NA STEPHANO MANGO, SONGEA
MAJIGAMBO na tambo za viongozi, wagombea na wapambe wa vyama vya siasa viwili vilivyoshiriki kwenye kampeni za kuwania kiti cha udiwani Kata ya Lizaboni Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma vimefikia tamati kwa wananchi kupiga kura kumchagua diwani waliokuwa wanamtaka
Wakati wa kampeni wananchi wa Kata ya Lizaboni walipata fursa ya kusikiliza sera za vyama hivyo ambapo wapigakura hao walihitimisha kwa kufanya uchaguzi wa kiongozi waliyemhitaji aprili mosi mwaka huu na kumfanya aliyekuwa mgombea wa Chadema Alanus Mlongo kuibuka kidedea katika uchaguzi huo.
Uchaguzi huo mdogo umefanyika baada ya Kata hiyo kuwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo Ally Said Manya(CCM) pia alikuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambaye alifariki dunia julai mwaka 2011.
Licha ya kampeni hizo kutawaliwa na vijembe, malumbano na kauli chafu kati ya vyama na wagombea, lakini wananchi wa Kata ya hiyo walizingatia sera zilizoonekana kuwa na tija kwao, ambazo pia zinatekelezeka na kumchagua kiongozi waliyekuwa wanamtaka kwa njia ya kumpigia kura.
Katika uchaguzi huo wapigakura waliopo kwenye orodha ya kudumu kwenye daftari la wapigakura walikuwa ni 7825 lakini waliopiga kura ni 3315 jambo ambalo limeonyesha wazi kuwa wakazi wengi wa Kata hiyo hawakuweza kujitokeza kupiga kura licha ya mgombea wa Chadema kupata kura 1712 wakati Mgombea wa Chama cha Mapinduzi katika Kata hiyo George Oddo Mbunda alipata kura 1579.
Nawapongeza wananchi wa kata ya Lizaboni waliotimiza wajibu wao wa kikatiba katika uchaguzi huo na kumpigia kura kiongozi ambaye alionekana kukidhi matakwa ya wananchi kutokana na sera alizokuwa anazinadi wakati wa kampeni.
Matokea hayo ni salamu tosha kwa viongozi wa Ccm na wa Serikali kuhusu kupuuza haki na matakwa ya wananchi huku wakibeza kuwa kelele za mlango hazimsumbui mwenye nyumba, pamoja na kuwa vijana wengi wanaoshabikia upinzani hawana shahada za kupigia kura
Hayo ni matokeo ya mbinu dhaifu za kimkakati zilizokuwa zinafanywa na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Songea mjini chini ya uwenyekiti wa Hemed Dizumba za kuamua kufanya siasa za kihuni katika kampeni zilizopita na za uchaguzi huu mdogo wa udiwani
Kitendo chake cha kukataa baadhi ya maoni yaliyo wazi na yaliyojificha yaliyokuwa yanatolewa na wadau wa chama hicho katika kuhakikisha chama hicho kinaibuka ushindi katika Kata hiyo ndiko kulikosababisha Chama cha Chadema kiibuke na ushindi na kuongeza idadi yake ya madiwani na kufikia nane sasa kupitia chama hicho
Siasa za kihuni kwa sasa hazitakiwi zitumike katika chama kikongwe kama Ccm ambacho kimepoteza dira machoni na mioyoni mwa watanzania, hivyo kufanya kampeni dhaifu zilizogubikwa na kwaya, mashairi, ngonjera na lugha zilizokosa staha hakuwezi kukivusha chama hicho katika chaguzi zinazokuja
Katika wimbi kubwa la ufisadi, ukosefu wa ajira kwa vijana, migomo na maandamano ya makundi mbalimbali na kila aina ya uchafu ambao Serikali ya Ccm inatupiwa huwezi kumtegemea hata kwa akili ndogo kiasi gani Lukas Ngongi, Grayson, Juma Kangala na Hamis Abdalah Ally waweze kuleta ushindi kwa mgombea yoyote yule ndani ya chama hicho kinachojichimbia kaburi
Ni watu ambao hawawezi kujenga hoja zenye mantiki katika kuleta ushindi stahiki kwasababu popote wanaposimama hawawezi kuzungumza lugha zenye staha, kueleza mikakati ya ushindi, kujibu hoja kwa mpangilio na kueleza miradi ambayo inatekelezwa na Serikali ya mtaa na hata ya wilaya katika maeneo wanayoishi
Kutokana na tabia zao ambazo zimejaa utata watu wenye akili timamu,hawawezi kushawishika na maneno yaliyojaa dhihaka, matusi katika jukwaa la kampeni walilokuwa wanalitumia watu wa Ccm kumnadi mgombea wake George Oddo na badala yake watu walikuwa wanazibeza kampeni zao kwasababu zimejaa hadithi tupu
Badala ya kujikita kueleza utekelezaji wa miradi mbalimbali uliofanywa na aliyekuwa Diwani wa Kata hiyo marehemu Said Ally Manya, wao wanahangaika kutoa ahadi au kumshambulia mtu ambaye hana uhusiano na ugumu wa kampeni waliokuwa wanaupata katika kampeni hizo
Kitendo cha uongozi wa Ccm kuwaweka watu hao waliojaa siasa za majitaka ambao walikataliwa kabla ya kuanza na baada ya kumaliza kampeni hizo ndiko kulikosababisha fedheha kubwa kwa wananchi kukataa kushabikia chama hicho wakati wa kampeni zake na mwisho kukataliwa katika uchaguzi huo na kuonyesha uhai mdogo siku za mbeleni na hasa katika uchaguzi mdogo wa Mletele
Hakuna sababu yoyote ya msingi utakayoambiwa na viongozi wa Ccm wilaya ya Songea mjini na wapambe wao kuhusu anguko kubwa tunalolishuhudia hivi sasa kwa wapinzani kuchukua kwa kasi ya ajabu uongozi kuanzia serikali za mitaa na sasa udiwani ambapo madiwani wa upinzania wanaingia kwa kasi kubwa
Washabiki wa chama cha Ccm kila siku wanaendelea kuamia upinzani huku waliobaki huko wakiwa wamekata tamaa kabisa na wengine wakiwasha endiketa ya kutaka kukimbilia chama hicho ambacho kimejaa majungu na siasa za kuviziana kila kukicha
Dizumba na viongozi wenzake wa Ccm wa wilaya na wapambe wao ndio wanaosababisha anguko la chama hicho katika Wilaya ya Songea mjini, hivyo kama kweli wanakitakia mema chama hicho wanapaswa kutambua kuwa utawala wa serikali inayofuata mfumo wa demokrasia, viongozi hawateuliwi bali huchaguliwa na hatma yao ipo mikononi mwa wananchi
Tambo na majigambo yao wanapokuwa kwenye kijiwe cha kisiwa ndui hazitakiacha chama hicho salama hata kidogo kwa sababu watu wengi wana malalamiko na majonzi kwa vitu vya ajabu wanavyovifanya ambavyo vitapelekea Ccm Songea mjini kionekana chama dhaifu cha upinzani kutokana na mwenendo huo
Wanapaswa kutambua kuwa uchaguzi maana yake ni utaratibu wa kuonesha utashi wa kile unachokitaka na usichokitaka, ni tendo la kuchagua kitu au mtu kwa sababu ya sifa nzuri. Ndiyo maana watu hupiga kura kuchagua wawakilishi wao kwenye vikundi mbalimbali vya kijamii, Halmashauri,bungeni na maeneo mengine
Suala la wagombea kusimama ili wapigiwe kura kamwe haliwezi kuhusishwa na utashi wa kiongozi kwani wanaohudhuria mikutano ya kampeni ndio wanaopima na kumchagua mtu anayefaa kuwawakilisha katika Halmashauri, bungeni na sehemu zingine kusudiwa
Kampeni ni wakati wa wagombea kunadi sera za vyama vyao kwa wananchi ili wajue ni kina nani, wa chama kipi wanaofaa kupewa ridhaa ya kuwawakilisha halmashauri,bungeni au kwingineko hivyo kuwatumia watu ambao toka wamezaliwa hawajawahi kuongoza hata kikundi cha watu kumi na wakati mwingine kutoa lugha za ovyo ni kutafuta anguko kubwa katika mizania ya siasa.
Chama cha Mapinduzi kinawasemaji wazuri wengi kuanzia ngazi ya shina hadi Wilaya pia kina madiwani, wabunge ambao wanafahamu kuzungumza na wapiga kura , hivyo kinapaswa kiwatumie watu hao kwani ni hazina kubwa, kwa sababu wao kuelezea mazuri ya chama na yale yaliyotekelezwa na Serikali ya chama wanauwezo mkubwa lakini kimewasahau au kuwadharau watu hao badala yake kinawaendekeza wahuni katika kuutafutia ushindi chama.
Wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 watu hao walitumika kukipigia kampeni chama na matokeo yake kata tano zilizopo mjini kabisa kuchukuliwa na Chama cha Chadema na katika uchaguzi huu mdogo uliofanyika hivi karibuni watu hao wametumika tena na kusababisha Kata hiyo ichukuliwe na upinzani.
Katika kampeni hizo zote zilifanywa kinyume cha makusudio yake kwa sababu badala ya wapiga debe kunadi sera za vyama vyao, walijikita zaidi kwenye maisha binafsi ya wagombea na familia zao wakiwachafua na kuwazushia mambo chungu nzima yasiyowahusu wapiga kura.
Waimbaji wakichukua jukumu la kuishauri na kuidhibiti serikali. Na matokeo yake tunayaona. Tupo tulipo kwa sababu tumejiweka tulipo na kama hatua madhubuti hazitachukuliwa uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Mletele Manispaa ya Songea yatajitokeza kama yaliyotokea katika uchaguzi wa Lizaboni.
Kwa maneno mengine ninachokisema ni kwamba tunakwama kimaendeleo kwa sababu tunafanya siasa zisizo na akili. Ushahidi wa kauli yangu hii ni kampeni tulizoshuhudia hadi sasa. Tuhuma za kutekwa na kuteswa tumezisikia.tuhuma za rushwa na matusi tumezisikia
Siasa zinazolindwa kwa mtutu wa bunduki haziwezi kuwa siasa zitakazomkomboa mwananchi. Siasa zinazoangalia uwiano wa jinsia badala ya uchangamfu wa ubongo haziwezi kuja na suluhu ya matatizo yetu katika Wilaya ya Songea na mkoa kiujumla
Wakati wengi walioingia katika fani ya siasa wameamua kupumzisha akili zao, wananchi nao wameanza kuwashabikia wanasiasa mithili ya mashabiki wa soka ambao hushabikia timu fulani bila kuwa na sababu za msingi.
Ushabiki wa mpira huwa ni ushabiki kutoka moyoni tu, hakuna mtu anakaa na kufikiria kisha kuamua aipende timu ipi. Ndipo tulipofika na matokeo yake sasa tunayaona na tutaendelea kuyaona.
Matokeo ya ushabiki bila fikra, tumejikuta tuna wanasiasa uchwara wengi na bahati mbaya sana katika fikra zao hizo zilizoshindwa kupevuka wanaendelea kuwa viongozi wetu na wanaoamua mustakabali wa maisha yetu na kesho ya taifa letu.
Siasa za leo kwanza zinaanzia maslahi binafsi, halafu maslahi ya chama na labda ndio yanafuata maslahi ya taifa. Na ushahidi wa hili ni tatizo la rushwa katika chaguzi zetu. Mtu mzima anakubali kumpigia huyu au yule kura kwa sababu yeye amepewa chochote bila kujali ukubwa au thamani ya alichopewa
Nachelea kutoa hitimisho kwamba inabidi tufike mahali tuweke mikakati ya kuwapima uelewa wale wanaotaka nafasi za uongozi katika ngazi zote. Lakini mchawi wa yote ni vyama vya siasa. Vyama hivi vina nafasi nzuri sana ya kuchuja wanaofaa na wasiofaa.
Kutokana na muktadha huo, anguko la Ccm katika uchaguzi wa udiwani wa Lizaboni nililitegemea na kama watashindwa kujirekebisha kutokana na hulka zao basi natarajia anguko kubwa zaidi katika uchaguzi mdogo kata ya Mletele na chaguzi zingine
Mwandishi wa Makala
Anapatikana 0715-335051
No comments:
Post a Comment