Aliyekuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa mafunzo ya Wawezeshaji Kongano Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya( MB) akimkabidhi Cheti cha kuhitimu mafunzo hayo mmiliki wa mtandao wa www.stephanomango.blogspot.com ,Stephano Mango,wa kwanza kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume Sayansi na Teknolojia Dkt Dugushilu Mafunda. wa kwanza kutoka kulia ni Wawezeshaji wa mafunzo hayo Dkt Flower Msuya na Mhandisi Peter Chisano
Mgeni rasmi aliyefunga mafunzo hayo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya (MB) akiwa kwenye picha ya pamoja naViongozi wa Tume ya Sayansi na Teknologia na washiriki wa mafunzo ya Wawezeshaji Kongano Tanzania yaliyofanyika Ukumbi wa The Beach Comber Hotel kuanzia Februari 27 hadi machi 1, 2012
NA STEPHANO MANGO,SONGEA
HAKUNA ubishi kuwa umaskini nchini Tanzania umebaki kuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya nchini yetu ingawa pia Tanzania ina matajiri wakubwa wachache na maskini wengi.
Kwa mtazamo wangu mtu maskini ni yule asiye na uchaguzi kwenye chakula, hawezi kuyakataa magonjwa wala ujinga katika maisha yake kwani kwake kila kitu ni kigumu na amekuwa sugu katika hali hiyo
Umaskini nchini umeota mizizi wanaishi kwa kipato duni sana kwani wengi wanaishi chini ya dola moja ya marekani kwa siku, umaskini upo mijini na vijijini watu wanatia huruma ukiwaona kutokana na ugumu wa maisha kutokana na sababu mbalimbali
Ikiwemo ya viongozi wetu wengi wanashindwa kutambua na kuifungua mifumo ya kiuchumi, kisiasa na hata kijamii ili kuwawezesha wananchi kwa wingi wao ili wawe washiriki na wadau muhimu katika kumiliki uchumi wao
Watanzania wengi kushindwa kuwa na maamuzi juu ya mustakabali wa Taifa lao leo na kesho kunaendelea kuwafanya wageni kutumia vibaya rasilimali tulizojaliwa kuwa nazo
Ni wazi kuwa watanzania tuna rasilimali za kutosha ambazo zinaweza kutukwamua kwenye tope zito la umaskini lakini hatujaweza kuzitumia vizuri na mbaya zaidi tumewaachia wageni ndio wamiliki na kuzitumia kwa ujeuri rasilimali zetu kwa muavuli wa uwekezaji
Hali hiyo inatufanya tuendelee kuwa maskini wa kutupwa na kujenga utamaduni mpya wa utegemezi kwa mataifa ambayo tumewaachia wachume mali zetu na kukimbizia huko kwao
Taifa letu, leo limekuwa na watu tegemezi kuanzia ngazi ya mtu binafsi, kaya, jamii, na hata Taifa, swali la kujiuliza sasa ni je tu wategemezi kwa kiasi gani na je, miaka 50 ijayo tunataka tuwe na Taifa la aina gani?
Utegemezi sio jambo zuri kwani unapunguza uhuru wetu, unatukosesha thamani, tunakosa sauti ya kimaamuzi na unatufanya tuwe wadogo mbele ya wahisani au wafadhiri tunaowategemea
Katika makala haya, nakusudia kujadili jambo chanya la kongano bunifu kama ishara ya kufanya mageuzi ya kiuchumi na kuondoa dhana ya utegemezi kama Taifa na jamii kiujumla kwani katika nchi nyingine jambo hili limesaidia kuinua na kuimarisha uchumi wao
Kongano bunifu zipo nyingi nchini ambazo ili ziweze kuleta mabadiliko ya kiuchumi katika ngazi ya kijamii hadi kitaifa zinahitaji kuunganika ili ziwe na nguvu ya pamoja katika soko la bidhaa kwa kushirikiana na sekta binafsi, serikali na wanataaluma katika kongano mahsusi kwenye maeneo mbali mbali hapa nchini kwetu.
Katika nchi nyingi ushirikiano huu umekuwa kichocheo kikubwa cha ubunifu ambao husaidia katika kutoa bidhaa zenye viwango na sifa zinazoweza kuhimili ushindani ndani na nje ya nchi kwa malengo kusudiwa
Kongano bunifu zina uwezo mkubwa wa kupunguza umaskini na kutoa nafasi nyingi za kazi kwa jamii pia vilevile Kongano hizi huleta mahusiano ya karibu sana kati ya wanachama wa kongano na wadau wengine wa maendeleo kama vile wanataaluma, sekta binafsi na serikali.
Wengi wanaweza kushangaa neno kongano bunifu kwani inawezekana halijazoeleka masikioni mwa watu wengi, ili niweze kuwatendea haki wasomaji na wananchi nieleze kidogo maana ya neno hilo
Kongano bunifu ni muunganiko wa shughuli za aina moja za wajasiliamali wenye malengo sawa na wanaofanya kazi katika eneo/ wilaya, mkoa na Taifa moja katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika shughuli yao
Mfano ni wachongaji vinyago, wahunzi, wakulima wa uyoga, mwani, alizeti, mahindi, maharage, ufuta mpunga, wavuvi, wafugaji kuku, watengenezaji batiki, wasindikaji wa mazao, wafugaji wa wanyama mbalimbali, wavuvi na vikundi vya wajasiliamali kama hao
Wajasiliamali wanaojishughulisha na ufugaji wa kuku katika wilaya nzima wanaweza wakatengeneza jukwaa lao(kongano bunifu) litakalokuwa linajadili namna bora ya kuimarisha ufugaji wa kuku ,soko, mitaji, changamoto nyingine zinazowakabili katika kufikia hali stahiki, hiyo ndiyo maana ya kongano bunifu
Kwa kutambua umuhimu wa kongano bunifu katika kuleta uchumi imara wa jamii na Taifa, kuanzia februari 27 hadi machi 1, mwaka huu wa 2012 Tume ya Sayansi na Teknolojia nchini iliweza kutoa mafunzo kwa wawezeshaji kongano katika ukumbi wa The beach Comber, jijini Dar es Salaam
Washiriki wa mafunzo hayo walitoka Tanzania bara na Visiwani ambapo jumla ya washiriki 46 kutoka kwenye kongano 26 nchini walifanikiwa kupata mafunzo hayo muhimu yenye lengo la kukuza kukuza uwezo wao katika kuhamasisha na kuanzisha ushirikiano kati ya sekta binafsi, serikali na wanataaluma katika kongano mahsusi kwenye maeneo mbali mbali hapa nchini kwetu.
Ili washiriki waweze kupata ujuzi wa kuweza kuimarisha kongano ambazo ziko katika mazingira wanakofanyia kazi ili kukuza mkakati wa kuongeza Ubunifu na Ushindani wa sekta binafsi kupitia kongano bunifu kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi nchini
Wawezeshaji wa mafunzo hayo walikuwa watanzania ambao ndio wamekuwa wawezeshaji katika nchi za Nigeria, Msumbiji, Ghana, Senegal, Tanzania na Kenya ambao ni Dkt Flower Msuya, Sostenes Sambua na Peter Chisano
Washiriki wa mafunzo hayo waliweza kutoa elimu stahiki ya kuimarisha kongano bunifu katika katika maeneo ambayo washiriki wanatoka ili ziweze kuwa na nguvu moja katika kufanya wazalishaji watengeneze bidhaa bora zenye kukidhi ushindani katika masoko ya ndani na nje.
Kutokana na hilo na kila mmoja akatimiza wajibu wake tuna kila sababu ya kuongoza bara zima la Afrika katika kuonyesha umuhimu wa Kongano bunifu jinsi zilivyoweza kusaidia katika kuongeza pato la taifa, ajira na maendeleo ya jamii , uchumi, ubunifu na Ushindani wa Taifa katika masoko ya nje
Ni vema sasa nchi ikaanza kuendeleza dhana ya kongano bunifu kama njia ya kufikia maendeleo ya kiuchumi nchini kwa kushirikisha wajasiliamali kutumia vema fursa zilizopo za maliasili zetu ili ziwe nguzo kubwa katika kufikia lengo stahiki
Kuanza upya kimtazamo ni fursa ya kubadilika na kuchukua mambo mazuri mapya ambayo kutoka kwa wengine au pale yanapopatikana hata ndani yetu kutasababisha kutuondoa kwenye utegemezi wa kiuchumi na kuondokana na umasikini uliokithili nchini
Kesho ya Tanzania hatuwezi kuongelea bila leo na kila tunachopanda leo ndicho tunachovuna kesho, hivyo msingi wa leo tuliujenga jana uwe mbovu au mzuri pia kwa sababu leo ipo kwa sababu ya kesho ipo na jana ilikuwepo basi leo tunapaswa kubadilika ili tuijenge vyema kesho yenye neema
Leo tukianza upya basi kesho tutazaliwa upya na tukizaliwa upya ndipo hapo tunapopaswa kuwa , hivyo kujifunza na kuanza upya ni ujasiri na ni njia ya kuleta mabadiliko katika dunia ya leo bila kujali gharama za kufanya hivyo
Tuanze upya kwa kuwa wajasiriamali mahiri chini ya kongano bunifu kwani ujasiriamali ni ile hali, uwezo na mkakati au mchakato wa kubuni, kuanzisha, kuendesha na kumudu shughuli halali ya maendeleo ya kiuchumi
Tunahitaji ujasiliamali wa kujiamini, kuthubutu, kubuni na kuendeleza zao tokeo la ubunifu huo kwa kuleta faida chanya katika maisha yake, jamii na Taifa kiujumla kwani ujasiliamali ni nguzo muhimu kwa uchumi wa kisasa wa karne ya 21
Dhana ya ujasiliamali inatimia endapo hali ya kugundua au kubuni biashara mpya au kuiendeleza ile ya zamani kwa ajili ya kuwekeza na kutoa huduma stahiki kwa jamii pana, hivyo tuamue sasa kuwa katika hali hiyo katika jukwaa la dunia ili kuzifaidi fursa za uchumi za ndani na nje ya nchi
Uchumi wa dunia umebadilika, uchumi wa soko katika utandawazi ndio unashikilia mfumo wa kiuchumi wa dunia ili kuharakisha maendeleo kwa kutoa ajira mbadala kwa kujiajili, kujitegemea na kujenga uwezo wa kujiamini katika maisha na biashara kubwa dhana ya ujasiliamali chini ya kongano bunifu inahitajika
Wahenga walisema huwezi kuzuia sikio lako kusikia lakini unaweza kuzuia mdomo wako usiseme, nami kwa hakika nasema nauzuia mkono wangu usiandike zaidi lakini siwezi kukuzuia msomaji kuendelea kusoma
Mwandishi wa Makala
Anapatikana 0715-335051
www.stephanomango.blogspot.com
No comments:
Post a Comment