Na Stephano Mango,Songea
MSINGI wa uchumi wa nchi kwa sasa ni lazima utazamwe katika kuanzisha na kufufua viwanda kwa ajiri ya maendeleo ya kiuchumi ili wananchi na taifa liweze kusonga mbele kwani kwa dalili zilizopo tutaendelea kulalamika na hatimaye kushindwa kujitegemea kabisa.
Ni wazi kuwa sehemu kubwa ya matatizo ya uchumi yanayoikabili serikali ya Rais Jakaya Kikwete, yana mizizi katika utendaji kazi wa awamu mbili zilizomtangulia kwani udhaifu ulijidhihirisha katika kupanga uchumi kwa maendeleo ya nchi
Kuna sura tatu za kuzingatia katika uchumi wa Tanzania na ule wan chi zote za Dunia ya tatu,kwanza ni dhaifu kiuchumi,pili kwa sehemu kubwa ni tegemezi kwa fedha kutoka nje,tatu,kadri utegemezi kiuchumi unavyoendelea ndivyo uhai wa kisiasa na kiuchumi utakavyoendelea kuwa tegemezi
Ufufuaji wa viwanda vilivyokufa na ujenzi wa viwanda vipya nchini uwe msingi mkubwa wa kuiondoa nchi hapa ilipo na kulijenga Taifa na watu wake wawe wenye uchumi imara ambao utasababisha kuwe na maendeleo ya vitu
Katika Dunia hii ambayo nchi zinazoendelea zinashindana kwa ujenzi wa viwanda,nasi hatuwezi kujiondoa kwenye sekta hiyo kama kweli tunataka kujikwamua kiuchumi ,kitendo cha kupuuza hoja hiyo ni kukimbilia kwenye uibuaji wa mipango mahututi ya kuokoa uchumi wa nchi na ile ya kuwajaza wananchi mabilioni ya Jk ambayo ni mipango mfu
Rasilimali tulizo jaliwa kuwa nazo hapa nchini hazitakuwa na maana kubwa kama zitashindwa kutumika katika kutokomeza umaskini wa watanzania kutokana na ukosefu wa ajira ambazo wangezipata kwa kuajiriwa kwenye viwanda ambavyo vingekuwa vinatumia rasilimali tulizonazo
Uwepo wa viwanda ni msingi mkubwa wa maendeleo katika nchi yeyote dunia licha ya kupunguza umaskini kutokana na watu wake kuajiriwa,pia husababisha wananchi kupenda bidhaa za kwao na kwamba fedha zinazotumika kununua bidhaa nje ya nchi kama vile viatu,kanga,vitenge,majembe,pini,sindano na bidhaa zingine ambazo zinaweza kutengenezwa hapa
Zingeweza kuchangia kasi ya mzunguko wa fedha ambapo matokeo yake yangeleta ustawi kwa wananchi na taifa kiujumla kwani pengo la wenye nacho na wasio nacho lingepungua sana na hata kupanda kwa gharama za maisha kungepungua
Ili kuweza kuleta hali chanya katika kuondokana na umaskini wa watanzania na uchumi goigoi,msingi wa kwanza ni kuasisi kwa makusudi uhusiano kati ya sekta mbili kuu za uzalishaji ambazo ni viwanda na kilimo ambapo sekta hizi zinaweza kuendelea kwa uhakika kama shughuli zake zitashabihiana na kutegemeana
Msingi wa pili ni kuweka uwiano wa ndani kwa hizi sekta mbili kwasababu ndani ya sekta ya kilimo kunapaswa kuwe na uwiano kati ya uzalishaji wa chakula na uzalishaji wa (mazao) malighafi za viwandani
Kati ya uzalishaji mkubwa na uzalishaji mdogo,kati ya mfumo wa sasa wa uzalishaji na ule wa kale,na kati ya uzalishaji binafsi na uzalishaji wa umma ambapo jambo muhimu hapa ni kuwa na kiunganishi kikuu katika kusukuma mbele maendeleo ya vingine
Hapa kiunganishi kikuu ni uzalishaji wa chakula kwasababu watu ambao ndio rasilimali muhimu na nguvu ya msingi kwa maendeleo hivyo lazima wale chakula bora kabla ya kupata nguvu ya kufanya mambo mengine
Msingi wa tatu ni kuwa na uwiano ndani ya viwanda ambapo idara muhimu katika sekta hii ni viwanda vikuu na viwanda vyepesi au vya kati,ikiwa jukumu la viwanda vikubwa ni kuvipatia viwanda vya kati mashine za uzalishaji mali
Kazi ya viwanda vikubwa ni kuzalisha mashine za kuzalisha mashine ambazo vinatumika kwenye viwanda vidogo kwa maana ya vipuri na kuondoa tatizo la kutegemea vipuri kutoka nje
Viwanda vya kati ni sekta inayozalisha bidhaa za walaji kama vile nguo,viatu,pamba(nyuzi),bia,zana za kilimo,vifaa vya kupasua mbao,mitambo ya maji na vingine vya aina hiyo ambapo pia viwanda vya kati ni sekta inayovigharamia viwanda vikuu kwa maana ya kuwa kule ambako inapata mashine na inatoa bidhaa za mlaji kwa watumishi wa sekta zote mbili
Siyo tu kwamba ujenzi wa viwanda vikubwa nchini ni muhimu katika kujenga msingi wa mapinduzi ya kiteknologia na uvumbuzi,bali pia unasaidia kuimarisha uwezo wa nchi katika kudhibiti vizuri mazingira
Katika mchakato wa maendeleo viwanda vikubwa vinajenga mabwawa ili kudhibiti mafuriko na kuhifadhi maji kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji,pia vinarahisisha kupeleka umeme vijijini,hatua ambayo ni muhimu na ya awali katika uwiano bora wa maendeleo ya viwanda,na upunguzaji tofauti ya maisha kati ya vijijini na mijini
Viwanda vikubwa ni muhimu pia katika kuendeleza mfumo imara wa uchukuzi na mawasiliano na kwa sababu ya umuhimu wake katika uchumi hakuna nchi iliyowahi kuendelea bila kuwa na viwanda vikubwa
Ni kutokana na nguvu ya eneo hili nchi zenye viwanda zimeweza kuzitawala na kuzidhibiti nchi maskini ikiwemo Tanzania ndio maana kutokana na maono stahiki ya kujenga Taifa linalopaswa kujitegeme,Serikali ya awamu ya kwanza ilijenga viwanda vingi vya kati ili kuondoa utegemezi kwa mataifa ya nje
Ilijenga viwanda vya nguo,mbolea,zana za kilimo na vya bidhaa karibu zote za mlaji,awamu hiyo ilifanikiwa kujenga viwanda vya kutengeneza mashine(Moshi Mashine Tools) viwanda vya kutengeneza magari(Nyumbu) kiasi cha kukaribia kujitosheleza kwa mahitaji ya ndani
Leo,viwanda hivyo havipo tena,vilitelekezwa,vikauzwa katika mkumbo wa ubinafsishaji,vikauawa na mabepari wa kimataifa ili kujenga na kuendeleza utegemezi wa Tanzania kwa bidhaa kutoka nje
Sababu nyingine ni ulimbukeni wa walioko madarakani na ushabiki unaoenezwa nao kwa bidhaa kutoka nje,jambo ambalo linaonyesha kujikana na kudharau chako na kuhangaika na bidhaa ambazo hawajashirikishwa
Kama nchi ingekuwa na watawala wabunifu wa maendeleo ya kweli,majengo ya minara pacha ya benki kuu yangejenga viwanda vingi ambavyo vingewezesha kuinua uchumi wa watanzania na nchi kiujumla lakini badala yake nchi imejiingiza kwenye ujenzi wa maghorofa yaendayo mawinguni na majumba ya anasa yasiyozalisha utajiri
Matumizi haya mabaya ya rasilimali yanafanya nchi kama Tanzania ziyapigie magoti mataifa makubwa kuomba mikopo zaidi,na wakati huo huo uchumi hauzalishi vya kutosha kuwezesha ulipaji madeni na riba ya mikopo hiyo
Misaada ya mabilioni tunatomwagiwa na nchi za China,Japan,Marekani na Uingereza na kufanya watawala kurukaruka kwa furaha kama ndama,ingekuwa ya manufaa zaidi kama ingetolewa kwa mfano wa viwanda ili kuliwezesha Taifa kujitegemea na kujiendeleza
Ilivyo sasa,ni misaada inayoongeza na kuimarisha utamaduni wa utegemezi kwani wanaotoa mikopo na misaada hawataki Tanzania iwe na ndoana wala ijue jinsi ya kuvua samaki kwasababu wanataka kila siku Tanzania na nchi za Dunia ya tatu zipige magoti langoni mwa tajiri na kuomba samaki
Ni wazi huu ni utumwa,je Mustapha Mkulo Waziri wa fedha na uchumi na wenzake Serikalini wanakubali kumeza dawa chungu ya kuponya ugonjwa unaolisumbua Taifa maskini lenye rasilimali zote muhimu zinazosababisha mchakato wa maendeleo kukamilika
Serikali inapaswa kuelewa kwamba bila ya kuweka mikakati bora,kasi ya ukuaji viwanda nchini itaendelea kuwa ndogo kama ilivyo sasa,hivyo inatakiwa kuona Serikali inaanzisha mpango wa kuendeleza viwanda na hatimaye kukuza na kuondoa umaskini
Mpango huo wa kuendeleza viwanda ni lazima uwe na sera na mikakati madhubuti ili ufanikiwe ambapo mbinu mbalimbali zina hitajika na mambo makuu mengine katika utekelezaji wenye ufanisi wa kuanzisha mchakato wa ufufuo na ujenzi wa viwanda kwa ukombozi wa Taifa letu
Mwandishi wa Makala haya
Anapatikana 0715-335051
www.stephanomango.blogspot.com
No comments:
Post a Comment