Mkurugenzi
Mtendaji wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido Mhando
akizungumza na wafanyakazi wa MCL jijini Dar es Salaam jana. Picha na Venance Nestory
CHANZO: MWANANCHI
Dar es Salaam. Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Tido
Mhando amewaaga wafanyakazi wa kampuni hiyo baada ya kumaliza mkataba
wake wa miaka miwili na nusu.
Mkataba wa Tido katika kampuni ya Mwananchi utafika kikomo mwishoni mwa mwezi huu.
Taarifa ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Nation Media Group (NMG), Linus Gitahi
kwa wafanyakazi wote wa Afrika Mashariki ambako kampuni hiyo inamiliki
vyombo vya habari, inasema Mhando anaondoka MCL huku akiacha mafanikio
makubwa katika nyanja zote na kwamba atakumbukwa kwa mchango wake.
MCL ni kampuni tanzu ya NMG inayochapicha magazeti ya Mwananchi,
Mwananchi Jumamosi, Mwananchi Jumapili, The Citizen, The Citizen on
Saturday, Sunday Citizen na Mwanaspoti.
Kabla ya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa MCL mwaka 2012, Mhando alikuwa
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kati ya
mwaka 2006 na 2010. Awali alikuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili ya Shirika
la Utangazaji la BBC (1999-2006).
Mhando aliiwezesha MCL kukua kwa kasi kubwa katika mapato na katika
mpango wa uchapishaji wa magazeti ya MCL Kanda ya Ziwa ambako wakazi wa
mikoa hiyo sasa wamekuwa wakisoma magazeti asubuhi tofauti na zamani.
Wafanyakazi wa MCL walimpongeza kwa kuboresha masilahi yao kwa kipindi
cha uongozi wake na kuandaa misingi bora ya uongozi, ikiwamo kumwandaa
mrithi wake.
Akiwaaga wafanyakazi jana asubuhi, Mhando aliwashukuru kwa ushirikiano
wao pia alisema amejifunza mambo mengi mapya, ikizingatiwa kuwa kwa
miaka mingi alikuwa kwenye sekta ya habari ya utangazaji tofauti na
uchapishaji. “Safari hii ilinipa uzoefu mpya na wenye changamoto nyingi
lakini kupitia ushirikiano wenu wa dhati tulifanikiwa kuiweka kampuni
katika hali nzuri,” alisema Mhando.
Gitahi alisema nafasi ya Mhando itachukuliwa na aliyekuwa Ofisa Mwendeshaji Mkuu wa MCL (COO), Francis Nanai.
Nanai alijiunga MCL , Agosti mwaka jana akitokea Kampuni ya Saruji ya
Mbeya Cement (Lafarge Tanzania) ya mkoani Mbeya akiwa Mkurugenzi wa
Biashara.