Mhe. Mwenyekiti wa CCM, Ndugu H. Matete,
Katibu Tawala wa Mkoa, Ndugu Salum M. Chima,
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa,
Waheshimiwa, Wakuu wa Wilaya,
Bibi Joyce Mgana, na Dr. Rajabu Lutengwe,
Wah. Wabunge,
Meya, na Wenyeviti wa Halmashauri zote za Mkoa wa Rukwa,
Wakurugenzi,
Wakuu wote wa Idara,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Rukwa Ruka!, Sumbawanga Ng’ara!
· Awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hai.
· Pili napenda kuwakaribisha katika Kikao hiki, na poleni kwa safari kwa wale mliotoka mbali.
Nachukua pia nafasi hii kuwakaribisha watumishi wageni wote waliohamia katika Mkoa wetu katika kipindi cha kuanzia Oktoba mpaka leo. Ni imani yangu kuwa wataungana na viongozi, pamoja na watumishi wenzao kuhakikisha kuwa Rukwa inaruka na Katavi inaimarika zaidi.
Waheshimiwa wajumbe,
Nichukue pia nafasi hii kwanza kuwashukuru sana ninyi Wajumbe kwa niaba ya wananchi wote kwa jinsi tulivyoshirikiana katika matukio yote makuu na ya muhimu katika Mkoa wetu wa Rukwa na Katavi. Naishukuru sana Kamati yangu ya Ulinzi na Usalama, Chama cha CCM na Vyama vya Siasa, Wakuu wa Idara mbalimbali, Watumishi wote, Wafanyabiashara, Wawekezaji na Wananchi wote kwa ujumla, kwa kufanikisha shughuli hizo kwa umakini mkubwa.
Shughuli kuu zilizofanyika ni pamoja na:-
1. Kongamano la Uwekezaji la Ukanda wa Ziwa Tanganyika ambalo lilifanyika tarehe 17/10/2012 mjini Mpanda, Kongamano hilo lilifunguliwa na Mgeni wetu rasmi Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Waliohudhuria wengine ni pamoja na Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda Mbunge wetu, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mary Nagu, Waziri wa Uwezeshaji na Uwekezaji katika Ofisi ya Rais, Mabalozi 34 kutoka nchi mbalimbali, Wakuu wa Mikoa 3 kutoka Kigoma, Mheshimiwa Issa Machibya, ambaye pia alikuwa muandaaji wa Kongamano, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Fatma Mwase, na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mheshimiwa Joseph Simbakalia, pia Wadau mbalimbali wa makampuni na mashirika ya umma, na kwa namna ya pekee wananchi wenyewe.
Kwa upande wa Vyama vya Siasa, Chama Tawala CCM chini ya Mwenyekiti wake wa Mkoa Ndugu H. Matete walishiriki, pamoja na Chama cha Chadema.
2. Mapokezi ya Mwenge yalifanyika kwa ufanisi mkubwa.
3. Tulifanya Tamasha la Wana Rukwa na Katavi kuanzia tarehe 25 – 27/11/2011 katika kijiji cha Makumbusho Jijini Dar es Salaam.
Tamasha hilo lilifana sana, hivyo napenda kuwapongezeni wote mlioshiriki katika kuandaa tamasha hilo, wakiwemo wazee wa mila, Viongozi wa Serikali pamoja na Wafanyabiashara wetu, na nimtaje ndugu Sumri kwa kutuweka vizuri kiusafiri
Aidha, nawashukuru na kuwapongeza sana Wana Rukwa na Katavi, waishio Dar es Salaam, chini ya Mwenyekiti Bibi Mwangaza Mwanisongole kwa kufanikisha tamasha hili kwa kiwango kikubwa.
Tamasha hili lilifunguliwa na Mheshimiwa Dkt Mohammed G. Bilal Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kufungwa na Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda (Mb) na Waziri Mkuu.
4. Miaka 50 ya Uhuru tuliadhimisha mjini Namanyere katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi 9/12/2011.
5. Tulipata Mgeni, ambaye ni Makamu wa Rais Dkt Mohammed Gharib Bilal kuanzia tarehe 18 – 24/2/2012 katika mikoa yetu ya Rukwa na Katavi. Ziara yake ilikuwa ya mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano mkubwa kati ya Chama Tawala na Serikali, Vyama vingine vya Siasa pamoja na wananchi wote waliohudhuria kwa wingi kwenye mikutano, kwa utulivu na heshima kubwa. Nawashukuruni sana.
6. Maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani yalifanyika tarehe 8/3/2012 Mjini Sumbawanga, na yalikuwa mazuri.
Pamoja na taarifa hizo ili ngoma inoge kuna wenyewe, hivyo basi nawashukuru sana Waandishi wa habari wa Mkoa wangu wa Rukwa pia Katavi pamoja na rafiki zao wa vyombo mbalimbali kwa jinsi wanavyotuunga Mkono na kuisaidia serikali ya Mkoa wa Rukwa, na taifa kwa ujumla. Pia navishukuru vikundi vya ngoma.
Mambo mengine muhimu.
1. Barabara zetu zinaendelea kujengwa vizuri kwa kiwango cha lami, japo katika zile tunazogharimia sisi wenyewe (Serikali ya Tanzania) zinakabiliwa na upungufu wa fedha kutokana na majukumu mbalimbali ya serikali ikiwemo umeme, madeni ya watumishi kama Madaktari, Walimu n.k.
2. Mkoa umeanzisha mpango wa Sumbawanga Ng’ara tuuunge mkono pamoja na Halmashauri zote zing’are.
3. Napenda kuwataarifu kuwa madaktari wetu wa Mkoa wa Rukwa pamoja na wauguzi wote wa Mkoa wetu kwa kweli hawakugoma kabisa katika migomo yote miwili. Wametujali sana wana Rukwa, na wametupa heshima kubwa sana na wamethamini sana uhai na maisha yetu. Mkoa utaangalia namna bora zaidi ya kuwapongeza. Lakini kwa kuanzia naomba niwapongeze wote katika Kikao hiki.
Kwa namna ya pekee nakiomba kikao hiki kiazimie pongezi kwa Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi alivyoshughulikia mgomo huu wa madaktari na kwa kuridhia kutupatia Mkoa mpya wa Katavi baada ya Mkoa wetu kugawanywa.
Waheshimiwa wajumbe, kutokana na ukubwa wa jiografia na maumbile ya Mkoa wetu tunashauri kuwa serikali ione uwezekano wa kuongeza ukomo wa bajeti. Na kwa vile Mkoa wa Rukwa umegawanywa, basi ni vema Mkoa wa Rukwa uendelee na ukomo wa zamani na Mkoa wa Katavi upewe ukomo mpya.
Waheshimiwa wajumbe, katika kuandaa bajeti ya mwaka huu kama ilivyoelezwa na Katibu Tawala wetu ndugu Chima, Mkoa unaazimia kuweka kipaumbele katika kumaliza miradi iliyopo na kuwa na miradi michache ili ikamilike na kutoa matukio badala ya kuwa na miradi mingi isiyoisha. Hali hiyo ni kuharibu fedha kidogo tunayopata bila kupata matukio mazuri.
Waheshimiwa wajumbe tunayo mengi ya kujadili, muda hautoshi, na naona hali ya RAS wetu kimfuko ni mbaya, lakini kikao hiki ni muhimu sana ikizingatia kuwa ni dira ya bajeti. Naomba tuchangie kwa makini ili kuufanya mkoa wetu uruke.
Kikao kimefunguliwa