Waandishi wa Habari wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) Kanda za nyanda za juu Kusini Stephano Mango na Juma Nyumayo wakitambulishana Kiraghabishi kwenye warsha ya majadiliano ya pamoja kuhusu utafiti mdogo wa vyombo vya habari mwaka 2011 iliyofanyika kwenye ukumbi wa Saccos ya Walimu wa Songea Vijijini leo
WANAWAKE WATAKIWA KUACHA UWOGA WA KURIPOTI TAARIFA ZA UKATILI WA KIJINSIA
Na Stephano Mango,Songea
WANAWAKE nchini wametakiwa kuacha uwoga wa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwenye vyombo vya habari ili kuweza kujenga mazingira ya kukomesha ukatili mbalimbali wa kijinsia uliokithili miongoni mwa jamii za Kitanzania
Wito huo umetolewa jana na Naibu Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mariam Dizumba alipokuwa akichangia mada ya wadau muhimu wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) kwenye warsha ya majadiliano ya pamoja kuhusu utafiti mdogo wa vyombo vya habari iliyofanyika kwenye ukumbi wa Saccos ya Walimu wa Songea Vijijini
Dizumba alisema kuwa vyombo vya habari ni wadau muhimu sana katika harakati za ukombozi wa mwanamke wa kimapinduzi hasa wakati huu ambao taifa letu linaelekea kwenye miaka 50 ya uhuru ili kuweza kuzibaini changamoto mbalimbali za wanawake zilizokuwa zinawakabili wanawake miaka hiyo na sasa tuweke mikakati mingine ya kuzikabili changamoto za sasa
Akizungumza kwenye warsha hiyo ya siku mbili Mwanaharakati wa Mtandao wa Jinsia Nyanda za Juu Kusini Juma Nyumayo alisema kuwa vyombo vya habari nchini vimetoa mchango mkubwa sana katika harakati za kuleta usawa ,uwiano wa kijinsia na haki sawa za kijamii ili kuboresha ustawi wao
Nyumayo alisema kuwa kwa muda mrefu sasa vyombo hivyo vimeweza kusambaza taarifa za ujengaji wa vuguvugu la ukombozi wa wanawake wa kimapinduzi hasa wanaoishi pembezoni ili kukuza uwepo na upatikanaji wa habari na maarifa kuhusu harakati za ujenzi wa vuguvugu hilo na kusaidia kujenga mitandao na kuendeleza vuguvugu hilo
Kwa upande wake Mwezeshaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) Badi Darusi alisema kuwa lengo kuu la majadiliano hayo ya siku mbili ni kuelewa ni kwa kiasi gani vyombo vya habari vimeweza kuchangia katika kazi za Tgnp na kusambaza habari kupitia kampeni ya na harakati za ukombozi wa mwanamke wa Kimapinduzi mkoani Ruvuma
Darusi alisema kuwa washiriki watapata fursa ya kuwatambua wadau muhimu wa Tgnp katika ngazi za jamii,fursa na changamoto zao,kuainisha na kuchambua hatua zilizochukuliwa na katika harakati za Tgnp,kupima kiwango cha uelewa wa kuhusu Tgnp na Waandishi wa habari katika dhana ya majadiliano,dodoso,visa mkasa,maswali chokozi,kazi za vikundi na uchambuzi wa pamoja
Mwezeshaji toka TGNP Badi Darusi akieleza maudhui ya warsha hiyo kwa washiriki
Washiriki wa warsha hiyo wakisikiliza mada mbalimbali zilizowasilishwa na Mwezeshaji Badi Darusi