About


Karibu ujiunge na chuo cha kisasa cha Easy Tech.Computer kwa mafanikio yako,Walimu waliobobea katika fani hiyo wanapatikana chuoni hapo

elimak

elimak

Pages - Menu

Sunday, February 26, 2012

MADEREVA YEBOYEBO WAMTEMEA NYONGO RC MWAMBUNGU RUVUMA

                              MKUU WA MKOA WA RUVUMA SAID MWAMBUNGU
Na Kassian Nyandindi, Songea

MADEREVA wanaoendesha pikipiki maarufu kwa jina la 'yeboyebo' katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, wamemlalamikia mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu wakisema kuwa chanzo cha machafuko na mauaji ya raia wawili waliopigwa risasi na askari polisi, yametokana na jeshi hilo kupuuza taarifa za uhalifu zilizokuwa zikitolewa na wakazi wa manispaa hiyo.

Malalamiko hayo yalitolewa na madereva hao kutokana na vifo vingi vinavyojitokeza katika manispaa hiyo wengi wanaouawa ni wao, walipokuwa wakizungumza katika kikao kilichoitishwa na mkuu wa mkoa huo kwa lengo la kujenga ushirikiano baina ya serikali na madereva hao ili machafuko yaliyotokea hivi karibuni yasiweze kuendelea.

Akichangia hoja katika kikao hicho mmoja kati ya madereva hao  Bonventura Njogopa, alisema kuwa mara nyingi askari polisi wapelelezi wamekuwa wakikaa vijiweni katika maeneo ya mjini na kuwafuatilia madereva hao kwa madai kwamba wanajihusisha na vitendo vya ujambazi wakati sio kweli badala yake walimweleza Bw. Mwambungu kuwa askari hao ni vyema muda mwingi wawe wanazunguka pembezoni mwa mji ambako mara nyingi wamekuwa wakijificha majambazi.

"Mheshimiwa mkuu wa mkoa askari wako wapelelezi wanatuambia sisi ndio chanzo cha kuwepo kwa majambazi, hii si kweli sisi ni raia wema tunachohitaji waache kukaa muda mwingi vijiweni hapa mjini badala yake wawe wanazunguka na sehemu zingine katika mji wetu wa songea ambako ndiko wahalifu wengi wanajificha", alisema Njogopa.

Naye Ali Omary alisema kwa muda mrefu polisi wamekuwa wakiwataka wao kama madereva wa pikipiki ambao huzunguka katika maeneo mbalimbali, kujenga ushirikiano na jeshi hilo kwa kutoa taarifa kwa njia ya simu au vinginevyo pale wanapobaini kuna dalili za uhalifu mahali fulani, lakini pamoja na wao kujitahidi kufanya mawasiliano na askari hao wamekuwa wakipuuzwa.

"Tunaiomba serikali yako hususani hawa polisi wakamate majambazi, lakini pia waache habari za kutuumiza sisi madereva wa pikipiki kwa kutupiga ovyo", alisema.

Pia walimweleza mkuu huyo wa mkoa kwamba askari wa usalama barabarani na polisi wa kawaida wote kwa pamoja wamekuwa wakijihusisha na ukamataji wa pikipiki jambo ambalo linawafanya washindwe kutambua nani hasa anapaswa kukagua vyombo hivyo vya moto.

Walielekeza malalamiko yao kwa mkuu wa usalama barabarani (RTO) mkoani Ruvuma  Sebastian Mtaki wakisema kuwa wanapotoa taarifa kwake, juu ya vitendo hivyo vinavyofanywa na askari wake hupuuzwa na hakuna hatua zinazochukuliwa.

"Utakuta pikipiki inakamatwa na kupelekwa kituoni, unapotakiwa kwenda kulipa faini ya makosa yako tunaambia tumfuate askari fulani kwenye baa fulani, je mkuu huu ndio utendaji halali wa kazi au ni ofisi zao binafsi", walihoji.

Kwa upande wake akijibu hoja hizo mkuu wa mkoa wa Ruvuma Mwambungu alisema kimsingi atafuatilia malalamiko yao na kuyafanyia kazi haraka na kwamba aliwataka kuheshimu sheria na taratibu zilizowekwa ili kuepuka uwezekano wa uvunjifu wa amani kama ilivyojitokeza siku mbili zilizopita.

Hata hivyo aliongeza kuwa ofisi yake imekwisha unda tume ya watu nane ambayo itachunguza machafuko na mauaji ya raia yaliyojitokeza mjini Songea na kutoa majibu kwake kwa kippindi cha siku saba zijazo.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment