Marehemu Edith Kambona
Na Steven Augustino,Tunduru
MAELFU ya wakazi wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma walijitokeza kumzika mwasisi wa Tawi la Chama cha TANU katika Tarafa ya Nampungu Wilayani humo marehemu Edith Angela Kambona (73) pichani aliyefariki akiwa nyumbani kwake mtaa wa Extended Tunduru mjini.
Akizungumzia tukio hilo mume wa marehemu kambona, Mzee Jerome Kambona alisema kuwa mkewe alifariki ghafla usiku wa kuamkia septemba 1, mwaka huu 2011 baada ya kupatwa na homa ya shinikizo la damu.
Akisoma wasifu wa marehemu katika maziko yaliyofanyika katika makaburi yaliyopo nyumbani kwao, msemaji wa familia hiyo Emmanuel kambona alisema kuwa marehemu ambaye alizaliwa mwaka 1938 alimaliza elimu ya msingi katika shule ya msingi Mindu mwaka 1957 na baadae kujiunga na shule ya wasichana ya Newala Middle School kuanzia mwaka 1958/1959 na baadae kujiunga na masomo ya uuguzi katika chuo cha Tukuyu Mkoani Mbeya.
Taarifa hiyo iliendelea kufafanua kuwa baada ya kumaliza elimu hiyo pia wakati wa uhai wake, marehemu Kambona ateuliwa kuwa Mwenyekiti na muasisi wa chama cha Tanu katika Tarafa ya Nampungu kuanzia mwaka 1962 wadhifa ambao aliutumikia kipindi cha mwaka mmoja ambapo mwaka 1963 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Tunduru hadi mwaka 1969.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mwaka 1970 marehemu Kambona aliteuliwa kuwa Katibu Tarafa na kutumikia wadhifa huo katika Tarafa za Kidodoma, Ligunga, Matemanga, Namasakata,Nampungu Wilayani Tunduru na Tarafa ya Lipalamba Wilayani Mbinga Mkoani Ruvuma nafasi aliyoitumikia hadi mwaka 1988.
Awali akisoma misa ya maziko ya marehemu kambona Padre Keneth Mathiani kutoka kanisa la Angalikana Tunduru aliwataka waamini wa madhehebu hayo kuzingatia maandiko ya vitabu vitakatifu ili waende kuishi maisha yenye furaha milele baada ya vifo vyao kama tuaminivyo kwamba Marehemu Kambona atapata tuzo hiyo vile aliishi kwa uadilifu wakati wote wa uhai wake
Aidha Marehemu Kambona wakati wa uhai wake akiungana na viongozi wenzake wa wilaya ya Tunduru ndio waliofanikisha adhima ya kuondoa njaa Tunduru kwa kauli mbiu ya Kunjatu ikiwa na maana ya kuondoa njaa Tunduru ,kampeni ambayo ilipelekea wakazi wote wa Tunduru kulima mazao ya chakula ekari mbili na mazao ya biashara ekali moja chini ya uongozi wa Kasapila aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Tunduru kwa wakati huo
Marehemu Kambona atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwa taifa hili hasa katika sekta ya elimu na jamii kwani alikuwa ana ndoto kubwa ya kuwaona watu wanaelimika kwa kusoma kwa bidii na kukataza utoro mashuleni na mamba kwa watoto wa shule
Marehemu ameacha Mgane, Watoto watatu, wajukuu 23 na vitukuu 14, mungu aiweke mahali pema peponi Roho yake, apumzike kwa amani amina.
Mwisho