About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Thursday, January 19, 2012

RAIS KIKWETE AMESHINDWA KUTULETEA MAISHA BORA WANANCHI TUTIMIZE WAJIBU WETU

                                                      Rais Jakaya Kikwete
 Na,Stephano Mango,Songea
SINA hata chembe ya shaka kuwa,Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kutimiza ahadi yake ya kuleta  maisha bora kwa kila Mtanzania na badala yake anaamua kuzungumzia maafa na majanga mbalimbali katika kuhararisha kushindwa kwake kuzikabili changamoto zinazomkabili za kutimiza ahadi yake kama alivyotuahidi
Mgombea wa nafasi ya Urais mwaka 2005 Jakaya Kikwete wakati wa kampeni alituahidi kutuletea maisha bora kila mtanzania kwa ari mpya,nguvu mpya na kasi mpya,ahadi hiyo alishindwa kuitimiza katika kipindi chake cha miaka mitano
Kushindwa kwake huko yeye pamoja na wenzake Serikali wakajikita katika kueleza majanga na maafa mbalimbali kuwa ndio kikwazo cha kushindwa kutimiza ahadi zao ingawa mpango wowote mkakati kabla na baada ya kutekelezwa lazima kuwe na faida na hasara
Kitendo chao cha kushindwa kufahamu hilo iwe kwa bahati mbaya au kwa makusudi toka mapema ni ishara iliyodhahiri kuwa wameamua kutuona mabwege nasi kutokana na ukondoo wetu wa kushindwa kuwachukulia hatua viongozi wanaoshindwa kutimiza ahadi zao nao wanajiziuka na kujinyakulia rasilimali zinazotuzunga kila kukicha
Wanafanya hayo wakishirikiana na wawekezaji uchwala ambao wanakuja nchini wakiwa maskini wa kutupwa lakini baada ya muda mfupi wanakuwa na ukwasi wa kutisha na kuwaletea jeuri wananchi na wakati mwingine wakiwaua kama wanyama huku viongozi wetu wakikaa kimya na kuendelea kutuhubiria kuwa nchi yetu ni maskini
Wakipata fursa ya kusema viongozi hao utasikia kuwa ugumu wa maisha unaowakabili watanzania ni kutokana na kutetereka kwa mfumo wa fedha wa kimataifa na kuanguka kwa masoko ya hisa katika mataifa yanayoendelea ndiko kunakosababisha makali ya maisha nchini kuongezeka kutokana na hilo ambalo linasababisha sekta zinazochangia pato la taifa kuporomoka
Hilo linatokana na nchi yetu kwa kiasi kikubwa kutegemea mauzo ya bidhaa za nje, ikiwemo na utalii ambapo kuporomoka huko kwa biashara ya nje ni dalili mbaya kwa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu ambalo toka mwaka 2008 mpaka 2011 katika hotuba zake Rais Kikwete amekuwa akirudia mara kwa mara kuwa uchumi wa taifa unatarajia kukua kwa asilimia 7.
 Ahadi ya maisha bora iliyeyuka mchana kweupe huku watanzania wakiwaona viongozi wao walivyojaa tongotongo za aibu kwenye macho yao lakini kwa kutuona watanzania ni mabwege wakati wa kampeni za mwaka 2010 wakatuletea utani mwingine chini ya kauli mbiu ya Ari zaidi,nguvu zaidi na kasi zaidi
Hali ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watanzania katika kipindi cha utawala wa Rais Kikwete umedorora na viongozi wanashindwa kutoa mwanga stahiki wa kupambana chini ya kauli mbiu iliyowaingiza madarakani mwaka 2005 na 2010 badala yake wanatoa hutuba za kuaga mwaka bila kuonyesha utekelezaji wa ahadi na malengo stahiki
 Viongozi kulalamikia majanga na maafa kuwa ndio kikwazo cha kushindwa kutengeneza mazingira ya kukua kwa uchumi na kuleta maendeleo ya uchumi unaonyesha dalili za wazi kuwa uongozi huo umeshindwa kukidhi matarajio ya wananchi wake na kwa mtu mwenye akili alipaswa kusema jambo ili kupisha watu wengine wenye mawazo chanya kuongoza bila kuweka porojo katika hotuba
Uchumi ndio dira ya kufikia maisha bora kwa kila mtanzania hivyo kushindwa kutathimini madhara ya uchumi usiokuwa imara kwa viwango stahiki kwa taifa na kwa wananchi kuna leta hofu ya kuiona kesho iliyosalama kwa watanzania
Katika muktadha huo nimesikitishwa na maneno ya Rais Kikwete wakati akitoa salamu za mwaka mpya wa 2012 na kuuaga mwaka 2011 alikuwa anatuambia watanzania hali ya kiuchumi ya Taifa letu maneno ambayo yanamaana iliyosawa na hotuba zake zilizopita 
Alisikika akiwaambia watanzania kuwa kwa upande wa uchumi mwaka 2011 ulikuwa na changamoto nyingi ,kulikuwa na mchanganyiko wa ukame,uhaba mkubwa wa umeme,upungufu wa chakula kwenye baadhi ya  maeneo nchini,kupanda kwa bei za mafuta na vyakula, kushuka kwa thamani ya shilingi,mfumuko wa bei kupanda na sasa mvua nyingi na athari zake

Rais Kikwete aliendelea kusema kuwa pamoja na changamoto hizo tunatarajia uchumi wetu utakuwa kwa asilimia 7 ingawaje wenzetu wa IMF wanakadiria kuwa utakuwa kwa asilimia 6.3,hata kwa kiwango hicho bado nchi yetu inabaki kuwa ni miongoni mwa nchi 20 duniani zinazoongoza kwa ukuaji wa uchumi,Ni dhahiri basi kuwa kama athari hizo zisingekuwepo hali ya uchumi wetu ingekuwa bora zaidi

Hayo ndio maneno ya Rais Kikwete wakati akiuaga mwaka wa 2011 na kuwatakia watanzania heri na fanaka kwa mwaka mpya wa 2012 wenye mashaka ya uchumi na mbinu hafifu za kukuza uchumi ili wananchi wawe na uhakika wa kuishi kesho

Serikali imekuwa na mipango mahututi kabisa ya kuimarisha uchumi wa nchi na kuongeza thamani ya shilingi imebaki ikiendelea kuwakamua kila kukicha wananchi kile kidogo walichonacho kwa kuwaongezea gharama za vyakula,maji,umeme na mahitaji mengine ya kimsingi ya kibinadamu huku ikiwa imeshindwa kutengeneza miundombinu stahiki ya upatikanaji wa maisha bora
Kwa sababu ukuaji wa uchumi unapimwa katika ongezeko la uzalishaji, uwekezaji, utalii, kudhibiti mfumuko wa bei na ongezeko la thamani ya fedha hivyo huwezi kupata maisha bora katika mazingira yanayo onyesha kuporomoka kwa uchumi na kushuka kwa thamani ya fedha
Hadi sasa tayari baadhi ya viashiria katika ukuaji wa uchumi vimekumbwa na dhoruba, kwa mfano thamani ya shilingi yetu inazidi kuporomoka na uzalishaji wetu unasuasua na kusababisha kile kidogo kinachozalishwa kuuzwa kwa gharama kubwa.
Kipimo kimojawapo muhimu katika kujua ubora wa mwelekeo wa uchumi wa nchi yoyote ile ni thamani ya fedha yake ambapo ikiwa thamani ya fedha ya nchi yoyote inapungua basi ujue uchumi wake upo hatarini, na unahitajika kuratibiwa upya na kutafuta mbinu bora za kuufufua.
Thamani ya fedha kwa nchi ni muhimu katika kukuza uchumi wake na kusababisha kuleta maisha bora kwa wananchi wake kwani inaeleweka kuwa ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kiuchumi ni dhana mbili tofauti, ingawa kimsingi zinategemeana.
Tofauti yake ni kuwa maendeleo ya kiuchumi yanapimwa kwa viwango vya upatikanaji wa ubora katika huduma za kijamii kama vile, miundo mbinu,afya, elimu,makazi ya watu huduma za maji n.k.
Ambapo ukuaji wa uchumi unazingatia kiwango cha uzalishaji, thamani ya fedha,udhibiti wa mfumuko wa bei na mengineyo, lakini maendeleo ya kiuchumi yanapimwa katika upatikanaji wa huduma za ustawi kwa wananchi.
 Katika mazingira ya kawaida ukuaji wa uchumi ukiratibiwa vizuri unaweza kusababisha maendeleo ya kiuchumi na hapo ndipo kunako wezesha upatikanaji wa maisha bora
Kimantiki nchi ambayo imeshindwa kulinda thamani ya fedha yake ni ndoto kuleta maisha bora kwa wananchi wake na haina sababu ya kujidanganya kuwa nchi hiyo inapiga hatua katika ukuaji wa uchumi lakini sio kusingizia majanga mbalimbali ndiyo yanayosababisha gharama za maisha kupanda.
Mara kadha viongozi wa serikali wamekuwa wakijivunia ukuaji wa uchumi lakini wamekuwa wakikiri waziwazi kuwa bado kuna tatizo katika maendeleo ya watu na kukimbilia kusifia maendeleo ya vitu .
Kitendo cha kuporomoka kwa thamani ya shilingi kwa kiasi kikubwa tunako kushuhudia hapa nchini kina ashiria dalili za hatari katika maisha ya watanzania hata kama wataendelea kutupandishia gharama za umeme,maji,afya na bidhaa.
Wakati Rais Jakaya kikwete anaingia madarakani mwaka 2005, dola moja ya marekani ilikuwa inabadilishwa kwa sh 1,128,leo dola moja ya marekani inabadilishwa kwa sh 1,595 hii ikiwa ni ongezeko la sh 467 kwa dola moja kwa takribani miaka sita
Hali hii inaonyesha kuwa kwa miaka sita ya utawala wa Rais Kikwete fedha yetu imepungua thamani yake kwa mwendo wa kupaa ambapo kwa mwenendo huo maisha bora yaliyo ahidiwa yanabaki kuwa ndoto, jambo hili linathibitishwa na ukali wa maisha kwa watanzania walio wengi kuongezeka kila kukicha
Kwa sababu ukuaji wa kiuchumi unaweza kusababisha maendeleo ya kiuchumi hasa pale ongezeko la uzalishaji mali linapotumika katika kuboresha maisha ya jamii kwa kuhakikisha huduma za kijamii zinapatikana hususani afya, elimu,maji safi, uhakika wa lishe na mambo mengine yanayo husiana na ustawi wa jamii.
Kutokana na kuzama kwetu kiuchumi tunawajibika kila mmoja wetu kwa nafasi yake kutimiza wajibu wake katika kulinda rasilimali za nchi na kutumia kwa manufaa ya jamii pana ili tuweze kutengeneza ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kiuchumi kisha tuyafikie maisha bora kwani viongozi wetu wametudanya
Kama tungekuwa makini katika matumizi ya mapato yetu tusingekuwa na haja ya kutembeza bakuli kuomba misaada katika kutekeleza baadhi ya miradi kwa sababu sehemu kubwa ya fedha tunayoiomba kwa ajili ya maendeleo yetu kutoka kwa wahisani tunayo hapa hapa nchini na inaweza kutuletea maisha bora endapo ikitumika ipasavyo
Kitendo cha kukaa vijiweni bila kufanya shughuli za kimaendeleo zitakazo sababisha ustawi wa kimaisha na mazingira stahiki katika jamii hakutawezesha maisha kuwa bora hivyo,kufanya kazi kwa maarifa na bidii kunapelekea kukua kwa maendeleo ya kiuchumi na ukuaji wa uchumi wenyewe na Serikali tuidai kuweka mazingira bora kwa wananchi wake ili waweze kufanikiwa katika adhima ya kujiletea maisha bora siyo kupewa maisha bora na wao kwa sera chakavu
Mwandishi wa Makala
Anapatikana 0715-335051