya alikiri kuwa Halmashauri yake ina upungufu wa Wataalamu kwenye Zahanati na Vituo na Afya.
 
Mbogo alisema kuwa Halmashauri hiyo ina Vituo viwili vya Afya ambapo alivitaja kuwa ni Kituo cha Afya cha Muhukuru na Kituo cha Afya cha Madaba ambavyo vyote vina waganga watatu tu badala ya kuwa na waganga wanne kila kimoja.
 
Alifafanua kuwa Halmashauri hiyo pia ina Zahanati za Vijiji 23 ambazo zina wauguzi na waganga wachache na baadhi ya Zahanati zilizopo hazina waganga na badala yake wauguzi ndiyo wamekuwa wakitoa huduma kwenye Zahanati hizo.
 
Alizitaja Zahanati ambazo hazina kabisa waganga kuwa ni Liyangweni,Nambendo,Gumbiro na Ngahokola na Kituo cha Afya cha  Muhukuru kina mganga na Madaba kuna waganga wawili wakati kila Kituo cha Afya kulipaswa kuwe na waganga wanne na kwenye Zahanati kunapaswa kuwe na waganga wawili.
 
Alieleza zaidi kuwa kutokana na hali hiyo kwenye vituo vya afya kuna upungufu wa waganga watatu na kwenye Zahanati kuna upungufu wa waganga 29 wakati mahitaji ya waganga kwenye Halmashauri hiyo bado ni kubwa na kusababisha kuwepo Changamoto kubwa ya upungufu mkubwa wa wataalamu wenye sifa wakiwemo wauguzi na waganga  jitihada inaendelea kufanywa ya kutafuta waganga na wauguzi wenye sifa kujaza nafasi zenye upungufu kwenye Zahanati
 

MIKARATUSI NI MITI HATARI KATIKA VYANZO VYA MAJI KWENYE MILIMA YA MATOGORO

                             Na Thomas Lipuka,Songea
 
IMEBAINI kuwa ukosefu wa maji kiangazi katika Manispaa ya Songea unachangiwa kwa kiasi kikubwa na aina ya miti ambayo ipo katika misitu ya milima Matogoro ambayo hunyonya maji kwa kiwango kikubwa kwa kipindi cha mwaka.
 
Afisa maliasili wa Mkoa Ruvuma Enock Buja akizungumza na mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ alisema utafiti uliofanywa na Taasisi inayoshughulikia utafiti wa misitu nchini ijulikanayo kama  TAFORMA, imebaini kuwa kuna aina kadhaa ya miti ambayo kwa kiwango kikubwa.
 
Ameitaja miti hiyo kuwa ni mikaratusi (Camaldulensis) ambayo hunyonya maji kiasi cha milimita 1240 kwa mwaka na mikaratusi aina ya (Microrhea) pia hunyonya maji milimita 1050 kwa mwaka.
 
Afisa maliasili huyo wa Mkoa amefafanua kuwa ,aina nyingine ya miti inayonyonya maji kwa wingi ni mikaratusi hujulikana kama patula wenye uwezo wa kunyonya maji kiasi cha milimita 665 kwa mwaka.
 
Katika ufafanuzi Buja amesema miti hiyo yote iliyo tajwa ipo misitu ya milima matogoro ambapo kiasi mingi imeondolewa kwa maji ikiwa kiasi, tu ikiwa na lengo la kuiondoa isilete hatari ya kukosekana kwa maji,kwa wakazi wa Manispaa ya Songea.
 
Afisa maliasili huyo ameongeza kusema kuwa kiasi kilichotajwa hunyonywa na miti hiyo ambapo  kwa mti mmoja na sio kwa uwingi wake katika misitu.
 
Katika utafiti huo imeelezwa kuwa ipo miti mingine kwa mfano mgunga na mvile inayoelekea kutumia maji mengi kuliko mikaratusi iliyotajwa hapo juu.
 
Amesema baadhi ya mazao ya kilimo mathalani mpunga na miwa nayo hutumia kwa kiwango ambacho karibu sawa ya mikaratusi.
 
Katika msukumo wa Kitaifa  wa kupunguza umaskini MKUKUTA mbinu nyingi zinafikiliwa kutumika katika kufikia azma hiyo bahati mbaya upandaji miti katika vyanzo vya maji haujatiliwa mkazo kwa umakini hasa miti gani ipandwe ili kuondokana na tatizo la miti kunyonya maji.
 
Ni sahihi kabisa kuvuna miti iliyopo misitu ya milima matogoro kwani miti hiyo ni hatari na ni adui mkubwa wa chanzo kikuu cha maji yatumiayo katika Manispaa ya Songea.
 
Hivi sasa Taifa limeagiza kuwa kila Wilaya ipande miti zaidi ya 1500 ili kurudisha jotoridi  na kuondoa hewa ya ukaa ambayo inatishia Taifa letu kwa tabia mbaya za baadhi ya watu wakatao miti bila kupanda au kwa ajili ya mkaa na shughuli za ujenzi na za kibinadamu.
 
Hali ya uchomaji moto ni tatizo la pili katika misitu ya milima matogoro mbali ya juhudi za mkoa za kurudishia miti hiyo mwaka hadi mwaka kwa utaratibu wa kupanda miti ya asili ambayo hainyonyi maji kwa wingi jambo hilo juhudi zake linafifishwa na watu waharibifu wanaoendeleza vitendo vya uchomaji moto katika mlima matogoro na misitu yake  Mkoani  Ruvuma.

MILIONI 215 KUTUMIKA KUNUNULIA MADAWA YA KUULIA WADUDU


                      Na Stephano Mango,Mbinga
 
SERIKALI kwa kushirikiana na wadau wa zao la kahawa Wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma imechangisha jumla ya shilingi milioni 215 kwa ajili ya kununulia madawa yatakayotumika kupambana  na wadudu waharibifu wa zao hilo.
 
Katibu tawala wa wilaya hiyo Idd Mponda alisema fedha hizo zimetumika kununulia madawa aina ya SUBA ambayo hutumika kuulia wadudu aina ya vidung’ata ambao wamekuwa wakishambulia miti ya kahawa.
 
Alisema kuwa jumla ya hekta 48 ya zao hilo zimeshambuliwa na wadudu hao na kusababisha uzalishaji wa kahawa kushuka.
 
 Mponda alisema kufuatia jitihada zilizofanyika kuanzia Julai mwaka jana hadi sasa za kutokomeza wadudu hao mashamba mengi yameonekana kwenda vizuri na kwamba katika msimu wa mwaka 20011/12 uzalishaji unatarajia kuongezeka hadi kufikia tani 9,000.
 
"Kinachotakiwa kwa wakulima ni kuhakikisha wanazingatia yale wanayoelekezwa na wataalamu wa kilimo na kwamba wajiunge pamoja na kuanzisha  mashamba darasa ili iwe rahisi kwa maofisa ugani kuwafikia", alisema Mponda.
 
Kuhusu wanunuzi wa zao hilo alisema wanapaswa kuzingatia masharti yaliyowekwa na uongozi wa wilaya hiyo na kwamba kwa wale ambao watabainika kutorosha kahawa kwa lengo la kukwepa kulipa ushuru watachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kunyang’anywa leseni ya biashara hiyo.
 
Pia alisema wakati umefika kwa wakulima wa zao hilo kuwa makini na wafanyabiashara wajanja wanaozunguka vijijini kununua zao hilo kwani baadhi yao wamekuwa wakiwarubuni wakulima kuwa bei ya kahawa imeshuka kwenye soko la dunia ili wanunue zao hilo kwa bei ya chini jambo ambalo sio sahihi.

Monday, August 29, 2011

KAMANDA WA POLISI MKOA WA RUVUMA MICHAEL KAMUHANDA

                                                
                                                   Na Cresencia Kapinga,Songea
WATU sita wamefariki dunia papo hapo na wengine wawili wamejeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka na kuwaka moto katika kijiji cha Chunya kilichopo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
 
Kamanda wa polisi mkoa wa Ruvuma Machael Kamuhanda akizungumza na mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ alisema kuwa tukio hilo limetokea jana majira ya saa 12 jioni na kwamba miongoni mwa waliofariki miili yao imeuungua vibaya huku maiti hizo zikiwa hazitambuliki.
 
 Kamuhanda alisema kuwa tukio hilo limehusisha Gari lenye  namba za usajili  T 270 BDG Landrover likiwa linaendeshwa na Dereva Stevin Ngoko (32) kupinduka na kuwaka moto na kusababisha vifo vya watu sita papo hapo katika kiji cha Chunya barabara iendayo Mbambabay toka Mbinga.
 
Kamuhanda amewataja waliojeruhiwa katika ajari hiyo kuwa ni Jeremia Masalo (38) mkazi wa nchi jirani ya Msumbiji na Anna Godfrey (3) mkazi wa Mbambabay ambao wote wamelazwa katika Hospitali ya Serikali ya Wilaya ya Mbinga kwa matibabu.
 
Alisema kuwa watu waliokufa majina yao hayajaweza kufahamika kutokana na maiti hizo kutotambulika kwa kuwa zimeungua vibaya na zote zimepelekwa  katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya wilaya hiyo.
 
Kamuhanda alisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi ambao ulimsababishia dereva wa gari hilo kushindwa kumudu usukani na kwamba jeshi lake linaendesha msako wa kumtafuta  dereva wa gari hilo Bw. Ngoko ambaye alitoroka mara tu baada ya kutokea ajali hiyo.
 

Sunday, August 28, 2011

WANANCHI WAMTAKA MKURUGENZI KUITISHA UCHAGUZI WA SERIKALI YA KIJIJI CHA MKILI

                                         Na Thomas Lipuka,Songea

WANANCHI wa Kijiji cha Mkili Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma wamemtaka Mkurugezi wa Halmashauri Wilaya ya Mbinga kusimamia zoezi la kupata uongozi wa kijiji hicho kwani  kijiji hicho kwa muda mrefu kina uongozi wa mda ambapo shughuli zote huendeshwa na Mtendaji wa kijiji, baada ya aliyekuwa Mwenyeketi wa kijiji hicho   John Isdori Tilia kusimamishwa uongozi na Serikali yake yote .

Tuhuma zilizopelekea Mwenyekiti huyo na serikali yake yote  kusimamishwa uongozi ni pamoja na kutoitisha mikutano ya serikali ya kijiji kutosoma mapato na matumizi ya kijiji kushindwa kusimamia miradi mbalimbali ya kijiji na wakati mwingine kujishughulisha zaidi na mambo ya starehe na kuacha yale yanayohusu maendeleo ya wanakijiji .

Wanakijiji  wa Mkili baadhi yao wametaja miradi ambayo ameshindwa kusimamia ni ujenzi wa kibanio cha mfereji wa maji kwa kilimo cha umwagiliaji ambacho kipo katika mto Ndumbi kijijini hapo ,ujenzi unaendelea wakituo cha afya kwa kujenga nyumba nne za waganga na ukarabati wa barabara itokayo bandari ya Mkili hadi Hospitari ya Litembo .

Wakitoa kero zao kupitia mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ baadhi ya wanakijiji hao walisema  toka serikali ya kijiji hicho ichaguliwe hawajasomewa taarifa ya mapato na matumizi ambapo shughuli zote huendeshwa na mwenyekiti aliyesimamishwa uongozi na mtendaji bila wanakijiji kuhusishwa.

Wameongeza kuwa kijiji hicho kina bonde la kutosha kwa fursa ya kilimo cha umwagiliaji  wa mpunga ambapo tayari Halmashauri ya Mbinga ilishatoa mradi wa umwagiliaji  katika kijiji hicho lakini kwa kukosa uongozi bora wa kijiji,kibanio kilisombwa na maji mara mbili jambo ambalo mkandalasi hakufuatiliwa namna alivyojenga  kibanio hicho  na ubora wake .

Wamesema kilimo hicho cha umwagiliaji katika bonde lililopo kijijini hapo kingeweza   kuwanasua  wanakijiji kwa kupata zao la mpunga mara mbili kwa mwaka hivyo wamemwomba mkurugezi wa Wilaya ya Mbinga kuharakisha zoezi la kuwapata viongozi wa serikali ya kijiji ili kuharakisha maendeleo yao.

Walipoulizwa kuhusu tatizo la sumu inayotiwa katika mito inayozunguka kijijini hapo hasa toka eneo milimani walisema vitendo  hivyo vya uharibifu vinatendwa na baadhi ya watu kutoka vijiji vya Mahande ,Siasa ,Lundumato,Mkoha,kwa uroho wa kutafuta Samaki ambapo madhara yake huua madhalia yote ya viumbe hai katika mito hiyo ambayo ni Ndumbi ,Mnyamaji,Chipindi,na Luhorochi.

Wanakijiji hao wamempongeza mkurugezi mtendaji wa Halmashauri wa Wilaya ya Mbinga kwa kuwatia moyo ili wafyatue matofari ya nyumba nne za waganga kwa ajili ya kuimarisha na kupanua kituo cha afya cha Mkili pia kwa ahadi ya kupatiwa gari la kusafirisha wagonjwa siku za usoni toka kituo cha afya Mkili hadi Hospitari za Lihili, Mbinga ,Litembo ,Songea na Peramiho.

Aidha wanakijiji hao wameiomba serikali kuwaimarishia mawasiliano ya simu kwa kuwajengea minara ya Voda,Airtel,Tigo na TTCL,mawasiliano ambayo wanayapata kwa shida kwa kupanda juu ya miti ama kwenye vichuguu.

AFYA ZA WAFANYABIASHARA SOKO KUU SONGEA ZIPO HATARINI KWA KUKUBWA NA MAGONJWA YA MLIPUKO


                                           Na Gideon Mwakanosya,Songea.
WAFANYABIASHARA katika Soko kuu katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma wapo katika hatari kubwa ya kukumbwa na magonjwa ya milipuko kikiwemo Kipindupindu kutokana na miundo mbinu ya maji taka yanayo simamiwa na mamlaka ya Maji safi na Maji taka Songea (SOUWASA) kuwa mibovu pamoja na wauzaji wa  nyama ya ng’ombe kwenye mabucha kutiririsha maji machafu wanayosafishia utumbo wa ng’ombe hadi maeneo wanayouzia nyanya,vitunguu na mbogamboga wafanyabiashara wadogo.
Mwandishi wa mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ jana alifanya mazungumzo na baadhi ya wafanyabiashara sokoni hapo ambapo walieleza kuwa miundo mbinu ya maji taka imekuwa ikipasuka na kutiririsha maji kwenye maeneo wanayouzia bidhaa zao na kusababisha adha kubwa kwa wafanyabiashara hao ambao wamekuwa wakilazimika kufanya kazi katika mazingira magumu.
Walisema katika hali ya kushangaza  soko hilo lina maafisa afya ambao wamekuwa wakifanya kazi kila siku kwenye eneo hilo ambalo lina mazingira machafu lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa.
Issa Hussen ambaye ni mfanya biashara katika soko hilo alieleza kuwa wafanyabiashara wa mbogamboga ambao wamekuwa wakitandika magunia chini kisha kuweka bidhaa zao kama nyanya, vitunguu wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu kwani kwenye maeneo wanayofanyia biashara hiyo maji yanayotiririshwa toka kwenye ma bucha ya nyama za ng’ombe wanayooshea utumbo wa ng’ombe pamoja na maji taka ambayo yanayo tiririka toka kwenye mtandao wa Souwasa yamekuwa yakipita kwenye eneo hilo wanayofanyia biashara na kuwaletea adha kubwa kwani wanunuzi wamekuwa wakikataa kununua bidhaa zao kutokana na maji machafu kuwa jirani na biashara zao.
 Kwa upande wake Afisa masoko wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Salum Homera alipoulizwa na mtandao huu kuhusiana na malalamiko ya wafanyabiashara kuhusiana na kukithiri kwa uchafu kwenye soko kuu ambalo limekuwa likitiririsha maji machafu kwenye ambayo yamekuwa yakipita jirani kabisa na maeneo ya biashara zao alikiri kuwepo kwa tatizo hilo lakini alisema kuwa tatizo hilo lipo juu ya uwezo wake.
Homera alisema kuwa Ofisi yake ilisha toa taarifa kwa idara ya Afya na kwamba maafisa afya ndiyo walitakiwa kuona umuhimu wa kudhibiti hali hiyo iliyojitokeza sokoni na kwamba mamlaka ya maji safi na maji taka songea (SOUWASA) nao walishapewa taarifa na waliahidi kufika kufanyia matengenezo mtandao wa maji taka.
 Kwa upande wake Afisa afya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Mahundi alipohojiwa na nipashe kuhusiana na kukithiri kwa uchafu katika soko hilo, alieleza kuwa tatizo hilo Ofisi yake ilikuwa bado haijalipata lakini Afisa masoko ndiye alitakiwa kutoa taaarifa ki maandishi kwenye ofisi ya idara ya afya ili tatizo hilo liweze kufanyiwa kazi kirahisi kwani yeye ndiye msimamizi mkuu wa masoko yote ya halamashauri.
 Jitihada za mtandao huu za kumpata Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na maji taka (SOUWASA) Fransis Kapongo ziligonga mwamba baada ya kumpigia simu yake ya mkononi zaidi ya mara tatu bila kupatikana na nipashe ilifanya jitihada zaidi ya kuwasiliana na kaimu katibu tawala wa mkoa wa Ruvuma Dr.Anselmo Tarimo na kumuuliza juu ya uchafu uliokithiri sokoni Songea amabye alikiri na kudai kuwa tatizo hilo linalazimika kufanyiwa utaratibu wa haraka ili kulimaliza kuanzia mwanzoni mwa wiki hii ambapo wataalamu wote wa afya watalazimishwa wawepo kwenye soko hilo ili waone ni jins gani wataweka mazingira mazuri sokoni hapo ambayo yatawafanya wafanyabiashar wasikumbwe na magonjwa ya milipuko.

MWEKEZAJI ADAIWA KUPORA ARDHI YA EKARI 5000 KWA WANAKIJIJI LIPOKERA

            Wananchi wa kijiji cha Lipokera wakiwaonyesha waandishi wa Habari ardhi yao ambayo wanadai wameporwa na mwekezaji
 Wananchi wakionyesha mahindi yao baada ya kuvuna haraka haraka kwa kumuogopa mwekezaji asije akawanyang'anya
Na Thomas Lipuka,Songea.
WAKAZI wa kijiji cha Lipokela wilayani Songea mkoani Ruvuma wanamuomba Waziri wa ardhi,nyumba na Maendeleo ya Makazi  Profesa Anna Tibaijuka kuwasaidia kuirejea ardhi yao yenye ukubwa wa zaidi ya hekari 5000  iliyochukuliwa kinyemela na mwekezaji.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika kijiji hicho baadhi ya wananchi walidai kuwa  mwekezaji mwenye asili ya Asia anayefahamika kwa jina moja la Merali  tangu mwaka 1985 alipewa ardhi kinyemela bila baraka za wananchi na kusababisha ardhi hiyo kuingia kwenye mgogoro mkubwa.
Wananchi  wamedai kuwa mwekezaji huyo alipewa  ardhi hiyo katika mazingira ya kifisadi kupitia aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji hicho  Joseph Komba pamoja na aliyekuwa katibu wake Gervas Mbonde .
Hata hivyo walisema mwekezaji huyo alipewa ardhi  kwa maamuzi ya wananchi yenye ukubwa wa hekari 1000 mwaka 1984 na kwamba mwaka 1985 aliomba tena ardhi hekari zaidi ya 5000 ambazo alipewa bila baraka za wananchi na kuleta mgogoro ambao unaendelea hadi sasa.
``Kuanzia mwaka 1985 wananchi wa kijiji cha Lipokela hawakujua kama ardhi yao ya hekari 5000 amepewa mwekezaji hadi mwaka jana  takriban miaka 25 ndipo ilipofahamika na kusababisha wananchi zaidi ya 250 wanaolima mashamba pamoja na makazi kwenye  eneo hilo  kuambiwa kuwa eneo hilo ni mali ya mwekezaji wa kiasia’’,walidai wananchi hao.
Akizungumza kwa niaba ya wenzao Mwenyekiti mstaafu wa kijiji hicho Faustine Komba alibainisha  kuwa ardhi hiyo yenye  mgogoro ilianza kutumika na wananchi kuanzia mwaka 1993 ambao walipimiwa kihalali na uongozi wa kijiji na kuendelea kuitumia mwaka hadi mwaka bila kutambua kuwa amepewa mwekezaji kinyemela.
Komba alisema mwekezaji alipewa kisheria hekari 1000 tu upande wa kulia mwa barabara ya Songea - Mbinga na kwamba eneo lenye hekari zaidi ya 5000 upande wa kushoto ambazo mwekezaji huyo anadai kupewa kinyemera sio zake kwa kuwa ni mali ya wananchi ambazo walipewa kihalali na serikali ya kijiji.
Uchunguzi ambao umefanywa na wanakijiji wanadai wamebaini kuwa mwekezaji huyo kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa kijiji hivi sasa amekuwa dalali wa kuwauzia ardhi wawekezaji wengine kutoka nchini Afrika kusini na Marekani hivyo wameiomba serikali na hasa waziri wa ardhi kuingilia kati mgogoro huyo.
Wananchi hao wakiwemo  Gofrey Lupindu,Agustino Komba,Filbert Kinunda, Vestina Hyera, Bomba Nchimbi wakizungumza kwa uchungu mkubwa ,walidai kuwa hivi sasa pia hawana imani na mwenyekiti wa kijiji aliyopo madarakani John Nchimbi ambaye anadaiwa kumsaidia mwekezaji badala ya kuwasaidia wananchi waliomweka madarakani.
Uchunguzi umebaini kuwa iwapo serikali haitachukua hatua za makusudi katika kutatua mgogoro huo wa ardhi kuna hatari ya kutokea machafuko makubwa kutokana na ukweli kuwa  wananchi wa kijiji hicho  wamedai hawapo tayari kuona mwekezaji anapora ardhi yao  kinyemela na kusababisha wananchi kuwa wakimbizi katika ardhi yao.
Uchunguzi mwingine ambao umefanywa katika kijiji hicho umebaini kuwa  mwekezaji huyo ambaye alipewa hekari 1000 na wananchi  katika kipindi  cha miaka mitatu alifanikiwa kulima hekari 15 tu na kitendo cha kutaka kuchukua hekari nyingine zaidi ya 4000 kinawapa mashaka kuwa kijiji hicho kipo katika hatari ya kuuzwa kwa kisingizio cha uwekezaji.
Afisa ardhi wa Halmashauri ya wilaya ya Songea Japhet Mungashwa amekiri kwamba  mwekezaji huyo amemilikishwa eneo la hekari 5000 kihalali kwa kipindi cha miaka 99 kwa sheria ya ardhi ya mwaka 1923 ambayo inawaruhusu wajumbe wa kijiji kupitisha maamuzi bila kushirikisha maamuzi ya wananchi wote kama ilivyo katika sheria mpya ya ardhi ya mwaka 1999.
 Wananchi hao wametoa mwito kwa serikali ya wilaya ya Songea,mkoa wa Ruvuma pamoja na Waziri  wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi kufika katika kijiji hicho  ili kujionea hali halisi ya ardhi ya mashamba na makazi ambayo wameporwa  na mwekezaji.
Sheria ya ardhi ya vijiji  namba tano kifungu cha tano ya mwaka 1999 inasema kuwa Halmashauri ya kijiji haitagawa ardhi au kutoa hakimiliki ya kimila bila ya kwanza kupata idhini ya mkutano  wa kijiji ambapo katika kifungu cha sita katika sheria hiyo kinaeleza  Halmashauri ya kijiji italazimika kutoa taarifa na kuzingatia maoni ya mkutano wa kijiji kuhusu uendeshaji na usimamizi wa ardhi ya kijiji.
Kwa mawasiliano andika lipukakomba@yahoo.com




Saturday, August 27, 2011

Diwani wa Kata ya Mshangano Faustine Mhagama akizungumza na ndugu na jamaa zake akiwa katika Kituo kikuu cha Polisi Songea baada ya kulipoti kituoni hapo akiwa nje kwa dhamana,katikati Joseph Haule ambaye alikuwa ni mtangazaji wa uwepo wa maandamano,kushoto ni dereva wa gari la matangazo ya maandamano Suzo Luoga



POLISI WAMKAMATA DIWANI NA WAZUIA MAANDAMANO SONGEA
Na,Stephano Mango,Songea

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma liliwakamata na kuwahoji zaidi ya masaa matatu wakazi wawili wa Kata ya Mshangano na Diwani wa kata hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi(CCM)kwa tuhuma za kutangaza maandamano ya amani ya wananchi wa kata hiyo wakidai kupimiwa ardhi yao na Kampuni ya Ardhi Plan na kumtaka Waziri mkuu Mizengo Pinda kuwatimua kazi Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea na Afisa Mipango Miji wa Manispaa hiyo ambao wameonyesha dhahili kutaka kuwadhulumu maeneo yao

Wakazi hao waliokamatwa na polisi ni Suzo Luoga ambaye alikuwa ni dereva wa gari ya matangazo lenye namba za usajili T 295 AJS aina ya Chesar mark II,Joseph Haule ambaye alikuwa mtangazaji na Faustine Mhagama ambaye ni Diwani wa kata hiyo ambao wote walikamatwa wakiwa kwenye gari hilo ambalo lilikuwa linapita kwenye mitaa ya kata hiyo kuwatangazia uwepo wa maandamano makubwa

Mmoja wa watuhumiwa hao Haule ambaye alikuwa mtangazaji alisema kuwa kazi hiyo alipewa na viongozi ambao wenyeviti wa serikali ya mitaa ya Namanyigu,Mshangano na Mitendewawa na kwamba shughuli hiyo ya utangazaji ilisimamiwa kikamilifu na Diwani wa kata lengo kuhakikisha ujumbe unawafikia wakazi wote wa kata hiyo

Naye wa Kata hiyo Mhagama akizungumza na mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ jana alikili kukamatwa na alidai kuwa yeye pamoja na wenzake walikamatwa na Polisi majira ya saa tatu usiku huko katika eneo la Mshangano na waliamriwa kuingia kwenye gari la Polisi wakiwa chini ya ulinzi mkali na kupelekwa kwenye kituo kikubwa cha Polisi

Alisema kuwa mara baada ya kufikishwa kituoni hapo waliamliwa kuvuliwa viatu,mkanda na kuanza kupekuliwa na kasha kuwekwa mahabusu ambapo baadae alifika Kaimu Mkuu wa Polisi wa Wilaya  akiwa ameongozana na Askari Kanzu wawili ambao walianza kuwahoji hadi saa tano na nusu usiku ndipo walipoambiwa wawatafute watu wa kuwadhamini ambapo Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea James Makene pamoja na Diwani wa Viti maalum Rehema Milinga walifika kituoni hapo na kuwadhamini

Kwa upande wake Makene ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Matarawe aliuambia mtandao huu kuwa kitendo cha kuwakamata Diwani na wenzake ni uonevu mkubwa na kinyume na utawala bora kwa kuwa Serikali ya Kata ya Mshangano ilipeleka barua ya kuomba kibali cha maandamano toka tarehe 19.8.2011 ambapo mpaka wanakamatwa walikuwa hawajapewa barua wala maelezo ya aina yoyote jambo ambalo liliashiria kukubaliwa ingawa baada ya kuwaweka mahabusu ndipo wakapewa barua ya maelekezo jambo ambalo limeleta utata mkubwa wa uadilifu wa jeshi hilo

Naye Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa wananchi wa kata ya Mshangano waliomba kibali cha kutaka kufanya maandamano makubwa ya amani lakini katika barua yao ilionyesha mapungufu mengi ikiwa ni pamoja na kutoeleza tarehe,muda na njia ambayo maandamano yatapita

Kamuhada alisema kuwa tayari Serikali ya Kata ilipewa barua ya maelekezo na Jeshi la Polisi yenye kumbukumbu namba.SOA.3.6/65 ya tarehe 25.8.2011 ambayo ilipokelewa na Diwani wa kata hiyo majira ya saa tatu usiku
MWISHO

Katibu Mpya wa Jimbo la Songea Mjini Chadema Masumbuko Paulo

CHADEMA SONGEA WAPATA KATIBU MPYA WA JIMBO
Na,Stephano Mango,Songea
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma kimempata Katibu mpya wa Jimbo la Songea Masumbuko Paulo katika uchaguzi wa wanachama wa chama hicho uliofanyika jana katika Ofisi ya Kata ya Mfaranyaki
 
Akitangaza matokeo hayo Mwenyekiti wa Jimbo hilo ambaye pia ni Diwani wa kata ya Majengo mjini hapa Idd Abdalah alisema kuwa wanachama waliopiga kura ni 80 ambapo Masumbuko Paulo amepata kura 54,Ajaba Nditi alipata kura 18, Zuber Tindwa alipata kura 8 ambapo Christopha Nyoni alipata kura 0
 
Abdalah alimtangaza Masumbuko Paulo kuwa ndiye ameibuka mshindi wa kwanza na hivyo kuanzia hapo anakuwa Katibu mpya wa Jimbo hilo na kwamba anatakiwa kuanza kazi mara moja ili kuweza kuendana na kasi ya chama hicho
 
Awali Mwenyekiti huyo aliwaambia wajumbe kuwa nafasi hiyo ya Ukatibu ilikuwa wazi kutokana na aliyekuwepo katika nafasi hiyo kuiacha na kwenda kufanya kazi kwenye Mashirika yasiyoya kiserikali
 
Alifafanua zaidi kuwa katika uchaguzi huo Wagombea walikuwa watano ambapo mgombea Said Ligema aliamua kujitoa dakika za mwisho za uchaguzi jambo ambalo viongozi wa Wilaya walikubaliana na uamuzi wake huo
 
Akiwashukuru wajumbe kwa kumchagua Masumbuko Paulo alisema kuwa imani na dhamana waliyompa ni kubwa sana hivyo atakitumikia chama kwa uadilifu mkubwa ili kiweze kupata ushindi stahiki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na chaguzi zingine zijazo
 
Masumbuko alisema kuwa Chama kipo katika harakati kubwa za kujiimalisha maeneo ya pembezoni mwa miji na vijijini hivyo kazi hiyo ya kujikita maeneo hayo kwa lengo la kukisambaza chama ni jukumu la wananchama wote wenye mapenzi ya dhati na chama hicho
 
Akifunga mkutano huo wa uchaguzi Mwenyekiti wa Chama hicho Wilaya ya Songea Peter Mboya alisema kuwa wanachama ndio nguzo stahiki ya chama chochote duniani hivyo ni vema popote pale alipo mwanachama anatakiwa afanye jambo kwa maslahi ya chama
 
Mboya alisema kuwa muda wa mabadiliko ya kitaifa umefika ambapo chama hicho kinatakiwa kuchukua dhamana ya kuwaongoza watanzania hivyo ni vema tukaonyesha kwa dhata mbele ya wananchi kuwa tunaweza kuwaondoha hapa walipo katika kipindi hiki cha miaka 50 ya uhuru na kuwapeleka katika hali nyingine ya ustawi wa maisha yao
MWISHO

Friday, August 26, 2011

Mwenyekiti wa mtaa wa Mshangano Paulo Mangwe akisoma tamko la Wenyeviti wa mitaa mitatu ya kata ya Mshangano mbele ya waandishi wa habari la kumtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda awachukulie hatua za kuwafukuza kazi Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Zakaria Nachoa na Afisa Mipango Miji wa Manispaa hiyo Kastori Msigara kwa vitendo vyao vya kukwamisha maendeleo ya wananchi wa kata ya Mshangano,kushoto ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Mitendewala Bernado Mahinya




WANANCHI KUANDAMANA KUSHINIKIZA KUPIMIWA ARDHI, KUNG’OLEWA MKURUGENZI SONGEA

Na Stephano Mango,Songea

WANANCHI wa Kata ya Mshangano, Halmashauri ya Manispaa ya Songea wanatarajia kufanya maandamano makubwa  ya amani ya kumtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwang’oa  kazi Mkurungezi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria na , Afisa Mipango Miji wake Castory Msigala kwajili yakuwa kikwazo cha maendeleo ya wananchi.

Akisoma tamko la wenyeviti wa serikaili za mitaa wa kata ya Mshangano ambayo imekumbwa na mgogoro mzito wa ardhi, Mwenyekiti wa  serikali ya Mtaa wa Mshangano, Paul Mangwe alisema kuwa (kesho) leo wanataria kufqanya maandamano ya amani yatakayo anzia kwenye ofisi ya kata hiyo hadi kwa mkuu wa wilaya ya Songea Thomas ole Sabaya kumfikishia ujumbe wa kutaka kupewa kibali cha kupimiwa ardhi yao na kumuomba Waziri Mkuu kuwang’oa viongozi hao wawili ambao wamekuwa kikwazo kwa zoezi hilo.

“ Sisi wenyeviti wa serikali za mitaa ya Mitendewawa, Namanyigu na Mshangano tulishaomba kibali kwa OCD  wa Songea kumjulisha kuhusu maandamano ya amani, kibali tutapata na hata kama hakitapatikana wananchi wamedai lazima waandamane kesho(Leo),” alisema Mangwe.

Alisema ifahamike kuwa wananchi wa kata ya mshangano tangu walipo kutana Agosti 13 mwaka huu walimtaka  Mkurugenzi huyo awe amesaini michoro na kibali cha kuiruhusu Kampuni ya Ardhi Plan ltd  yenye Makao makuu Dar es Salaam ambayo imekwisha wahi kufanya kazi kama hiyo kwenye Kata ya Mwenge Mshindo mjini hapa iweze kuwapimia wananchi maeneo yao ambayo wamesitisha shughuli ya kuyaendeleza tangu Disemba 2010.

Katika taarifa hiyo Wenyeviti wa Mitaa wa Kata hiyo walisema kwakuwa Mkurugenzi Nachoa na Afisa Mipango Miji wake Msigala wamekaidi matakwa ya wananchi wenye ardhi wa kata ya Mshangano kushindwa kujibu barua ambazo walizipeleka za kutaka kupimiwa ardhi takribani miezi tisa sasa wameshindwa kumuelewa ni kitu gain anachotaka kutoka kwa wakazi wa kata hiyo.

“Tunapata mashaka makubwa na kukosa imani na Viongozi hao wawili(Nachoa na Msigala) kwani pamoja na kutokujibu barua zetu lakini mazingira yamejionyesha kuwa wao wana maslahi binafsi,” walisema wenyeviti hao katika mkutano na waandishi wa habari.

Hata hivyo, walisema wao wapo tayari kufa kuliko kuiachia ardhi ya wapiga kura wao waliowachagua mwaka 2009 katika uchaguzi wa serikali za mitaa kuwaletea maendeleo.

Walisema kuwa hawaoni mtu mwingine atakaye suluhisha mgogoro huu mkubwa uliodumu kipindi kirefu zaidi ya mtoto wa mkulima  Waziri Mkuu Mizengo Pinda mwenye uchungu na watu wanyonge hapa nchini.

Walisema wameshangazwa sana na viongozi wa serikali ya mkoa wa Ruvuma kulifumbia macho swala zito kama hili  na hivi sasa wameona wana mtu mmoja tu ambaye wanaamini ana ujasiri wa kumfikishia ujumbe waziri Mkuu na si mwingine bali ni DC wa Songea Thomas Ole Sabaya ambaye hata kama atasema hana mafuta ya kwenda na kurudi Dodoma wao wako tayari kuchanga nauli hiyo ilimradi Waziri Mkuu Pinda apate ujumbe huo wa kutaka kurasmishiwa makazi yao badala ya kujenga kiholela kwenye eneo la Manispaa.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Michael Kamuhanda, alisema kibali cha maandamano hayo hakijakamilika kwakuwa hakijakidhi matakwa kama yale ya kuonyesha njia, muda na tarehe ya maandamano.

Kamuhanda amefafanua kuwa tatizo hilo ni kubwa na tayari linatarajiwa kupelekwa kwenye kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa ili kuangalia wapi chanzo cha kuendeleza mgogoro huo hadi watu wafikie hatua ya kutaka kuandamana.
Mwisho

Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Oley Sabaya


MADEREVA TAKSI SONGEA WAMCHARUKIA MKURUGENZI
Na Stephano Mango,Songea
MADEREVA taksi wanaoegesha gari zao kwenye eneo la soko kuu katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoa wa Ruvuma wameiomba Serikali ione umuhimu wa kusikiliza kilio chao baada ya Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo kushindwa kuwasikiliza wala kuwajibu kuhusiana na pingamizi walilotoa la kufukuzwa kwenye eneo la Soko kuu kwa madai kuwa eneo hilo ni jirani na Benki ya Nmb tawi la Songea.
Wakizungumza na mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com hapa jana Wawakilishi wa madereva hao Peter Vicent,Pashens Mkinga,Christopher Komba na Hussein Mhagama wameeleza kuwa kitendo cha Halmashauri ya Manispaa ya Songea cha kuwakataza kuegesha magari yao kwenye eneo la Soko kuu ni cha unyanyasaji kwani wao ni madereva wa magari madogo(taksi) ambayo yamekuwa yakiegeshwa kwenye eneo hilo kwa ajili ya kusubiri wateja wanaotoka Sokoni na wengine kwenye Taasisi za fedha ambazo zipo jirani na eneo hilo.
Walisema kuwa pamoja gari hizo kuegeshwa kwenye eneo hilo zimekuwa zikilipiwa stika shilingi 35,000 kila baada ya miezi sita kwa kila gari moja fedha ambazo zimekuwa zikipokelewa na Halmashauri hiyo.
Walieleza zaidi kuwa pia wamekuwa wakilipa ushuru wa kuegesha taksi hizo kwenye eneo hilo shilingi 250 kwa kila gari kila siku na Manispaa hiyo na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Ruvuma imekuwa ikiwatoza shilingi laki 291,000 kwa kila gari dogo (taksi) kwa mwaka.
Walifafanua zaidi kuwa wao ni wadau wakubwa kwa kuchangia maendeleo ya Manispaa hiyo pamoja na Serikali kuu lakini wanashangaa kuona kuwa uongozi wa Halmashauri hiyo umechukua uamuzi mkubwa wa kuwafukuza kwenye eneo la Soko kuu kwa kuwatumia askari wa kikosi cha usalama barabarani bila kuwapa taarifa ya maandishi ya kuwahamisha kwenye eneo hilo.
Waliongeza kusema kuwa baada ya kuona wamefukuzwa kwenye eneo hilo walimwandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Songea ya kupinga kufukuzwa kwenye eneo la Soko kuu tangu Julai 20 mwaka huu lakini mpaka leo hawajapewa jibu la aina yeyote na juzi mchana walikwenda kufuatilia barua yao ya pingamizi kwa Mkurugenzi ambaye aliwajibu kuwa barua yao ya pingamizi alishaipata na anaamini kuwa tayari walishajibiwa jambo ambalo lilianza kuonyesha kuwa lina utata kwa vile wao walikuwa bado wanasubiri majibu toka Manispaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Nachoa Zakaria alipohojiwa na mtandao huu jana kwa njia ya simu kuhusiana na madereva taksi hao kufukuzwa kwenye eneo walilokuwa wakiegesha magari yao na kuto kuwajibu barua ya pingamizi waliyomuandikia alieleza kuwa ana kiri kuwa ofisi yake ilipokea barua ya pingamizi ambayo walikuwa wameiandika madereva taksi ambao wanaegesha kwenye Soko kuu na kwamba zipo sababu za kiusalama zilizofanya waondolewe kwenye eneo hilo .
Zakaria alieleza zaidi kuwa eneo hilo la Soko kuu lipo karibu na benki ya NMB hivyo kwa kuweka usalama kamati ya ulinzi na usalama iliamua gari hizo ndogo (taksi) zinazoegeshwa kwenye eneo hilo ziondolewe na badala yake zipangiwe eneo jingine ambalo alilitaja kuwa eneo la wazi kwenye barabara inayotoka TTCL kwenda Hospital ya Serikali ya Songea ambapo wao wameamua kupinga maamuzi hayo kwa madai kuwa eneo hilo halina miundo mbinu mizuri ya vyoo na maji
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo alisema kuwa Halmashauri yake inafanya utaratibu wa kuweka miundo mbinu wanayodai madereva hao hivyo wanapaswa kukubali kuhamia kwenye eneo hilo na kwamba barua yao waliyoandika ya kupinga pingamizi ofisi yake ilisha wajibu kwamba ni lazima wahamie kwenye eneo lililopangwa na si vingenevyo.
 MWISHO

Aliyekuwa Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Ally Said Manya


MADIWANI NANE WA CCM KUCHUANA KUGOMBEA UMEYA SONGEA
Na Stephano Mango,Songea.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM ) Wilaya ya Songea mjini Mkoa wa Ruvuma kimeanza mchakato wa uchaguzi wa kura za maoni kujaza nafasi ya aliyekuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Ally Said Manya aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa kisukari Julai 29 mwaka huu katika Hospitali ya Misheni ya Peramiho iliyopo wilaya ya Songea vijijini ambapo madiwani wanane na mgombea mmoja binafsi wamechukuwa fomu ya kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza na mtandao wa http://www.stephanomango.blogspot.com/ jana ofisini kwake Katibu wa CCM wilaya ya Songea mjini  Alfonsi Siwale alisema kuwa wagombea wa kiti cha Umeya kupitia CCM tayari wamechukua  fomu na kuzirudisha ofisini hapo mapema jana majira ya saa 10.30 jioni.
Siwale amewataja Madiwani waliojitokeza kuchukuwa za kuwania nafasi hiyo kuwa ni  Charles Mhagama diwani wa kata ya matogoro,Merius Ponera Diwani wa kata ya Tanga, Jemes Makene diwani wa kata ya Matarawe, Victor Ngongi diwani wa kata ya Ruvuma,Faustin Mhagama diwani wa kata ya Mshangano, Mariam Dizumba diwani viti maalumu, Genrida Haule diwani viti maalum, Christian Matembo diwani wa kata ya Seedfam pamoja na Willy kayombo ambaye ni Mwenyekiti wa jumuia ya wazazi Mkoa wa Ruvuma ambaye ndiye mgombea pekee binafsi aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo.
Alisema kuwa ofisi yake ilipata barua toka kwa Mkurugenzi wa Manispaa hiyo ya kumtaka aanze mchakato wa kumuandaa mgombea kwa nafasi ya umeya kupitia CCM na chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) ambacho kinamadiwani kwenye halmashauri hiyo kwa lengo la kutaka kujaza nafasi ya meya ambayo iliachwa wazi baada ya Manya kufariki dunia.
Alieleza zaidi kuwa kwa sasa chama cha CCM wilayani humo kimepokea majina nane ya madiwani pamoja na mgombea mmoja binafsi ambao wote wamerudisha fomu za kutaka kugombea nafasi hiyo na baada ya hapo majina yatapendekezwa katika vikao mbalimbali vya chama wilaya na mkoani na kutoa maoni kwa kamati kuu ya CCM Taifa ambayo ndio itakayofanya uteuzi wa mwisho na kurudisha majina ambayo ndio yatapaswa kupigiwa kura na madiwani ndani ya baraza la madiwani wa CCM.
Siwale alifafanuwa kuwa baada ya madiwani hao kumpata mgombea ndipo jina la mshindi litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa hiyo ambaye ndie atakayepanga tarehe ya uchaguzi wa kujaza nafasi hiyo kwa kumkutanisha na mgombea mwingine wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) endapo nao watampendekeza mgombea.
Ally Manya alikuwa diwani wa kata ya Lizaboni na alichaguliwa kuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri hiyo Novemba mwaka jana na alifariki dunia baada ya kuuguwa kwa muda mrefu ugonjwa wa kisukari.
 MWISHO.

Wednesday, August 24, 2011

 
 
 
Wakina Mama wajasiliamali katika Kata ya Mshangano Manispaa ya Songea wakiuza mazao ya mbogamboga chini katika Soko la Mshangano ambapo wamekuwa wakitozwa ushuru wa kati ya Shilingi 200 na 500 kwa siku kutokana na biashara hiyo,licha ya kuwa ni hatari kwa afya za watumiaji,imekuwa ikishangaza kuona Manispaa inachukua ushuru bila kujali kutengeneza miundombinu stahiki katika soko hilo jambo ambalo linatafsirika kama ni kuwadhulumu wakina mama hao miaka 50 ya uhuru(Picha na Stephano Mango)

Wednesday, August 17, 2011

Aisha Abdalah akizungumza na Mwandishi wa Makala haya katika eneo lake la kazi Bombambili nyuma niWanawake wenzake wakiwa kwenye shughuli yao ya kupepeta pumba za mchele ili waweze kupata chenga za mchele kwa ajili ya mahitaji ya chakula na kujikimu kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili kwa sababu ya mgawanyo usio sawa wa rasilimali za taifa(Picha na Stephano Mango)





WANAWAKE NA UFANYAJIKAZI ZISIZO TIMILIFU MIAKA 50 YA UHURU
Na,Stephano Mango,Songea
WANAWAKE wengi nchini wamekuwa wakifanya kazi ama za kuajiriwa au za kujiajiri wenyewe ambazo hazina staha au sio timilifu kutokana na mifumo mibovu ya ufanyaji kazi hizo kwa sababu ya ugumu wa maisha unaowakabili

Wakina mama hao wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mbalimbali na kushindwa kumudu gharama za maisha kama vile matibabu,ukosefu wa makazi,elimu na huduma nyinginezo muhimu za kijamii

Hali hiyo hupelekea wanawake wengi kutafuta kazi ili waweze kuzifanya licha ya kuwa sio timilifu na hazina staha ili waweze kujipatia fedha za kujikimu na kupunguza ukali wa maisha unaowakabili katika maeneo yao

Licha ya kufanya kazi hizo kama vile kufagia barabarani,kutengeneza bustani katika maeneo ya miji,kupika mama lishe,kupita kwenye majumba ya watu na kuomba kusafisha vyombo au kufua nguo na kazi zinginezo wamekuwa wakidhurumiwa kupata ujira wao

Aisha Abdalah mwenye umri wa miaka 55 mkazi wa kata ya Ruvuma Halmashauri ya Manispaa ya Songea anasema kuwa mme wake alifariki mwaka 1997 na kumuachia watoto wawili wa kike ambapo kwa sasa anawajukuu 6 kutoka kwa watoto wake hao ambao wanamtegemea

Abdalah anasema kuwa watoto wake wameshindwa kumletea huduma muhimu kwa mahitaji yake na ya wajukuu zake ambao amepewa jukumu la kuwalea bila kuwa na kipato chochote kile hali ambayo inamuongezea ukali wa maisha zaidi

Alisema kuwa wajukuu hao wanne wanasoma katika shule ya msingi Mburani iliyoko katika kata hiyo ya Ruvuma lakini mara nyingi watoto hao wamekuwa wakishindwa kuendelea na masomo kutokana na ukosefu wa michango mbalimbali katika shule hiyo ukiwemo mchango wa ulinzi

“Watoto hao mara nyingi wamekuwa wakila mara moja kwa siku tena chakula ambacho kwa kweli kinakatisha tamaa hata kukiangalia lakini tunalazimika kula kwa sababu hamna njia nyingine ya kusogeza siku za kuishi duniani”alisema Abdalah kwa uchungu mkubwa

Kutokana na ugumu huo wa maisha aliradhimika kutafuta kazi katika mashine za kukoboa mpunga wa wafanyabiashara mbalimbali na kubahatika kupata kazi hiyo na kupangiwa siku maalum ya kuanika mpunga,kutandaza,kuanua na kuupeleka mashine kwa ajili ya kuukoboa

Alisema kuwa katika kazi hiyo licha ya kuwa sio timilifu amekuwa akiifanya kwa zamu kutokana na wanawake wengi kuifanya kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili katika familia zao

Alieleza zaidi kuwa kazi hiyo wakati mwingine inakuwa mara moja kwa wiki kutokana na kuwekeana zamu ya kufanya shughuli hiyo kwani wakina mama wengi wamekuwa wakiifanya kutokana na ukosefu wa ajira timilifu

Alifafanua zaidi kuwa ujira wanaoupata katika kazi hiyo ni kuzoa pumba za mpunga na kuweka kwenye mifuko kwa ajili ya kwenda kuzipepeta ambapo wanapata chenga za mchele ndizo zinakuwa kama mshahara wao

“Maisha tunayoishi yanakatisha tama kabisa lakini hatuna jinsi……tunaanika mpunga wakati mwingi siku mbili ili ukauke kulingana na uwepo wa jua,tunauanua na kuupeleka mashine halafu tajiri anatupa ujira wa kuzoa pumba ili tuweze kupata chenga za kwenda kupika”alisema Abdalah

Alisema kuwa wanapopepeta pumba hizo bila kuwa na vikinga fumbi hulazimika kupata mafua na kukohoa kila mara kutokana na kuvuta hewa iliyochanganyika na pumba laini hali inayopelekea mara nyingi kuugua na kupona bila kupata tiba

Alieleza zaidi kuwa akibahatika kuzoa angalau gunia tatu za pumba na kuzibebelea huku akiwa na njaa kali kuzipeleka eneo la bonde la Bombambili ambako ndio kunakofanyika shughuli hiyo ya kupepeta hupata walau robo tatu kilo ya chenga hizo

Alieleza kuwa kiasi hicho huenda nacho nyumbani kukipika na kula na wajukuu wake kwa milo mitatu ya siku tatu kwa kipimo cha robo kwa mlo wa siku ya kwanza.siku ya pili tena robo na siku ya tatu robo

Alisema kuwa endapo siku nyingine anapopata kilo moja au mbili za chenga hulazimika kiasi kingine kuuza kwa wapikaji wa vitumbua ambapo hujipatia fedha za kununua mafuta ya taa,kupaka,mboga na sabuni

Alifafanua analazimika kupunguza mlo ili aweze kufanikisha pia mambo mengine ya kifamilia kwani wakati mwingine wajukuu wake wanaumwa homa ambazo haziwezi kupona bila kupata angalau nusu dozi ya dawa za hospitali

“Namshukuru mungu kwani mara nyingi nimekuwa nikipata homa ndogo ndogo ambazo kutokana na ugumu wa maisha zimekuwa zikipona zenyewe bila kupata matibabu yoyote yale lakini wajukuu wangu wamekuwa wakinyemelewa na magonjwa mbalimbali ambayo mengine wanapona kutokana na dawa za asili na mengine kwa dawa za hospital”alisema Abdalah

Wanawake wengi wamekuwa wakiishi kwa kuhurumiwa na wasamaria wema na wengine wamekuwa wakipambana hivyo hivyo na ugumu wa maisha bila mfumo waliouchagua na kuwaahidi ahadi za maisha bora

Wakati taifa linaelekea kuadhimisha sherehe za miaka 50 ya uhuru tunapaswa kujiuliza ni nani atakayewapa au kuwatengenezea nguvu wanawake waweze kuikabili serikali yao kuanzia ile ya kijiji hadi taifa katika kuweka mizania sawa ya matumizi ya rasilimali za nchi ili ziweze kuwanufaisha watu wote

Ili waweze kupata huduma muhimu za afya,maji,elimu,miundombinu na huduma nyingine stahiki za kijamii kwani jambo hilo kwa kushirikiana na mashirika ya kutetea haki za kijinsia TGNP,FemACT inawezekana kufikia hatua stahiki kwa ustawi wa makundi yaliyo pembezoni

Nilazima kuwe na mfumo mzuri wa kuyafikia makundi hayo kwa kutumia rasilimali za taifa ili kujua kila kinachowatatiza ili kuweza kuwajengea uwezo wa kimaamuzi,kufahamu haki zao na kuweka nguvu ya pamoja ya kiukombozi

Kwa lengo la kujitetea,kudai haki,kujilinda dhidi ya mifumo onevu katika itikadi,dini,kabila na jinsia ili kujenga agenda ya kimaisha kulingana na mazingira  ya eneo ambalo mtu anaishi na mahitaji yake kwa ujumla

Wakati taifa likiadhimisha miaka hiyo ya uhuru na Mtandao wa Jinsia Tanzania kuadhimisha Tamasha la Jinsia 2011 tunapaswa tutafakari kwa umakini changamoto zinazowakabili wanawake na makundi yaliyopo pembezono ili tuweze kujenga suluhisho la kitaifa

Kwasababu miaka 50 ya uhuru inatukumbusha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya katika kurekebisha sheria,sera,mifumo,mienendo na utekelezaji wa mambo mbalimbali ya maendeleo ili kureta mabadiliko chanya huko tuendako

Ili kuweza kuweka jitihada hizo kwenye mizania sawa na kuleta mabadiliko chanya katika sekta zote na makundi yote kufaidi rasilimali za taifa hili kongwe kiumri lenye umaskini mkubwa licha ya rasilimali kuzagaa kila eneo kuna hitaji nguvu za pamoja ambapo tumeamua kuthubutu,tunaweza na tuzidi kusonga mbele

Mwandishi wa Makala haya
Anapatika simu 0755-335051
Baruapepe;stephano12mango@yahoo.com

Monday, August 15, 2011

Diwani wa Kata ya Mshangano Faustin Mhagama akitoa tamko la wananchi wa kata hiyo kuhusu kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuiruhusu Kampuni ya ARDHI PLAN ipime maeneo ya wananchi mshangano




WANANCHI WATANGAZA MGOGORO MKUBWA WA ARDHI SONGEA
Na Stephano Mango,Songea

WANANCHI zaidi ya 1200 wa Kata ya Mshangano Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Songea  kurasimisha mali zao kwa kuiruhusu Kampuni ya Ardhi Plan  iwapimie viwanja na makazi walioanza kuyaendeleza kiholela.

Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi wa kata hiyo ambao chini ya uenyekiti wa Diwani wa Kata hiyo Faustine Mhagama walisema kuwa kata yao imekumbwa na mgogoro mkubwa wa ardhi baina ya wananchi wa eneo hilo na Halmashauri ya Manispaa ya Songea

Mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na madiwani mbalimbali na viongozi wa serikali uliofanyika jana kwenye viwanja vya ofisi ya kata  waliohudhuria wengi wao wakiwa wanawake walisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa kurasimisha mali zao na kupata hati miliki za maeneo yao ili waweze kufanya kazi za kujipatia kipato na kukuza uchumi wao kutokana na urasimu wanaofanyiwa na Idara ya mipango miji ya Manispaa hiyo

Walisema kuwa maeneo yao wanataka kuyaendeleza kwa kuyafanyia shughuli mbalimbali za kiuchumi lakini hawajapimiwa na wala hayana hati hivyo wananchi kwa kushirikisha serikali zao za mitaa na kata hiyo kwa mamlaka iliyokuwa nazo ziliamua kuitafuta kampuni na kuweka michoro stahiki ya eneo hilo na kuiwasilisha kwenye Halmashauri hiyo ili waweze kupimiwa ardhi yao.

Anastasia Ndumbaro mkazi wa kata hiyo alisema kwa uchungu mkubwa huku akidondosha machozi kuwa wanasikitika kwa kitendo cha Manispaa ya songea kukwamisha zoezi hilo.
“tunasikitika kwa kitendo cha kuizuia kampuni kutupimia viwanja vyetu kwani tumekuwa tukihitaji sana kurasimishiwa maeneo yetu ili tuyaendeleze,”alisema Ndumbaro.

Ndumbaro alisema kuwa familia yake ina mashamba ya ekari 10 katika eneo hilo na Baba yake alifariki toka mwaka 1992 ambako amekuwa akifuatilia idara ya mipango miji ili iweze kumpimia viwanja hivyo na kugawana na ndugu zake mirathi lakini amekuwa akiyumbishwa hadi leo hii.

Naye Mwenyekiti  wa mkutano huo Diwani  Faustine Mhagama akifunga mkutano huo alisema kuwa amesikiliza kwa umakini kilio cha wapiga kura wake na matamko mbalimbali waliyoyatoa na kwamba anawaunga mkono.

Mhagama alisema atayawakilisha maazimio ya mkutano huo kwa maandishi  kumtaka Mgurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Zakaria Nachoa kukaa na kuutazama mpango huo mzuri wa wananchi wa kata hiyo na kuiruhusu kampuni hiyo iwapimie wananchi maeneo yao.

Alifafanua zaidi kuwa ardhi hiyo ni mali ya wananchi wa kata hiyo na wao wameitaka kampuni iwapimie maeneo yao ili waweze kufanya shughuli zao za kukuza uchumi na kwamba kampuni kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa yote ya kata hiyo walifanya mikutano na wananchi walipeleka taarifa kwenye mamlaka husika bila kupata majibu kwa wakati ambapo sheria inatamka muda wa majibu ukichelewa ina maanisha mpango umekubaliwa

Alieleza zaidi kuwa Kampuni hiyo imekubali kuwapimia wananchi maeneo yao ili kurasmisha mali zao na kuendeleza makazi holela waliyonayo, kuweka alama maeneo hayo, kuwatafutia wananchi hati za kumiliki maeneo yao,kuchonga barabara za eneo hilo kwa gharama nafuu kwa lengo la kuharakisha maendeleo kama masterplan inavyoelekeza.
 “Tunamtaka Mkurugenzi ndani ya siku saba airuhusu kampuni kuendelea na kazi iliyoelekezwa na wananchi endapo atakaidi agizo hilo wananchi wataamua vinginevyo ikiwa ni pamoja na kufanya maandamano ya amani ili kushinikiza Mgurugenzi na Afisa Mipango miji waondolewe kwenye nafasi zao na kumpeleka mahakamani,” lilisema azimio hilo.

Mwisho.