About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Friday, September 20, 2013

WAZIRI AMTISHA JK

Na, Betty Kangonga

WAZIRI wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe amemtisha Rais Jakaya Kikwete akisema kuwa endapo hatasaini muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013, atakuwa ameingia kwenye mgogoro na Bunge.

Muswada huo uliopitishwa hivi karibuni na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Augustine Mrema wa TLP (Vunjo), unapingwa vikali na vyama vya upinzani pamoja na makundi mbalimbali ambayo sasa yanamshinikiza rais asiusaini kuwa sheria.

Makundi hayo ambayo yamepata msukumo wa vyama vitatu vya CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi ambavyo wabunge wake walikataa kuujadili muswada huo wakipinga uchakachuaji uliofanyika wa kuongeza vifungu na kutoishirikisha Zanzibar, tayari yametishia kwenda kortini ikiwa watapuuzwa.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Chikawe alisema kuwa ni vyema makundi mbalimbali yakaacha kumlaghai Rais Kikwete ili asiusaini muswada huo.

Kwa mujibu wa Chikawe, iwapo Rais Kikwete ataliafiki suala hilo la wapinzani na makundi mengine, na kuacha kutia saini muswada huo, atakuwa ametengeneza mgogoro na mhimili wa Bunge kutokana na chombo hicho kukamilisha kazi yake.

Alisema kuwa taratibu zote zilifuatwa kuhusiana na kupitishwa kwa muswada huo, na kudai kushangazwa na baadhi ya makundi yanayopiga kelele.

“Hao wanaolalamikia juu ya jambo hilo hawatendi haki kwani sheria zote zilifuatwa na hayo mapendekezo wanayotoa ya kutaka Rais Kikwete asitie saini sio sahihi hata kidogo, huko ni kutaka ‘kumblack mail’ na kumsababishia mgogoro na Bunge,” alisema.

Waziri Chikawe alisema kuwa ameshangazwa na baadhi ya matamshi yanayotolewa juu ya kuwepo kwa fujo au kumwagika damu na kusema jambo hilo haliwezi kufanikiwa kama halijapangwa.

“Fujo zinapangwa, hivyo wale wanaotaka kumwaga damu ni vyema wakajitaja na kusema kuwa ‘sisi tutamwaga damu’ kwa kuwa naamini damu haiwezi kumwagika yenyewe,” alisema.

Waziri huyo alisema kuwa ni vyema wale wanaotaka kuzunguka kwa wananchi na kufanya udanganyifu juu ya suala hilo, wangekubali kuwasilisha hoja hizo ndani ya Bunge na si mahali kwingine.
Kuhusu Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kutopeleka muswada huo kwa wananchi wa Zanzibar, 

Chikawe alisema kuwa utaratibu uliotumika ni hisani tu, kwani hakuna sheria inayotaka muswada wa aina yoyote kupelekwa kwa Watanzania.

“Utaratibu wa kupitisha muswada huo sio huo tu, bali zipo njia nyingi ambapo anaweza kuandika anayohitaji na kuwasilisha kwa kamati ya Bunge na wapo waliofanya hivyo,” alisema.
Chikawe aliongeza kuwa inawezekana Kamati ya Katiba na Sheria ikawa na  sababu za kushindwa kuwafikia wananchi wote, lakini kwa upande wao walipokea maoni ya Serikali ya Zanzibar yaliyotolewa Mei 27, mwaka huu.

Alisema kuwa moja ya pendekezo lililotolewa na Serikali ya Zanzibar ni juu ya kuongezwa kwa siku 20 kati ya 70 zinazotakiwa kutumiwa na Bunge Maalumu la Katiba.
Chikawe alisema kuwa ni vyema yale yanayoenda kutolewa kwenye mkutano wa wapinzani kesho katika viwanja vya Jangwani, yangepelekwa bungeni kwa kuwa hata wakitoa katika viwanja hivyo haitasaidia.


ju





Thursday, September 19, 2013

WAANDISHI WAKWIDWA , WANYANYASWA NA KUPOKEA KIPIGO




Na Dixon Busagaga, Moshi

WAKATI watuhumiwa wanne zaidi wakiongezwa katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini ya tanzanite mkoani Arusha, Erasto Msuya, waandishi wanaoiripoti jana walionja joto ya jiwe kwa kukwidwa na kutaka kunyang’anywa vitendea kazi vyao.

Tafrani hiyo ilitokea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Moshi saa 5:30 wakati kesi hiyo inayowakabili washtakiwa saba wanaodaiwa kushiriki kupanga na kutekeleza mauaji ya Msuya ilipofikishwa mbele ya mahakama kwa ajili ya kutajwa.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa waandishi hao, Fadhili Athuman alisema kuwa walipata wakati mgumu walipojaribu kuchukua picha za ndugu wa Msuya.

Athuman alisema kuwa baada ya kupiga picha kadhaa, alikwidwa na wanafamilia hao, wakitaka kumpora kamera huku mwandishi mwenzake akishikwa na kupigwa kibao.

“Baada ya kesi kuahirishwa iliibuka tafrani, walitaka kuninyang’anya kamera ili wafute picha nilizokuwa nimepiga. Mwenzangu yeye alikamatwa na kupigwa vibao kabla askari wa kikosi cha FFU kumuokoa,” alisema.

Kwa mujibu wa mmoja wa watu wa karibu na familia ya Msuya ambaye aliomba kuhifadhiwa jina, wamechukizwa na hatua ya baadhi ya waandishi kutochapisha picha za watuhumiwa, na badala yake zinatolewa za wanafamilia hiyo.

Hali ya taharuki ilianza mapema baada ya chumba kilichozoeleka kuendeshea kesi hiyo kubadilishwa kwenda kwenye chemba kutokana umati wa watu uliohudhuria kuwa mkubwa.

Wakati huo huo, vilio viliendelea kutawala mahakamani hapo baada ya kesi hiyo kuahirishwa. Mama mzazi wa Msuya, Marry Msuya alipoteza fahamu na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.

Awali mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Ruthi Mkisi, mawakili wa serikali, Stella Majaliwa akisaidiwa na Janeth Sipule waliieleza mahakama kuwa washitakiwa wanne wameunganishwa katika kesi hiyo na kufikia saba.

Majaliwa aliwataja waliounganishwa kuwa ni mshitakiwa wa nne hadi saba ambao ni Jalila Zuberi, Karimu Kihundrwa, Sadiki Jabiri (Chusa) na Joseph Mwakipasile ambao wote walifika mahakamani hapo.

Hakimu Mkisi alisema kesi hiyo imeahirishwa kutokana na upelelezi kutokamilika na hivyo kutaka washitakiwa hao kurudi rumande hadi Oktoba 2, mwaka huu.

Agosti 21, mwaka huu, washitakiwa watatu; Sharifu Mohammed, mkazi wa Kimandolu Arusha, Shaibu Mpungi, mkazi wa Kijiji cha Songambele wilayani Mererani na Musa Mangu mkazi wa Shangarai kwa Mrefu Arusha, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza.

Washitakiwa wote saba waliondolewa mahakamani hapo chini ya ulinzi mkali wa askari wenye silaha za moto wakiwa ndani ya gari lenye namba za usajili T 743 ADC lenye vioo vyeusi.

Msuya aliuawa Agosti 7 mwaka huu saa 6:30 mchana kwa kupigwa risasi 13 kifuani, kando ya barabara kuu ya Arusha – Moshi katika eneo la Mjohoroni wilayani Hai.

Friday, September 13, 2013





 Mkurugenzi  Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TGNP) U ssu Mallya

Na,Alpius Mchucha—Namtumbo

BAADHI ya wanawake wa wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,wamesema wangetamani  siku moja kuona katika katiba ijayo kunakuwa na kipengele maalum cha kuwabana wanaume wanaowakashifu wanawake kwa kutaja sehemu za siri za wanawake hao kwani tabia hiyo imekuwa ikiwadhalilisha sana kwa jamii na kuwavunjia heshima na utu wao.

Wakizungumza katika mdahalo wa siku moja jana uliowakutanisha wanawake zaidi ya 50 kutoka katika vijiji mbalimbali  vya wilaya hiyo wanawake hao walisema,wameshachoshwa na matusi yanayotolewa na wanaume ambayo yanataja sehemu za mwili wa mwamke hivyo ni lazima  kutafuta njia ya kukomesha kwakuwa matusi hayo yamewafanya kuonekana kama siyo watu wanaotoa mchango kwa jamii na  nchi.

Mdahalo huo wenye lengo la kujadili,kubadilishana uzoefu, kujifunza masuala ya  kijinsia na elimu ya uraia uliandaliwa kwa pamoja na shirika lisilokuwa la kiserikali la Oxfam na mradi wa kuwawezesha vijana wa Restless Devolopment ulifanyika katika ukumbi wa Parokia mjini Namtumbo.

Mmoja wa wanawake hao Christina Kuhimini alisema, sasa wameshachoshwa na  udhalilishaji dhidi yao  hivyo kuiomba serikali kutokuwa na huruma na watu hao  wasiokuwa na hata  chembe ya aibu ambao kila kukicha wanatafuta maneno mapya ya  kuwakashifu wanawake licha ya kutambua kuwa bila ya  mwanamke  basi hata wanaume hao wasingeweza kutokea hapa Duniani kwa kile alichoeleza kuwa hakuna binadamu anayeweza kuzaliwa na mwaume bila ya kuwa na mwanamke.

“bahati mbaya sana muda wa kutoa maoni kwa ajili ya katiba mpya umekwisha,lakini kupitia vyombo vya habari vilivyopo hapa leo naomba  sana watufikishie ujumbe wetu sisi wanawake wa Namtumbo tumechoshwa sana na matusi yanayotolewa na wanaume kila siku,tena ni mibaba mizima nayo utoa lugha za kuwakashifu wanawake ambao hawana hatia yeyote,ili siyo jambo jema hata kidogo ni baya linalowadhalilisha wanawake”alisema.

Aliongeza kuwa,  tabia hiyo  ya matusi licha ya kutaja maumbile ya ndani ya mwanamke lakini kwa bahati mbaya sana imekuwa ikiwarithisha watoto wadogo wanaohitajki kusikia au kufundishwa matendo  mazuri kutoka kwa watu wazima,lakini cha kushangaza hakuna hatua inayochukuliwa hivyo kuendelea kuota mizizi na kuonekana kama jambo la kawaida.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtandao wa polisi wanawake  na mratibu wa dawati la jinsia mkoani hapa Mrakibu wa jeshi la  polisi Anna Tembo alisema tatizo kubwa lililopo ni  wazazi kushindwa kuwafundisha maadili mema watoto wao tangu wakiwa wadogo hivyo kujikuta wakiiga tabia mbaya za mitaani ambazo hazina misingi bora kwao.

Pia amewataka wanawake kubadilika na kuanza kujitambua kwa kutojihusisha katika matukio yanayowafedhehesha ambayo yanawafanya kuonekana vituko kwa jamii ya kistaarabu na ambayo kwa kiasi Fulani yanawapa kiburi wanaume kufanya watakalo kwa wanawake.

Tembo alieleza kuwa,wanawake wengi wanafanya matukio   ambayo ndiyo yanayowapa hamasa wanaume kufikiria kuwa mwanamke ni chombo cha kutumika vibaya badala ya pambo ndani ya nyumba na kuendelea kuwafanyia unyama wa kila aina akina mama.

Alitaja uvaaji wa nguo fupi,  zinazobana na zinazoonesha maumbile yao,kucheza shoo nyakati za usiku katika sehemu za starehe,kujiuza, na hata ukatili kwa watoto navyo ni sababu kubwa ya kudhalilika kwao.
                 MWISHO

Wednesday, September 11, 2013

WANAJESHI WAJERUHI RAIA, KAMANDA AKANUSHA




Na Julieth Mkireri, Kisarawe

MKAZI wa Tondoroni, Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani, Omary Mohamed (47), amejeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa ni wanajeshi katika mapishano yanayodaiwa kuhusiana na kugombea mpaka.

Tukio hilo lilitokea juzi, majira ya saa 3 asubuhi baada ya wanajeshi hao kutembelea katika eneo lao na kukuta familia moja ikiwa imejenga nyumba katika eneo ambalo linadaiwa kuwa ni mali ya jeshi.

Inaelezwa wanajeshi hao walijaribu kuzungumza na familia hiyo kwa kuwasihi kuondoka, lakini hali hiyo iliibua mzozo mkali kutokana na wanafamilia kukaidi amri hiyo.

Hata hivyo, baada ya kuona hakuna maelewano, ghafla Mohamed alipigwa risasi moja na watu hao wanaodaiwa kuwa wanajeshi.

Baada ya tukio la kupigwa risasi kwa mwananchi huyo, wanajeshi hao walitokomea kusikojulikana na ndipo wananchi waliamua kufunga barabara hadi polisi walipofika na kwenda kutuliza ghasia.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ulrich Matei, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema majeruhi huyo amepigwa na kitu chenye ncha kali na kuwa bado haijajulikana kama waliomjeruhi ni askari ama la na kama amepigwa na risasi.

Alisema kuwa kwa sasa anafanya mawasiliano na kiongozi wa jeshi ili kubaini ukweli kama ni askari wa jeshi na wametumwa kwenda kwa wananchi hao au walikwenda wenyewe.

Kamanda Matei alisistiza kuwa si rahisi kumtambua askari kwa kuwa tu amevalia sare za polisi lakini pia ni lazima namba za wahusika zijulikane, kambi gani na uthibitisho kutoka kwa kiongozi wa jeshi kwani baadhi ya watu huvalia mavazi hayo kwa manufaa binafsi.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Tumbi, Peter Datani, amekiri kumpokea majeruhi huyo akiwa na jeraha kwenye mguu wake wa kulia, na hali yake inaendelea vizuri.