HATA kama tumetangaziwa kwamba aliyemteka na kumtesa Dk. Stephen Ulimboka alitoka nje ya nchi, imetajwa Kenya, ina maana itawaponya baadhi ya watu hapa nchini kuwajibika kwa tukio hilo? Vyovyote vile ni lazima mtu au watu wawajibishwe! Uzembe unajionyesha wazi wazi. Bila kuziba ufa huu, tutalazimishwa kujenga ukuta! Kama kikundi cha watu wabaya kutoka nje wanaweza kuingia ndani ya nchi bila kutambuliwa na kutekeleza kazi yao na kuondoka bila ya kukamatwa, mpaka wao waamue kwenda kanisani kuungama, ulinzi wa taifa letu si uko mashakani? Zamu hii ametekwa Ulimboka, je kesho watu hawa wakiingia na mabomu na kuyatega sehemu mbali mbali si itakuwa hatari kwa taifa letu? Je polisi wanaotiliwa shaka kushiriki sakata zima la kumteka na kumtesa Ulimboka, wataweza kukwepa kuwajibika kwa vile mhusika mkuu amejitokeza? Kwa maelezo ya Kamanda Kova, si kwamba mtu huyu (Aliyemteka na kumtesa Ulimboka) amekamatwa na Polisi, bali mtu mwenyewe alikwenda kanisani kuungama na “Mchungaji” akafanya kazi ya usalama wa taifa. Hadi hapo Polisi, hawawezi kukwepa kuwajibika! Wanashindwa kufanya kazi yao ya upelelezi hadi wasaidiwe na “Mchungaji”? Ni bahati mbaya kwamba Kamanda Kova, hakutaja kanisa ambalo mtu huyo alikwenda kuungama. Tungependa kulijua kanisa hilo na mchungaji huyo. Tujuavyo sisi ni kwamba maungamo ni “siri” kati ya anayeungama na anayeungamisha. Na kamwe, hata kama ni chini ya tishio la kupoteza maisha, mchungaji au padri, anakatazwa kutoa siri ya maungamo. Kutoa siri ya maungamo ni dhambi ya mauti na haina msamaha popote labda kwa Mungu Mwenyewe. “Usiri” huu wa maungamo ndo uliwajengea watu imani ya kuendelea kukumbatia mfumo huu wa kutubu dhambi. Mtu anataja dhambi zake, anasafishwa na kuendelea na maisha. Nje ya imani, huu ni mfumo mbaya kabisa; mtu anaweza kuendelea kutenda dhambi na kuwanyanyasa wengine kwa vile anajua kuna “mchungaji” wa kusafisha dhambi zake. Ni mfumo wa mtu kuufungua mdomo wake (kusema yote machafu) na kuufunga mdomo wa “mchungaji”. Kama wachungaji na mapadri wangejenga utamaduni wa kuzitangaza siri za maungamo, basi mfumo huu ungekufa zamani sana. Sasa huyu “mchungaji” aliyeamua kutoa siri za maungamo, na kuamua kufanya kazi na polisi ni nani? Huyu amesoma chuo gani cha teolojia? Au ni uchungaji wa kujipachika? Mchungaji mchana na usiku ni Polisi? Sijasema alichokifanya ni kibaya kwa taifa letu; sijasema amekosea kushiriki kazi ya ulinzi na usalama wa taifa letu; sijasema amekosea kumfichua huyu mtu aliyetenda unyama wa kumteka na kumtesa Dk. Ulimboka. Sote tumechukia na kuguswa na tukio hili na tungependa kumfahamu aliyetenda hivi na ni kwa nini? Hoja hapa ni namna mchungaji huyu alivyoshiriki. Mchungaji huyu anataka tuamini kwamba makanisa ni usalama wa taifa? Kwamba makanisa yanafanya kazi na serikali? Waislamu wamekuwa wakipiga kelele nyingi kwamba serikali inapendelea wakristu na kwamba makanisa yamekuwa yakifanya kazi kwa karibu sana na serikali ya Tanzania. Tumekuwa tukilipinga jambo hili kwa nguvu zote, lakini sasa baada ya Kamanda Kova, kutangaza kwamba mtu aliyemteka na kumtesa Ulimboka, ameibukia kanisani kwa njia ya maungamo, ni lazima tushawishike kwamba madai ya Waislamu yana ukweli fulani? Je, mchungaji huyu ametoa hili la Ulimboka tu, au anatoa mengine? Ushawishi huu wa kanisa kufanya kazi kwa karibu na polisi, unaishia hapo au unaendelea? Je “Mchungaji” huyu anashirikiana na polisi tu au ushawishi wake unaendelea kwenye idara nyingine za serikali? Tuna haki ya kujua, maana kama Kamanda Kova, ameamua kulifichua hili ni lazima aliweke wazi! Vinginevyo ni kuleta vurugu na kuvuruga amani ya watanzania. Inawezekana kabisa kwa kutaka kujikosha, Polisi wanatuingiza kwenye matatizo mengine makubwa: Tutaanza kuhoji umakini wa polisi wetu, tutaanza kuhoji kwa nguvu zote uhusiano wa serikali na kanisa na wenye imani zao wataanza kuhoji uadilifu wa wachungaji na mapadri juu ya siri za kitubio. Lakini pia kuna hili tatizo kubwa la kufunika mambo ambayo kesho na keshokutwa yatafumuka na kuliingiza taifa kwenye majanga makubwa. Kwa kumkamata mtuhumiwa huyo kutoka Kenya, na kama alivyoeleza Kamanda Kova kwamba atafunguliwa kesi; suala la Ulimboka, litakuwa halijadiliwi tena, kwani tutaambiwa kwamba liko mahakamani. Utamaduni wa mahakama zetu, kesi inaweza kwenda zaidi ya miaka mitatu; suala kama hili la Ulimboka, ambalo limegusa hisia za watu wengi na zaidi vijana wa nchi hii, kulifunika na kuzuia mjadala kwa kisingizio cha kesi kuwa mahakamani ni kuchokoza mzinga wa nyuki. Na kuna tatizo jingine la kuleta mahusiano mabaya kati ya nchi na nchi. Tunaweza kuanza kuinyoshea Kenya kidole kwa kutuingizia makundi ya majambazi ya kuwateka na kuwatesa. Hata Kenya, wanaweza kuja juu kwa kuitumia nchi yao kuficha madhambi ya baadhi ya watu wetu. Utamaduni huu wa kuitumia Mahakama kama kinga ya maovu, umeanza hivi karibuni nchi yetu ilipotumbukia kwenye dimbwi la mambo ya ovyo kama vile ufisadi na uporaji wa rasilimali za taifa. Hadi sasa mambo mengi yamefunikwa kwa kisingizio cha kesi kuwa mahakamani. Serikali inaposhikwa pabaya inakimbilia mahakamani. Suala likishafikishwa mahakamani, halijadiliwi tena bungeni, kwenye jamii na kwenye vyombo vya habari. Njia pekee ya kuwanyamazisha watu, kuwazuia watu kutetea haki zao za msingi ni kukimbilia mahakamani. Ile dhana nzima ya Mahakama kama chombo cha kutetea na kutoa haki sawa kwa kila mwananchi imeanza kupotea. Kinachojitokeza ni Mahakama kugeuka kuwa chombo kandamizi na kulinda maslahi ya wakubwa, serikali na watu wenye fedha. Mbali na kutumia maungamo kumfichua mtu aliyemteka na kumtesa Dk. Ulimboka, na mpango mzima wa kutaka kuitumia mahakama kuzuia mjadala juu ya sakata hili, kuna jambo jingine la kushangaza: Katika hali ya kawaida, tulitegemea mtu aliyetoka nje ya nchi kuja kutekeleza kazi ya “Mauaji”, angetoroka na kurudi nchini kwao mara baada ya kumaliza kazi yake. Sasa huyu “Mtu wa Ulimboka”, baada ya kazi yake, ambayo aliifanya na kuimaliza bila kukamatwa, akaendelea kuishi Tanzania, bila wasi wasi wowote na bila Polisi kutambua, mpaka Roho wa Bwana alipomwingia akaamua kwenda kanisani kwa mchungaji kuungama? Na je, aliungama kwa lengo la kusafishwa dhambi zake ili aendelee kutenda dhambi nyingine? Ili aendelee kuwateka na kuwatesa watu wengine? Au aliungama kwa kuchukia dhambi aliyoifanya? Na kama ni hivyo si angejisalimisha moja kwa moja kwa polisi na kwa kufuata mantiki, angejisalimisha nyumbani kwao Kenya. Kilio cha madaktari na watetezi wa haki za binadamu ni kwamba suala la kutekwa na kuteswa kwa Ulimboka liundiwe tume huru. Tume ambayo badala ya kukimbilia kanisani na nje ya nchi na mahakamani itachunguza kiini cha tukio lenyewe hapa hapa nchini. Kwa vile suala hili linaelekea kuwagusa watu wengi na kuibua dalili za kutoaminiana na kulituhumu moja kwa moja Jeshi la Polisi, hekima pekee ni kuliundia tume huru. Vinginevyo tutaendelea kusikia “hadithi” ambazo hazitatusaidia kuleta maelewano. Vyovyote vile kwa suala la Kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka, ni lazima mtu awajibishwe, vinginevyo ni kuendelea kuwalazimisha watu kujichukulia sheria mkononi! |
No comments:
Post a Comment