ASKARI WAKITULIZA GHASIA JANA
Mmoja wa marehemu aliyeuawa kwa kupigwa risasi na Polisi
Na, Stephano Mango ,Songea
VURUGU zilizojitokeza wakati wa maandano ya amani ya wananchi wenye hasira kali katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma zimesababisha hasara kubwa ya mali zenye thamani ambayo haikufahamika mara moja na kwamba katika sakata hilo Askari Polisi wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuwapiga risasi za moto watu wawili ambao wamefariki kwenye maandamano hayo
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma Michael Kamuhanda alisema kuwa hali ya mji kwa sasa hivi ni tulivu na hatua mbalimbali za kiusalama zinaendelea kuimarishwa ili wananchi waendelee na shughuli zao za kila siku
Kamuhanda alisema kuwa kwenye vurugu hizo watu 54 walikamatwa na wamefikishwa Mahakamani kujibu tuhuma za kufanya maandamano bila kibali na kusababisha uvunjifu wa amani katika maeneo mbalimbali ya mji wa Songea na vitongoji vyake
Alisema kuwa Askari Polisi waliohusika na kupiga risasi raia kwa sasa wanahojiwa na Jeshi hilo ili kupata uhalali wa kutumia risasi za moto katika tukio la maandamano yaliyofanyika jana na kwamba ikidhibitika kuwa walifanya uzembe watachukuliwa hatua za kisheria
Alieleza zaidi kuwa wananchi wakiwa kwenye maandamano hayo walivamia Ofisi za Chama cha Mapinduzi Manispaa ya Songea na Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea Vijijini walipiga mawe milango na kisha kuchoma bendera na kuleta hasara za mali nyingine za chama hicho, walivamia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma,walivamia Ikulu ndogo walipiga mawe, walivamia Kituo cha Polisi na kupiga mawe na kuharibu baadhi ya magari ya wananchi
Alieleza kuwa waandamanaji walirusha mawe hovyo na kuwajeruhi wananchi wenzao, kufunga barabara kwa kutumia mawe makubwa, magogo na kuchoma mataili moto ili gari zinazoingia na kutoka nje ya mji zisiweze kuendelea na safari zake pia waandamanaji walivamia gari la Polisi na kuanza kurusha mawe na kusababisha Askari waanze kujihami kwa kurusha mabomu ya machozi
Alifafanua kuwa fujo hizo zinadaiwa kuwa zimetokana kwa sababu wananchi wamekuwa wakilalamikia matukio mfululizo wa mauaji mbalimbali likiwemo la mwendesha Pikipiki aliyeuawa februari 22 mwaka huu majira ya 2 asubuhi huko katika eneo la mto Matarawe, kuwa Jeshi la Polisi halichukui hatua ya kuwadhibiti wauaji hao
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Thomas Oley Sabaya alisema kuwa baada ya kutokea matukio hayo ameitisha viongozi wa Serikali za mitaa ya yote na kuwapa maagizo kuwa kuanzia sasa ulinzi shirikishi unatakiwa kuanza kwa kasi zaidi na kwamba kama kunawatu wanajihusisha na mambo ya uhalifu wajisalimishe haraka kwenye vyombo vya dola badala kusubiri wakamatwe
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu amelaani kitendo kilichotokea juzi ambacho amesema sio cha kawaida hivyo kufuatia tukio hilo ameunda tume huru ya watu nane ambayo itafanya kazi ya siku saba ya kuchunguza kwa kina juu ya hali iliyojitokeza juzi mjini Songea na ripoti inapaswa kuwasilishwa arahamisi ijayo asubuhi ofisini kwake na kwamba hiyo tume inahusisha vyombo vyote vya dola
Baadhi ya wananchi wameiomba Serikali ichukue hatua za haraka kudhitibi hali iliyojitokeza juzi ambapo watu wawili waliuawa kwa kupigwa risasi na Polisi wakati wa wenye hasira kali walipokuwa wakipita mitaani kufanya vurugu huku wakidai kuwa Jeshi la Polisi limeshindwa kufanya kazi na mwingine kufa baada ya kutumbukia kwenye shimo na Pikipiki wakati wa vurugu hizo
Wananchi hao ambao ni wakazi wa maeneo ya Mfaranyaki, Majengo, Bombambili na Mjini ambao wameomba majina yao yahifadhiwe walisema kuwa hali iliyojitokeza juzi haikuwa ya kawaida hivyo ni vyema Serikali ikatafuta njia muafaka ya kudhibiti chanzo cha vurugu badala ya kujishughulisha na kuzuia maandamano ya amani ya wananchi na kwamba thamani yake haikuweza kufahamika mara moja
MWISHO
No comments:
Post a Comment