Tuesday, August 21, 2012
WANANCHI WAHIMIZWA ULINZI SHIRIKISHI WA MALIASILI ZA TAIFA
Na Steven Chindiye, Tunduru
WAKAZI wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma wamehimizwa kutoa ushirikiano katika ulinzi wa maliasili za Taifa zikiwa ni juhudi za kuwafanya wananchi wote kufaidi matunda ya rasilimali zetu.
Sambamba na maagizo hayo pia wito umetolewa kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwa kujitoa kwa hali na mali katika ukamilishaji wa miradi ya ujenzi wa majengo ya ofisi za askari wa vijiji zikiwa ni juhudi za serikali na wadau wa maendeleo kujidhatiti na uzuuiaji wa vitendo vya
ujangili.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Chande Nalicho wakati akifungua mafunzo ya siku 15 kwa wanajumuiya wanaojishughulisha na uhifadhi wa maliasili kwa jamii za Jumuiya za hifadhi za Nalika na Chingoli.
Akifafanua taarifa hiyo Nalicho mbali na kupongeza juhudi za uendeshaji wa mafunzo hayo alisema kuwa kupitia mafunzo hayo serikali ina amini kuwa kila mtu atatimiza wajibu wake na kutokomeza ujangili.
Awali akizungumzia faida za mafunzo hayo Mkurugenzi wa mradi wa kuhifadhi Ushoroba mtambuka wa Selous – Niassa Kumrwa Ngomelo alisema kuwa mradi huo unaofadhiliwa kwa hisani ya Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya wananchi wa Ujerumani – KfW, unalenga kuwashirikisha wananchi katika uhifadhi wa Rasilimali za maliasili hususani Wanyamapori kwa kuunda jumuiya za uhifadhi (Wildlife Management Areas).
Alisema mafunzo hayo yanalenga kupambana na tatizo la ujangili ambao wananchi pia wamekuwa ni miongoni mwa washiriki wa vitendo hivyo na kufichiana siri kwa matukio hayo.
Wakizungumzia hali ya Ujangili Wilayani Tunduru afisa wanyama pori Peter Mtani na mshauri idara ya maliasili Wilaya ya Tunduru mradi wa Wanyamapori Selous – Niassa Elias mungaya walisema taifa lisipo chukua hatua za makusudi kudhibiti Uwindaji haramu kupitia uanzishwaji wa jumuiya hizo ubinafsishaji na uwindishaji wa kitalii hauta kuwa na faida yoyote kwa watalii na wawindaji hao hawata waakuta wanyama katika misitu hiyo.
Akiongea kwa niaba ya wanajumuiya hao, mwenyekiti wa jumuiya ya Chingoli Dauda Mohamedi alisema kuwa baada ya mafunzo hayo wajumbe hao watatekeleza majukumu yao bila uoga tofauti na awali ambapo kulikuwa na tabia za kutupiana majukumu kati ya viongozi wa Serikali na Jumuiya hizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mratibu wa mfunzo hayo Meys Mkwembe alisema kuwa katika kipindi hicho wanajumuiya hao kujifunza mbinu za kuwashirikisha wananchi kupambana na Ujangili pia watajifunza masomo ya Utawala bora,Uongozi bora kwa vikundi,Kanuni za uhifadhi,Rushwa kama kikwazo kikuu cha utawala bora na sera ya wanyamapori, ufugaji nyuki, uvuvi na sera za ardhi katika uhifadhi wa maliasili.
Mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment